Kesi za kusadikika shuleni

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,339
51,863
KESI ZA KUSADIKIKA SHULENI

Kwa Mkono wa, Robert Heriel.

Kesi ya leo huko shuleni ndio imenifanya niandike uzi huu, yaani kesi zingine zinachekesha sana, nitaandika kama nazungumza mwenyewe huku natembea barabarani, wewe utachora mazingira ya Taikon nikiwa natembea pembezoni mwa barabara ya vumbi, majira ya saa tano hivi kajua kakiwa kamekolea; pia chora nimevaa suruali ya kadeti na Fulana ya kijivu, chini nimevaa sendo, kichwani ninanywele nyingi kama kawaida yangu lakini wakati huu nimezichana; tufanye niko mbele yako yaani unanifuata kwa nyuma kisha unanisikia nikisema mwenyewe kama mwehu, lakini hutaki kuamini kuwa ni mwehu kutokana unaona jinsi nilivyovaa.

Haya sawa!
" Kikao cha shule kiliitishwa, nikaitwa kama mlezi wa huyo mdogo wangu, nilikuta baraza la shule likiwa limeshaketi na aliyekuwa akisubiriwa ni mimi na mwenyekiti wa Bodi ya shule, nikaketi nikisalimiana na wajumbe wa baraza lile, haikupita dakika kumi Mwenyekiti wa baraza la shule aliwasili. Kikao kikaanza Rasmi kwa Mkuu wa shule kutoa utambulisho na kueleza agenda ya kikao kile. Mkuu wa shule alitambulisha wafuatao; Mwenyekiti wa Bodi, Mtendaji wa kijiji, Mwalimu wa Nidhamu, mwalimu wa taaluma, Mwalimu Kidawa(huyu alikuwa mwalimu wa zamu), Mwalimu wa Darasa, Mlinzi wa shule, Mpishi wa shule, Mwalimu mkuu msaidizi, wajumbe sita wa bodi ya shule, wazazi wanne na mimi nikiwa watano. Wote tulitambulishwa kwa majina.

Kisha Mkuu wa shule akamng'ata sikio mwalimu mkuu msaidizi aliyekaa pembeni yake, muda huo huo mwalimu mkuu msaidizI akasimama na kuondoka akimuacha Mwalimu mkuu akiendelea kuzungumza. Kitambo kidogo Mwalimu mkuu msaidizi akaingia akiwa kaambatana na wanafunzi watano wakiwa na mgambo nyuma yao aliyeshika kirungu. Wakaamrishwa wapige magoti, wakafanya hivyo. Nikamuona na mdogo wangu uso wake ukiwa umejawa na simanzi.

Mwalimu Mkuu akaelezea kuwa wanafunzi hao wanashtakiwa kwa makosa yafuatayo;
1. Kutaka kuchoma shule, kwa kuunguza madarasa, maabara, maktaba,
2. Kuwapiga na kuwajeruhi waalimu na viranja wa shule hasa mwalimu wa nidhamu na mwalimu kidawa
3. Kuhujumu utoaji wa elimu shuleni hapo kwa kuiba zana za ujifunzaji na kufundishia
4. Kuitisha maandamano na kuvuruga utulivu wa shule kwa kile kinachodaiwa kutoridhika na chakula cha shule pamoja na adhabu za shuleni hapo
5. Kupanga njama za kutaka Mwalimu mkuu aondolewe na uongozi mzima wa shule hiyo
6. Kuharibu miundombinu ya shule kama kung'oa maua, kuiba vitabu na kuvunja vunja chaki.
7. Kutia Mimba wanafunzi

Mashtaka yaliyosomwa ni sita, Mkuu wa shule akawa anaongea kwa ukali hasira zikimla usoni mwake, Baraza lilikuwa kimya tukimsikiliza.
" Vijana hawa ni majambazi, wezi, wapenda ngono na wanaweza kuwa wauaji, ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya shule kikao hiki kimekuita hapa na kimeita wajumbe wote kwa ajili ya kumalizana na hawa vijana. Hawa vijana wamekuwa kero kubwa katika shule hii, wanasumbua waalimu na wanafunzi wangu.

Hawa vijana hawapaswi kuendelea kusoma katika shule hii, leo tutahitimisha mchakato huu na hawa vijana waende wakafanye uhuni wao huko mitaani ili wakutane na mkono wa serikali vizuri" Mkuu wa shule anameza mate kisha anaacha kumtazama Mwenyeketi wa bodi alafu anatugeuka sisi wazazi.

