Kutoka BASATA: Mwongozo Mahsusi wa Uzingatiaji wa Maadili Katika kazi za Sanaa

Msanii

Platinum Member
Jul 4, 2007
22,603
29,748
Heading inahusika kama ilivyo. Lakini kwa mtazamo wangu hili jambo linaenda kuibua mjadala mkubwa huko mbeleni.

Najaribu kuweka link ya rasimu ya Kanuni hizo. Mnaweza kupeleka maoni kabla kisu hakijawekwa View attachment MWONGOZO- MAADILI.docx

=======

Simu: 255 22 2863748
Barua pepe: info@basata.go.tz
Tovuti: www.basata.go.tz


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO
BARAZA LA SANAA LA TAIFA (BASATA)

8 Barabara ya Kivukoni,
S.L.P 4779,
Dar es Salaam, Tanzania

MWONGOZO MAHSUSI WA UZINGATIAJI WA MAADILI KATIKA KAZI ZA SANAA

(Umeandaliwa chini ya Kifungu cha 4(l) na (j) cha Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 5 ya mwaka 2019)

YALIYOMO
1.0 UTANGULIZI. 4
2.0 MADHUMUNI. 5
3.0 MAANA YA MAADILI. 5
4.0 MAMBO YA KIMAADILI YA KUZINGATIA KATIKA UANDAAJI KAZI ZA SANAA. 6
5.0 WAHUSIKA WA UTEKELEZAJI WA MWONGOZO HUU. 6
5.1 WATUNZI NA WABUNIFU WA KAZI ZA SANAA. 6
5.2 MSANII. 7
5.3 WAZALISHAJI WA KAZI ZA SANAA. 7
6.0 WAMILIKI VYOMBO VYA HABARI AU MITANDAO YA KIJAMII. 8
8.0 WAJIBU WA JAMII KATIKA KUSIMAMIA MAADILI. 9
9.0 MAMLAKA YA BARAZA KATIKA KUSIMAMIA MAADILI. 10
10.0 MAREKEBISHO. 10
11.0 TAREHE YA KUANZA KUTUMIKA. 10

TAFSIRI ZA MANENO MBALIMBALI YALIYOTUMIKA KATIKA MWONGOZO HUU

BARAZA
- Maana yake ni Baraza la Sanaa la Taifa
MWONGOZO - Maana yake ni taratibu za kimaadili za kuzingatia wakati wa kutengeneza au kupeleka kwa umma kazi ya sanaa.
MSANII - itakuwa na maana kama ilivyofafanuliwa katika Sheria
SHERIA - maana yake ni Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa Sura ya 204 kama ilivyofanyiwa marekebisho.

MWONGOZO WA UZINGATIAJI WA MAADILI KATIKA KAZI ZA SANAA

1.0 UTANGULIZI

1.1 Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ni Taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Na. 23 ya mwaka 1984 (Sura 204), kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Bunge Na. 5 ya mwaka 2019 Sehemu ya IV. Kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Sheria hiyo Majukumu ya BASATA ni pamoja na kufufua, kukuza na kuhimiza uzingatiaji wa maadili katika sekta ya Sanaa na kuchukua hatua stahiki dhidi ya uvunjifu wa maadili.
1.2 Katika zama hizi tumeshuhudia wasanii wakiongezeka kwa kasi sana (hasa katika fani ya muziki wa kizazi kipya) kiasi kwamba wasanii hao wanahitaji kukumbushwa na kuhamasishwa kufuata maadili ya kazi zao. Ongezeko hilo limeambatana na ukiukwaji wa maadili hali iliyopelekea Baraza kufanya marekebisho ya Sheria yake na kuongeza Vipengele vya (l) na (q) katika Kifungu cha 4 (1) ili kulipa Baraza mamlaka ya kusimamia maadili.
1.3 Ongezeko hilo la wasanii limechangiwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia na kusababisha idadi ya wasanii na kazi za sanaa kuongezeka kwa kasi. Ni dhahiri kuwa kwa sasa, usimamizi unaofaa katika sekta ya sanaa ni ule unaoweka mazingira yanayoijenga sekta kuwa rasmi na kazi za Sanaa kuwa njia ya uchumi badala ya burudani pekee, lakini hayo ni lazima yafanyike kwa kuzingatia maadili katika utendaji wa kazi.
1.4 Mwongozo huu wa uzingatiaji wa maadili katika kazi za sanaa ni maelekezo kwa watunzi, waimbaji, wanenguaji (dancers), mameneja wa wasanii, wazalishaji wa kazi za sanaa, wakuzaji, wamiliki wa vyombo vya habari, wamiliki wa mitandao ya kijamii, wamiliki wa vyombo vya usafiri, pamoja na wasambazaji wa kazi za sanaa. Wadau wote hawa na jamii kwa ujumla wanao wajibu wa kulinda, kuzingatia maadili na kutoa taarifa ya uvunjifu wa maadlili kwa mujibu Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo au taratibu mbalimbali zinazosimamia sekta ya sanaa ambayo ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla.

