ASKARI polisi watatu akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nguruka, Uvinza mkoani Kigoma, Ramadhan Mdimi, wameuawa kwa kupigwa na silaha mbalimbali za jadi ikiwamo mishale wakati wakitekeleza majukumu yao pembezoni mwa mpaka wa kijiji cha Mpeta .
Mauaji hayo yanatokana na mgogoro wa ardhi katika eneo la Ilunde na askari hao walifika kuwaondoa wananchi eneo hilo walioanzisha makazi na kufanya shughuli za kilimo na ufugaji bila kufuata sheria na taratibu za ardhi tangu mwaka 2004.
Gazeti hili lilifanya mahojiano na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpeta, Petro Kejo, kuhusu mgogoro huo na kukiri kwamba kazi ya kuwaondoa wananchi hao imetumia nguvu kubwa.
"Sababu kubwa ni eneo kubadilishwa matumizi kutoka ardhi ya kawaida ili iwe ranchi ya uwekezaji. Sasa raia wanahisi hawatendewi haki kwa nini igeuzwe ranchi wakati wanatozwa fedha za michango ya maendeleo ya jamii na wanapiga kura kuwachagua viongozi.
“Kama shida ni mwekezaji, wako tayari walipe gharama hizo lakini waachwe waendelee na shughuli zao za kilimo na ufugaji. Hakuna eneo lililotengwa kwa ajili ya wakulima na wafugaji," alisema.
Alisema wananchi wamechukizwa na kitendo cha askari polisi kuwapora mazao kama mahindi, mchele na kuku katika kaya zao huku wakichoma moto baadhi ya nyumba wakati wa operesheni ya kuwaondoa katika eneo hilo, iliyofanyika Alhamisi wiki hii.
Alisema hali hiyo ilisababisha hasira kwa wananchi ambao walijikusanya na kuwavamia askari hao na kusababisha mauaji ya watu watano.
"Wananchi waliopigwa risasi na kufa ninaowajua ni wawili na majeruhi watano. Maiti moja iko katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Maweni na aliyeuawa Salu Deusi (21). Polisi hawasemi ukweli kwa ndugu wa marehemu kama maiti iko hospitalini, wanadai hawajui. Hii inawaumiza raia kwa uongo wakati wanaishi hapo kwa zaidi ya miaka 15," alisema.
Alisema juzi ndipo waliokota maiti ya Mkuu wa Kituo cha Polisi, Ramadhan Mdimi, huku miili ya askari wenzake wawili ikiwa bado inatafutwa na vyombo vya dola.
"Operesheni hii imeathiri utulivu wa wananchi na mali zao na tunaishauri serikali ya wilaya ifanye mazungumzo na wananchi kwa kushirikiana na serikali ya kijiji na iwe imetenga maeneo rafiki ya wafugaji na wakulima kutoka mikoa ya karibu hasa wafugaji na wakulima kutoka Shinyanga," alisema Kejo.
Nipashe ilizungumza na Diwani wa Mganza, Evodius Kapukutu, kuhusu mgogoro huo na kukiri kuwa, aliyekuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nguruka na mwenzake wawili, walipoteza maisha wakati wakitekeleza majukumu yao .
"Hawa wafugaji wametoka Shinyanga na wameingia kinyemela na kila wanapoelezwa kufuata sheria za ardhi na taratibu, hawaelewi. Wao wanajua ardhi ni ya wote, mbaya zaidi hufanya mikutano yao ya siri baada ya kikao cha wazi na serikali," alisema.
Chanzo gazeti la nipashe