Kivuli cha falsafa za Hayati Magufuli ni fumbo linaloishi ndani ya mawazo ya Rais Samia

Deogratias Mutungi

Senior Member
Oct 1, 2019
137
179
Kivuli cha falsafa za JPM, ni fumbo linaloishi ndani ya mawazo ya Rais Samia

Deogratias Mutungi


Ukweli wenye mantiki ndani yake upo wazi kuwa kivuli cha falsafa za JPM ni fumbo linaloishi sasa na litakaloendelea kuishi ndani ya mawazo ya rais Samia Suluhu Hassan, dhana hii inajengwa kifikra zaidi kutokana na wawili hawa kuwa karibu katika kupanga, kufikri na kushauriana jinsi ya kuwatumikia Watanzania kiuchumi, kimaendeleo, kisiasa na kijamii, kinadharia ni vigumu sana kutenganisha falsafa za viongozi hawa wawili wakuu wa serikali ambao walikuwa wanafanya kazi kwa ukaribu zaidi na katika mifumo ya utekelezaji wa sera, mipango, ahadi na ilani ya chama chao.

Kifalsafa JPM na Samia wanasimama katika dhana ya upacha wenye misingi ya uwajibikaji uliojitoa kuitumikia nchi na Watanzania wenye uhitaji zaidi “Wanyonge” kwa moyo wote wa kizalendo, Falsafa ya kimantiki kati ya Samia na JPM ilinuia kuongoza na si kutawala kwa lengo la kuacha alama na nyao kwa umma wa Watanzania.

Mapacha hawa kisiasa walijenga falsafa iliyofanikiwa kushika hatamu kwa muhula wa kwanza wa awamu ya tano, wawili hawa wamejenga uaminifu kwa umma kulingana na utendaji wao wa kazi usio na mfano kisiasa na kwa jinsi walivyo wajibika kwa watu wa hali ya chini. Ni dhahiri kuwa chini ya Samia na JPM, Tanzania imejengwa na kujengeka, nchi imejitambulisha na kujidhihirisha kimataifa kuwa ina uwezo wa kukusanya kodi za ndani na kujenga miradi yake mikubwa ya kiuchumi bila nyenzo kutoka nje.

Falsafa za mapacha hawa wawili zilisimama katika mawazo ya kiukombozi zaidi hasa katika kuvusha nchi kwenye daraja la uchumi unaolegalega kwenda kwenye uchumi wenye matumaini ya watu na vitu, Ukombozi wa kiuchumi kutoka kwa mabepari wa ndani na nje wanaoinyonya nchi kwenda kwa wanyonge wa kawaida, haikuwa rahisi kwa viongozi hawa kukabiliana na magenge ya unyonyaji bali vita kati ya viongozi hawa na magenge hayo, lakini mwendazake JPM na Samia wamepiga hatua chanya na kuonesha mfano wa kuigwa miongoni mwa mataifa ya Kiafrika na duniani kwa ujumla.

Kwa sasa inawezekana swali la msingi linalogonga vichwa vya watanzania walio wengi ni, Je Samia Suluhu Hassan ataweza kutimiza malengo ya kifalsafa ambayo ameachiwa na mwendazake JPM? Ni swali gumu kimtazamo na kifikra, lakini uenda likawa swali rahisi zaidi kihistoria na kimkakati na kimfumo kwa serikali ya sasa iliyo chini ya Samia Suluhu Hassan. Makala haya yatapambanua swali hili kwa kutumia vigezo vya sayansi ya siasa hili kuondoa hofu kwa umma wa Watanzania katika kipindi hiki cha mpito.

Tukianza na dhana ya historia rais Samia Suluhu ni kiongozi mbobevu na muwajibika aliyehudumu ndani ya serikali kwa kipindi cha muda mrefu, aidha Samia amehudumu bara na visiwani katika nafasi tofauti tofauti ni mwanamama shupavu aliyeacha alama ya ufanisi na mafanikio kila ofisi ya umma aliyopita, Rais Samia ana misimamo yenye dira ya kutatua na kuwajibika kwa watu wake pia ni kiongozi mwenye maono chanya yenye kuleta mabadiliko kwa kila agenda anayoikusudia kuifanyia kazi, Ni mwana mapinduzi na mwanasiasa mwenye tamaa ya mafanikio kiuongozi.

Aidha kwa kumulika dhana ya kimkakati na kimfumo, Rais Samia Suluhu ni kiongozi anayesimamia na kutekeleza sera za serikali zinazo hitaji usimamizi na utekelezaji chanya wa moja kwa moja, dhana hii inajitambulisha wazi kwa Samia pale alipokuwa waziri wa Afya, Jinsia na Watoto mwaka 2000, chini ya serikali ya rais Aman Karume, licha ya ugeni wake katika wizara hiyo lakini Samia alionyesha uwezo na weledi uliotukuka katika kusimamia sera, mipango na mikakati ya wizara na serikali kwa ujumla wake.

Umahiri na Uwezo wa Samia ulijitambulisha zaidi mwaka 2005, pale alipopewa Wizara ya Utalii Biashara na Uwekezaji, ndani ya Wizara hii Samia Suluhu alionyesha uwezo na kipawa chake cha uongozi wenye kuacha alama na nyayo kwa kutunga sera zenye tija kwa utalii wa visiwa vya Zanzibar, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha kanuni za kimkakati katika baraza la wawakilishi ili kuifanya Zanzibar kukusanya mapato mengi kupitia dirisha la utalii.