" Ndugu wazazi, tunafahamu ni kiasi gani uamuzi wetu utawaathiri na kuwahuzunisha, lakini hatuna chaguo kwa sasa, hatufanyi hivi kuwakomoa isipokuwa tunafanya haya kwa kufuata kanuni na sheria za shule za wizara ya elimu. Hatuwezi endelea kuruhusu majambazi, wabakaji na walaghai wa binti zetu kuendelea kusoma, tunajua fika kesi ya kumpa mimba binti ni miaka thelasini, hata hivyo tunawalaumu ninyi wazazi kwa kushindwa kuwalea vizuri watoto wenu, haya ndio matokeo sasa"

" Nitamkaribisha Mwalimu wa Nidhamu aongee machache na ataje kila mwanafunzi na kosa lake, kisha Mwenyeketi wa bodi atazungumza kwa uchache kabla maamuzi ya mwisho ya wajumbe kutoka. Karibu mwalimu wa nidhamu" Mwalimu Mkuu akamkaribisha Mwalimu wa nidhamu, Mr. Kibiriti. Mr. Kibiriti anasalimia wajumbe;

" Mimi sina mengi ya kusema, kazi yangu ni kutaja majina na kueleza ilivyokuwa, hivyo nitaeleza kwa ufupi sana. Nitaanza na Mwanafunzi wa kidato cha kwanza aitwaye Denis" Mr. Kibiriti anachukua moja ya mafaili yaliyokuwa juu ya meza yake, lilikuwa faili la kijani lilioandikwa juu yake Denis Kabori.

" Denis anashtakiwa kwa kosa la kumpa Mimba mwanafunzi mwenzake wa kidato cha kwanza aitwaye Donatila Zaburi, habari za mahusiano ya Donatila na Denis zilitufikia tangu mwezi wa pili, ukaribu wao ulitia shaka tukajaribu kuwaonya, lakini bado kwa kiburi wakaendeleza, ni mpaka tulipokamata barua za mapenzi zilizoandikwa na Denis kwenda kwa Donatila. Barua zenyewe hizi hapa" Mr. Kibiriti anazitoa zile barua na kuzionyesha kama kielelezo muhimu katika baraza hilo kwa shauri linaloendelea.

" Kama hiyo haitoshi, ili kuthibitisha kuwa Denis alikuwa kwenye mahusiano hatari ya kimapenzi na Donatila, tulikamata pia picha za Donatila katika Begi la Denis, picha zenyewe ni hizi hapa" Anazionyesha kisha anaendelea.

" Licha ya kumuonya lakini Kijana Denis akawa mkaidi, musimuone na sura yake ya upole, kijana huyo anakiburi na jeuri isiyo na mfano. Mwezi wa tisa mwaka huu ilibainika kuwa Donatila anamimba, na alipohojiwa moja kwa moja akasema mwenye mimba ni Denis. Hakuna aliyeshangazwa na majibu yake kwani ukaribu wao shule nzima iliufahamu. Kwa maelezo haya naomba kuwasilisha na kuliomba baraza hili lipokee vielelezo hivi kama ushahidi muhimu katika shauri hili" Mwalimu wa nidhamu anamaliza kisha anaketi.

Mwalimu mkuu anamnyooshea kidole Mwalimu Kidawa naye aseme; Mwalimu Kidawa anasimama anasalimia kisha anaendelea;
" Ilikuwa ni juma ambalo nilikuwa mwalimu za zamu. Nikiwa katika majukumu yangu majira ya mchana nilienda kuangalia jikoni chakula cha wanafunzi kama kipo tayari, njiani mkono wa kulia ulipo ukumbi wa shule wa kulia chakula nikaona shati jeupe likiishilizia kwenye pembe ya ukumbi.

Nikafanya hima kulifuata ili nijue alikuwa ni mwanafunzi gani, nilipokaribia nikasikia sauti ya wanafunzi wakiongea, nikasogea polepole kisha nikawasikiliza, walikuwa wakipanga mipango ovu ya kumpiga mwalimu Kibiriti, huyu Chuma huyu nilimsikia akisema watamvamia usiku wa ile siku wampige mpaka wamuumize, wengine sikuwajua ila sauti ya chuma niliisikia kabisa, kwa vile walikuwa wakivuta bangi nikarudi ofisini upesi ili kumuita mwalimu wa kiume tuje tuwakamate, lakini niliporudi sikuwakuta. Jioni yake Mwalimu Kibiriti akapigwa na watu wasiojulikana kama wote mnavyojua, lakini mimi ninauhakika Chuma na wenzake ndiye waliyempiga Mr. Kibiriti. Mimi ni hayo tuu"

