Kurunzi

JF-Expert Member
Jul 31, 2009
7,124
2,000
MONDAY MAY 24 2021

Haijawahi kuwa rahisi kwa familia nyingi kumaliza mashauri ya mirathi kwa amani, hata pale inapotokea marehemu alionesha mgawanyo wa mali zake katika wosia aliouacha.

Tafrani na hali ya kutoelewana huwa kubwa zaidi kama aliyefariki na kuacha ama kutoacha wosia alikuwa tajiri aliyemiliki mali nyingi.

Moja ya familia za kitajiri zilizotumbukia katika mgogoro mkubwa wa mirathi ni ile ya marehemu Reginald Mengi, mfanyabiashara bilionea na mmiliki wa kampuni za IPP ambaye alipenda kujibainisha kama mtu mkarimu na mwenye kusaidia wahitaji.

Wiki chache baada ya kifo cha tajiri huyo kilichotokea Mei 2, 2019 katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Dubai, watu wanne walifungua maombi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakiitaka iwathibitishe kuwa wasimamizi wa mirathi ya tajiri huyo kupitia wosia aliouacha.

Katika wosia wake aliouandika Agosti 17 2017, Mengi amemtaja mke wake, Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wake mapacha kuwa wamiliki wa mali zote pindi atakapoaga dunia, huku ukiwaweka kando watoto wengine aliozaa na mke wake wa kwanza.

Mengi alifunga ndoa na mlimbwende wa Tanzania mwaka 2000, Ntuyabaliwe na kuibua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutokana na tofauti ya umri.

Mtoto wa Mengi, Abdiel na mdogo wake Mengi, Benjamin, walishitushwa na taarifa za kuwepo kwa maombi hayo mahakamani.

Haraka haraka walipeleka zuio la kisheria kutaka mahakama kusitisha uthibitishwaji wa wasimamizi wa mirathi waliotajwa kwenye wosia wa baba yao hadi hapo malalamiko yao yatakaposikilizwa.

Waliweka zuio hilo chini ya kifungu cha 58 (1) cha Sheria ya Urithi na Usimamizi wa Mirathi ambacho kinatamka kuwa mtu yeyote ambaye anadai kuwa mnufaika wa mali za marehemu anaweza kuweka zuio la kuthibitishwa msimamizi wa mirathi au mrithi hadi pale mahakama itakaposikiliza hoja zake.

Hoja za watoto wa Mengi
Abdiel na mdogo wake Mengi, Benjamin walidai katika moja ya hoja tano walizowasilisha mahakamani kuwa wosia uliodaiwa kuandaliwa na baba yao haukuwa halali kisheria, kwa kuwa alikwishapoteza uwezo wa kuandaa wosia kutokana na matatizo makubwa ya afya yaliyomsumbua tangu mwaka 2016.

Pia walitaka mahakama isiuthibitishe wosia huo kwa kuwa ulikuwa wa kibaguzi kwa kuwaweka kando watoto wake halali na kumpa mali zote Ntuyabaliwe na watoto wake mapacha.

Katika hoja nyingine watoto hao walidai kuwa wosia wa baba yao haukuwa umefungwa lakiri (seal) na kwamba sain zilizopo katika wosia huo zilikuwa tofauti na saini halisi ya baba yao.

Walidai pia kuwa wosia huo haukushuhudiwa na ndugu yeyote au mke wa baba yao, wakihofia kuwa kitendo hicho kitaleta mkanganyiko na ugumu kwa walionyimwa urithi kulienzi jina la familia yao na urithi wa baba yao.

Kwa mujibu wa watoto hao, wosia huo ulikiuka sheria inayohusu uandaaji wa wosia, wakidai ulikuwa wa kibaguzi na ulifanywa kwa ushawishi mbaya wakati baba yao akiwa amepoteza uwezo wa kutumia dhamira yake kwa uhuru kamili.

Walipinga pendekezo lolote kuwapa waleta maombi haki ya urithi na usimamizi wa mirathi hawakuwa na nasaba wala kuhusika katika mali za marehemu, wakidai wote walikuwa ni ‘wageni’ kwa mali ya baba yao, hivyo wangesababisha ugumu na mashaka katika usimamizi wake.

Waliiambia mahakama kuwa wao ndio walioteuliwa na ukoo wao kusimamia mali za marehemu Reginald Mengi.

Majibu ya waleta maombi
Waliofungua maombi ya usimamizi wa mirathi waliiambia mahakama kuwa wao wanaamini kuwa wosia unaobishaniwa ni halali, huku wakiiomba mahakama kutamka hivyo.

Katika hatua hii ya kesi, mahakama iliamua kuligeuza shauri na kulisikiliza kwa mfumo wa kesi kamili ya madai kwa mujibu wa kifungu cha 52 (b) cha Sheria ya Urithi na Usimamizi wa Mirathi.

Katika kesi hiyo, waleta maombi waliwakilishwa na wakili Elisa Abel Msuya, Regina Kiumba na Irene Mchau wakati waleta zuio waliwakilishwa na wakili mwandamizi, Nakazael Lukio Tenga na mawakili Roman Masumbuko, Hamis Mfinanga na Grayson Laizer.

Masuala kuamuliwa na mahakama
Baada ya kusikiliza hoja za awali za pande zote, mahakama pamoja na pande zote walikubaliana masuala manne ambayo mahakama itatakiwa iyaamue ili haki itendeke.

Suala la kwanza lililowekwa mbele ya mahakama kuamua lilikuwa ni kama wosia wa Dk Mengi wa Agosti 17, 2017 uliandaliwa kukiwa na sababu thabiti na halali.

Mahakama ilitakiwa pia kuamua kama wosia huo uliandaliwa kwa usahihi na kama mahakama iwakubalie waleta maombi au kutoa hati ya usimamizi wa mirathi kwa waleta zuio.

Pia ilitakiwa kuamua ni nafuu gani wa kisheria kila upande unastahili.

Mashahidi wa waleta maombi
Katika usikilizwaji wa kesi hiyo, waleta maombi walileta mashahidi wanne ambao ni Sylivia Novatus Mushi (Katibu wa kampuni za IPP), Florence Sawaya Msaki (katibu/msaidizi binafsi wa marehemu Mengi), Grace Delicia Maleto (mhudumu wa mapokezi) na Benson Benjamin Mengi aliyedai kuwa mpwa wa Mengi.

Mashahidi wa utetezi
Upande wa utetezi ulileta mashahidi watatu ambao ni watoto wa marehemu, Abdiel Alese Mengi na Regina Anchelita pamoja na kaka yake Mengi, Benjamin Abraham Mengi.