2.0 MADHUMUNI
2.1 Lengo la uwepo wa maadili katika jamii ni kujenga misingi ya imani za maisha zinazokubaliwa na kufuatwa na jamii katika mawazo na akili za watu wa jamii ya Watanzania, hasa watoto na vijana, ili jamii iweze kufikia na kudumisha malengo na mategemeo yake toka kizazi hadi kizazi.
2.2 Mwongozo huu umeandaliwa ili kutatua changamoto za ukiukwaji wa maadili zitokanazo na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika sekta ya sanaa.

2.3 Sera ya Utamaduni Sehemu ya sita (6.1.6) na Kifungu cha 4(1) (l) cha Sheria, Sura 204 vinatoa maelekezo kwa Serikali kupitia Baraza, kusimamia maadili na kuhakikisha kuwa shughuli za burudani zinazofanyika hazivunji maadili ya Taifa.
2.4 Vilevile dhumuni la Mwongozo huu ni kulinda jamii dhidi ya maadili yasiyofaa, ikiwemo kulinda;
(a) jamii dhidi ya vitendo viovu,
(b) watoto dhidi ya maudhui yasiyofaa kwa makuzi yao,
(c) usalama wa nchi
(d) kuleta amani na mshikamano katika jamii.

3.0 MAANA YA MAADILI
3.1 Kwa muktadha wa Mwongozo huu neno maadili litajumuisha tabia njema, misingi, kanuni, na taratibu zinazofuata mienendo inayokubalika katika jamii, ambayo inaongoza mahusiano katika makundi ya jamii husika. Maadili yanamtaka mtu kufanya jambo lililo sahihi, mahali sahihi na kwa wakati sahihi. Kimsingi, maadili ni zao la mila na desturi za utamaduni wa jamii husika.
3.2 Sambamba na tafsiri ya maadili tajwa hapo juu, vilevile mambo yote yaliyoainishwa katika kipengele cha 4.0 (a)-(k) cha Mwongozo huu yatakuwa ni sehemu ya tafsiri ya maadili kwa muktadha wa Mwongozo huu.

4.0 MAMBO YA KIMAADILI YA KUZINGATIA KATIKA UANDAAJI KAZI ZA SANAA
Pamoja na tafsiri ya maadili katika Kipengele cha 3.1 hapo juu, kazi ya sanaa itaonekana imekidhi matakwa ya Mwongozo huu wa maadili iwapo itakuwa imezingatia mambo yafuatayo;
(a) Haivunji heshima ya mwimbaji, msikilizaji au mtazamaji,
(b) Haina upotoshaji wa aina yoyote,
(c) Haichochei ghasia ya aina au namna yoyote
(d) Haina maneno ya uongo, uchochezi au yanayokashifu watu wengine,
(e) Haihudhurishi lugha chafu au matusi
(f) Haina ujumbe wa unyanyasaji au ukatili
(g) Haitukuzi ubaguzi wa rangi, kabila au dini
(h) Haikashifu taifa la Tanzania au mataifa mengine,
(i) Haidhoofishi umoja, ushirikiano, na ustawi wa jamii,
(j) Haishawishi vitendo vya kihalifu, au uvunjifu wa Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kimataifa au Sheria za mataifa mengine,
(k) Haishawishi wala kuhamasisha vitendo vya ngono, ushoga, usagaji au matumizi ya dawa za kulevya
(l) Inazingatia masharti ya Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba mbalimbali ya kimataifa katika masuala ya haki miliki na masuala mengine yote yanayohusiana na haki za ubunifu.

