KIFO CHA HAWARA (mkono wa jinni)
SEHEMU YA TATU
MTUNZI :
Mbogo EDGAR
ILIPOISHIA SEHEMU YA PILI : Nilifanikiwa kupata nafasi kwenye Toyota hiace, na safari ya kwenda Chake Chake ikaanza, ukweli sikuwa na raha hata kidogo, nilijikuta naichukia Pemba bila hata sababu, hata nilipokuwa naitazama barabara nyembamba yenye kona nyingi sana kali na za ghafla, huku nikishuhudia karafuu zikiwa zimeanikwa pembeni ya barabara, ghafla nikajikuta nikiichukia ile harufu ya karafuu, huku ule wimbo wa marashi ya pemba ukinijia kichwani na kujikuta na wenyewe nauchukia vibaya sana, nikiona kama unanisanifu,…… endelea…………..
Saa sita mchana tayari nilikuwa nimesha fika sehemu ambayo nilipangiwa kufikia, ni pembezoni kidogo mwa mji wa chake chake mashariki mwa Pemba, sheia (kata) ya Vitongoji, tukiwa tume katiza mji wa Chake chake ambapo tulikuta watu wengi na uchangamfu wa hali ya juu japo ilikuwa ni barabarani, pia tuka katiza macho manne ambako tuliacha barabara ya wete na kuifuata ile ya Vitongoji na kupita Wawi kuelekea Vitongoji.
Kwanza nilienda moja kwa moja kwenye shule ya sekondali ya Feidel Castor, ni moja ya shule kubwa sana za Sekondali nchini Tanzania, shule ambayo viongozi wengi wakubwa na watu mashuhuri hapa nchini hasa kisiwani pemba walisoma kwenye shule hii, ambayo nilipangiwa kuja kuwa kama mwalimu wa computer, ikiwa kama kificho cha kazi yangu, (cover) “hooo assalamu Alaykum mwalimu Eric” alinisalimia mwalimu mkuu wa shule hii, mara baada ya kuingia ofisini kwake kwa lengo la kureport, nilisha julishwa kuhusu salamu za huku kisiwa cha pemba ya kwamba salamu yoyote kwa wenyeji ni asalamu alaykum” walaykum salam mwalimu” niliitikia salamu ile ambayo iwe mtu mzima au mtoto ungepaswa kumsalimia hivyo, “karibu sana mwalimu, naona umewahi kabla ya vifaa havijafika” alisema mwalimu huyu ambae alinipa maelezo mafupi na utaratibu wa pale shuleni na kisiwa kwa ujumla wake, ikiwa ni miiko na maadili kwa ujumla huku akisisitiza sana kuhusu ukaribu na wanafunzi wa kike, pamoja na waschana wa huko mtaani, maana hilo swala lilikuwa ni baya kuliko swala jingine kisiwani hapa, “kwani umebahatika kuwa na mke?” aliuniliza mwalimu mkuu, na hapo nilicheka cheka kidogo maana achilia kuwa na mke ukweli sikuwa na hata mwamke mmoja wa kumuita mchumba, “bado sija bahatika mwalimu, lakini nadhani nikirudi nitaoa” nilisema kwa sauti ya kujiamini, maana kiukweli nilijiona bado mdogo kuwa na mke, nikamuona mwalimu mkuu anatoa macho kwa mshangao, unangoja nini kijana? hebu ona una taaluma nzuri ya ufundi wa computer na network ambayo inakupatia kipato kikubwa, wakati wenzako wanaishi kwa kazi ngumu zenye ujira mdogo, lakini wametimiza ibada ya ndoa” alisema yule mwalimu ambae kiukweli ni mzee wa makamo alievalia baraghashia kichwani mwake huku chini akiwa amevalia shati refu ambalo hakuchomekea kwenye suruali yake, na miguuni alivalia viatu vya wazi yaani sendo, “unajuwa mwalimu, muda mwingi nilikuwa masomoni, hivyo sasa nimerudi naamini nitafanya hivyo” nilijibu tu kwa lengo la kumtuliza mwalimu yule ili maongezi yaishe na mimi niondoke zangu kwenda sehemu niliyopangiwa kufikia japo nikapumzike kwa uchovu wa safari, “ni vyema, ila nahakika utaondoka na mke huku huku pemba” alisema yule mwalimu mkuu, huku nikimuona anaachia kicheko cha furaha, hapo nika jitabasamulia kidogo, maana nilikumbuka wale waschana niliokuwa nawaona kule njiani, japo ni wazuri wa sura na rangi lakini maumbo yao haya kunivutia, “kwanini mwalimu, ina maana huku kuna waschana wazuri kuliko sehemu nyingine?” niliuliza kwa sauti yenye udadisi, maana sikutaka kumfanya yule mwalimu anione mwenye dharau, “kwani uzuri wa mwanamke ni nini, maana huku ndiko kwenye wake wenye maadili na hekima, mwanawake wacha mungu, hata kwa uzuri ni wazuri haswaaaa” alisema mwalimu mkuu kwa sauti ya kusifu na kunadi, “na kisiwani hapa wavulana wenye maumbo kama yako ni wachache sana, hakika utawavutia wengi sana, hivyo inakubidi uwe makini sana kwa sababu huku pemba hakuna mtu anaependa binti yake achezewe na matokeo yake huwa mabaya sana” aliniambia tena mwalimu mkuu akinisisitiza.
