Lycaon pictus
JF-Expert Member
- Jan 31, 2021
- 7,224
- 12,729
SURA YA 1
KWA mara nne mfululizo katika wiki ile, Luteni Maige alijiwa na ndoto ile ile usingizini. Aliamka kwa mshtuko, jasho likimtoka huku akihema kwa kasi.Safari hii, hata alipofumbua macho, alikuwa na hakika kabisa kuwa risasi mbili alizofyatua zilimpata kiongozi wa nchi kichwani na hapana daktari yeyote ambaye angeweza kuzuia mauti yake. Na hata risasi hizo zisingeweza kumuua, alikuwa na hakika mwanguko wa gari lake baada ya dereva kurukwa na akili kutokana na shambulizi hilo na kulibamiza gali hilo kwenye nguzo ya taa, ungemmaliza kabisa.
Maige alifumbua macho akatikisa kichwa kwa nguvu. Alipoyafumbua, akayainua taratibu akayatuliza kwenye saa kubwa ya ukutani. Zilibaki kama dakika saba kutimia saa nane kamili.
Usingizi mzito aliokuwa nao usiku ule, baada ya kunywa pombe kali, ulimruka kabisa. Angependelea sana arudi kulala lakini maumivu ya kichwa na mchanganyiko wa mawazo mazito aliyokuwa nayo, ndivyo vilivyomfanya atoke kitandani.
“Vipi?” sauti ya mkewe, Veronika, ilimpa mshtuo mwingine.
Kwa muda wote tangu Maige alipoamka, Vero alifumbua macho akamtazama. Alimwona akitokwa jasho huku akihema kwa nguvu. Alimwona alivyoduwaa kama aliyeota ndoto ya kutisha. Alimwona pia alipofumba macho na kutikisa kichwa kwa nguvu kisha akaitazama saa ya ukutani.
Maige aligeuza macho akamtazama. “Kumbe uko macho? Unasemaje?” Alijaribu kuituliza sauti yake. Hakupenda Vero ajue lililomo moyoni mwake.
“Nimeshtuka ulipoamka,” Vero alisema kwa sauti ndogo ya uchovu. “Naona jasho linakutoka. Vipi, unajisikia vibaya?”
Maige alivuta pumzi ndefu akazishusha. “Hata, najisikia kiu imebana sana. Nipe maji baridi?”
“Kiu tu ndio ikutoe jasho namna hiyo?”
Hakujibu. Aliiendea friji, akatoa chupa ya maji baridi akajimiminia kwenye glasi na kuibugia.
Maige alikuwa na umri wa miaka thelathini na minane. Alijiunga na jeshi miaka kumi iliyopita.
Tangu utotoni, maisha ya Maige hayakuwa ya kuridhisha. Pamoja na jitihada zote walizofanya wazazi wake kumpatia elimu, hakwenda mbali zaidi ya kidato cha kwanza.
Alipofikia umri wa miaka kumi na mitano, rafiki zake walianza kumshuku kuwa Maige alikuwa na hitilafu fulani akilini. Si kwamba alidhihirisha uendawazimu kamili, lah!. Ila tabia yake ya kufurahia sana madhara yoyote ayafanyayo kwa wenzake bila ya kujali maumivu au msiba atakaosababisha ndicho kilichowatia hofu.
Kwa Maige mwenyewe hiyo haikumaanisha athari yoyote ya akili. Ilikuwa ni shauku kubwa iliyokuwa ikimjia mara kwa mara ya kufanya jambo litakalodhihirisha ujasiri wake.
Alipofikia utu uzima akaingia jeshini. Akilini mwake aliamini kuwa jeshini ndipo mahali pekee ambapo angeweza kuua au kufanya madhara yoyote bila ya kufikishwa mahakamani. Angeweza kuua bila ya kuitwa na kuhojiwa, angweza kuvunja mkono, miguu, au hata shingo ya mtu bila ya kusumbuliwa, na mengine mengi.
Alikua akiomba Mungu usiku na mchana izuke vita ili aue au atese watu kwa kuwavunja viwiliwili vyao.
Haikupita hata miaka mitano ombi lake lilikubaliwa. Iddi Amin alizusha zogo lisilomithilika kwa watanzania na watanzania wakalazimika kukata kilimilimi cha nduli huyo na kunyamazisha zogo alilolianzisha.
Zikapigwa!
