Na Waandishi Wetu Dar, Dodoma
WAKATI Spika wa Bunge, Samwel Sitta, akiagiza wabunge wa kambi ya upinzani kukatwa posho zao kwa kugomea kushiriki vikao vya Bunge, Kiongozi wa Kambi hiyo, Hamad Rashid Mohamed, amesema agizo hilo ni ukiukwaji wa sheria na Katiba ya nchi.
Hamad ambaye pia ni Mbunge wa Wawi (CUF) na Waziri Mkuu Kivuli, alisema mbali ya kukiuka sheria na Katiba ya nchi, agizo hilo la Spika Sitta, pia ni ukiukwaji wa misingi ya demokrasia na ustaarabu kwa wananchi katika kudai haki zao.
Agizo hilo la Spika ambalo alilitoa bungeni jana baada ya kipindi cha maswali na majibu, litawaumiza zaidi wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), ambao wameondoka kabisa bungeni tangu juzi kurejea Dar es Salaam.
Wabunge wengine vyama vya Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na United Democratic (UDP), ambao jana walirejea bungeni, watakosa posho ya siku ya juzi ambayo ilikuwa ya kwanza kwa mkutano wa 11 wa Bunge.
Wabunge hao walifikia uamuzi huo, wakipinga uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM) wa kutaka ifanyike kura ya maoni visiwani Zanzibar ili kupata ridhaa ya wananchi ya ama kuundwa au kutoundwa kwa serikali ya mseto visiwani humo, ni wa vyama vya CUF, Chadema na UDP.
Akizungumza na gazeti hili jana, Hamad, alisema wameshangazwa na agizo hilo la Spika Sitta, kwa kuwa suala la kugoma, ni haki ya msingi ya Kikatiba na kidemokrasia na pia ndio njia pekee ya kistaarabu kwa wananchi katika kudai haki wanazohisi kudhulumiwa.
" Tunashangaa sana kusikia kwamba, kuna kanuni inayowazuia wabunge kugoma," alisema Hamad ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF Taifa.
Akifafanua, alisema siku zote vinavyogoma ni vyama, viwe ni vya kisiasa au vya wafanyakazi na kutolea mfano wa mgomo uliofanywa hivi karibuni na wafanyakazi wa Kampuni ya Reli nchini (TRL) kupitia chama chao (TRAWU).
Alisema kwa kuwa mgomo ni haki ya Kikatiba, kidemokrasia na pia ndio njia pekee ya kistaarabu kwa wananchi kudai haki, serikali haikuwachukulia hatua yoyote wafanyakazi hao, badala yake iliwafuata, ikasikiliza madai yao na kuyashughulikia.
Alisema utaratibu wa kugoma, uliwahi kutumiwa hata na Tanzania ambayo iliwagomea makaburu kwenye Jumuiya ya Madola kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi walivyokuwa wakiwafanyia wazalendo wa Afrika Kusini.
Kutokana na hali hiyo, alisema kwa vile hapa nchini hakujawa na utaratibu wa mgombea binafsi, uamuzi wa wabunge wa kambi ya upinzani kugoma, ni wa haki kwa kuwa ulifanywa na wabunge hao wakiviwakilisha vyama wanavyotoka.
Hata hivyo, alisema huenda wakarejea Bungeni Jumatatu wiki ya ijayo kuendelea na vikao baada ya kujadili suala hilo kwenye chama na kuangalia namna mipango yao ilivyo.
Hamad, alisema jana jioni, wabunge hao walitarajiwa kukutana na Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam kujadili, pamoja na mambo mengine, namna ya kwatakavyofanikisha maandamano ya amani visiwani Zanzibar keshokutwa.
Maandamano hayo yatakayoongozwa na Profesa Lipumba, yanatarajiwa kufanywa na CUF kwa lengo la kuishinikiza CCM isaini rasimu ya makubaliano ya mwafaka wa kisiasa visiwani humo, uliofikiwa kati ya vyama hivyo viwili baada ya kufanya mazungumzo ya kutafuta mwafaka huo kwa miezi 14.
Akitangaza uamuzi huo jana, Spika Sitta, alisema alipata mwongozo wa kisheria na kubaini kwamba, uamuzi huo wa kambi ya upinzani ulikuwa na kasoro.
Spika Sitta alifafanua kwamba, kutokana na kasoro hizo katika maamuzi ya kambi hiyo, Kamati ya Kanuni. itakutana leo kupata taarifa zaidi za kisheria kisha kutoa matangazo ya uamuzi bungeni.
Alisema kasoro hiyo imezingatia ukweli kwamba, suala hilo linahusisha vyama hivyo kuliingiza bungeni haikuwa sahihi.
Sitta aliongeza kwamba, iwapo suala hilo litaachiwa, linaweza kuwa na athari kwani ugomvi baina ya vyama, unaweza kuingizwa bungeni.
Alisema kutokana na wabunge hao kutoka nje ya bunge na kwenda kufanya kazi ambayo si ya bunge, hawastahili kulipwa posho.
?Jana (juzi) kulikuwa na tukio la wabunge wa CUF wakiungwa mkono na wenzao wa upinzani, kutoka nje ya ukumbi wa bunge, jana (juzi) nimetafuta ushauri wa kisheria, nikaibini jambo hili lina kasoro,? alisema Spika na kuongeza:
? Hapa kilichopo ni mazungumzo ya vyama, tukiruhusu ugomvi wa vyama kuingia hapa, basi itakuja kuwa na athari zaidi?.
Spika Sitta aliongeza kwamba leo (jana), wanasheria walikuwa wakiaanda taarifa ya taratibu ambayo itatolewa kwa Kamati ya Kanuni ambayo itakaa leo kisha itatangaza maamuzi bungeni.
Juzi wabunge wote wa upinzani walitoka bungeni, muda mfupi mara baada ya kumalizika wimbo wa taifa, wakionyesha mshikamano wao kupinga hatua ya kusuasa kwa utekelezaji wa mwafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar.
Uamuzi huo unatokana na kiini macho ambacho kimefanywa na Chama cha Mapinduzi (CCM), katika mkutano wake katika kijiji cha Butiama, ambao tamko la NEC-CCM, lilitaka suala hilo la serikali ya mseto lipigiwe kura ya maoni na wananchi wa visiwani humo.
Hata hivyo, tangu kutangazwa kwa uamuzi wa NEC-CCM, hali ya kisiasa (Political Climate) hasa visiwani humo, inaonekana kuchafuka, huku CUF ikitaka Jumuiya Kimataifa kuingilia kati na kutupa lawama hizo kwa Rais Jakaya Kikwete, kwamba anahusika na usanii huo.
Source: Mwananchi