Baada ya hapo mwalimu mkuu akanieleza kuwa kutokana na usalama kuwa mdogo hasa kwa watu kutoka nje ya pemba, ambao mara nyingi kwa miaka hii ya uchaguzi huonekana wanakuja kufanya hujuma kwenye uchaguzi, wameniombea ukae kwenye kambi moja ya Jeshi la ulinzi, ambalo lipo jirani kabisa na shule hii ya sekondari, kambi hiyo inaitwa Ali Khamis Camp, (sikuwahi kupata historia ya huyo bwana Ali Khamis alikuwa nani, ila ninacho kumbuka niliambiwa kuwa eneo lilipo kambi hilo, liliwahi kuwa kambi la mtu huyo alieitwa Ali Khamis).
Nakumbuka wakati natoka pale shule, shule ya mchanganyiko wa wanafunzi wakike na wakiume, niliweza kuona wanafunzi wa kike waliojitanda vilemba vyeupe vichwani mwao, wakichungulia madirishani huku wengi wao wakiwa ni waschana wenye sura nzuri kweli kweli, ukweli niliona wazi kuwa kuna ugumu sana kuishinda mitihani ya huku pemba, lakini kwa kuzingatia nilicho elezwa na mwalimu mkuu nikaachana nao na kuendelea na safari yangu, japo ilihitaji moyo mgumu sana kupotea.
Nikaenda pale jeshini ambapo palipakana na shule ile, nikapokelewa na askari mwenye kuvalia sale za jeshi la ulinzi na bega la kulia alivalia kitambaa cheupe chenye maandishi makubwa begani kwake, MP, ikiwa ni kifupi cha neno Military Polisi, yaani polisi wa jeshi, ambae alinipeleka moja kwa moja kwa afisa wa utawala wa kikosi kile, ambae alionyesha tayari anataarifa za ujio wangu kwa jinsi alivyo nipokea, “hooo bwana Eric, karibu pemba pelemba” alinikaribisha yule afisa wa utawala wa kambi lile kwa sauti iliyojaa uchangamfu na ucheshi, ambae alikuwa na nyota mbili pande zote za mabega yake, tena alionekana ni kijana ambae kama alinizidi umri, basi mwaka mmoja au miwili au hata naweza kuwa nimemzidi umri, ambae cheo chake kinaitwa lutein, “asante sana kamanda, kweli hii ni pemba pelemba” aliitikia kwa sauti ya ucheshi na uchangamfu kama yule lutein wa jeshi ambae alikuwa ni mcheshi sana.