Pia mahakama kwa kutumia busara yake na nguvu ya kisheria iliyonayo iliamua kuita mashahidi wake ambao ni mke wa Mengi, Jacqueline Ntuyabaliwe pamona na aliyekuwa daktari wa Mengi, Valentina Ochieng Khoja kutoa ushahidi ili waisaidie mahakama kutenda haki.

Akitumia kesi ya John Magendo dhidi ya N.E. Govani, iliyowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufani kufafanua kwa nini mahakama iliamua kuita mashahidi wake, jaji aliyesikiliza shauri hilo, Yose Mlyambina alisema ili kufikia uamuzi wa haki, Sheria ya Mwenendo wa Madai inampa jaji au hakimu, si tu nguvu za kuita mashahidi anaoamini wataisaidia mahakama kutenda haki, bali ni lazima kwa wao kufanya hivyo, endapo itaonekana kufanya hivyo kutasaidia kufikia uamuzi wa haki.

Mahakama yapokea ushahidi
Shahidi wa kwanza wa waleta maombi, Sylivia Novatus Mushi aliieleza mahakama kuwa amekuwa akifanya kazi na marehemu tangu mwaka 2007 na kwamba, alikuwepo wakati marehemu Mengi akisaini wosia wake wa mwisho ambao ulimteua yeye pamoja na wengine kama wasimamizi wa mirathi.

Katika hali iliyoishangaza mahakama, Mushi aliongeza kuwa hakuwahi kujua kilichoandikwa kwenye wosia huo kwa kuwa haukusomwa kwao siku ulipoandikwa.

Aliendelea kueleza kuwa Oktoba 2016, marehemu alipatwa na tatizo la kiharusi, hali ambayo iliathiri uwezo wake wa kutembea na kufanya kazi.

Alidai hali hiyo pia iliathiri kumbukumbu zake hadi hatimaye kufikwa na mauti.

Si wosia wa kwanza kwa Mengi
Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa Mengi aliwahi pia kuandaa na kusaini wosia nyingine ambamo aligawanya mali zake zote kwa wote waliostahili kurithi, wakiwemo watoto wake Regina na Abdiel, wa mwisho ukiwa ule aliouandaa mwaka 2014.

Alidai kuwa wosia wa mwisho wa Mengi ulitayarishwa na Sabas Kiwango ambaye alitoa nyaraka za wosia huo kutoka kwenye kompyuta yake ya mkononi kwa kutumia diski mweko (flash disk) na kuzileta ofisini kwa marehemu kwa ajili ya kudurufiwa na baadaye alizisaini.

Sylivia aliendelea kuieleza mahakama kuwa baadhi ya mali zilizoorodheshwa katika wosia huo hazikumilikiwa na marehemu wala marehemu hakuwa na hisa katika kampuni hizo.

Akasema, kwa mfano, kampuni inayoitwa Tanzania Diamonds Limited, Tanzania Oil & Gas Limited na ile ya Oil & Gas Resources East Africa Limited hazikuwa zikifanya kazi kwa muda mrefu.

Alieleza pia kuwa baadhi ya kampuni zilizotajwa zilikuwa zilizomilikiwa na familia ambapo Abdiel na Regina walikuwa pia wakurugenzi.

Kwa upande wake, shahidi wa pili wa waleta maombi, Florence Sawaya Msaki naye alidai kuwa alishuhudia wosia huo wa Mengi.

Ushahidi wake haukutofautiana na ule wa shahidi wa kwanza, Sylivia kuwa hawakupewa fursa ya kujua kilichoandikwa ndani ya wosia ule mbali na kuitwa kama mashahidi. Shahidi wa tatu, Grace Delicia Maleto pia alieleza kushuhudia wosia huo na kuongeza kuwa hakuwahi kujua kilichoandikwa hadi mauti yalipomfika Dk Mengi.

Alisema hakujua hata kama marehemu aliwatoa kwenye urithi hata watoto aliowazaa. Hata hivyo, Grace alikiri wakati akihojiwa na wakili wa waleta zuio kuwa hakuna ndugu yeyote wa marehemu aliyekuwepo wala kushuhudia wakati wa kusainiwa kwa wosia ule, akiongeza kuwa marehemu alipatwa na ugonjwa wa kiharusi na kupoteza nguvu.

Shahidi wa mwisho wa waleta maombi alikuwa ni Benson Benjamin Mengi, aliyedai kuwa marehemu alikuwa baba yake mdogo na alikuwa na uhusiano naye mzuri. Benson alidai ndiye alimsaidi marehemu kumalizia uchapishwaji wa kitabu chake cha “I Can, I Must, I Will”.

Alidai kuwa marehemu hakuwa na afya nzuri tangu alipopatwa kiharusi Oktoba 2016 na kupelekwa nchini Afrika Kusini kwa matibabu.

Kwa mujibu wa Benson, watoto wakubwa wa marehemu walikuwa na ugumu kumtembelea baba yao kwa kuwa mke wake, Jacqueline aliwazuia kufanya hivyo.

Kesho tutaangalia watoto wa marehemu Mengi wakitoa ushahidi wao na kufafanua kwa nini wanapinga kutekelezwa kwa unaodaiwa kuwa wosia wa mwisho wa baba yao.

UPDATES

TUESDAY 25 MAY 2021

Baba alishawishiwa

Katika kulipa nguvu zuio walilofungua mahakamani, shahidi wa kwanza ambaye pia ni mtoto wa marehemu, Abdiel Mengi, alianza kwa kuwasilisha mahakamani cheti chake cha kuzaliwa ili kuthibitisha kwamba alikuwa mtoto wa marehemu mengi.

Abdiel alitoa maelezo mafupi kuhusu maisha ya baba na mama yake (mke wa kwanza wa Mengi ambaye pia amefariki) yalivyokuwa, akilenga kuishawishi mahakama iamini kuwa baba yao alikuwa katika uhusiano mzuri na familia yake na kwamba hakuwa katika hali ya kutoelewana na watoto wake.

Aliieleza mahakama kuwa baba yake alianza kuishi na vimada kabla hata ya kuachana na mama yake na kwamba hata wadogo zake wawili mapacha ambao aliwazaa na mke wake wa pili, Jacqueline, walizaliwa kabla hajaachana rasmi na mama yake.

Akasisitiza kuwa marehemu aliheshimu mila na desturi za Kichaga na alizikwa Machame, Kilimanjaro.

Kuhusiana na wosia, unaobishaniwa, Abdiel alisema baba yake aliandaa wosia ule wakati afya yake ikiwa imetetereka baada ya kupatwa na kiharusi Oktoba 2016, na tangu hapo hakuwahi kupata nafuu.

