21st January 2011
Nipashe
Kilichowasilishwa ni viambatanisho tu
Mahakama yasema bado inaisubiri
Siku tatu baada ya Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Ignas Kitusi, kueleza kwamba, hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) iliyoamua kesi ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited dhidi ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), imewasilishwa Mahakama Kuu, sasa imebainika kilichowasilishwa mahakamani hapo si hukumu, bali viambatanisho vya mwenendo wa kesi hiyo.
Hukumu hiyo iliyotolewa na ICC iliyoko nchini Ufaransa, Novemba 16, mwaka jana chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhihi Swithin Munyantwali na Jonathan Parker, inaiamuru Tanesco kuilipa Dowans Sh. bilioni 94, zikiwa ni fidia ya kuvunjiwa mkataba wake (Dowans).
Habari kutoka Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam zilizothibitishwa na baadhi ya maofisa waandamizi wa mahakama hiyo, zinaeleza kuwa viambatanisho hivyo vilibainika baada ya Ofisi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, ambayo inashughulikia suala hilo, kufungua kifurushi kilichohifadhi nyaraka hizo.
"Hadi sasa hukumu ya ICC bado haijawasilishwa mahakamani. Kitusi alipoeleza vile, kifurushi kilikuwa hakijafunguliwa. Alitoa jibu la jumla. Kilichowasilishwa na ICC ni Annexture (viambatanisho vya mwenendo wa kesi) ile," alisema Afisa mmoja mwandamizi wa Mahakama Kuu kwa sharti la jina lake kutochapishwa kwa maelezo kuwa sio msemaji.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, hukumu hiyo inaitaka Tanesco kuilipa Dowans Tanzania Limited dola za Marekani 65,812,630 (Sh. bilioni 94) zikiwa ni fidia ya kuvunjiwa mkataba wake.
Ngeleja alisema malipo ya fidia hiyo hayatafanywa endapo hukumu hiyo haitasajiliwa katika Mahakama ya Tanzania.
Wakati hayo yakijiri, habari zilizothibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Francis Kiwanga, zinaeleza kuwa wanaharakati wa mashirika 17 nchini, jana waliwasilisha barua Mahakama Kuu ya Tanzania kuomba waruhusiwe kupeleka maombi ya kutaka hukumu hiyo ya ICC isisajiliwe katika mahakama yoyote itakapopelekwa.
Akizungumza na NIPASHE jana mara baada ya barua yao kuwasilishwa Mahakama Kuu, Kiwanga alisema nakala ya barua hiyo wameipeleka kwa wasajili wote wa Mahakama kwa vile wana maslahi na hukumu hiyo kwa niaba ya Watanzania.
Alisema wamelazimika kufanya hivyo baada ya kusikia kuwa hukumu hiyo imewasilishwa Mahakama Kuu wakati walikwisha kufungua kesi kupinga suala hilo katika Mahakama ya Biashara, ambayo hadi sasa haijasajiliwa.
Kiwanga alisema kesi yao imeshindwa kusajiliwa katika Mahakama ya Biashara kwa vile hukumu hiyo ya ICC haijawasilishwa katika mahakama hiyo kwa ajili ya kusajiliwa.
Wanaharakati hao kupitia mashirika 17 yasiyokuwa ya kiserikali, walifungua kesi hiyo katika mahakama hiyo kuitaka ikatae kusajili hukumu hiyo ya ICC ili kuzuia malipo hayo kufanyika kwa Dowans.
Hata hivyo, kesi ya wanaharakati hao awali ilielezwa kuwa imesajiliwa na kupewa namba 4 ya mwaka 2011 na kupangiwa Jaji Robert Makaramba.
Prof. Saffar naye aipinga Dowans
Wakati huo huo, mwanasheria aliyebobea, Profesa Abdallah Saffar, amesema hakuna haja ya kulipa fedha hizo kwa sababu kampuni hiyo ilirithi mkataba mwenye utata.
Profesa Saffar alisema hata sheria za kimataifa zinasisitiza haja ya kuheshimu mikataba ya kimataifa, lakini iliyo halali.
"Sheria za kimataifa hazisemi tuheshimu mikataba feki kama huu wa Dowans unaojulikana wazi kwamba kulikuwa na mizengwe na mazingira ya rushwa," alisema.
Alikumbusha kwamba mwaka 1961 baada ya Tanganyika kupata uhuru, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza kutoutambua mkataba wa Mto Nile uliokuwa ukizikataza nchi za Afrika Mashariki kutumia maji ya ziwa Victoria na Tanzania haikupata madhara yoyote.
"Mimi nakubaliana kabisa na Samuel Sitta (Waziri wa Ushirikiani wa Afrika mashariki) kwa sababu hakuna sababu yoyote ya kuilipa kampuni ya Dowans, kufanya hivyo ni kutapanya rasilimali za taifa," alisema Profesa Saffar.
Alisema Ibara ya 9 (c) ya Katiba ya nchi, inaeleza pamoja na mambo mengine, kuwa shughuli za serikali zitatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha kwamba utajiri wa taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla na pia kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine.
Amepinga azma ya serikali kuilipa kampuni ya Dowans siku chache baada ya Waziri Sitta kueleza waziwazi kwamba ulipaji wa Dowans ni sawa na kuhujumu uchumi kwa kuwa ni mpango wa watu watatu wenye malengo ya urais mwaka 2015.