Naam baada ya kusalimiana na afisa wa utawala, ambae kwa majina anaitwa Simon Malambo, tuliongea mawili matatu kisha akampigia simu askari mmoja kuwa aje mara moja pale ofisini kwake, dakika chache baadae tukiwa tunaendelea kuongea hili na lile kwa kiasi kikubwa tulikuwa tuna zungumzia juu ya mambo ya computer, ikiwa kama taaluma yangu, mara akaja askari mmoja mwenye cheo cha koplo ambae alipiga saluti, “chumba kipo tayari?” aliuliza yule afisa utawala mara baada ya kuitikia ile salamu ya kijeshi, “kipo tayari toka jana afande” alisema yule askari mwenye cheo cha koplo, akimueleza yule afisa utawala wa kambi lile la Ally Khamis, hapo yule afisa akamueleza yule askari mwenye V mbili mabegani, kuwa anipeleke kwenye nyumba waliyo iita ya kijani, “mpeleke Green House, hakikisha unapeleka taarifa kule mess ili awe anapewe chai na chakula cha mchana” alisema yule afisa na kabla sijajiuliza kuhusu chakula cha jioni yule afisa akanipa jibu, “bwana Eric, kuhusu chakula cha jioni utakuwa unakula staring Mess, nadhani utakuwa unahitaji kwenda ku refresh akili mida ya jioni” alisema yule afisa na mimi nikaitikia japo sikujuwa ana maamisha nini anaposema kurefresh, ila jioni ya siku ile nilielewa alicho kuwa anamaanisha.
Ilikuwa hivi, baada ya kupelekwa kwenye jengo moja dogo lenye bati za kijani iliyopo ndani ya kambi lile lile, tena upande ule ule karibu na shule ya Fidel Castor, jengo hilo likitazamana na barabara kubwa ya lami inayoenda vitongoji mpaka makaani pwani ya mashariki ya pemba, nikaonyeshwa chumba ambacho kiliandaliwa kwaajili yangu, nikweli kilikuwa chumba kidogo lakini kizuri, chumba kilicho kuwa na kila kitu mpaka bafu na choo ndani, ukweli kilikamilika, ukiachilia kitanda kimoja kidogo cha chuma, pia meza ndogo ya mbao na kochi moja dogo la kisasa, aina ya sofa jipya kabisa, hapo nikapata wazo la kuongeza baadhi ya vitu ambayo vilipungua mule ndani ikiwa pamoja na ki TV kidogo na deck yake, kwa sababau niliona kuepusha kuingia kwenye vishawishi na mabalaa ya mtaani, bora wakati mwingine niwe na jifungia ndani ya chumba hiki natazama filamu, “samahani bro, eti huku nako wanauza vifaa Used kama unguja?” nilimuuliza yule askari koplo, kwa sababu nilishawahi kusikia habari za vitu hivyo vyenye bei rahisi, “tena huku unaweza kupata kitu kizuri utadhani akija tumika” alisifia yule jamaa, hivyo nikapanga jioni ya siku ile niende Chake, nikafanye uchunguzi wa mambo mawili, kwanza sehemu ya kufanyia mazoezi ya baskert, kwa sababu sikutaka kusahau mazoezi, pili kuchunguza bei ya vifaa hivyo, ambavyo vita nisaidia kwa kipindi ambacho nitakuwa huku Pemba, kwa sababu sikufikiria kukamilisha uchunguzi, sasa jini mimi nitalichunguzaje, ukweli nilipanga kukaa miezi kadhaa kisha nipeleke report ya uongo halafu nigeuze zangu kurudi Dar es salaam, “ila bro, kama unaenda Chake inabidi uwahi kabla hawajafunga maduka” alisisitiza yule afande koplo, na mimi nikachukulia kuwa ni msisitizo wa kawada tu! Kwa sababu niliona muda bado mwingi sana.***
Ukweli nyumba hii ya kijani ilikuwa imekaa sehemu nzuri sana, ilikuwa inatazamana na makazi ya askari na familia zao, ikitenga nishwa na barabara ambayo ilikuwa ni ya lami iliyo kuwa inatoka mjini kwenda makaani ambako ni baharini, ikipita Vitongoji mjini, mbuyuni mpaka huko baharini, ambako kulikuwa kuna fahamika kama makaani, baada ya kupanga vifaa vyangu vizuri ikiwepo na Lap top yangu, ambayo huwa siiachi popote ninapo kwenda, kutokana na kuwa ndio kifaa pekee cha kutunzia kumbu kumbu nilicho kuwa nacho, nikaweka vizuri vifaa vyangu vya kazi, ikiwepo pisto (bastora) yangu ndogo sana aina ya A. G. P -5.2mm, hii niliipata Russia inaitwa Automatic Gun Pistor, yenye mzingo wa mm 5.2, nikaihifadhi na risasi zake box mbili, camera ndogo ikiwa ni digtal, kisu kidogo kikiwa ni Automatic spring knife, ambavyo nilivihifadhi vizuri kabla sijafuatwa na kuambiwa kuwa natakiwa kwenda kula ndani ya mesi, hapo nikajuwa kuwa wanajeshi siku zote hufanya mambo yao kwa ratiba iliyonyooka, muda wa kula ni muda kula na muda wakazi ni muda wakazi, nikaelekea huko messi ambapo nilikuwa nakula pamoja na maafisa wa jeshi, ambao walikuwa wengi kidogo, hapo licha ya kuanza kuzoeana nao na kunifanya nipunguze uoga na upweke, pia niliweza kuanza kusikia habari za hiyo sehemu inayoitwa staring Mess, ambako niligundua kuwa kulikuwa na bwalo kubwa la jeshi huko mjini karibu na macho manne, yaani wawi, ambapo wakati mwingine huwa kama bar kwaajili ya askari wenyewe na raia ambao wanahitaji kuja kupata vinywaji hasa vilevi ambavyo kwa kipindi hicho vilikuwa vina patikana hapo pekee, pia hapo hapo kulikuwa na hotel kubwa kwaajili ya wale maafisa, hata mimi nilitakiwa nikale pale, story zile zilinivutia sana maana nilisikia kuwa ni sehemu iliyochangamka na kufanana na sehemu za starehe kama za Tanzania bara, hapo nikapanga kuwa baadae nikitoka mjini chake chake nitapitia sehemu hiyo ili nikapate na chakula cha jioni kama nilivyo elekezwa.
Wakati tuna kula nika muona afisa utawala nae akija mule ndani, akanieleza kuwa kama ningependa kwenda kutembea uwanja wa ndege kuna gari lilikuwa linampeleka kiongozi fulani, hivyo naweza kupata lifti, na mimi nikasema japo sitoenda huko uwanja wa ndege ila nitapanda mpaka mjini nikatazame sehemu ya mazoezi na maduka ya vifaa used, bahati nzuri na yeye afisa utawala akanieleza kuwa, “uwanja wa baskert ball, upo upande wa hospital ukifika pale kwa nyuma utaona uwanja, jioni kunakuwa na vijana wengi wanafanya mazoezi” alisema yule afisa na kunieleza kuwa hata pale kambini kwao pia huwa wanafanya mazoezi siku za juma nne na ijumaa asubuhi, nikaahidi kushiriki siku hizo huku akinieleza kuwa kuna watu huwa wanafanya mazoezi ya mpira wa volley ball kila siku jioni, kama ninge penda kwenda kushiriki, ukweli nikwamba mchezo huo japo nilikuwa naucheza wakati mwingine lakini sikuupa kipaumbele kama ulivyo mchezo wa mpra wa kikapu.**
Naam, saa kumi na robo ndio muda ambao nilishuka toka kwenye gari la jeshi pale chake chake, nikalitazama gari lile ambalo liliendelea na safari yake upande wa madungu kuelekea uwanja wa ndege, likitokomea zake, mimi nikiwa nimevalia tishert na jinsi na raba, nilisimama barabarani na kutazama kwa mshangao kushoto na kulia pasipo kuelewa nini kimetokea hapa mjini, maana hakukuwa na dalili ya uwepo wa watu mida ile ya saa kumi hapa mjini Chake chake, kwa kifupi usinge weza kuamini kuwa hapa ndio chake chake mjini, ambapo masaa kadhaa yaliyopita nilipita mahali hapa nakukuta watu ni wengi kweli kweli, lakini sasa palikuwa kimyaa kabisa hata magari machache yaliyo kuwa yana katiza kutokea macho manne au upande wa madungu haya kuwa yakisimama pale Chake chake mjini, lakini kwa mbali sana upande wa kuelekea upande wa madungu nikaliona duka moja tu likiwa wazi, kilicho nionyesha kuwa lipo wazi ni bidhaa na mtu mmoja aliesimama nje.
Hapo japo nilikuwa na wasi wasi, lakini nikaanza kutembea taratibu kueleka ndani ya mitaa, ambayo kosa kuwa majengo ambayo yapo vizuri tungesema ni magofu, maana hakukuwa na watu kabisa, nikatembea taratibu kufuata barabara inayo ingia ndani ya mitaa nikidhania kuwa pengine huko ndiko kwenye mji mkubwa na watu wengi zaidi, hakukuwa na mtu wa kumuuliza, mji ulikuwa mweupe na kimya kabisa.
