Kibano wanafunzi watoro chawadia

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
1576478594340.png

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha waraka kudhibiti utoro shuleni ambao pamoja na mambo mengine, utapunguza siku na kuwa chini ya 90.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki jijini hapa na Mkurugenzi Msaidizi Msingi na Uendelezaji wa Sera wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Yesse Kanyuma ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Leonard Akwilapo wakati wa kufunga Kongamano la 14 la Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA).

Alisema siku zitapunguzwa ili kuwe na siku kidogo mwanafunzi asipoonekana shule hatua zichukuliwe haraka.

"Lengo la serikali si kumfukuza mtoto bali ni kuwataka wamalize masomo yao pale wanapoanza darasa la kwanza wafike hadi la saba na watakapoanza kidato cha kwanza wafike kidato cha nne, utoro ni tatizo tusipodhibiti utatutia doa," alisema.

Alisema waraka huo utabainisha wajibu wa wadau wote katika suala zima la utoro.

“Awali zilikuwa siku 90 mtoto asipoonekana basi anafukuzwa shule, sasa tutapunguza zitakuwa kidogo ili kudhibiti utoro," alisema.

Alisema waraka huo utaangalia ni namna gani mwalimu wa darasa, mkuu wa shule, mwalimu wa nidhamu wanaweza kutimiza wajibu wao katika suala zima la usimamizi katika suala zima la utoro katika shule.

"Taarifa zilizopo ni kwamba mtoto anapopotea shuleni wakati mwingine hakuna mawasiliano ya aina yoyote ile kati ya uongozi wa shule na mzazi au mlezi au kiongozi wa serikali eneo husika ili kujua ni tatizo gani limemsibu mwanafunzi, na kuwa mtoro katika siku zote hizo," alisema.

Alieleza kumekuwa na pengo kubwa kati ya uongozi wa shule na wazazi au walezi na mtoto mwenyewe, wakuu wa shule watakuwa wasimamizi wakuu.

Aliwataka wakuu wa shule kuwa na kamati hai za nidhamu na ushauri ili kuondoa hali ya sasa ya fukuza fukuza ya wanafunzi.

Kanyuma alisema kuanzia mwaka ujao, serikali inatarajia kuanza kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za sekondari kwa kujikita katika kuzalisha uchapaji wa vitabu, kuboresha miundombinu na kuendeleza walimu.

Alisema ili kutekeleza mradi huo kwa wakati, wakuu wa shule watatakiwa kusimamia miradi hiyo kwa uadilifu na uaminifu mkubwa kwani itatumia mfumo wa force akaunti ambao hautahusisha mkandarasi.

Aliwahimiza kufuata sheria, kanuni na taratibu kusaidia kuleta ufanisi katika shule zao na kuondoa mlolongo wa mashauri ya walimu kwenye Tume ya Utumishi wa Walimu kwa walimu ambao wanakwenda kinyume.

Naye Kaimu Mkurugenzi Idara ya Elimu kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Jidamva, alisema kongamano hilo lililenga kuwajengea uwezo wakuu wa shule za sekondari nchini wa kusimamia sekta ya elimu.

"Yapo mambo mengi yanalenga kuimarisha utendaji kazi, zipo changamoto zimeainishwa na zitatafutiwa ufumbuzi kama vile upungufu wa walimu wa sayansi, vitabu," alisema.

Chanzo: IPP Media
 
Back
Top Bottom