DC ampinga Lowassa hadharani
Friday, 28 September 2007 08:26
na Sitta Tumma, Mwanza
KATIKA hali isiyo ya kawaida, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza, Kanali Peter Madaha, ameonyesha jeuri ya kumpinga waziwazi Waziri Mkuu, Edward Lowassa, baada ya kuikataa taarifa ya wilaya hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya alilazimika kumjibu Lowassa hadharani na papo hapo, baada ya kuikataa taarifa hiyo ya wilaya na kisha akamweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa uongozi wake ni dhaifu.
Malumbano hayo yaliyozua gumzo kwa viongozi na watendaji wa serikali yalitokea jana, saa 3:45 asubuhi, Ikulu ndogo jijini hapa wakati mkuu huyo wa wilaya akitoa taarifa ya maendeleo ya wilaya hiyo.
Katika taarifa hiyo, Lowassa alionekana kutoridhishwa nayo hususan katika sekta ya elimu na kilimo, ambayo ilielezwa kuwa na udanganyifu mkubwa hata waziri mkuu kulazimika kuikataa na kusema mkuu huyo wa wilaya hana uongozi thabiti katika wilaya yake.
Huwezi ukaniambia mimi sina uongozi imara...mimi ni kiongozi na nina miaka 24 nikiwa kama kiongozi wa Serikali ya Tanzania. Mimi ni kiongozi, tena mzuri sana, alisema DC huyo kwa kujiamini na kwa sauti ya juu.
Katika hali hiyo, Lowassa hakuweza kubishana naye wala kumjibu lolote, isipokuwa alisisitiza kuikataa taarifa hiyo ya wilaya na kuonyesha kusikitishwa na kushangazwa na kauli ya DC huyo.
Source: Tanzania Daima: Friday, 28 September 2007 08:26