Katika mapigano hayo, Maige, siku hizo akiwa askari mpiganaji wa ngazi ya chini, alionyesha miujiza. Alipigana bila woga huku akiishangilia kwa sauti kubwa kila risasi yake iliyoangusha adui. Vita ilivyopamba moto na adui alivyozidi kujiimarisha, mkuu wa kikosi chake alimpandisha cheo. Ujasiri wake uliendelea kumpandisha ngazi
hadi ngazi, hatimaye, mwaka 1984 akawa Luteni.
Lakini pamoja na mafanikio hayo aliyoyapata kwa muda mfupi jeshini, Maige hakuridhika. Vita ilipomalizika na jeshi la Tanzania kurudi nyumbani na ushindi mkubwa, Maige alikuwa askari wa pekee aliyelaani kumalizika kwa vita hiyo. Angepata wapi nafasi ya kuua ili aridhishe nafsi yake?
Pamoja na kujiwa mara kwa mara na shauku hiyo, lakini alitambua ya kwamba asingeweza kuchukua bastola au bunduki kubwa na kuanza kuua watu hovyo barabarani. Angethubutu kufanya hivyo angekamatwa na kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kuua kwa kukusudia. Pengine angehukumiwa kifo.
Alipomaliza miezi sita huku shauku yake ya kuua ikizidi kukua, Maige alikata shauri. Aliamua kufanya shambulizi moja litakalompa nafasi ya kufanya mauaji ya kutisha yatakayokumbukwa milele. Halafu basi.
Lakini lazima yawe mauaji yatakayomtambulisha yeye kama jasiri wa kweli. Lazima yawe mauji yatakayosimuliwa usiku kucha majumbani mwa watu na mchana kutwa kusomwa magazetini na kusikilizwa redioni. Ndiyo, lazima yawe mauaji ya namna hiyo.
Watu wakubwa watatu walimjia haraka mawazoni. Aliwafikiria watu hao huku akijaribu kuunda picha tofauti za hekaheka zitakazotokea kwa kila kifo cha mmoja wao.
Akaamua wawili kati yao wasingeleta msiba mkubwa alioutarajia, wala vifo vyao visingejaza hata nusu ndoo ya machozi ya watakaowalilia endapo machozi hayo yangekusanywa pamoja. Aliwaondosha mawazoni mwake, akambakiza mmoja. Kiongozi mkuu wa nchi. Na hata kusaidia uasi na kufanya mapinduzi.
Mtu wa kwanza nje ya jeshi aliyemweleza habari hizo alikuwa bepari mmoja, mfanyabiashara maarufu, Mohsin Hilal.
“Mwendawazimu!” Ndivyo Mohsin alivyomwita Maige baada ya kumsikiliza kwa muda mfupi. “Haiwezekani.”
“Haiwezekani?” Maige alitoa macho. “Kwanini isiwezekane?”
“Kama itawezekana ni baada ya kufanya mipango mikubwa na nchi za nje ili wasaidie. Na lazima ziwe nchi ambazo hazina uhusiano wowote na Tanzania. Na mpaka wakubali, ni zaidi ya mwaka au miaka miwili. Kwanza nchi ipi itakayokubali kujikita katika janga kama hilo? Ndio sababu nakuita mwendawazimu.”
Maige alianza kupandwa na hasira ambayo alijua isingemsaidia lolote. Kitu ambacho alitambua haraka ni, angehitaji fedha. Shughuli kubwa kama hiyo huthubutu kuifanya peke yako. Lazima utahitaji watu wa kukuunga mkono na kukusaidia.
Na kupewa msaada wa kuitoa roho ya Rais wa nchi yataka kishawishi kikubwa na kilichonona. Alijua kuwa kutokana na uhusiano uliyopo kati yake na Mohsin, Mohsin angeweza kumpa Maige kiasi chochote cha fedha ili atekeleze dhamira yake. Baada ya kumpa fedha hizo, isingemwia tatizo hata kidogo kupata msaada aliouhitaji.
“Sikiliza, Mohsin,” alianza upya. “Hili si jambo la mzaha. Wala hii si ndoto niliyoota jana usiku na leo na kusimulia. Tafadhali nisikilize vizuri.”
“Nakusikiliza sana. Endelea.”
Ndipo Maige alipomweleza mipango kamili anayotarajia kuifanya ili kukamilisha mauaji hayo, na jinsi ambavyo angeweza kupata msaada kutoka kwa askari kadhaa kama yeye (Mohsin) angemwazima kiasi cha pesa ambazo kwa ajili ya maandalizi na maangamizi; pesa ambazo Maige angezilipa maradufu baada ya mambo kukamilika. Mohsin alimsikiliza Maige kwa makini sana huku akijaribu kuyapima yote aliyomweleza. Aliamini kwamba maelezo yake hayakuwa na hitilafu yoyote na wala Maige hakuonyesha kubabaika wala kuwa na dalili yoyote ya hofu alipokuwa akieleza.
Si hivyo tu, bali pia ahadi ya kumkopesha hela kisha baadae kumrejeshea faida maradufu ilikuwa kishawishi kikubwa zaidi. Isitoshe, Mohsin alikuwa na hakika endapo Maige atafanikiwa lengo lake, kwa vyovyote patakuwa na faida kubwa sana kwake kibiashara na hata kicheo. Hakutaka kujidanganya kwamba baada ya mauaji ya mkuu huyo wa nchi pasingetokea machafuko yoyote.
Alijua fika pangetokea mvurugano mkubwa ambao pengine ungefuatiwa na mauaji zaidi ya wananchi wasio na hatia. Lakini hatimaye pangekuwako utulivu na amani. Ni katika kipindi hicho cha utulivu na amani ambacho Mohsin alikuwa akitegemea na ambacho alikuwa na matumaini nacho. Pengine kutokana na msaada atakaotoa, angeweza kufikiriwa kupewa wadhifa mkubwa serikalini, baada ya kuchaguliwa kiongozi mwingine wa nchi. Au pengine, japo asipate huo wadhifa, angekuwa na uhuru mkubwa wa kupanua ubepari wake wa kueneza biashara zake za magendo nchi za nje.
Lakini Mohsin hakutaka kumuonyesha Maige kwamba alishaanza kupata moto wa tamaa. Badala yake alimtazama kama aliyekuwa na wasiwasi naye.
“Sikiliza, Maige. Kiasi unachotaka cha pesa ni kikubwa sana kwa mtu kutoa kwa mpigo kwa shughuli ambayo haijawa na uhakika wa mafanikio. Si kwamba sina kiasi hicho au labda najaribu kukupiga chenga, lah!. Huo ndio ukweli wenyewe. Sijui unanielewa?”
“Nakuelewa sana,” Maige alijibu, akachukua pakiti ya sigara ya Mohsin iliyokuwa mezani, akatoa moja akawasha. “Tatizo ni kwamba ugumu na urahisi wa shughuli hii nauelewa mimi, Bwana Mohsin. Kimaelezo mtu anaweza kudhani kuwa hii ni ndoto, kama unavyodhani hivi sasa.
Na hiyo ni kwa sababu hili si jambo tulilolizoea huku kwetu. Lakini, Bwana Mohsin, napenda uelewe kuwa kutolizoea jambo fulani si sababu hata kidogo ya kumfanya mtu ashindwe kulifanya jambo hilo. Naelewa kuwa fedha ninayohitaji ni nyingi, tena nyingi sana. Hata hivyo niazime. Matunda yake yatakuburudisha. Yatakunufaisha”
“Sikatai kukuazima” Mohsin alisema, akainamisha kichwa kwa nukta mbili tatu hivi. Alipokiinua akauliza. “Ulikua ukizitaka lini?’’
“Mapema sana. Hata kesho.’’
“Umeshaongea na hao wenzako wakukusaidia?’’
“Nimeongea na kama watano hivi.’’ “Ulikua ukihitaji wangapi?’’
“Kumi wangetosha kabisa.’’
“Basi ongea na wote kwanza mkubaliane. Usiharakishe. Hili si jambo la kuchukua wiki moja tu likakamilika. Lipe muda wa kutosha ili pasiwe na makosa madogo madogo yanayoweza kuharibu mipango kisha ikawa balaa. Utakapoona kila kitu umekinyoosha vizuri, njoo siku yoyote uchukue fedha.’’
Kwa mwezi mzima na nusu uliofuata, Maige amekuwa akifanya makutano ya siri na askari wenzake na baadhi ya watu wenye vyeo vikubwa lakini waliojawa na tamaa. Kutokana na hao alioongea nao na jinsi walivyomuunga mkono, alikua na hakika pasingekuwa na kosa lolote. Na ndio maana usiku ule, kwa mara ya nne mfululizo katika wiki ile ile, Luteni Maige alijiwa na mdoto ile ile.
Alipokuwa akirudisha chupa ya maji ya baridi ndani ya friji baada ya kunywa glasi mbili, Maige alirudi kitandani. Vero alimtazama huku akiwa na mashaka kwamba mumewe hakuwa akiumwa.
Kwa kuepuka maswali ambayo Vero alishaonyesha dalili ya kuuliza, Maige alivuta shuka akajifunika gubigubi. Moyoni aliahidi kwamba asubuhi lazima aonane na Kapteni Shaibu ili waamue lini waanze kazi.
SURA INAYOFUATA