Hakuna lenye mwanzo lisilokuwa na mwisho.
Hakuna lenye marefu lisilokuwa na mapana.
Hakuna lenye butu lisilokuwa na ncha.
Hakuna lenye baridi lisilokuwa na joto.
Huu ni mwanzo wa mwisho wa ubeberu wa CCM na serikali yake iliyowaasi wananchi wake kuanzia takriban miaka 10-20 iliyopita.
Huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM na serikali yake ya kifisadi iliyoamua kuiuza nchi na rasilmali zake kwa bei ya kutupa kwa wawekezaji uchwara wanaokuja bila senti mfukoni, huku wakiwanyanyasa raia na kuwaua pasi na sheria kuchukua mkondo wake.
Huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM na serikali yake kuisigina katiba kwa kumtuma DPP kuwafungulia wapinzani kesi mfu za uchochezi na ugaidi, huku wapinzani hao wakikamatwa na kuteswa na polisi kabla ya kufikishwa mahakamani, ambako hatimaye mashtaka yote dhidi yao hufutwa na serikali kuamriwa kulipa fidia kubwa huku serikali ikikosa nafasi ya kukata rufaa kwa kuwa ofisi ya DPP ilipeleka mashtaka ya kitoto?
Huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM na serikali yake kulitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kuwa hatimaye Tume ya Haki za Kibinadamu na Utawala Bora umelitia hatiani jeshi hilo kuhusu mauaji ya Arusha ya Januari 5, 2011 huku IGP Mwema na RPC Andengenye wakiwa wahusika wakuu.
Na huu ni mwanzo wa mwisho wa CCM na serikali yake kuukandamiza upinzani kwa utawala wake wa kimabavu.
IGP Mwema,
RPC Andengenye,
DCP Chagonja,
DPP Feleshi...na viongozi wengine mlioshindwa kutumia vema madaraka yenu, mnangoja nini kuwajibika badala ya kusubiri kuwajibishwa?
Kwa kuwa tayari Katiba imevunjwa, kwa misingi hiyo hiyo, tutamshtaki Rais na serikali yake ICC, The Hague, potelea mbali kinga zake.
Huyu ataweka rekodi ya kuwa rais wa kwanza barani Afrika kushtakiwa ICC akiwa bado madarakani. Aibu na fedheha kwake na serikali yake na chama chake.
Wawakilishi wa kidiplomasia wa nchi za nje mnasubiri nini kufunga ofisi zenu? Au mpaka machafuko yaanze?
Dr. Slaa aliposema nchi haitatawalika, alimaanisha kwamba CCM ndiyo itasababisha hali hiyo na si CHADEMA. Hatimaye utabiri huo, kwa masikitiko yangu, umetimia.
Ee Mungu sikia kilio changu. Watoto wako wanakulilia. Katika safari ya ukombozi wengi wamekufa na wengi watakufa kwa mkono wa Shetani na mawakala wake. Kwa nini iwe hivyo?
Ninakushukuru Baba kwa wema wako kwa kutulinda na waovu hawa. Usituache Baba kwani tone moja tu la damu ya Yesu linaweza kuiokoa nchi hii na maafa. Ee Mungu tunasubiri utakaso wako kwani Mafarisayo wanatuzuia kuiona nchi yetu ya ahadi, Caanan. Ulitutoa Misri. Baba utakubali turudi huko?
Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.
Amina.