Lycaon pictus
JF-Expert Member
- Jan 31, 2021
- 7,204
- 12,698
kitabu hiki kiliandikwa mwaka 1907 na JH Patterson kikiitwa The man-eaters of Tsavo. kilitafsiriwa kwa kiswahili miaka ya 1960's kikiitwa Simba wa Tsavo. Unaweza kukisoma bure ndani ya Maktaba app(by pictuss), app hiyo ipo playstore.
SURA YA I
KUFIKA KWANGU TSAVO
SIKU HIYO, ikapata adhuhuri, nikaona tunaingia Mombasa, bandari moja nyembamba yenye taabu na hatari kabisa kuiingia katika pwani ya Afrika ya mashariki. Tuliingia Mombasa tarehe 1, mwezi wa Machi, mwaka 1898.
Tuliikuta bandari imetapakaa majahazi ya Waarabu. Moyoni mwangu nalikuwa na mashaka sana, nikifikiri jinsi manahodha wa vyombo vidogo kama hivi walivyoweza kusafiri toka bandari hata bandari kama walivyokwisha zoea wenyewe bila msaada wa dira na jinsi wanavyomudu kuvuka salama katika dhoruba za mawimbi zifikazo hata bahari za mashariki katika majira fulani ya mwaka.
Merikebu yetu ilipokuwa ikienda kutia nanga, nilikumbuka moyoni visa vingi vya matendo yaliyotendwa na maharamia na wauzaji wa watumwa, ambavyo, nilipokuwa mtoto nalipendelea mno kuvisoma. Ndipo mahali papa hapa yule msafiri mkuu Vasco da Gama alipofika katika mwaka 1498. Katika njia kuu, Mombasa-ambavyo ingekuwa haki yake kuitwa barabara ya vasco da Gama-mpaka leo hivi upo mnara wa ajabu usemwao kuwa ulijengwa na baharia huyu ili uwe ukumbusho wa kufika kwake Mombasa.
Kusudi langu lililonileta huku Afrika ya Mashariki ni kushika kazi ya kuendeleza kuchimba reli inayokwenda Uganda. Kwa hiyo nilimwuliza mmoja wa mabwana Forodha anionyeshe mahali ilipokuwa afisi kuu ya reli, nami nikaambiwa kuwa afisi hiyo iko mahali kunakoitwa Kilindini, kiasi cha mwendo wa maili tatu ng’ambo ya pili ya kisiwa. Nilivyokuwa na bahati njema, nikapata troli moja inayosukumwa na waswahili wawili. Haya, nikapitishwa mbio njiani, ambayo huko nje ya mji ilipita katika sehemu kubwa iliyoshikamana miembe, mibuyu, migomba, na minazi iliyofungamana na mitambaazi yenye maua mengi ya kupendeza katika matawi yake.
Nilipokuwa nimefika Kilindini nikashika njia kwenda kwenye Afisi za reli, huko nikaambiwa kuwa maskani yangu yatakuwa bara na ya kuwa nisubiri kupata maagizo mengine zaidi baada ya siku au mbili hivi. Palikuwa na minazi mikinda mingi iliyofanya vivuli; nikapiga hema langu karibu na reli ya gari, ikawa tena nikijishughulisha kutembeatembea mjini nikinunuanunua vifaa na mahitaji yatakayonifaa huko bara nitakakokaa kwa muda mrefu.
Nalikaa mombasa kiasi cha juma zima hata tena nikaingiwa na wasiwasi wa safari yangu. Siku mojaasubuhi nikapata barua; kuisoma, nikaona ni ya kuniamuru kuondoka kwenda Tsavo, kiasi cha mwendo wa maili mia moja na thelathini na mbili hivi toka Mombasa mjini, nikashike kazi ya kuchimba reli ambayo ndiyo kwanza wakati huo iishilie hapo. Asubuhi yake mchana tukaondoka; baada ya mimi, bwana Anderson, msimamizi wa kazi, na daktari, McCullock, bwana mganga mkuu, katika gari letu maalum tulilofungiwa.