Mbali na matatizo ya kiafya, Abdiel alidai kuwa bahasha iliyokuwa imehifadhi wosia ulidaiwa kuandikwa na baba yao ilikuwa haikufungwa kwa rakili, hivyo kuacha uwezekano mkubwa wa kuchezewa.

“Wosia huo ulishuhudiwa na watu ambao hawakuwa ndugu wa marehemu na pia haukushuhudiwa hata na mke wa marehemu,” alidai shahidi huyo.

Aliongeza kwa wosia huo umezitoa kama urithi mali ambazo hazikuwa zikimilikiwa na marehemu, kwa mfano, mali alizochuma na kuzimiliki kwa pamoja na mke wake wa kwanza.

Abdiel alidai pia baba yake aliheshimu na kuishi maisha ya kimila kama inavyothibitishwa kwa kuwapa watoto wake majina ya Kichaga, na kuongeza kuwa ingawa baba yake alikuwa na ndoa ya Kikristu alikuwa na mahusiano ya waziwazi ya kimapenzi nje ya ndoa.

“Baba asingeweza kuandika wosia kama si kulazimishwa na mke wake wa pili kwa kuwa alikuwa na uwezo wa kupata ushauri wa wataalamu wengi wa sheria.Ni kwa sababu ya ugonjwa, ndio maana alifanya hivyo. Kama marehemu alikuwa na nia ya kutunyima mali zake angesema,” alidai shahidi huyo.

Ushahidi uliotolewa na shahidi wa pili Benjamin Mengi (kaka wa marehemu) na shahidi wa tatu Regina Mengi (mtoto wa marehemu) ulifanana kwa kiasi kikubwa na ule wa Abdiel, huku Benjamin akifunga ushahidi wake kwa kueleza nini atafanya endapo mahakama itamteua kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu.

Benjamin alisema endapo mahakama ingemteua kuwa msimamizi wa mirathi atahakikisha kuwa mjane na watoto wake wanapata mgao halali wanaostahili.

Pia aliahidi kuwaongoza watoto wakubwa wa marehemu pamoja na mama yao kwa kuwashauri kuwatunza watoto wadogo wa marehemu ambao wana miaka minane tu na kuwasaidia kukua kitaaluma na kimaadili.

Akaahidi pia kuhakikisha uhusiano mzuri kati ya watoto wakubwa wa marehemu na wale wadogo ili waishi pamoja kama familia moja ya Reginald Abraham Mengi. Mwisho aliahidi kuwaandaa kiakili wajue nao ni warithi wa mali za baba yao.

Ushahidi wa Jacqueline, daktari
Jacqueline na daktari wa Mengi, Valentina Ochieng Khoja hawakuwa sehemu ya maombi yaliyofunguliwa mahakamani lakini mahakama iliamua kuwaita kama mashahidi wake muhimu ili waisaidie kufikia uamuzi sahihi.

Jacqueline alianza kwa kuieleza mahakama kuwa uhusiano wake na Mengi ulianza mwaka 2011 na baadaye kufunga ndoa ya kiserikali mwaka 2015. Aliongeza kuwa alizaa watoto na marehemu kabla ya kufunga ndoa.

Katika ushahidi wake Jacqueline alisema mwake 2016 Mengi alipata tatizo la kiharusi cha muda mfupi (mini-stroke). Alitembea kwa maumivu lakini aliweza kuongea kawaida tu. Baadaye tulienda Dubai kwa ajili ya mapumziko na tukiwa huko Mengi alifanya uchunguzi wa afya yake na kugundulika alihitaji kuwekewa pacemaker (betri ya moyo) mwaka 2019,” alisema Ntuyabaliwe na kuongeza:

“Baada ya kuwekewa pacemaker alianza kupata maumivu ya kifua na baadaye alifariki dunia.”

Ntuyabaliwe aliuunga mkono wosia wa mume wake na uteuzi wa waleta maombi wanne kama wasimamizi wa mirathi ya mume wake kwa kuwa walitajwa kwenye wosia huku akipinga zuio lililowasilishwa mahakamani.

Kwa upande wake, daktari aliyekuwa akimtibu Mengi kwa zaidi ya mara kumi tangu 2015 hadi Desemba 2017, Valentina Khoja alidai kuwa mteja wake alikuwa na magonjwa matatu yaliyohitaji uangalizi wa daktari mbobezi.

Aliyetaja magonjwa hayo kuwa ni pamoja na shinikizo la damu, tezi dume pamoja na shinikizo la damu lililomsababishia kiharusi. Alidai kuwa Mengi alipatwa na kiharusi Oktoba, 2016.

“Marehemu alipatwa na kiharusi ambacho kiliathiri sehemu ya ubongo wake inayodhibiti mwenendo wa misuli,” alisema daktari huyo.

Aliongeza kuwa Mengi alikuwa pia akisumbuliwa na ugonjwa wa gauti lakini hakumbuki kama aliwahi kuwa na tatizo la kumbukumbu.

UPDATES

26 MAY 2021

Kikao cha ukoo kilivyokataa wosia wa mwisho wa Mengi (3)

Jana katika mapitio ya kesi ya mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa mmiliki wa kampuni za IPP, marehemu Reginald Mengi tuliona mmoja wa watoto wa tajiri huyo akiieleza mahakama kuwa hawakuwa tayari kuutambua wosia uliodaiwa kuandikwa na baba yao kwani ulikuwa wa kibaguzi kwa kuwatupa nje ya urithi watoto wake wakubwa na kumpatia mali zake zote mke wake wa pili, Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wake pacha.

Tuliona pia Ntuyabaliwe akiunga mkono wosia ulioandikwa na mume wake, huku akiiomba mahakama iwathibitishe watu wanne ambao mpenzi wake huyo aliwateua kuwa wasimamizi wa mirathi.

Watu aliodai waliteuliwa na Mengi kuwa wasimamizi wa mirathi – Benson Benjamin Mengi, William Onesmo Mushi, Zoeb Hassuji na Sylvia Novatus Mushi – walifungua maombi Mahakama Kuu wakitaka wosia uthibitishwe na wao watambuliwe kama wasimamizi.

Kufuatia maombi hayo, mtoto mmoja wa Mengi na Abdiel na kaka yake Mengi, Benjamin, walipeleka zuio la utekelezaji wa wosia huo hadi hapo hoja zao za kupinga zitakaposikilizwa na kuamuliwa.

Endelea ...

Baada ya kuwasikiliza mashahidi, mahakama iliwapa mawakili wa pande zote mbili kufanya majumuisho na ufafanuzi wa hoja zao.

Mawakili wa waleta maombi walijikita katika masuala makubwa mawili; uhalisi (validity) na usahihi (appropriateness) wa wosia wa Mengi.