Hata hivyo, kitendo cha Serikali ya awamu ya nne Chini ya Jakaya Kikwete kumuamini na kumpa Wizara ya maswala ya Muungano akihudumu chini ya Makamu wa rais Mohamed Gharib Bilal kulidhihirisha rasmi uwezo wa Samia Suluhu kuwa ni kiongozi mwenye uwezo na maono yenye fikra ya utatuzi wa matatizo yanayohitaji kutatuliwa na kutafutiwa ufumbuzi kwa maslahi ya umma,

Aidha tukio la mwaka 2014, la Samia Suluhu Hassan kushika nafasi ya makamu mwenyekiti wa bunge maalumu la katiba na kupata ushindi wa nafasi hiyo kwa asilimia 74.6% zidi ya mwenzake Amina Abdalla Amour aliye pata asilimia 24% inaonyesha ni ushindi alioupata kutoka kwa wajumbe waliokuwa na imani na uwezo wake wa kutenda, kuwajibika na kusimamia maslahi ya umma ndani ya bunge maalumu la katiba.

Kwa nukta hiyo tunaweza kulinganisha dhana mbili za kihistoria, Kimkakati na kimfumo kadri zilivyo fafanuliwa hapo juu na kung’amua ukweli wa jibu la swali letu la uwezo wa rais wetu Samia Suluhu Hassan kuwa ni mkubwa na ataweza kutuvusha kifalsafa na kufikia malengo ya serikali yake iliyokuwa imekusudia kuyafanya awali kabla ya kifo cha hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Kwa muktadha huo Tanzania na Watanzania kwa ujumla tupo mikononi salama mwa rais Samia Suluhu Hassan.

Watanzania tunao wajibu wa kufungamana kwa pamoja katika kipindi hiki kigumu katika kuenzi yale mazuri tuliyoachiwa na mwendazake haya ti Dkt. John Pombe Magufuli, tujenge umoja kwa maslahi ya ustawi wa taifa letu na tuzike na kusahau tofauti zetu hasi, huu si wakati wa kufukua makaburi bali kuonyesha upendo wenye amani sambamba na kumuunga mkono rais wetu Samia Suluhu Hassan hili tufike kwenye kilele cha malengo kwa mustakabari wa ufanisi na ukombozi wa taifa letu.

Kwa mujibu wa Katiba yetu ya mwaka 1977, ibara ya 37 kifungu cha 5, tayari Samia Suluhu Hassan ameshakula kiapo na sasa ni rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mantiki hapa ni kuwa mikoba yote ya kifalsafa, ndoto na baadhi ya mipango aliyokuwa nayo JPM ina baki mikononi mwa rais Samia Suluhu Hassana, Ni matumaini ya makala haya kuwa rais Samia atasimamia kwa weledi na ufanisi kama walivyokuwa na fikra za pamoja kabla ya mwendazake hayati Magufuli kutangulia mbele ya haki.

Kama Taifa la Tanzania na Afrika kwa ujumla lazima tukubaliane na ukweli ulio wazi kuwa, tumepoteza kiongozi mwenye maono ya pekee na mtu aliyekusudia kwa dhati kabisa kuivusha nchi katika janga la utumwa na utegemezi wa kiuchumi kutoka mataifa ya nje na kuifanya Tanzania kuwa jabali la uchumi wa Afrika unaotegemea rasilimali za ndani kuendesha na kupanua wigo wa kipato cha mtu na taifa kwa ujumla wake.

Tutamkumbuka Mwendazake hayati Dkt. Magufuli kwa falsafa zake zenye misimamo ya uwajibikaji kwa kile anachokiamini hasa falsafa zile zilizojipambanua kuwatumikia wanyonge na maskini wa chini kabisa, nadharia ya wanyonge kwake ilikuwa kama wimbo husio isha kuimbwa kinywani mwake kila tukio aliloshiriki hakusita kurejea kwenye utumishi wa wanyonge, ni Kiongozi aliyefanikiwa kutimiza mawazo yake kifalsafa na hatimaye akakubalika kwa wanyonge walio wengi katika nchi yetu.

Hata hivyo falsafa za utumishi wa wanyonge na kubana mifumo ya rushwa na ufisadi wa mali za umma kwa namna moja au nyingine ilizalisha uadui hasi kati ya hayati Dkt. Magufuli na baadhi ya Watanzania na mataifa mengine ya nje, Dhana ya chuki na visasi kisiasa ni jambo la kawaida ambalo kiongozi yeyote yule hawezi kukwepa kikombe hicho cha lawama, Kiongozi mwenye misimamo ya kulinda maslahi ya walio wengi kamwe hawezi kukosa maadui wa ksiasa na kiuchumi vinginevyo kiongozi huyo awe ni malaika aliyeshuka kutoka mbinguni.

Mwendazake hayati Dkt. Magufuli hakuwa Malaika bali binadamu aliyejitoa kuitumikia nchi yake kwa uwezo na moyo wake wote, tutamkumbuka daima kwa sera zake zenye nadharia na mantiki ya ukombozi wa Mtanzania wa kawaida na bara zima la Afrika na watu wake, Tunayo imani pana kwa rais wetu Samia Suluhu Hassan kuwa hatafanya makubwa pengine zaidi ya mtangulizi wake kulingana na uwezo wake wa kiungozi ndani ya medani za siasa, aidha imani yetu kwa rais Samia inatokana na falsafa za mwendazake hayati Magufuli kuwa fumbo linaloishi ndani ya fikra na mawazo ya rais wetu Samia Suluhu Hassan.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

dmutungid@yahoo.com

0717718619
 
Mataga mmeshaanza kutumia kila aina ya mbinu ili mumvuruge na huyu! Mmeanza kumpamba ili mumgeuze na yeye kuwa dikteta uchwara! Mpo kama mashetani vile!

Nyinyi ni watu wa hovyo sana.
 
Back
Top Bottom