Baada mwendo wa maili ishirini, gari letu likaelekea moja kwa moja upande wa juu, tukipita ndani ya vichaka vizuri vilivyoshikamana. Kila mara tulipochungulia madirishani kutazama nyuma tunakotoka, tuliweza kuona upeo wa Mombasa na Kilindini pamoja na bahari yake ikimeremeta kwa jua kwa mbali kiasi cha upeo wa jicho. Kiasi cha kupita vilima vya Rabai tukaingia katika mbuga ya jangwa la taru, nyika yenye vichaka duni kabisa na miti mifupi mifupi ambayo wakati wa kiangazi ni kama vumbi jekundu tupu. Gari wakati wa kupita katika nyika hii vumbi hilo lilipenya ndani likatapakaa kila mahali. Katika sehemu hii wanyama hawakuonekana kwa sababu ya vichaka vingi. Ingawaje, walakini, tuliweza kuwaona wachache wao madirishani, pia tukawaona Wanyika, wenyeji wa nchi hiyo.
Mwisho wa mbuga hii yenye vumbi jekundu ni Maungu, kiasi cha mwendo wa maili themanini tokea Mombasa mjini, kwani kutoka hapo vumbi lake ni la rangi nyingine. Tokea hapo hatukuvuta hatua mara tukaingia Voi, kiasi cha mwendo wa maili mia moja kutoka Mombasa mjini, kwa kuwa hapa ni kituo kikuu ambacho tulikuwa hatujapata kufika, tukatua kidogo ili kutazama jinsi kazi ilivyokuwa ikiendelea. Katika kuendelea na safari yetu, huko mbele tuliona kuwa hali ya nchi imebadilika na ni ya kupendeza. Tokea mji uitwao Ndii, kwa mwendo mrefu reli imepita katikati ya mbuga yenye vichaka vingi vilivyopendeza mno kuliko nyika tuliyokwisha ipita. Kushotoni kwetu tuliweza kuona safu ya milima ya Ndii, nchi ya Wataita, na kwa upande wa kulia kulikingamiwa na genge la Ndungu lililozunguka kwa mbali upande wa magharibi. Hapa mwendo wetu ukawa wa taratibu kwa kuwa kila mara ilitubidi kusimama kutazama maendeleo ya kazi za kila siku zinazofanywa; vivyo hivyo kidogo kidogo hatimaye tukafika Tsavo mwisho wa safari yetu. Usiku ule nililala katika kibanda cha makuti kilichokuwa kimejengwa na wasafiri wenzangu waliotangulia. Kibanda chenyewe kilikuwa karibu kuanguka na hasa kilichakaa mno, mwisho hata mlango hakina; usiku nilipokuwa nimejinyoosha penye kirago changu naliweza kuona nyota zikiangaza kwa nje juu ya paa. Sikujua hatari gani zilizokuwa jirani nami, kama ningalijua kwamba wakati ule ule walikuwapo wanyama wawili habithi wakizungukazunguka kutafuta watakachoweza kupata wajilie, sidhani kama ningalipata usingizi katika kibanda kibovu kama hicho.
Asubuhi yake naliamka na mapema kabisa. Nilipanda juu ya kilima kidogo kilichokuwa karibu yangu, nikaona kuwa nchi yote, kwa kadiri ya upeo wa macho yangu, ni miti mitupu mifupi mifupi iliyoshikamana na miiba ya ‘subiri kidogo.’ Mahali palikuwa peupe ni sehemu ile iliyochimbwa reli tu. Mbali kwa upande wa kusini naliweza kuona pepesi za kilele chenye theluji cha mlima Kilimanjaro. Karibu ni mto Tsavo. Mto huu huenda kwa kasi kabisa nao haukauki; maji yake sikuzote yanazizima, na kwa pande hizi za Afrika ya Mashariki, mito iendayo hivi ni michache.
Nilirudi kibandani kwangu, nikatumia juhudi yangu yote kujitengenezea maskani yangu. Vitu vikafunguliwa na watumishi wangu wakanipigia hema langu mahali peupe kidogo karibu na pale kibandani nilipolala jana na si mbali na kambi ya wafanyaji kazi. Wakati huu reli ilikuwa imefika upande wa magharibi ya mto na kambi ya makuli wa Kihindi na vibarua wengine ilikuwa huko huko.