" Ahsante sana Mwalimu Kidawa, Enhee! Mwalimu wa Darasa, Mr. Katema" Mwalimu Mkuu akasema. " Mimi sina mengi, miundombinu ya shule hii inaharibiwa vibaya na vijana hawa wawili, Kaboma na Tariki, wameharibu Buistani za shule hii, wao ndio wezi wa vitabu, wao ndio wanampango wa kuchoma shule hii. Tukio la juzi ambalo bustani zote za shule yetu kukatwa katwa na kung'olewa niliitisha kikao cha shule cha wanafunzi kwa dharura, kisha tukaitisha wanafunzi waandike kwa siri kupitia vikaratasi ni nani anahusika na uharibifu ule. Asilimia 50% walisema hawajui, 40% wakawataja Kaboma na Tariki, 10% wakataja wengine. Tuliona wawili hawa ndio wahusika wa wizi na uharibifu wa bustani kwa sababu vikaratasi vile vya kura ya siri vilieleza hivyo. Nitatoa vikaratasi hivyo kama ushahid. Naomba vipokelewe" Mwalimu anakaa

Ananyanyuka Mwalimu Mkuu Msaidizi
" Maandamano makubwa yaliyofanyika ya kupinga uongozi wa shule, chakula kumwaga yalisababishwa na huyo dogo hapa, yeye ndiye aliyechapisha kwa siri karatasi na kuzibandika ukutani, milango ya madarasa, Ubao za matangazo, ubao wa kufundishia shule nzima na madarasa yote. Karatasi hizo ni hizi hapa" Ananyanyua moja ya karatasi na kuwaonyesha wajumbe huku na huku. Karatasi ilikuwa na maneno yaliyosomeka " SHULE SIO GEREZA, TUNALIPA ADA NYINGI CHAKULA KIDOGO NA KIBAYA, TUGOMEE! UONGOZI WA SHULE UONDOLEWE. TUNATAKA UONGOZI MPYA. LEO NI MGOMO!

" siku ile wote tulishangazwa na matangazo hayo tulipofika shuleni kwani yalikuwepo mpaka kwenye nyumba za waalimu ambazo baadhi yao zipo hapa shuleni. Sasa tukajiuliza nani kafanya mambo haya, kina nani aliyebandika matangazo haya ya kuchochea maandamano. Tukiwa tunazuia hayo, ndipo Mlinzi wa shule akasema alimuona mida ya saa nane za usiku mtu kama BARAKA, akasema huenda ni yeye kwa sababu alikuwa kabeba bahasha kubwa la kaki. Ndio tukamkamata lakini maandamano yaliendelea na yalikoma nilipoita usaidizi wa polisi. Hivyo kijana huyu ndiye mhusika wa maandamano" Mwalimu mkuu msaidizi akamaliza.

Mkuu wa shule akamkaribisha mwenyeketi wa baraza la shule.
" Nafikiri tumesikia wote, ushahidi upo wa kutosha na sioni kama tuendelee kupoteza muda hapa, barua zao si mlishaziandaa?" Mwenyeketi wa Bodi akauliza huku akitazamana na mkuu wa shule. Baada ya kujibiwa akaendelea kusema;

" Hatuwezi kuvumilia upumbavu huu utendeke, tutawafukuza shule na pia tutawachukulia hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine. Tutaenda Paredi, mtachapwa viboko sita kila mmoja mbele ya shule, kisha mtaondoka na ndio mtakuwa mmefukuzwa shule moja kwa moja. Mwalimu embu kaamrishe kengele Igongwe wanafunzi wakae paredi zoezi liende upesi upesi"
Mwalimu kidawa anatoka lakini Mama Mpishi akaonekana ananyosha Mkono sisi muda huo tumelowa jasho kwa tulioyasikia.

"Ndio Mama Mpishi, unalolote la kuongezea?" Mkuu wa shule akasema
" Nashukuru sana Mkuu, Mimi nafikiri ingekuwa busara kwa watu wa heshima kama sisi, tungejaribu kuwasikiliza wanafunzi nao wajitetee hata kama wamefanya lakini wanaweza eleza kwa nini walifanya au hata kuomba msamaha. Nafikiri hiyo ni haki na ni busara hata kwetu. Kama hatutafanya hivi ikisikika kwengine wote hapa tunaweza onekana hatukuiamua vizuri kesi hii. Mimi ni hayo tuu" Mama Mpishi anakaa.

" Mama! Hivi mwizi unampa muda wa kujitetea kweli, labda hujawahi ibiwa Mama!" Mwalimu Kibiriti akasema huku akiyakanyaga maneno ya Mama Mpishi.
" Nafikiri hakuna haja ya kujitetea hapa" Mkuu wa shule akaunga mkono.
" Sisi tunaona wajitetee kila mmoja dakika moja moja" Wajumbe sita wa baraza wakasema.

