Kilichotokea jana Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam: Profesa Mkumbo na Profesa Mkandala watuhumiana u-Nkurunzinza
-
Profesa Kitila Mkumbo ni Mwenyekiti wa UDASA, Chuo Kikuu cha DSM. Kwa sasa yupo likizo ya ndani ya kunoa ubongo maarufu kwa kimombo kama Local Sabbatical Leave. Katika likizo hii wanataaluma huomba muda wa kuweza kuandika vitabu na machapisho mengine ya kitaaluma. Akiwa katika likizo hii ameendelea na nafasi yake ya uenyekiti wa UDASA na kazi zingine za kitaaluma Chuo Kikuu ikiwemo kusimamia wanafunzi wa shahada ya uzamivu.
-
Akiwa Mwenyekiti wa UDASA yeye ndiye huhudhuria vikao vya Baraza la Chuo akiwakilisha wanataaluma. Hata hivyo, tarehe 23 Aprili 2015 uongozi wa Chuo Kikuu kupitia kwa mwanasheria wa chuo hicho Profesa Palamagamba Kabudi walimwandikia barua Katibu wa UDASA wakimtaka wawasilishe jina la mwanachama mwingine wa UDASA atakaykuwa anahudhuria vikao vya Baraza kwa kuwa Profesa Mkumbo alikuwa likizo ya kunoa ubongo. Hata hivyo baada ya majadiliano ndani ya kikao cha Kamati Tendaji ya UDASA ilikubaliwa kwamba hakuna sheria yeyote ya chuo inayomzuia Prof. Mkumbo kuendelea na uwakilishi wake katika Baraza la Chuo kwa kuwa tu yupo sabbatical leave. Hata hivyo, ilikubaliwa kwamba jambo hili liwasilishwe kwa Mkutano Mkuu wa UDASA kwa majadiliano na maamuzi zaidi.
-
Kikao cha Mkutano Mkuu wa UDASA kilipangwa jana tarehe 22 Mei 2015. Wanataaluma wengi walihudhuria. Kama kawaida Profesa Mkumbo alikuwepo na alipanda jukwaani kuendesha kikao. Mara baada ya ajenda kuthibitishwa na kuanza kujadili ajenda ya Kumbukumbu za kikao kilichopita, alisimama Prof. Luoga ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo kwa upande wa taaluma. Prof. Luoga alitoa hoja ya dharura iitwaye kwa kimombo point of order. Hoja ya Prof. Luoga ikawa kwamba Mwenyekiti hana uhalali wa kuendesha kikao kwa kuwa yupo likizo akamtaka aache kwanza kuendesha kikao hadi hiyo hoja ijadiliwe. Prof. Mkandara akiwa mkali kama mbogo naye alipigilia mstari akisema kwamba Prof. Mkumbo analeta virusi vya Nkurunziza kwa kutaka kuendelea na madaraka wakati yupo likizo.
-
Baada ya maelezo hayo, Prof. Mkumbo akamwita Makamu Mwenyekiti wa UDASA apande juu ili aendeshe kikao ili hoja ipate kujadiliwa. Prof. Luoga akarudia hoja yake na mjadala ukaendelea. Baada ya utawala kumaliza kutoa maelezo yao, alisimama Prof. Majamba, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Tendaji na Dean wa School of Law. Katika maelezo yake, Prof. Majamba akaeleza kwamba uamuzi wa jambo hili lazima ufuate katiba ya UDASA. Akasoma katiba ya UDASA na kueleza kuwa sifa pekee ya kuendelea kuwa Mwenyekiti wa UDASA ni kuwa mwanachama wa UDASA, na unakuwa mwanachama wa UDASA kwa kuwa mwanataaluma wa Chuo Kikuu cha DSM. Akaeleza pia kwamba ukiwa sabbatical leave huachi kuwa mwajiriwa na ndiyo maana unaendelea kulipwa mshahara wako wote. Hivyo, Prof. Mkumbo ni mwajiriwa na mwanachama halali wa UDASA na hakuna kinachomzuia kuendelea na nafasi yake. Baada ya hapo wajumbe wengi waliofuata waliunga mkono hoja ya Prof. Majamba. Hata hivyo uongozi wa chuo ukasisitiza hata kama hakuna sheria inayomzuia busara lazima itumike.
-
Hatimaye akapewa nafasi Prof. Mkumbo. Katika maelezo yake akaweka wazi kwamba yeye ameendelea kufanya kazi za UDASA kama kawaida na wenzake katika Kamati Tendaji hawajawahi kumlalamikia. Akaeleza pia kwamba akiwa katika likizo yake ameendelea kufanya kazi za taaluma, ikiwemo kusimamia wanafunzi wa shahada ya uzamivu. Kilichowaumiza zaidi wajumbe ni pale Prof. Mkumbo alipoweka wazi kwamba ni hivi majuzi tu uongozi wa chuo umemteua kuwa Mtahini wa Kujitegemea wa Ndani (Independent Internal Examiner). Akahoji, kama kweli siruhusiwi kufanya kazi za chuo ilikuwaje uongozi wa chuo ukamteua kufanya kazi hiyo?
-
Kuhusu uNkurunziza, Prof. Mkumbo akamrushia dongo Prof. Mkandala kwamba yeye hasa ndiye anayestahili kuitwa Nkurunziza kwa kuwa anaendelea kuwa Makamu Mkuu wa Chuo huku akiwa ameshastaafu na anajua kabisa sheria za chuo haziruhusu mtu ambaye amestaafu kuendelea kutumikia katika nafasi ya uongozi.
-
Baada ya maelezo ya Prof. Mkumbo, Mwenyekiti wa Kikao Dk Vincent Anney akwahoji wajumbe wanaotaka Prof. Mkumbo aendelee kuwa mwenyekiti na wale wasiotaka. Ukumbi mzima isipokuwa uongozi wa chuo ukanyoosha mikono juu ukitaka Prof. Mkumbo aendelee na arudi mezani kuendesha kikao.
-
Hata hivyo Prof. Mkumbo alipoitwa kuchukua nafasi yake akasimama na kueleza kuwa kwa mazingira aliyoyaona kati yake na menejimenti haoni kama ni busara yeye kuendelea kuendesha kikao. Na zaidi akaomba kwamba aruhusiwe kuandika barua ya kujiuzulu. -Kwa hiyo Dk Anney akaendelea kuendesha kikao.
-
Hata hivyo wajumbe wengi hawakubaliana na wazo la Prof. Mkumbo la kujiuzulu na kuna uwezekano mkubwa barua yake ya kujiuzulu ikakataliwa katika Mkutano Mkuu wa UDASA. Kwa mujibu wa Katiba ya UDASA ataendelea kuwa Mwenyekiti hadi pale uamuzi wa barua yake utapokuwa umetolewa.
-
Mwana UDASA aliyekuwepo kikaoni jana.