5.0 WAHUSIKA WA UTEKELEZAJI WA MWONGOZO HUU
Mwongozo huu umetaja wahusika ambao watakuwa na wajibu wa kutekeleza maelekezo kama ifuatavyo;

5.1 WATUNZI NA WABUNIFU WA KAZI ZA SANAA
Utunzi ndio msingi wa kazi ya sanaa. Mtunzi anao uhuru wa kufanya kazi katika mawanda mapana katika kubuni/kutunga, uhuru wa kuonyesha ustadi na kuelezea mawazo yake kwa jamii. Kwa vile kazi anayoifanya inakwenda kwa jamii yenye mchanganyiko wa aina na makundi ya watu tofauti, hivyo ana jukumu la kuhakikisha kuwa, kazi ya sanaa anayoiandaa imezingatia maadili kama ilivyofafanuliwa katika Mongozo huu.

5.2 MSANII
5.2.1 Msanii ana wajibu wa kujiridhisha na kuelewa kazi ya sanaa aliyoiandaa imezingatia maadili kwa mujibu wa Mwongozo huu.
5.2.2 Msanii ana wajibu wa kumtaka mtunzi (kama kazi hiyo ina maneno yaliyotungwa) kurekebisha maneno ya kazi ya sanaa kama maneno hayo yatakuwa hayajazingatia masharti yaliyoanishwa katika Mwongozo huu.
5.2.3 Kwa muktadha huo msanii hatatakiwa kuimba maneno ya mtunzi kama maneno hayo hayajazingatia maadili.
5.2.4 Msanii atatakiwa kuzingatia maadili kama ilivyoainishwa katika Mwongozo huu awapo jukwaani au sehemu nyingine yoyote akiwa anafanya kazi za sanaa.
5.2.5 Msanii anapaswa kuwa mfano bora wa uzingatiaji wa maadili kwa waanii wenzake na jamii nzima kwa ujumla.

5.3 WAZALISHAJI WA KAZI ZA SANAA
5.3.1 Mzalishaji wa kazi ya sanaa ni mtu muhimu katika kuhakikisha kuwa kazi ya sanaa inaandaliwa kwa kuzingatia viwango bora na kuhakikisha kuwa kazi anayozalisha haikiuki masharti yaliyoainishwa katika Mwongozo huu.
5.3.2 Mzalishaji wa kazi ya sanaa haruhusiwi kuzalisha kazi ya sanaa iwapo kazi hiyo itakuwa haijazingatia masharti yaliyoanishwa katika Mwongozo huu.
5.3.3 Meneja wa msanii, mkuzaji wa kazi za sanaa au mtu yeyote anayehusika na kazi ya sanaa kwa namna yoyote ile, atakuwa na wajibu wa kuhakikisha kuwa kazi ya sanaa anayoshughulika nayo imezingatia maadili kwa mujibu wa Mwongozo huu.

5.4 WASAMBAZAJI WA KAZI ZA SANAA
5.4.1 Mwongozo huu pia utawahusu wasambazaji wa kazi za sanaa. Msanii au mzalishaji wa kazi ya sanaa au mtu mwingine yeyote anayehusika na usambazaji wa kazi yoyote ya sanaa atapaswa kuzingatia masharti yote yaliyoainishwa katika Mwongozo huu.
5.4.2 msambazaji wa kazi ya sanaa au mtu yeyote yeyote anayejihusisha na usambazaji wa kazi ya sanaa atakayekiuka masharti yaliyoainishwa katika Mwongozo huu, atakuwa ametenda kosa na ikithibitika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria, Kanuni au Taratibu zinazoongoza tasnia husika.
5.4.3 Itakuwa ni kosa kwa msambazaji wa kazi ya sanaa kusambaza kazi ya sanaa iliyofungiwa na Baraza au kukatazwa kuonwa au kusikilizwa kwa umma kwa namna yoyote ile, na ikithibitika mhusika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.

6.0 WAMILIKI VYOMBO VYA HABARI AU MITANDAO YA KIJAMII
6.1 Mmiliki wa chombo cha habari kupitia au mmiliki wa mtandao wa kijamii, anao wajibu wa kuzingatia Mwongozo huu, kabla ya kurusha hewani kazi zake za sanaa au za mtu mwingine zilizopelekwa na msanii, meneja wa msanii au mtu mwingine yeyote.
6.2 Mmiliki wa chombo cha habari au mtandao wa kijamii hataruhusiwa kucheza kazi ya sanaa kama kazi hiyo itakuwa haijazingatia maadili kwa mujibu wa Mwongozo huu.
6.3 Ikitokea chombo cha habari au mmiliki wa mtandao wa kijamii amepokea kazi ya sanaa ambayo kwa sehemu haijazingatia maadili kwa mujibu wa Mwongozo huu, chombo hicho cha habari kinaweza kuchukuliwa hatua stahiki ili sehemu ya kazi hiyo ambayo imekiuka maadili, isisikike au kuonekana kwa umma.
6.4 Chombo chochote cha habari au mmiliki wa mtandao wa kijamii atakayekiuka masharti yaliyoainishwa katika Mwongozo huu, Baraza likijiridhisha na ukiukwaji huo litawasilisha taarifa kwenye mamalaka inayosimamia chombo hicho cha habari ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa Sheria.
7.0 WAMILIKI WA VYOMBO VYA USAFIRI
7.1 Mmiliki au mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba ya mmiliki wa chombo cha usafiri anao wajibu wa kuhakikisha kwamba kazi ya sanaa inayochezwa katika chombo chake cha usafiri, imezingatia maadili kwa mujibu wa Mwongozo huu.