Lakini basi baada ya kuingia ndani kidogo na licha ya kufuata barabara kubwa za mitaa, sikuona dalili ya mtu yoyote bora hata kule barabarani nilikuwa naona magari, hapo nikapigwa na butwaa, unajuwa msomaji huwezi kupata picha kamili, yaani sawa na kwamba unafika sehemu kama kariakoo mida hii ya saa kumi jioni unajikuta upo peke yako, “au wanakimbia majini” ndivyo nilivyo jiuliza huku natembea taratibu kusonga mbele, Maduka na ofisi zote zilikuwa zimefungwa zaidi kilicho nionyesha kuwa haya ni maduka ni majina ya maduka yale kwenye viambaza au juu ya nguzo za milango yake,
Naam katika zunguka zunguka yangu niliibukia sehemu moja ambayo ilionyesha kuwa ni sokoni, tena soko kubwa, hata hivyo nilikuta sehemu ile imeshafungwa na bidhaa zimefunikwa kwa vipande vya magunia au maturubai makubwa kwenye vibanda vyake, ukweli nilishangaa sana kiasi cha kusimama kabisa na kukodolea macho soko lile la chake chake, hapo nikapata wazo la kuitafuta hospital ili nikaone kama kutakuwa na watu wanafanya mazoezi kama nilivyo ambiwa, lakini ile nageuka kutazama mbele nilikokuwa na elekea usawa wa macho mita hamsini mbele, “mama yangu jini” nilijikuta nashtuka na kujisemea kwa sauti ya kunong’ona, ni baada ya kumuona mschana mmoja mwenye urefu wa wastani, ambao ungelingana kidogo na mimi, akiwa amevalia baibui jeusi lenye kudaliziwa kwa nyuzi rangi ya blue na dhahabu,sikujuwa ametokea wapi na nilipomtazama vizuri nilibahatika kuona viatu vyake vya mikanda, vyenye rangi ya dhahabu na visigino virefu vilivyoonekana kidogo kwenye miguu yake, huku sehemu kubwa ya viatu ikifunikwa na baibui lake jeusi lililo shonwa kwa mtindo wa kipekee na wa kisasa, likiukamata mwili wake vizuri na kuonyesha vyema uumbaji, maana ukiachia hips zake pana na makalio makubwa tofauti na waschana wengi niliopata kuwaona toka alipo ingia ndani ya kisiwa hiki, mschana huyu mzuri ambae alionyesha wazi kuwa ni chotara wa kiarabu alikuwa na sura nzuri kweli kweli, japo alikuwa amefunika nywele zake kwa ushungi alio ubana kwa pini fulani nazo rangi ya dhahabu, lakini niliweza kuhisi kuwa alikuwa na nywele ndefu zilizo lala kwenye mgongo wake, mschana huyu mrembo alikuwa anatembea taratibu kuja upande niliokuwepo na ukweli ni kwamba hakukuwa na njia ya kuchepuka wala kukatiza, upende wa kushoto kwangu kulikuwa na safu ya maduka na kulia kwangu kulikuwa na soko, dada huyu alitembea kwa mwendo wa madaha huku akinikazia macho, japo uso wake ulionyesha tabasamu.
kwa kifupi tulikuwa wawili tu ndani ya eneo la soko kuu la chake chake, na mbaya zaidi mwanamke huyu niliweza kumfanisha na mwanamke ambae nilisoma sifa zake kwenye maelezo ya mwanamke alieingia na bwana Abdulqadir kwenye nyumba ya wageni, na kisha kukutwa amekauka na kubadilika rangi.