Walianza kwa kujadili maana ya neno ‘validity’ kama lilivyotafsiriwa katika kamusi ya Black’s Law Dictionary ambayo kuwa ni ‘inayojitosheleza kisheria, inayofunga, na kwa upande mwingine, likimaanisha ‘sahihi’ au ‘inayojitosheleza’.

Pia walifanya marejeo katika kesi iliyowahi kuamuliwa na Mahakama ya Rufaani Tanzania kuhusu uhalali wa wosia katika kesi iliyofunguliwa na Mark Alexander Gaete na wengine wawili dhidi ya Grigitte Gaetje Defloor, ambapo mahakama ilitamka yafuatayo:-

Katika maombi ya kuthibitisha wosia mahakama hujikita katika kuthibitisha uhalali wa wosia. Maswali ambayo yatahitaji kujibiwa ni kama wosia ulisainiwa kwa usahihi ili uweze kutekelezwa kisheria; kama mtoa wosia alikuwa na uwezo wa kuandaa wosia; pale inapotokea mtoa wosia ana mapungufu au ulemavu fulani kama vile kipofu, kiziwi au kutojua kusoma wala kuandika (kama alijulishwa yaliyomo kwenye wosia au la na kadhalika na yeye akauridhia); kama kulikuwa na ushawishi usio halali au la; kama kulikuwa na kughushi au udanganPia waliangalia kama wosia huo ulikwishatenguliwa au la.

Kama wosia huo umekidhi vigezo vilivyotajwa hapo juu, basi wosia huo utachukuliwa kuwa umethibitishwa na mahakama itampa msimamizi wa mirathi nguvu/ruhusa ya kisheria kusimamia mirathi hiyo.

” Moja ya hoja walizotoa mtoto wa Mengi, Abdiel na kaka yake Mengi katika kutaka kusimamishwa utekelezwaji wa wosia wa tajiri huyo, ni kwamba wosia huo uliwatupa nje ya urithi watoto wakubwa wa marehemu bila kutoa sababu yoyote.

Wakili wa waleta maombi alipinga hoja hiyo kwa maelezo kuwa Gazeti la Serikali Namba 436 la mwaka 1963 chini ya jedwali la 3, sura ya 35 inatoa nafasi kwa watoto na wanufaika walionyimwa urithi kufungua maombi mahakamani ili iamue kama kubaguliwa kwao kulikuwa halali, jambo ambalo watoto wa Mengi hawakufanya.

Kuhusiana na wosia wa baba yao kuwa mikononi mwa mjane wa marehemu (Jacqueline) ambaye pia ni mnufaika, wakili wa waleta maombi alikiri kuwa wanufaika wa wosia wahatakiwi kuwa pia watunza wosia, akirejea kesi ya Shan Arshad Yusuf dhidi ya Zuberi Abdallah na wengine wawili.

Hata hivyo, alidai msimamo huo lazima utofautishwe na kesi iliyopo mbele yao kwa kuwa shahidi wao wa pili, mtunzaji nyaraka aliyeaminiwa, alitoa pia nakala ya wosia wa marehemu ambao ulilinganishwa na ule aliokuwa nao mjane na kuonekana kuwa sawa.

Aliongeza kuwa hoja kuwa wosia ule unaweza kuwa wa kughushi halikuthibitishwa kwa viwango vinavyotajwa katika vifungu vya 110 (1) (2) na 111 vya Sheria ya Ushahidi. Vifungu hivyo vinatamka kuwa mtu yeyote anayetaka mahakama iamini ukweli au jambo atalazimika kuthibitisha na si kuuachia upandemwingine wa kesi.

Kuhusu hoja kuwa afya ya akili ya marehemu alikuwa imetetereka (dementia) kutokana na umri na maradhi mengine wakati akiandika wosia, wakili wa waleta maombi alidai kuwa mtu sahihi kuthibitisha hilo ni Florence Msaki (katibu muhtasi wa Mengi) na Grace Maleto (mhudumu wa mapokezi wa IPP) ambao alidai walishuhudia wosia huo na kuusaini.

Sehemu ya mwisho upande wa waleta maombi ni kuhusu mashahidi waliosemekana kushuhudia wosia ule. Wakili wao alikubali kuwa wosia haukushuhudiwa sawasawa kwa kuwa mashahidi hawakuwa wanaukoo wa Mengi.

Akanukuu kanuni ya 19 ya Gazeti la Serikali Namba 436 la mwaka 1963 ambao jedwali la tatu la Sheria ya Tamko la Sheria za Kimila linalosema “wosia unaoandikwa hushuhudiwa na mashahidi wanaojua kusoma na kuandika, yaani mashahidi wasiopungua wawili, (mmoja wa ukoona mmoja mtu baki) ikiwa mwenye wosia anajua kuandika.

Endapo mwenye wosia hajui kusoma wala kuandika patatakiwa kuwe na mashahidi wanne (wawili wa ukoo na wawili wengine).

Alikiri wosia uliopo mahakamani haukuwa halali katika kipengele cha mashahidi waliousaini na si vinginevyo.

Watoto wa Mengi wajibu

Wakili wa waleta zuio alianza kwa kudai kuwa wosia unaodaiwa kuwa wa marehemu Mengi haukuwa halali kwa msingi kwamba mwenye wosia hakuwa na uwezo wa kuandika wosia na mashahidi pia hawakuwa na uweza wa kisheria kushuhudia na kusaini wosia ule.

Alidai pia wosia huo ulitoa kwa ajili ya urithi mali ambazo hazikumilikiwa na marehemu na kwamba marehemu alitupa nje watoto wake wa kuzaa katika wosia huo. Kuhusu uwezo wa marehemu kuandaa wosia, wakili huyo aliendelea kueleza kuwa mashahidi wanne walioletwa mahakamani walikuwepo wakati marehemu alipopatwa na kiharusi Oktoba, 2016 ambao uliathiri kumbukumbu yake na tangu wakati ule hakuwahi kupata nafuu hadi mauti yalipomfika.

Akanukuu Kanuni ya 7 ya jedwali la tatu la Sheria ya Tamko la Sheria za Kimila inayosema kuwa wosia hutenguliwa kama mwenye wosia atagundulika kuwa na tatizo la akili kwa sababu ya ugonjwa wa akili, ugonjwa na ulevi au hasira za ghafla, akirejea pia Sheria ya Urithi ya India, 1865 inayosema mtu yeyote mwenye akili timamu na si mtoto anaweza kugawa mali zake kwa kutumia wosia.

Kuhusu uwezo wa kisheria wa mashahidi wa wosia, wakili huyo aliikumbusha mahakama kuhusu ushahidi wa mashahidi walioshuhudia wosia ule—Florence Sawaya na Grace Maleta—ambao waliiambia mahakama kuwa hawakuwahi kuusoma wosia ule.

