Kigoda aivunja bodi ya TBS


BabuK

BabuK

JF-Expert Member
Joined
Jul 30, 2008
Messages
1,847
Points
1,225
BabuK

BabuK

JF-Expert Member
Joined Jul 30, 2008
1,847 1,225
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, ameendeleza kasi yake ya kulisafisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambapo sasa ameivunja rasmi bodi ya shirika hilo kuanzia Novemba 21, mwaka huu.
Itakumbukwa kuwa hiyo ni mara ya pili kwa Kigoda kufanya mageuzi ndani ya shirika hilo kwani Mei, mwaka huu, aliiagiza bodi ya TBS kumsimamisha kazi Mkurugenzi wake Mkuu, Charles Ekelege.
Mkurugenzi huyo alisimamishwa kazi ili kupisha taratibu za kisheria ikiwamo suala la uchunguzi dhidi yake kufanyika.
Taarifa ya wizara iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi jioni ilieleza kuwa sababu ya uamuzi huu wa kuivunja bodi hiyo ni kutekeleza nia ya wizara ya kuboresha utendaji wenye tija na ufanisi katika shirika hilo lenye dhamana kubwa ya kusimamia viwango vya ubora wa bidhaa nchini.
Baadhi ya wajumbe waliokuwa wakiunda bodi hiyo iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Oliver Mhaniki, ni pamoja na Odilo Majengo kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Peter Machunde kutoka Mfuko wa Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Donald Chiidowu, Dk. Bertha Maegga na Suzy Laiser.
Taarifa hiyo ya wizara iliongeza kuwa utaratibu wa kuunda bodi mpya unafuata baadaye.
Mara baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hiyo, Dk. Kigoda amekuwa akichukua hatua za haraka kuisafisha TBS kutokana na kulalamikiwa na wabunge wakidai inanuka rushwa.
Katika mkutano wake na waandishi Mei 19 mwaka huu, Dk. Kigoda alisema kuwa moja ya sababu iliyomfanya Rais Jakaya Kikwete afanye mabadiliko ya uongozi katika wizara hiyo ni shirika la TBS.
“Kulikuwa na mjadala mkubwa bungeni kuhusu utendaji wake. Nimeitaka bodi ya shirika hilo kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo mara moja ili kupisha utaratibu mwingine wa kisheria kuanza,” alisema.
Wakati akitangaza baraza hilo, Rais Kikwete alizungumzia azma ya serikali kuchukua hatua kwa watendaji wengine wa serikali na taasisi zake ambao alisema ni chanzo cha mabadiliko hayo.
Alisema mawaziri wamekuwa wakijiuzulu hata kwa makosa ambayo si yao na kwamba serikali itaanza kuchukua hatua kwa watendaji wakiwamo makatibu wakuu, wakurugenzi wa wizara, watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma pamoja na bodi za mashirika husika.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), chini ya Makamu Mwenyekiti wake, Deo Filikunjombe, ilimtuhumu Ekelege baada ya kubaini kuwepo kwa udanganyifu kwenye mpango wa TBS wa kukagua bidhaa.
Filikunjombe alieleza kuwa waligundua madudu baada ya kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore na mjini Hong Kong, China.
“Tulikwenda Hong Kong na Singapore na tumegundua kwamba TBS ni wababaishaji, huwezi kuamini anachokifanya mkurugenzi (Ekelege) huko nje.”
Alidai kuwa Ekelege aliwapeleka katika ofisi hewa ambayo baadaye waligundua kuwa haikuwa ya ukaguzi wa magari.
“Tumekwenda Hong Kong na akatupeleka katika ofisi feki na tulipombana akasema kuwa aliomba kwa muda kuitumia ofisi hiyo,” alisema.
 

Forum statistics

Threads 1,285,566
Members 494,675
Posts 30,866,948
Top