7.2 Mmiliki au mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba ya mmiliki wa chombo cha habari, hataruhusiwa kupokea na kucheza kazi ya sanaa ambayo haijazingatia maadili kwa mujibu wa Mwongozo huu.

7.3 Mmiliki au mtu yeyote anayefanya kazi kwa niaba ya mmiliki wa chombo cha usafiri, atakayekiuka masharti yaliyoainishwa katika Mwongozo huu atakuwa ametenda kosa na Baraza likijiridhisha litawasilisha taarifa katika mamlaka inayohusika ili mmiliki huyo aweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria zinazosimamia sekta ya usafirishaji.

8.0 WAJIBU WA JAMII KATIKA KUSIMAMIA MAADILI
8.1 Suala la maadili linaanzia katika ngazi ya familia, hivyo wazazi na walezi wanatakiwa kutimiza wajibu wao wa malezi kwa watoto wao kwa kuwafundisha misingi ya maadili wangali wadogo.

8.2 Mtu yeyote atakayeona kuna uvunjifu wa Maadili katika kazi yoyote ya sanaa kama ilivyoainishwa katika Mwongozo huu, ana wajibu wa kutoa taarifa katika mamlaka zinazohusika ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

9.0 MAMLAKA YA BARAZA KATIKA KUSIMAMIA MAADILI
9.1 Mamlaka ya Baraza katika kushughulikia maadili yameainishwa katika kifungu cha 4(1) (p) cha Sheria. Kwa mamlaka hayo, Baraza litaweka utaratibu mzuri wa usimamiaji wa maadili kwa wasanii na watu wengine wanaojishughulisha na kazi za sanaa.
9.2 Baraza litakuwa na jukumu la kutoa elimu ya maadili katika sanaa ili wasanii, wadau na jamii kwa ujumla ielimike na kuzingatia maadili kama yalivyoainishwa katika Mwongozo huu.
9.3 Baraza litashirikiana na mamlaka zingine za nchi katika kushughulikia masuala ya maadili kwa wasanii, vyombo vya habari, vyombo vya usafiri na wadau wengine wa Sanaa.
9.4 Inapotokea msanii au mtu yeyote amekiuka taratibu za kimaadili kama ilivyoainishwa katika Mwongozo huu, Baraza litachukua hatua stahiki kama ilivyoainishwa hapa chini.
9.4.1 Kwa wasanii na wadau wengine wa Baraza watachukuliwa hatua kama ilivyoinishwa katika Kanuni.
9.4.2 Kwa vyombo vya habari na vya usafiri, Baraza litawasilisha taarifa za ukiukwaji huo katika mamlaka zinazosimamia vyombo hivyo.

10. 0 MAREKEBISHO
Baraza linaweza kufanya marekebsho katika vipengele vya Mwongozo huu wakati wowote inatakapohitajika kufanya hivyo.

11.0 TAREHE YA KUANZA KUTUMIKA
Mwongozo huu wa maadili utaanza kutumika mara baada ya kutangazwa katika Gazeti la Serikali. Mtu yeyote anayehusika na Mwongozo huu na ambaye hatafuata maelekezo ya Mwongozo huu, atakuwa ametenda kosa la kimaadili na hatua zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na taratibu zinazoongoza sekta husika.

Mwongozo huu umetolewa na Katibu Mtendaji-Baraza la Sanaa la Taifa

UMETOLEWA NA:
KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA SANAA LA TAIFA
S.L.P 4779
DAR ES SALAAM
20 JULAI, 2021
 

Attachments

  • Barua petition.docx
    18.3 KB · Views: 9
Back
Top Bottom