Aliongeza kuwa hata mkutano wa ukoo wa mengi uliukataa wosia ule kwa sababu mashahidi waliousaini hawakuwa ndugu wa damu wa marehemu kama sheria inavyotamka.

Zaidi ya hapo, alidai mke wa marehemu hakuwepo wakati wa kusainiwa kwa wosia ule, akirejea kesi ya Jackkson Reuben Maro dhidi ya Halima Shekigenda na ile ya Jackson Reuben Maro dhidi ya Hubert Sebastian ambapo Mahakama ya Rufani Tanzania ilitengua wosia kwa kuwa mke wa marehemu hakuwepo wakati wosia ule ukiandaliwa.

Akifafanua kuhusu suala la marehemu kutoa urithi wa mali ambazo hakuzimiliki, wakili huyo alidai kuwa wosia wa marehemu ulihusisha mali ambazo hakuzimiliki kinyume na Kanuni ya I ya Jedwali la 3 la Local Customary Law (Declaration)

Namba 4. Kanuni hiyo imeweka wazi kuwa mwenye wosia haruhusiwi kurithisha mali asizomiliki. Aliongeza kuwa wosia wa Mengi ulihusisha mali ambazo zilikuwa chini ya mgawanyo katika kesi ya marehemu Mengi na mke wake wa kwanza, Mercy Anna Mengi, kitu ambacho marehemu alikijua.

Akihitimisha, wakili huyo alidai kuwa wosia huo uliwaweka kando watoto wa marehemu bila sababu, huku akinukuu Kanuni ya 38 ya Jedwali la 3 la Local Customary law (Declaration) (Namba 4) inayosema “kama itaonekana mtu amenyimwa urithi katika wosia pasipokuwa na sababu ya haki, wosia unavujwa na urithi utagawanywa kufuata mpango wa urithi usio wa wosia.

Aliongeza kuwa marehemu aliwanyima watoto aliozaa na mke wake wa kwanza, Abdiel na Regina, haki yao ya kurithi bila kutoa sababu yoyote. Wakili huyo akaendelea kueleza kuwa wosia unadaiwa kuandikwa na Mengi ulitokana na ushawishi usio halali (undue influence).

Hapa aliitaka mahakama kuzingatia mahusiana ya siri ambayo hutengeneza ushawishi kati ya mnufaika na mwenye wosia, kwa mfano, katika mazingira ambapo mwenye wosia anaumwa na anamtegemea mnufaika kwa uangalizi, matibabu au mahitaji mengine muhimu ya maisha.

Akadai pia kuwa hata mke wa Mengi, Ntuyabaliwe pia alijua kuhusu suala wa watoto wengine wa Mengi kuwekwa pembeni katika urithi.

Akasema hata Ntuyabaliwe alikiri kuwa siku ya kwanza walipowasili na mwili wa marehemu kutoka Dubai alifungua sefu ambamo wosia ulikuwa umehifadhiwa na kuuweka katika sefu nyingine katika chumba chake.

Kesho tutaangalia mahakama ikichambua mfumo wa maisha ya Mengi ili kupata sheria sahihi itakayotumika kufikia hukumu.

UPDATES

27 MAY 2021

Mahakama yachambua mfumo wa maisha ya Mengi ikiamua mirathi

Katika kesi ya mirathi ya mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, jana tuliona jinsi kikao cha ukoo kilivyokataa kutambua wosia wa mwisho wa tajiri huyo kwa madai kwamba hakuna mwanafamilia aliyeushuhudia.

Katika kesi hiyo watu wanne walifungua maombi ya kutaka Mahakama iwathibitisha kuwa wasimamizi wa mirathi kupitia wosia ambao Mengi alimrithisha mali zake zote mke wake wa pili, Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wake pacha.

Kufuatia maombi hayo, watoto wa marehemu waliweka zuio la mchakato huo hadi mahakama itakapowasikiliza na kuamua mapingamizi yao. Endelea…

Baada ya kupitia ushahidi na majumuisho ya mawakili wa pande zote, mahakama ilifanya uchambuzi wa ushahidi na kutoa msimamo wake katika kila hoja iliyoletwa mbele yake.

Katika utaratibu wa sheria, kabla ya kuamua shauri la wosia unaogombaniwa, mahakama huanza kwa kuchagua sheria itakayoitumia kuamua kesi ya mirathi husika kabla ya kuamua kuhusu uhalali wa wosia na mambo mengine yanayohusu usimamizi wa mirathi ya marehemu.

Nchini Tanzania kuna sheria tatu zinazoongoza masuala ya mirathi na usimamizi wa mirathi – Sheria Bunge (Statutory Law), Sheria za Kimila (Customary Law) na Sheria za Kiislamu (Islamic Law).

Uchaguzi wa sheria itakayotumika kuamua shauri la wosia unaobishaniwa, huja baada ya Mahakama kuchambua mfumo wa maisha ya mwenye wosia na kujiridhisha aina ya mfumo uliotawala zaidi maisha yake.

Kama aliishi kwa kufuata mwongozo wa dini ya Kiislamu, basi Mahakama hutumia Sheria ya Kiislamu kuamua shauri lake la mirathi pindi anakapofariki na ukatokea mvutano katika mirathi yake.

Sheria Bunge (Statutory Law) ambayo kwa Tanzania hutumiwa Indian Succession Act au Sheria ya Mirathi ya Serikali, hutumika kwa Wakristu na watu wengine wote ambao hawaongozwi na Sheria ya Kiislamu au ya Kimila, ambayo hutumika kwa watu walioishi zaidi kwa kufuata mila, desturi na tamaduni za kabila au jamii yao.

Mahakama zimeandaa vigezo vya kuamua chaguo sahihi la sheria itakayotumika kuamua kuhusu wosia au usimamizi wa mirathi wenye mgogoro.

Kigezo cha kwanza ni kuchambua mfumo wa maisha (Mode of Life) ya marehemu na cha pili ni kujua nia ya kuandika wosia (Intention of Test—pale mtu anapoacha wosia, anapofanya matamko ya maandishi au ya mdomo kuhusu usimamizi wa mali zake wakati akiwa hai).

Mahakama huzingatia ushahidi ulioletwa mahakamani na pande zote mbili kupata majibu ya vigezovyote viwili na hatimaye huamua ni sheria ipi itumike katika usimamizi wa mirathi ya marehemu.

Maisha ya sura mbili Katika kesi ya mirathi ya Mengi, Mahakama ilichagua kuongozwa na kipimo cha mfumo wa maisha aliyoishi marehemu ili kujua sheria ipi ingefaa kuamua suala la usimamizi wa mirathi yake.