" Embu tuache wajitetee" Mwenyekiti wa bodi akaungana na wajumbe sita huku wazazi nasi tukiomba hisani hiyo.
Haya Denis utaanza;
" Shikamoni..."
" Hakuna cha shikamoo hapa, jieleza unamuda mchache ohoo! " Mwalimu Kiberiti akamkatiza kwa sauti kali.
" Mimi naomba nijitetee Donatila akiwepo hapa, yeye si ndiye nimeambiwa nimempa mimba. Naomba aitwe!" Wazo hilo linapingwa na Kiberiti lakini wajumbe wanaungana na hoja ya Denis. Donatila analetwa na bodaboda kwani hakai mbali na shule.
Akaingia kwenye baraza hilo tumbo lake kubwa likiwa limetangulia.
" Sasa naweza kujitetea. Mimi na Donatila ni kweli ni marafiki wakubwa, barua zilizoonyeshwa hapa ni kweli nilimuandikia, picha zilizoonyeshwa kwenye baraza hili nilipewa na Donatila mwenyewe. Ikiwa nitashtakiwa kwa kuandika barua hizo na picha hizi basi ni halali yangu kufukuzwa shule, lakini hili suala la kumpa mimba Donatila ni hila na uongo. Sijampa mimba Donatila, labda kama sijui elimu ya uzazi. Mimi sijawahi kujamiiana na Donatila tangu nikutane naye hapa shuleni hivyo mimba nashangazwa na wanaosema nimempa mimba" Denis anakatishwa na Mwalimu Kiberiti.
" Wewe mtoto muongo sana, unafikiri tutaamini maneno yako, shule nzima inajua wewe ndio umempa mimba Donatila, unatufanya sisi watoto wenzako, Nitakutandika hapa!"

" Mimi ninachosema ndio ukweli, hata kama Donatila alisema na wengine mmesema mimi ndio nimempa mimba lakini ukweli ni kuwa sijawahi kulala na Donatila, Ati Donatila embu sema ukweli wa Mungu, wewe ni rafiki yangu, unafahamu tabu itakayonipata endapo utapindisha maneno na kunisingizia.."
" Acha kumshawishi, mwambie asema ukweli sio umpe maneno ya huruma akuonee huruma hapo" Mkuu wa shule akaingilia.
" Sawa! Donatila hiyo mimba niyakwangu?" Denis akasema huku akimtazama Donatila.
Donatila akainua uso wake wakawa wanatazamana na Denis, kwa kitambo kidogo Donatila akasema; " Ndio, mimba hii ni yako"
Watu wote wakabaki wameduwaa wakimtazama Denis.
" Nafikiri wote tumesikia naona utetezi wa Denis umeishia hapa" Mwenyekiti wa bodi ya shule akasema
" Wazazi wangu, waalimu mimi hata bado sijapevuka, bado sijaanza kuziona shahawa zangu, iweje nimtie mtu mimba? Nimesema sijalala naye hamjanisikiliza, basi hata ningelala naye ningewezaje kumtia mimba wakati mimi bado sijapevuka kumwaga shahawa?"
Denis akaongea huku akilia machozi yakitiririka.

Maneno hayo yakalifanya baraza likae kimya, kisha Mama Mpishi akasema hiyo haiwezekani, huyo mtoto mnamsingizia.

Punde Mlango ukafunguliwa akaingia Mama yake Donatila, akamfuata Mwalimu Kiberiti na kuanza kumvamia akimpiga;
" Mshenzi mkubwa wewe, umemharibu binti yangu, umemtia mimba binti yangu, alafu unadhani pesa zako zitafunika uhalifu wako umbambikizie kesi mtoto wa watu. Jamani Denis hajamtia mimba binti yangu. Huyu Mbwa ndio kafanya yote haya. Usiku wa leio Donatila kanieleza yote"

Leo tuishie hapa. Hii kesi hii acheni tuu.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Sinza, Dar es salaam
 
Donatila anataka Denis afungwe wakati mimba kaitia Mwalimu Kiberiti. Halafu ndio amekaa kwenye jukwaa la watoa hukumu! Ama kweli, Ukweli unapotalamaki Uongo hujitenga. Ni suala la muda muda tutasikia mengi pale Uongo unapotumika kukandamiza mnyonge.
 
Donatila anataka Denis afungwe wakati mimba kaitia Mwalimu Kiberiti. Halafu ndio amekaa kwenye jukwaa la watoa hukumu! Ama kweli, Ukweli unapotalamaki Uongo hujitenga. Ni suala la muda muda tutasikia mengi pale Uongo unapotumika kukandamiza mnyonge.


Inavyosadikika Mwalimu Kiberiti njiti 36 amemwaga pesa Kwa Mkuu wa shule na mwenyeketi wa Bodi ya shule ili Denis afunguzwe shule na baadaye akashtakiwe
 
Back
Top Bottom