MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imewaachia huru washitakiwa 31 kati ya 36 waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kuvua samaki bila kibali katika Bahari ya Hindi, eneo la Tanzania. Washitakiwa watano, kapteni wa meli Hsu Chin Tai (61), wahandisi wa meli ya Tawariq 1, Cai Dong Li (44) na Chen Rui Hai (34) na mawakala Zhao Hanquing (39) na Hsui Sheng Pao (55), wameonekana wana kesi ya kujibu. Mahakama pia imeamuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuwarudishia hati za kusafiria na kuwaandalia utaratibu wa kuwarudisha makwao washitakiwa walioachiwa huru. Imeamuru Jackson Toya (39), ambaye hana hati ya kusafiria arudishwe nchini Kenya.
Jaji Augustine Mwarija alitoa uamuzi huo jana, na kupokewa kwa hisia tofauti na wahusika, baadhi wakitokwa machozi ya furaha, wengine wakikumbatiana na hata kuzungumza Kiswahili, kwamba wamechoka kuishi Tanzania, hivyo ni bora warudi kwao. Mmoja wa washitakiwa hao raia wa Vietnam, alisema kukaa kwake gerezani kumemwezesha kujifunza Kiswahili, jambo lililomwezesha kupata marafiki wa Kitanzania, waliokwenda kumjulia hali gerezani na kumpatia chakula.
Kesi hiyo awali ilikuwa ikiwakabili washitakiwa 37 kutoka mataifa mbalimbali, ambao Juma Juma, raia wa Kenya aliyefariki dunia wakati kesi ikiendelea kusikilizwa. Walikuwa wakidaiwa Machi 8, mwaka 2009, saa 6.00 usiku, katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ndani ya eneo la Tanzania, walikamatwa wakivua bila kibali. Jaji Mwarija akitoa uamuzi jana, alisema, amewaachia huru washitakiwa hao kwa kuwa hati ya mashitaka haielezi bayana ni washitakiwa gani walikuwa wakivua samaki, kwani wengine walikuwa wapishi na walikuwa wanatimiza majukumu yao ya kazi. Alisema kapteni alikuwa msimamizi mkuu wa meli hiyo, hivyo pamoja na wenzake wanne wana kesi ya kujibu, hivyo watatakiwa kujitetea katika kikao kijacho cha mahakama.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, mawakili wa washitakiwa hao, Ibrahimu Bendera na John Mapinduzi, waliiomba mahakama iwapatie hati za kusafiria ili waweze kurudi kwao, kwani zilitolewa mahakamani kama vielelezo. Wakili wa Serikali, Biswalo Mganga, alidai vyombo vinavyohusika ni lazima vifanye utaratibu ili waweze kuondoka na kurudi kwao. Washitakiwa hao kutoka China, Indonesia, Kenya, Vietnam na Philippines, Machi 10, mwaka huu, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu walikosomewa mashitaka, kabla ya kesi kuhamishiwa Mahakama Kuu.
Uhuru