Hapo siku jiuliza mara mbili, nikageuka mara moja na kutazama nilikotoka kisha nikaanza kutembea kwa haraka kurudi nilikotoka, moyoni nikajilaumu kwa kuto kubeba bastora yangu, pengine ningeweza kulitisha lile jini, (kama nilivyo amini kuwa yule ni jini) niliendela kwa mwendo wa kawaida ili lile jini lisishtuke kuwa nalikimbia lenyewe, huku kila baada ya hatua kadhaa nikitazama nyuma kumtazama yule mwanamke, kama ana nikaribia au bado yupo mbali, ambae nilimuona kama aliongeza mwendo pia, kwa sababu alikuwa anazidi kunisogelea kila nilipo geuka kumtazama, hapo nikapata wazo la haraka kwamba nikipata njia yoyote inayochepuka, nibadili njia ilinione kama mwanamke huyu atakuwa ananifuata mimi au alikuwa na safari zake, ili kama ananifuata mimi ikiwezekana nichukue uamuzi mwingine wa kujiokoa, na hakukuwa na njia nyingine ambayo nilikuwa na uhakika kama itaniokoa zaid ya kutimua mbio mpaka barabarani, niliamini kuwa kule barabarani, huyu jini asinge weza kunidhuru zaidi linge yeyuka na kupotea zake.
Niliendelea kutembea sasa nikiwa nimeongeza mwendo na lipopiga hatua kama kumi mbele niliweza kuona barabara moja upande wa kulia nikaifuata hiyo barabara nyembamba kidogo, ambayo niliamini kuwa inaenda kutokea barabara kuu tena usawa wa lile duka, maana ni upande huo huo nilitembea mita thelathini mbele kwenye ile barabara nyembamba huku nikipita chochoro nyingine nyingi tu ambazo siku zifahamu, zinaelekea wapi, vinginevyo ningeifuata moja wapo, pengine ingekuwa msaada kwangu, lakini hatua tano mbele nilipo tazamana nyuma nikamuona yule mwanake nae akikata kona kufuata upande ule ule niliokuwepo mimi, “hii pemba pelemba” nilijisemea kwa hofu, ukweli nilihisi miguu inakosa nguvu, lakini nikajuwa nikilegea tu! nita kwisha kweli, nikaongeza mwendo, haraka kuwai mwisho wa barabara hii ambako kulikuwa na kona flani upande wa kushoto, ikionyesha barabara ilielekea barabara kuu, itokayo mkoani.
Lakini nilipo ifikia ile barabara, nika geuka nyuma kutazama, yule mwanamke ninae mkimbia amefikia wapi hapo nikaduwaa kwa mshangao, maana sikumuona yule mwanamke wala dalili ya uwepo wa mwanamke huyo wala dalili ya kiumbe chochote eneo lile, nikatazama kule nilikokuwa na elekea na huku nazidi tembea kwa speed nikihofia isije kuwa lile jini likaja kuibuka mbele yangu, kwa sababu hata upande ule niliodhania kuwa naelekea barabara kuu sikuweza kuona mbele kuna nini kutokana na majengo marefu ambayo yalijengwa na waarabu kabla ya mapinduzi, pamoja na kona fupi fupi ambazo zilinikinga nisione mwisho wa ile barabara nyembamba, lakini baada ya kutembea kama mita sabini mbele nikaweza kuona barabara kuu ikiwa mbele yangu kama mita ishirini au thelathini toka nilipo kuwepo, hapo nikapunguza mwendo na kutabasamu kidogo huku nikishusha pumzi nzito ya kusema afadhari, maana nilikuwa na uhakika kuwa ile barabara ipo mbele yangu, na kilicho nipa uhakika ni lile duka lililokuwa wazi maana nililiona mbele yangu, Sasa nilikuwa natembea taratibu kwa kujiamini huku nikiwa na lisogelea lile duka.
Naam nikiwa nime bakiza mita kama kumi au ishirini kulifikia lile duka lililokuwa barabarani ghafla nikamuona yule dada akiibuka toka kwenye chochoro moja ya upande wa kushoto ukweli nilitamani kukimbia au kupiga kelele, lakini nikamuona akigeuka na kutazama upande ninao tokea mimi huku sura yake ikiwa katika hali fulani ya tabasamu ………. Haya sasa Eric siku yake ya kwanza kisiwan pemba anakutana na dada ambae anafanana na yule jini ambae anakuja kumchunguza, je ni jini kweli? Na kama ni jini kwahiyo kajua kuwa kaja kufuatiliwa? Ni nini atafanya baada ya kugundua kuwa anafuatiliwa? Basi nawe usiache Kufuatilia mkasa huu hapa hapa JamiiForums...