Jaji Yose Mlyambina aliyesikiliza kesi hiyo alisema uamuzi wa sheria ipi iongoze suala hilo unaweza kujulikana kutoka kwenye aina au mfumo wa maisha ya marehemu.

Alisema ushahidi uliotolewamahakamani ulionyesha wazi kwamba maisha ya marehemu Mengi yalikuwa na sura mbili.

“Kwa kiasi fulani yalikuwa katika mfumo wa kimila na kiasi fulani katika mfumo wa maisha ya kisasa, vyote katika kiwango kinacholingana. “Hii inamaanisha kuwa Sheria ya Kimila au Sheria Bunge inaweza kutumika katika mirathi ya marehemu Mengi,” alisema Jaji Mlyambina.

Hata hivyo, sheria zote mbili haziwezi kutumika kwa kuwa sheria zilizopo na maamuzi ya Mahakama yaliyowahi kutolewa siku za nyuma vinataka sheria moja tu itumike katika kuamua mgogoro waJaji Mlyambina anakiri kuwa Mahakama ilikabiliwa na ugumu wa kipekee pale ilipothibitika kuwa Mengi aliishi, aliheshimu na kutekeleza kwa vitendo mila na desturi za Kichaga kwa kiwango karibu sawa na jinsi alivyoishi, kuheshimu na kutekeleza kwa vitendo maisha ya kisasa kama Mkristo.

Katika hatua hiyo jaji anasema Mahakama hupima ni mfumo upi kati ya ule wa maisha ya kimila na wa maisha ya kisasa ulitawala zaidi maisha ya marehemu. Mahakama inaporidhika kuwa mfumo wa maisha ya kimila ulitawala zaidi mfumo wa maisha ya marehemu, hutamka kuwa sheria ya kimila ndiyo itakayotumika katika mirathi ya marehemu.

Pale inaporidhika kuwa mfumo wa maisha ya kisasa ulitawala sehemu kubwa ya maisha wa marehemu, mahakama itatamka kuwa Sheria Bunge itumike. Mahakama ilisema kwa mujibu wa shahidi wa kwanza, Sylvia Mushi (katibu wa kampuni ya IPP) pamo[1]ja na mtoto wa Mengi, Abdiel na kaka yake, Benjamin, marehemu aliheshimu na kutekeleza mila, des[1]turi na utamaduni wa Kichaga kama sehemu muhimu ya maisha yake sambamba na mfumo wa maisha ya kisasa wakati wa uhai wake.

Kwa mujibu wa ushahidi wao, marehemu Mengi alikuwa mwe[1]nyekiti wa ukoo wa Mengi; aliwapa watoto wake wote majina ya Kichaga; kama walivyo Wachaga wengine, pia alitembelea sehemu za wazee huko Machame, Kilimanjaro kila Desemba.

Pia eneo la makaburi ya ukoo wake yalikuwa Machame na alizikwa kati[1]ka makaburi hayo na kwamba tarati[1]bu za Kikristu na za kimila zilifuatwa katika mazishi yake.

Ingawa pia alifunga ndoa ya Kikris[1]tu na mke wake wa kwanza, tamadu[1]ni na mila za Kichaga zilifuatwa na kuheshimiwa.

Ushahidi ulionyesha pia kuwa Mengi alitembelea mara kwa mara maeneo ya mababu zake Machame na alijenga nyumba yake huko. Ushahidi unaeleza kuwa Men[1]gi alizaliwa na kukulia Machame na alishiriki katika kanuni zote za Kichaga, zikiwemo kuchinja ndafu na kusimika mkuu wa familia, maarufu kama ‘kuvisha koti.’

Kutokana na ushahidi huo, Jaji Mlyambina akahitimisha kuwa kuto[1]kana ushahidi ulioletwa mbele yake, hakukuwa na shaka kuwa Mengi ali[1]tekeleza mila, desturi na utamaduni wa Kichaga kama sehemu muhimu ya maisha yake.

Akaongeza kwamba mfumo wa maisha ya kisasa uliendelea kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa mai[1]sha ya marehemu Mengi. “Mengi alikuwa mtu aliyependa mfumo wa maisha ya kisasa (mor[1]denist),” alisema.

Mahakama ilisema hilo liliungwa mkono na ushahidi kuwa alifunga ndoa ya Kikristu na mke wake wa kwanza na pia alifunga ndoa ya Kiserikali na mke wake wa pili mwa[1]ka 2015 katika Wilaya ya Kinondoni na baadaye alikwenda Mauritius kufanya sherehe ya harusi.

Pia aliwabatiza watoto wake kwa kuwapa majina ya Kikristo na alitu[1]mia sehemu kubwa ya maisha yake ya utu uzima jijini Dar es Salaam ambalo ndilo kitovu cha maisha ya kisasa kuliko nyumbani kwa mababu zake Machame.

Hoja nyingine ni kuwa taratibu za Kikristu zilifuatwa wakati wa mazishi yake na alikuwa akifanya uchunguzi wa afya yake Uingereza, Afrika Kusini na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Pia kwa asili ya shughuli zake kama mmoja wa wafanyabiashara tajiri Tanzania na mwenyekiti wa kam[1]puni za IPP, haikuwa rahisi kwake kukwepa kabisa maisha ya kisasa. Uamuzi wa Mahakama Jaji Mlyambina alisema japokuwa, kwa ukadiriaji wa Mahakama, Mengi aliishi mfumo wa maisha mchang[1]anyiko (hybrid mode of life), ilion[1]ekana kuwa mfumo wa maisha ya kisasa ulitawala zaidi mfumo wake wa maisha, hivyo Mahakama iliamua kutumia sheria inayofaa kulingana na mfumo wa maisha wa marehemu.

“Kwa kuwa ni hitimisho la mahaka[1]ma hii kuwa mfumo wa maisha ya kisasa ulitawala mfumo wa maisha ya Dk Reginald Abraham Mengi kuliko mfumo wa maisha ya kimila, mahakama hii inatamka kuwa She[1]ria ya Bunge ndiyo itakayotumika katika kuamua shauri la usimamizi wa mirathi ya marehemu Reginald Mengi, ikiwemo kuamua uhalali wa wasia wake wa mwisho,” alisema Jaji Mlyambina.

Baada ya hapo Mahakama ilijikita katika kuamua kama wosia wa mare[1]hemu Mengi aliouandika Agosti 17, 2017 Dar es Salaam uliandikwa kiha[1]lali na kama wosia huo uliodaiwa kuandikwa Agosti 17, 2017 na Mengi ulikuwa kwa usahihi.

