Jengo la Victoria House lililopo pembeni ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini, Dar es Salaam linalomilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa alisema jana kuwa kigogo mmoja wa shirika hilo anajinufaisha nalo.
NHC lawamani kwa rushwa
KATIBU Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa, amesema kati ya mashirika mabovu nchini, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linaongoza na hakuna asiyejua kuwa kila anayetaka nyumba lazima atoe rushwa.
Amesema NHC inatakiwa kujua ipo kwa ajili ya kuhudumia umma na si kujinufaisha na lazima ijirekebishe kiutendaji na kukabiliana na changamoto na kufahamu zilipo mali zake.
Rutabanzibwa alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akifungua kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NHC na kuwapongeza wafanyakazi wa shirika hilo kwa kuvumilia licha ya matatizo yanayowakabili.
"Hili ni shirika, ni kubwa sana katika Afrika Mashariki, kiutendaji mjirekebishe ili mkabiliane na changamoto zinazowakabili, mjue mali zenu ziko wapi na zikoje," aliwambia Rutabanzibwa.
Aliitaka NHC iangalie mikataba iliyonayo na sifa mbaya iliyoko katika shirika hilo iondoke, kwa kuwa hakuna asiyejua kuwa rushwa imepewa kipaumbele ili kupata nyumba ya shirika hilo.
"Lazima sifa hiyo ifutwe kwa vitendo, kuwe na taratibu za wazi za kuweka wapangaji … matumizi mabaya ya vyeo yachukuliwe hatua, kwani wanatumia nyumba za shirika kuweka wafanyabiashara wao kwa mfano Victoria House," alisema Rutabanzibwa.
Katika mfano huo wa Victoria House, alisema viongozi wa shirika hilo wamepangisha wafanyabiashara wao kwa manufaa yao na si ya shirika.
Alisema ni vyema shirika likafahamu kuwa mali hiyo si ya viongozi, bali ni ya umma na isitumike kujinufaisha binafsi, ilindwe kwa niaba ya wote.
Awali akizungumza, Mkurugenzi wa NHC, Nehemiah Mchechu, alisema sasa Shirika linapitia mikataba 76 ya biashara na watachukua uamuzi mgumu ikiwa ni pamoja na kunyang'anywa baadhi ya miradi kwa kuwa shirika liko katika hali ngumu.
Alisema kwa waliovunja mikataba na NHC watanyang'anywa nyumba ili viwanja hivyo viboreshwe zaidi na kulipatia shirika mapato na si hasara.
"Hakuna anayetaka kunyang'anywa kiwanja chake, waliovunja mkataba, yaani alikubali kujenga kwa miaka mitatu, lakini bado hajafanya chochote atanyang'anywa eneo hilo," alisema Mchechu.
Aliongeza kama wapo wenye viwanja na havijaendelezwa kwa miaka minane NHC lazima ichukue eneo hilo na utekelezaji huo utaanza kwa wenye miradi mikubwa.
"Hakuna asiyejua kuwa nyumba za NHC zina kodi ndogo, jambo ambalo linatukwamisha hata kujiendeleza na kulisababishia shirika hasara, kwa mfano kuna nyumba Singida ambapo gharama za ukarabati ni Sh milioni 33 lakini kodi ni Sh 45,000," alisema Mchechu.
NHC ilianzishwa mwaka 1962 kwa lengo la kujenga nyumba za makazi na biashara kwa ajili ya wananchi.
Chanzo: Habari Leo