Anaandika Askofu Bagonza PhD
MARIDHIANO YASIYOHITAJI KUKAA MEZANI
Kwa hali ilivyo, wito wa maridhiano haupokelewi kirahisi. Hatuna watu wengi wenye uadilifu wa kuaminika pande zote. Tuna mfumo unaoamini kila mtu ana bei na kwamba serikali HAIJAWAHI kushindwa. Mazingira haya ni magumu kupata maridhiano. Nashauri tujikite katika maridhiano yasiyohitaji kukaa mezani. Yakifanyika, ndipo kukaa mezani “labda” kunawezekana. Ni haya;
1. Sitisha utekaji na ukamataji kwa kauli na vitendo. Utekaji na ukamataji unachochea mpasuko.
2. Achia bila masharti waliotekwa, walio mahabusu na wanaoshtakiwa kisiasa.
3. Ruhusu watu wapate miili ya ndugu zao na “kama” kuna iliyofukiwa waonyeshwe ili wachukue udogo au kuweka shada la maua. Itawafanya wamalize matanga.
4. Lifanye taifa liwe la wote - wanaopinga na wanaounga mkono. Si afya wanaopinga kuwa wakimbizi. Inaongeza chuki na kuanika mambo yetu.
5. Acha siasa uchwara (spinning) za kukanusha kanusha na kuficha ficha. Inaongeza hasira. Wajaluo wanasema “binti hawezi kuficha matiti; yakiota yameota”. Tuna msiba mkubwa. Ruhusuni taifa liomboleze. Ni njia ya kuridhiana.
6. Acha fikra za kipumbavu kuhusu dini. Walioua wamo wa dini zote. Hawakutumwa na dini zao kuua. Waliouawa wamo wa dini zote. Hawakufa kwa sababu ya dini zao.
Mali za waumini wa dini zote akiwamo Mtani wangu Wasira ziliharibiwa. “Aliyeruhusu kuua” kama yupo, hakuagiza kuua watu wa dini fulani tu. Ukitumia dini katika hali tuliyo nayo, unaiponza serikali kwa kudhani unaisaidia. Pia unaifanya dini yako ionekane ni bangi inayoondoa uhalisia.
7. Serikali ibadili mkao wake na “kujionyesha” iko upande wa wanaoomboleza. Itoe tamko linalokiri kuwa katika kulinda mali na uhai, kuna kitu kilienda vibaya. Baada ya tamko, watu waone vitendo vya kuwajibishana au kujiwajibisha. Hiyo itaponya na kuunganisha taifa. Tusisubiri kulazimishwa kuwajibika au kuwajibishana.
8. Serikali iwe na mtu anayetoa matamko na msimamo wa serikali. Kwa sasa umma ndiyo wenye haki ya maoni. Walio serikalini na chama tawala wasiwe na maoni nje ya vikao vyao. Eti, “Wananchi waridhiane na wananchi”!? Kweli?😳😳
9. Penye msiba, kuna waombolezaji huwa wanaondoka na vijiko na sahani.
Sitisheni matumizi ya fedha katika kuzima moto huu. Wanaoishi kwa kutegemea posho za kushughulikia “wachochezi” ni wezi wa vijiko na sahani msibani. Asiyetaka kujitolea akae pembeni.
10. Tukubali kuna mgogoro wa madaraka ndani na nje ya CCM. Kuutatua kwa mtutu ni kuuongeza. Kabla ya kukaa mezani, iruhusuni CCM kiwe chama kifanye siasa. Kiwe huru kukemea na kukaani dhuluma katika nchi. Hivi sasa dhambi za serikali ni za CCM na dhambi za CCM ni za serikali. Amkeni kumekucha.
11. Wanaohubiri amani tu hawajipanga kama wanaoharibu amani. Gen Z na serikali wamejipanga vilivyo kuharibu amani. Nawashauri wanaohubiri amani tu, wajipange vizuri. Haki ya kuishi haihojiwi na mamlaka yoyote.
Siasa isiyo na dini ndani yake ni ubabe.
Dini isiyo na siasa ndani yake ni bangi.