=======
UPDATES

28 MAY 2021

Mahakama yahitimisha wosia wa Mengi haukuwa halali

FRIDAY MAY 28 2021

Katika toleo la jana kwenye mapitio ya kesi ya mirathi ya mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa mmiliki wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, tuliona jinsi mahakama ilivyochambua mfumo wa maisha ya tajiri huyo ili kuamua sheria ipi kati ya sheria tatu zinazotumika kuamua uhalali wa wosia au mgogoro wa mirathi—Sheria Bunge, Sheria ya Kimila na Sheria ya Kiislamu na ilivyoamua itumike Sheria ya Bunge.

Katika toleo la jana kwenye mapitio ya kesi ya mirathi ya mfanyabiashara maarufu na aliyekuwa mmiliki wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, tuliona jinsi mahakama ilivyochambua mfumo wa maisha ya tajiri huyo ili kuamua sheria ipi kati ya sheria tatu zinazotumika kuamua uhalali wa wosia au mgogoro wa mirathi—Sheria Bunge, Sheria ya Kimila na Sheria ya Kiislamu na ilivyoamua itumike Sheria ya Bunge.

Katika kesi hiyo, mtoto mmoja wa marehemu, Abdiel Mengi na kaka wa marehemu, Benjamin Mengi, walikuwa wakipinga maombi yaliyofunguliwa Mahakama Kuu na watu wanne waliotaka kuthibitishwa kuwa wasimamizi wa mirathi ya bilionea huyo.

Katika sehemu hii ya mwisho tunaona mahakama ikichambua uhalali wa wosia wa marehemu na jinsi ilivyotoa hitimisho. Endelea…

Baada ya kuamua sheria inayostahili kutumika kuamua mirathi yake, mahakama ilijielekeza katika suala kuu la kesi hiyo, yaani kuamua endapo wosia ulioandikwa na Mengi Agosti 17, 2017 Dar es Salaam, uliandikwa kihalali; na iwapo uliandaliwa kwa usahihi.

Katika uchambuzi huo, Jaji Yose Mlyambina alianza kwa kueleza maana ya neno wosia kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 2 (1) cha Sheria ya Mirathi ya usimamizi wa mali za marehemu.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa wosia ni ‘tamko la kisheria linalotolewa na mwenye wosia kuhusiana na mali zake, ambalo angependa litekelezwe baada ya kifo chake.’ Kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi wa kwanza wa waleta maombi, Sylvia Mushi (katibu wa kampuni za IPP), wosia wa Mengi uliandaliwa na Wakili Sabas Kiwango na utiaji saini ulishuhudiwa na watu wawili; Florence Sawaya (katibu binafsi wa Mengi) na Grace Maleto (mhudumu wa mapokezi wa ofisi za IPP).

Ushahidi unaonyesha pia kuwa baada ya kusainiwa, wosia huo ulitunzwa na Florence Msaki, aliyekuwa shahidi wa pili wa waleta maombi. Msaki alidai kuwa baada ya kupokea wosia huo aliutunza katika sefu iliyokuwa katika ofisi za IPP hadi Juni 22, 2019 pale wosia huo uliposomwa katika kikao cha familia ya Mengi.

Mahakama iliupokea wosia huo pamoja na mihtasari ya vikao viwili vya familia (cha Mei 11, 2019 na Juni 22, 2019) kama vielelezo.

Wosia huo unaonyesha kuwa Mengi alimrithisha mali zake zote mke wake wa pili, Jacqueline Ntuyabaliwe na watoto wake pacha–Jayden Kihoza Mengi na Ryan Saashisha Mengi – na kuwaweka kando watoto wake wakubwa wawili aliozaa na mke wake wa kwanza, Mercy Anna Mengi ambaye walitengana.

Mercy alifariki dunia Novemba 2018. Wosia huo haukueleza kwa nini Mengi aliamua kuwatupa nje ya mirathi watoto wake hao ambao hawakupewa haki ya kusikilizwa.

Uchambuzi wa mahakama
Kabla ya kuamua kuhusu uhalali wa wosia wa Mengi, mahakama ilijikita katika kujua uwezo wa kiakili wa marehemu wakati akiandika wosia unaobishaniwa.

Watoto wa Mengi waliopeleka zuio la kutekelezwa kwa wosia wa baba yao, walidai kuwa baba yao alikwishapoteza uwezo wa kuandika wosia halali kwa kuwa afya yake ya mwili na kiakili ilikuwa imetetereka baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi.

Kisheria, mtu anachukuliwa kuwa na uwezo mzuri wa akili timamu kama anaelewa jambo analolifanya na matokeo yake kisheria. Katika kufafanua zaidi, Mahakama ilirejea uamuzi wa kesi ya Leah Ntambula dhidi ya Francis Wenceslaus Ntambula na mwenzake ambapo iliweka wazi kuwa ni muhimu mtoa wosia aelewe maana ya jambo analofanya na matokeo yake kisheria.

Katika kesi hiyo, mahakama iliendelea kueleza kuwa mwenye wosia lazima aelewe ukubwa wa mali anazorithisha na kwamba asiwe na tatizo la kiakili ambalo linaweza kuathiri hisia ya kujua jambo lililo sawa na lisilo sawa au matamanio yake.

Pia Jaji alieleza kuwa urithishaji wa mali unatakiwa usitokane na ushawishi haramu utakaomfanya mtoa wosia mwenye uwezo hafifu wa kiakili kugawa mali zake tofauti na kama angekuwa na akili timamu.

Wosia si halali
Baada ya uchambuzi huo, mahakama ilihitimisha kuwa Mengi alipoteza vigezo vya uwezo wa kuandika wosia.

“Katika kesi iliyo mbele yetu, mahakama inaona na inatamka kwamba wosia wa marehemu (Mengi) si halali kisheria kwa sababu umeshindwa kukidhi vigezo vinne kuhusu uwezo wa marehemu kuandika wosia,” alisema Jaji Mlyambina.

Mengi alivyopoteza uwezo
Mahakama ilisema kuwa kulikuwa na ushahidi wa kutosha kutoka kwa Sylivia, Abdiel, Benjamin, Jacqueline na daktari wa Mengi, Valentina, kwamba marehemu alipatwa na kiharusi tangu Oktoba 2016 na hakupata nafuu hadi mauti ilipomfika.

“Hii ina maana kuwa uwezo wake wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi uliathirika na kumfanya asiweze kuelezwa maana ya uamuzi sahihi wa usimamizi wa mirathi yake,” ilisema mahakama.

Pia mahakama iliridhika kuwa wosia wa Mengi ulirithisha hata mali ambazo hakuwa akizimiliki kisheria, ikisema kuwa ikiwa ni yeye aliyerithisha mali hizo, basi hakuwa na uwezo wa kuelewa mipaka ya mali zake kwa kuwa uwezo wake wa kiakili haukuwa sawa.

