AGANO LA AJABU
ANTONIO na Bassanio walikwenda pamoja kwa Shylock. Antonio akamwomba yule Myahudi amkopeshe shilingi ishirini na saba elfu. Naye aliahidi kulipa faida iwayo yote atakayotaka Shylock. Shylock aliposikia hivi, aliwaza nafsini mwake, “Mara nikimpata Antonio katika uwezo wangu nitamtesa kwa ajili ya madhara yote aliyonitenda. Anatuchukia sana sisi Wayahudi; anakopesha fedha nyingi wala hataki faida; na huko katika Rialto hunisibabi na biashara yangu.' Lakini Shylock hakujibu kwa haraka, hata Antonio alikosa subira kwa sababu ya kutaka fedha, akasema: Shylock, unasikia? Utanikopesha fedha ?"
Kwa hoja hii yule Myahudi alijibu hivi: "Bwana Antonio, wewe kule Rialto mara nyingi umenisuta kwa sababu ya namna ninavyokopesha fedha, nami nimestahimili maneno yako kwa subira. Tena, umeniita mimi kafiri, hata pengine umenipiga mateke kwa mguu wako kama kwamba mimi ni mbwa. Vema, imetukia sasa ya kwamba unahitaji msaada wangu. Umekuja kwangu na kusema, Shylock nikopeshe fedha.' Je, Mbwa ana fedha? Yawezekana mbwa akukopeshe wewe shilingi elfu ishirini na saba? Naweza kujinyenyekea na kusema, Bwana adili; Jumatano iliyopita ulinicheka; wakati mwingine uliniita mbwa; na malipo kwa ajili ya haya uliyonitenda, ndiyo mimi nikukopeshe fedha "!"
Kwa maneno haya Antonio alijibu hivi, “Napenda kukuita mbwa tena, na kukusibabi kati ya wafanyi biashara wa Rialto, hata napenda kugeuza uso wangu ninaposema na wewe. Ikiwa utanikopesha hiyo fedha, nikopeshe, wala si kama rafiki, lakini kama adui. Kwa hivi kama nikihalifu miadi, utaweza kuchagiza malipo kamili pasipo haya."
Shylock akasema, "Angalia jinsi ulivyohamaki. Mimi nataka tuwe marafiki, tusuhubiane. Mimi tayari kusahau maovu uliyonitenda. Nitakidhi matakwa yako, wala sitatoza faida kwa ajili ya fedha yangu."
Ahadi hii njema ya kinjenje ilimshangaza Antonio vikubwa mno. Ndipo Shylock, kama kwamba akitaka kuzidi kwa wema kulinasa pendo la Antonio, alisema tena ya kwamba atamkopesha shilingi elfu ishirini na saba, wala hatatoza faida kwa fedha yake. Ila alifanya sharti moja tu- ndiyo kwamba Antonio na yeye waende kwa mwana sheria, na huko wakaandike sahihi zao kwa kicheko na furaha agano ya kuwa Antonio asipolipa fedha kwa siku watakazowekeana miadi, itamlazimu kulipa ratli ya nyama, ikatwe katika sehemu yo yote ya mwili wake atakaporidhia Shylock.
Antonio akasema, Nakubali, nitaandika sahihi yangu kwa sharti hii, na kusema ya kuwa Myahudi ana uhisani mwingi."
Bassanio hakutaka Antonio aitilie sahihi sharti kama hii kwa ajili yake; lakini Antonio alizidi kusisitiza ya kwamba ataiandika sahihi, kwa sababu alikuwa na hakika kwamba merikebu zake zitarejea kabla ya siku ya malipo, zitamwasilishia mali nyingi zaidi kushinda thamani ya ile fedha.
Shylock aliposikia mabishano yao, alisema, "Ohoo, angalia jinsi hawa Wakristo wasivyokuwa na muamana! Mambo magumu yao wenyewe yafunza kutowaamini wengine. Tafadhali Bassanio, ebu niambie neno moja: Kama Antonio atahalifu agano lake kwa kukosa kunilipa katika au kabla ya siku tuliyowekeana miadi, nitapata faida gani kwa kuchagiza maneno ya agano letu ? Ratli ya nyama ya mwanadamu kutwaliwa katika mwili wa mtu, haina thamani wala faida kama nyama ya kondoo au ya ng'ombe.
Mimi nasema hivi ili nipate upendeleo wake, nami namtolea mapenzi yangu, akiyakubali, nitafurahi, la sivyo, basi kwa herini."
Hata mwisho, kinyume cha shauri la Bassanio, ambaye hakuyaamini maneno ya yule Myahudi, na kwa sababu hiyo hakuridhia rafiki yake ajitie hatarini kwa ajili yake, Antonio aliiandikia sahihi yake ile sharti. Kwa habari ya ratli ya nyama, yeye alidhani sharti imetiwa katika agano (kama alivyosema yule Myahudi) kwa mzaha tu.