Nawaheshimu sana wazee, maana wazazi wangu wamepitia hatua hiyo, na mie najua nitapitia, Mungu akibariki. Hata hivyo ni ukweli usiofichika kwamba ule msemo "kuna watu wanazeeka vibaya" unakuwa kweli sana ninapochunguza kauli za Kingunge kuhusu uteuzi wa CCM wa mgombea uraisi.
Nimeshindwa kabisa kumwelewa mzee huyu, na ninachoweza kusema ni kwamba pengine Kingunge anazeeka vibaya.
Wengi tunajua Kingunge, licha ya kuwa kiongozi wa CCM, ni kiongozi wa "kitaifa", na katika hili amejijengea heshima kubwa kwa muda mrefu. Ninachoshindwa kuelewa ni kwa nini huyu mzee ameamua kuiweka heshima yake rehani kwa kuwa msemaji wa kambi ya Lowassa?
Mie nilitarajia Kingunge angekuwa muwakilishi na mshauri wa wagombea wote wa CCM, badala ya kujikita katika kambi moja tu ya Lowassa, ukizingatia historia yake Kingunge katika uongozi wa CCM na kitaifa. Hivi amewaza nini huyu mzee na kuamua kuwa sambamba na Lowassa?
Na mbaya zaidi, kwa namna moja au nyingine ameamua kuendeleza ule mkakati wa kuishinikiza na kuitishia nyau CCM ili kumteua Lowassa kama mgombea wao wa uraisi. Amefikia kudiriki kuonyesha kwamba CCM wasipomteua Lowassa basi CCM itafia awamu ya nne! Hivi Kingunge haelewi kwamba lolote analolisema sasa, ushauri au maonyo yeyote anayoyatoa hadi sasa kuhusu CCM watu wote wenye akili wanaona kabisa yanalenga kumsaidia mgombea wake aliyeamua kwa sababu anazozifahamu yeye, kupalilia njia ya kuelekea hiyo inayosemwa safari ya matumaini?
Lowassa amemuahidi nini Kingunge hadi mzee wa watu aamue kujishusha hadhi kisiasa kwa kiasi hiki?
Watu wote wenye akili wangeona labda Kingunge anaongea jambo la maana ikiwa angesema haya anayosema dhidi ya CCM bila kuwa amejiweka kambi ya mgombea mmojawapo wa CCM, Lowassa. Kinyume cha hapo ni kwamba Kingunge anadhani viongozi wa CCM wana upeo mdogo sana wa kufikiri na kutambua anachofanya, kwamba anatumiwa na Lowassa kuishinikiza CCM. Sidhani kama mbinu hii itamsaidia Lowassa au Kingunge mwenyewe.
Anachofanya Kingunge ni usaliti wa kiwango cha juu kwa CCM, na CCM inapaswa kutambua hilo. Kingunge anataka kuleta mgawanyiko mkubwa ndani ya CCM ili tu amnufaishe Lowassa. Ameamua kwamba liwe na liwalo, the end justifies the means. Kama JK bado hajamuita Kingunge na kumweka sawa bila kumuonea aibu, basi ningeshauri JK afanye hivyo haraka sana, kabla huyu mzee hajawaharibia CCM hata zaidi.
Ushauri wangu kwa Kingunge ni kwamba baada ya haya yote uliyofanya, makosa makubwa sana ya kisiasa, nenda kijijini ukakae kimya huko na kuwa mjamaa halisi, kama ambavyo siku zote ulijionyesha kwa Nyerere, kwamba wewe ni zaidi ya mjamaa.