Ikasema kuwa mashahidi katika wosia huo hawakuwa wataalamu katika masuala ya afya ili kuweza kuthibitisha utimamu wa akili ya marehemu. “Hakukuwa na sababu zilizotolewa kuwanyima urithi watoto wake wakubwa.

Hiki ni kielelezo kuwa mwenye wosia aliathirika kiakili kiasi kwamba hakuweza kujua watoto wake halali na kuwanyima urithi makusudi,” ilisema mahakama.

Jaji akaongeza kuwa mashahidi wa wosia ule akiwemo Sylvia (katibu wa kampuni za IPP Media) walikuwa wanajua kusoma na kuandika lakini hawakupewa nafasi ya kusoma yaliyomo katika wosia.

“Mbaya zaidi, usafi wa wosia huo unatia shaka kwa msingi kwamba mke wa marehemu, Ntuyabaliwe alikuwa ndiye mtunzaji wa wosia ule wakati akiwa mmoja wa wanufaika wakuu.

“Mahakama hii inaona wosia huu si halali chini ya kanuni ya ‘uhuru usio kamili wa mwenye wosia kugawa mali zake kwa kigezo cha kuwatupa nje ya urithi watoto halali,” ilisema mahakama.

Angalizo muhimu
Jaji aliendelea kutoa angalizo kuwa inapaswa kujulikana kuwa kifungu cha 46 Sheria ya Mirathi ya Serikali (Indian Succession Act, 1865) kinasema kila mtu mwenye akili timamu na umri wa kutosha ana haki ya kugawa mali zake kupitia wosia wake wa mwisho.

Hakuna kifungu kingine chochote cha sheria hiyo au sheria nyingine zozote zilizoweka mipaka au kulazimisha mtoa wosia kurithisha mali zake kwa watu anaohusiana nao kwa damu, kwa ndoa au kuasili kama vile mke, watoto wa kiume na kike au ndugu yeyote isipokuwa kifungu cha 36 cha Sheria ya Mtoto inayotoa wajibu kwa wazazi kurithisha watoto waliozaliwa nje ya ndoa.

“Hata hivyo, kukosekana kwa kifungu cha sheria katika Sheria ya Mirathi ya Serikali ambayo inampa mtoa urithi haki ya kuwanyima urithi ndugu au wanafamilia yake, hakumnyang’anyi haki ya kuwanyima urithi chini ya mfumo wa sheria za kawaida (common law system) kwa sababu tu mahakama za Tanzania zinatakiwa kutoa haki na kutafsiri sheria kulingana na matakwa ya mfumo wa kawaida wa sheria,” alisema Jaji Mlyambina.

Waleta zuio
washinda Baada ya uchambuzi wa hoja zote na kuharamisha wosia wa Mengi, mahakama iliwateua waleta zuio la mchakato wa wosia wa Mengi—Abdiel Mengi na Benjamin Mengi kuwa wasimamizi wenza wa mirathi ya Mengi.

Ikawaarifu pia wajibu wao, ukiwemo wa kupeleka mahakamani orodha ya mali za marehemu ndani miezi sita.


Mwisho....
 

Gentleman96

JF-Expert Member
Mar 12, 2019
884
1,000
Swali la muhimu ni
1. Je Jackline kweli alitaka huo wosia ufatwe 100 % yaani yeye na mapacha wake wachukue Mali zote bila huruma?

2. Jackline kweli anataka watoto wa Mengi wapewe hizo buku buku kama wosia unavotaka?

3. Ongezeni maswali hadi mahakimu wa JamiiForums washtuke
 

mdudu

JF-Expert Member
Feb 6, 2014
5,060
2,000
Swali la muhimu ni
1. Je Jackline kweli alitaka huo wosia ufatwe 100 % yaani yeye na mapacha wake wachukue Mali zote bila huruma?...
4. Je hao mashahidi hawakusaini hiyo mirathi ili kuupa nguvu huo wosia?

5. Je Jackline hajui kuwa Mengi hakuwa anamiliki mali moja kwa moja, bali alikuwa mwana hisa na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP?

6. Je Jackline Kama alikuwa na nia njema, kwa akili ya kawaida alishindwa kumshauri marehemu kuwa lazima wawepo wanafamilia wa upande wa marehemu ili washuhudie wosia huo?

7. Je Jackline hajui kuwa kughushi wosia na sahihi ni kosa na anasitahili kushitakiwa?

Tuendelee kumuuliza maswahi huyu mjane.
 

Emiir

JF-Expert Member
Dec 15, 2013
26,209
2,000
4.Je hao mashahidi hawakusaini hiyo mirathi ili kuupa nguvu huo wosia?

5. Je Jackline hajui kuwa Mengi hakuwa anamiliki mali moja kwa moja,bali alikuwa mwana hisa na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP?...
8. Je kama Dkt Mengi alipatwa na Kiharusi 2016 huo wosia aliusaini vipi au aliweka dole gumba?
9. Na je kama aliweka dole gumba alama zilizomo zinashabihiana na alama sahihi za Dkt Mengi?
 

Bufa

JF-Expert Member
Mar 31, 2012
6,742
2,000
Ukioa muombe Mungu akupe mke Mwenye either aibu au huruma.

Awe pisi kali tu akili tutatumia zangu.

Unaweza kuoa mcharuko na mali zikabaki mikono salama, hapa tatizo ni moja tu mzee Mengi alichelewa kuandaa mirathi na inaonekana aliandaa kienyeji too many loopholes, natilia mashaka uwezo wa wanasheria wake kwa mtu wa hadhi yake.

Mirathi ingeandaliwa mapema na wanasheria nguli ingekua vile ambavyo mwenye mali anataka iwe. Kama angetaka watoto wake wakubwa wasilambe kitu hakika wasingepata kitu kama tu angeandaa mapema.

Kwa hali ilivyo sasa Jack ajiandae maana there's no way akashinda hapo hata akikata rufaa.
 

mpuko

JF-Expert Member
Dec 21, 2013
662
1,000
8. Je kama Dkt Mengi alipatwa na Kiharusi 2016 huo wosia aliusaini vipi au aliweka dole gumba?
9. Na je kama aliweka dole gumba alama zilizomo zinashabihiana na alama sahihi za Dkt Mengi?
10. Na kama aliweka dole gumba na alama za dole ni zake, aliweka kwa msaada wa nani wakati tayari alikuwa na kiharusi? Je, halikuwa shinikizo la hao wanaodai ndio wasimamizi wa mirathi?

Sent from my S20 Ultra using JamiiForums mobile app
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom