Waufukweni
JF-Expert Member
- May 16, 2024
- 4,393
- 14,500
Kesi ya Uhaini namba 19605/2025 inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo 'CHADEMA' Tundu Antiphas Lissu inatarajiwa kuendelea leo Febriari 9, 2026 Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es salaam.
Kupitia taarifa Rasmi iliyotolewa na CHADEMA jumapili jioni Februari 08, 2026 imeeleza "Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, inayojulikana kama Criminal Session Case No. 19605/2025, imepangwa kuendelea kusikilizwa kuanzia kesho, tarehe 09 Februari 2026, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam."
"Mahakama imepanga kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo kwa mfululizo kuanzia tarehe 09 Februari 2026 hadi tarehe 06 Machi 2026. Kesi hi inasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, ambao ni: Mheshimiwa Jaji D. Ndunguru, Mheshimiwa Jaji J. Karayemaha, na Mheshimiwa Jaji Kiwonde."
"Kwa sasa, ipo katika hatua ya usikilizwaji wa mashahidi wa upande wa Jamhuri, ambapo ushahidi unaendelea kutolewa kwa kina na kwa mujibu wa taratibu za kisheria, Chama kinatoa wito kwa wanachama, wafuasi, wananchi wote, na Jumuiya ya Kimataifa kufuatilia mwenendo wa kesi hii. Kesi hii ni taswira muhimu ya demokrasia na haki nchini Tanzania."
Zaidi >
Fuatilia mwenendo wa Kesi hii hapa;
Ukumbi wa Mahakama tayari umejaa, sasa anasubiriwa Mhe. Lissu na Majaji waingie ili kesi iweze kuanza.
Furaha na kelele za shangwe zimeibuka katika chumba cha Mahakama wakati Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu alipoingia ndani ya chumba hicho kwa ajili ya kufuatilia na kusikiliza shauri la Uhaini linalomkabili ambapo leo ushahidi unaendelea kutolewa huku akijitetea peke yake.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara John Heche alivyoingia kwenye chumba hicho cha Mahakama.
Kada wa ACT Wazalendo na mbunge wa zamani wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara (Bwege), pamoja na mwanasiasa mkongwe na kada wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini, ni miongoni mwa watu waliofika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, leo kufuatilia kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.
UTANGULIZI KUHUSU KESI YA LISSU
Leo ni Februari 9, 2026 tunaendelea na Kesi ya Uhaini Na. 19605 inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Taifa itaendelea Katika Mahakama kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dar es salaam.
Kama mnakumbuka vizuri tuliishia shahidi Na. 4 ambae ni P11 yaani shahidi wa siri.
Alivyoingia Mahakamani Novemba 11, 2025 shahidi huyu wa siri hakuonekana kokote hata kwa Majaji ndio Mheshimiwa Lissu akaweka pingamizi kuhusu kibox kilivyowekwa na namna ambavyo sheria inahitaji shahidi wa siri kutoa ushahidi wake.
Lakini pia katika pingamizi lake alielezea kuhusu kanuni za ulinzi wa mashahidi zinataka lazima shahidi wa siri atajwe na amri husika iliyoamua kuwa shahidi huyo awe wa siri lakini katika amri iliyopo mahakamani shahidi huyu hakuna mahali ametajwa kuwa anapaswa kuwa wa siri.
Baada ya pingamizi hilo kesi iliahirishwa na zoezi litakaloendelea leo ni upande wa Jamhuri kujibu hoja za Mh. Tundu Lissu kuhusu uhalali huu wa shahidi huyu wa siri.
Baada ya Mawakili wa Serikali kujibu hoja hizo zoezi litakalofuata ni Mheshimiwa Lissu kutoa hoja za nyongeza (rejoinder) kwa pingamizi lake na baadae Mahakama itatoa uamuzi wa uhalali wa Shahidi huyo wa 4 ambae ni P11.
Hapo ndipo tulipoishia na leo tutaendelea hapo.
Kwa kifupi hali ya Mahakama iko sawa wafuatiliaji kwa maana ya Wanachama wapo wakutosha.
Mawakili wa Pande zote mbili wameshafika na maandalizi ya mwisho mwisho yanaendelea hapa so tujiandae kuendelea kula Darasa huru la sheria kutoka kwa Mwalimu wa umma wa Sheria ambae ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Mhe. Tundu Antipas Lissu.
SEHEMU YA 151.
Ameingia Mheshimiwa Lissu, zimepigwa kelele nyingi sana hapa Mahakamani ni kelele za Rais! Rais! Rais!
Mhe. Lissu amepiga kombati ya kaki, ameingia kwa vibe sana.
Amebeba makabrasha yake, mavifurushi mengi sana ya vitabu.
Imepigwa sauti ya Courttttt ikiwa na ukali watu hawanyamazi wanaendelea na minong'ono fulani ya kushangilia.
Wameingia Majaji na kuketi eneo lao.
Jaji anasema tuendelee
Karani anasoma namba ya shauri.
Anasimama Renatus Mkude wakili wa Serikali Mkuu, yuko na Ajuaye, Nasoro Katuga, Cathbert Mbiringe, Thawabu Issa wanawakilisha upande wa Jamhuri na Mshitakiwa Tundu Lissu yupo.
Leo tumekuja kujibu hoja za Tundu Lissu kama yeye atakuwa tayari, sisi upande wa Serikali tuko tayari Waheshimiwa Majaji.
Mhe. Lissu anaulizwa uko tayari?
Anasema niko tayari lakini nahitaji kuzungumza mambo yaingie kwenye rekodi za Mahakama.
Niwatakie heri ya Mwaka Mpya nyie Majaji, Mawakili wa Serikali na wote waliopo hapo.
Maswala mawili kati ya matatu ninayotaka kuzungumza nitasema kwasababu kifungu cha 11(1)(2) cha sheria ya magereza nyie majaji ni visiting justices kule magereza.
Majaji wanaodhuru magereza mna wajibu wa kuhakikisha magereza yanaendeshwa kwa mujibu wa sheria na wafungwa iwe wamehukumiwa au mahabusu kama mimi wanapata treatment kwa mujibu wa Sheria.
Na kwa mujibu wa kifungu hicho mna mamlaka ya kutoa maelekezo na mapendekezo kuhusu treatment ya wafungwa na mahabusu.
Sisi tunaoishi huko magerezani tumepewa Haki kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha sheria hiyo kuwaeleza juu ya mambo yalivyo na tunavyotendewa huko magereza.
Jambo la 1 ni kuhusu haki ya mfungwa kuwasiliana na Mawakili wake.
Wafungwa wana haki ya kufanya mawasiliano na mawakili au washauri wa kisheria bila kusikilizwa na maafisa wa magereza Kanuni ya 13 ya kanuni za uendeshaji wa magereza GN. NO. 60/1987. (Prison Management Regulations)
Kanuni inasema kila mfungwa atapewa fursa ya kuwasiliana na mwanasheria wake na atakapomtembelea maafisa wanaweza kumuona ila sio kumsikiliza. Anaisoma hiyo kanuni kwa kingereza hapa.
Sasa Waheshimiwa majaji kumekuwa na tatizo kubwa kuhusiana na haki yangu ya kuzungumza na mawakili wangu bila kusikilizwa na maafisa wa magereza.
Muda wote wako pembeni yangu hadi ninapozungumza na mawakili.
Tatizo hili sio jipya lilianza toka niko Kisutu.
Anasimama Nasoro Katuga anasema tulikuwa na concern aliweka pingamizi halijaamuliwa anaanza kusema mengine. Naomba mwongozo katika hili.
Jaji anaandika kidogo.
Anamuuliza Lissu unasemaje?
Lissu anasema kifungu cha 48 nilichosema kinasema ni draw attention yenu sio kuomba chochote. So i'm drawing the attention to you. Mkiona mnachakufanya fanyeni mkiona hamna msifanye. Wajibu wangu ni kuwaeleza kinachoendelea.
Jaji anasema nafikiri uendelee haya madai ya Katuga ameeelewa baada ya jibu lako.
Tarehe 12/11/2025 tulivyoahirisha kesi mambo yakabadilika tena wakili akifika anapelekwa ofisi ya Mkuu wa Usalama wa Gereza na mimi na Wakili wangu tunapelekwa huko huku wakitusikiliza nikiwa nazungumza na kikundi, kuanzia Mkuu wa Gereza, maafisa wengine zaidi ya watano wanatusikiliza wakati sheria haitaki hivyo.
Siku 88 toka kesi imeahirishwa mwaka jana wananisikiliza kila Mawakili wangu wanaponitembelea.
Mimi na Mawakili wangu tukiuliza, tunaambiwa ni Maagizo kutoka juu, Huko juu ni wapi juu mbinguni au wapi? Mungu anajua.
Hilo ni jambo langu la kwanza.
Nimewapa taarifa kwa mujibu wa kifungu cha 48 mtajua chakufanya ili kuhakikisha sheria inalindwa.
Jambo la Pili, linahusu kutembelewa na watu wengine wasiokuwa wanasheria. Kanuni zinasema unaruhusiwa kutembelewa na watu sio ndugu pekee.
SEHEMU YA 152
Tuna haki yakutembelewa, waheshimiwa Majaji kuna masharti kwenye hiyo kanuni ikiwemo sharti la kutembelewa na mfungwa mwenzako, sharti lingine ni askari magereza wakuone na kukusikiliza ila kwa Mawakili kanuni haisemi hivyo.
Waheshimiwa Majaji tangu tarehe 10/04/2025 mpaka 12/11/2025 nilikuwa natembelewa bila tatizo.
Na ndugu, familia, marafiki na Mimi ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, walikuwa wananitembelea wana Chadema Tanzania nzima.
Niliitwa kwa Bwana Jela nikaambiwa ni marufu kwa viongozi na wanaChadema kukutembelea Gerezani.
Chadema ni Chama halali na sio kosa kwa wanaChadema na viongozi wenzangu kunitembelea lakini kuanzia Tar. 12/11/2025 hawajaruhusiwa.
Maafisa magereza ni maafisa wa umma so yale magereza sio mali zao binafsi.
Hawana mamlaka ya kubagua nani aje gerezani nani asije. Katiba inasema usibague watu kwa mtizamo wao wa kisiasa, dini au kabila na hili vilevile naomba niwaeleze mlifahamu kuhusu violation ya haki ya Mfungwa kutembelewa.
Waheshimiwa Majaji sasa naomba swala la tatu niliseme.
Linahusu uendeshaji wa kesi hii. Na naomba niweke wazi kuwa siwalaumu kwa chochote nitakachosema hapa. Na hiki nitakachosema siwalaumu mawakili wa serikali na nyie majaji.
Haki zangu zimekiukwa sio kwa kosa lenu wala la Mawakili wa Serikali.
Waheshimiwa Majaji leo hii ni siku ya 307 tangu niwekwe mahabusu.
Miezi 10 week 44 niko mahabusu. Waheshimiwa majaji katika siku zote hizi kesi hii imesikilizwa kwa siku 14 tu na leo ni siku ya 15 kesi hii inasikilizwa katika siku 307.
Kuna siku 88 ambazo kesi haijasikilizwa kabisa, niko gerezani hakuna kinachoendelea.
Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokiukwa. Justice delayed is justice denied.
Na Katiba yetu inaelekeza Mahakama ziendeshe mashauri kwa namna ambayo haitachelewesha Haki. Ibara ya 147 ya Katiba inasema.
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinasema mashauri yanaendeshwe kwa haraka.
Tatizo lipo kwenye utaratibu wa session ndio tatizo na hilo ni tatizo la wanaoamua kesi iendeshe kwa njia ya session.
Naomba niwasomee kilichosemwa na Tume ya Haki jinai kuhusu kuendesha mashauri ya jinai kwenye ripoti ya July 2023, ukurasa wa 17 na 18 unasema kuhusu vikao vya mahakama kuu (high court session) tume inasema uendeshaji wa mashauri kwa njia ya vikao huchelewesha mashauri hayo.
Kati ya mashauri 2000 ni mashauri 700 tu ndio yalisikilizwa pekee kwa mtindo wa session.
Hivyo basi uendeshaji wa kesi kwa kutumia session unaamuriwa na Jaji Mkuu zikiisha siku tunasubiri aseme tena ndo maana zimepita siku 88 bila kesi hii kuendelea hadi atakapopanga tena huyo Jaji Mkuu.
Ucheleweshaji huu sio kosa lenu wala mawakili wa Serikali ni kosa la utaratibu tulionao.
Je huu utaratibu wa session uko wapi kwenye CPA ambayo ni sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Leo hapa High Court Dar es salaam kuna majaji wakutosha lakini ili kesi yangu isikilizwe lazima Jaji atoke Songea, mwingine Mtwara sijui na lazima walipwe, Usafiri, Chakula na kila kitu.
Usipowalipa kesi haiendelei na mimi mtuhumiwa nateseka huko jela. Walishindwa nini kuwapangia majaji wa hapa ili kesi isikilizwe kila siku.
Zamani majaji walikuwa wachache sana lakini siku hizi kila mkoa kuna majaji. Nashangaaa mambo haya kwa utaratibu huu sasa.
Jaji anasema soma kifungu cha 185 na anakisoma hapa kinasema Mahakama inamamlaka ya ku conduct seatings.
Mhe. Lissu anasema kuna tofauti kati ya seatings na sessions.
Kwahiyo kwenye hili ni tofauti na ku conduct seatings. Mahakama kuu zote zinakaa kusikiliza kesi hizo ni seatings zote.
Mimi nasema utaratibu wa sessions ni mbaya zaidi kwa kesi kama ya Uhaini.
Jaji ameleta kifungu namna Lissu alivyolitafsiri ameishia kusema hebu tuendeleee basi mshitakiwa
Kosa la Uhaini ni Sue Generis sio sawa na wizi wa kuku, ujambazi na makosa mengine.
SEHEMU YA 153
Hili ni kosa la kipekeee, angalieni ibara ya 28(4) ya Katiba ya JMT ndo kosa pekee la Jinai lililotajwa kwenye Katiba kwasababu sio kosa la kawaida.
Kama hiyo ndio hoja kosa hili pia la Uhaini linapaswa kuwa na kipaumbele maana ni tofauti na makosa mengine yote.
Kwenye kuthibitisha hilo hii sio kesi ya kwanza ni kesi ya tatu toka tumepata uhuru. Kesi ya Grey Likungu miaka 56 iliyopita ilikuwa na washitakiwa 9 lakini ilichukua miezi 6 tu hadi kufika Mahakama ya Rufani.
Kwasababu uhaini ni kosa kuu kuliko mengine yote ilipewa uzito huo.
Khatib Gandi na wenzake 18 kutoka Mahakama Kuu hadi Court of Appeal kuanzia ilipoanzia hadi ilipoishia ilichukua miezi 14 na mashahidi 140. Sisi tuna miezi 10 tumemaliza mashahidi watatu tu.
Watu wanacheka hapa.
Vyovyote itakavyokuwa kesi hii inachukuliwa kama kesi ya kawaida ya Jinai. Haiwezi chukuliwa poa hata kidogo lazima hili lieleweke vizuri.
Kwa utaratibu huu tutafika mwaka 2030 kama mtakuwa hamjastaafu bado kwa speed hii ya miezi 10 mashahidi watatu
Watu wanacheka hata Majaji wameshindwa kujizuia nao wamecheka.
Sasa kuna mtego mkubwa ambao unaweza kuchelewesha zaidi kesi hii.
Mtego wa pannel constitution rule kuna mtego unaoweza kutuchelewesha sana kwa kanuni hizo mmoja wenu akipata mafua hapa basi kesi haiendelei.
Hamjautengeneza nyie wala mawakili wa Serikali ila ameutengeneza Jaji Mkuu.
Sasa kesi ya Grey Likungu Mataka ilisikilizwa na Jaji mmoja na kesi ya Khatib Gandi Ilisikilizwa na Jaji mmoja pia.
Kesi ya tatu Jaji Mkuu anasema mmoja hawezi ndio maana anawateua muwe watatu kusikiliza kesi hii.
Majaji wanaangaliana hapa.
Kwenye kesi hii Jaji mkuu asipowatumieni hela hamji. Kesi hii ina ugumu gani hadi muwe watatu?
Sasa nimesema ili siku moja msije kusema mbona hakusema chochote.
Nimesema kuweka kumbukumbu sawa. Maana anayeumia gerezani ni mimi na jambo hili linanihusu mimi kwahiyo ni muhimu sana nikasema wakusikia na asikie.
Ahsante nimemaliza hapo.
Majaji wanaandika na kushauriana pale. Sijui wanajadili kitu gani naona wanachukua muda kidogo.
Wapo kama wamepigwa butwaa kama sio kuingiwa na ubaridi.
Wamemaliza kuandika sasa anawasha kipaza sauti Jaji Ndunguru kiongozi wa Jopo.
Sasa Mshitakiwa ulisema lengo lako ni ku draw attention yetu.
Sisi tumekusikia na sasa tuendeleee.
Upande wa Serikali wanaitwa anasimama Nassoro Katuga kujibu hoja zile za Pingamizi la shahidi P11.
Katuga: Alipofika shahidi Tar. 12/11/2025 hoja ya kwanza alisema kizimba maalumu si kizimba kama lilivyotafsiriwa kwenye kanuni ya 3 ya kanuni za Ulinzi wa mashahidi 2025.
Alisema kizimbi hicho kilivyokaa hakimuwezeshi yeye wala Mahakamaa kumuona shahidi hivyo kwa tafsiri yake mahakama haiwezi ku assess deminor ya shahidi.
Anaendelea Katuga.
Shahidi P11 amelindwa kwa amri ya Mahakama hii tukufu. Baada ya maombi ya jinai 17059/2025 Mahakama hii iliamuru shahidi huyu na wenzake ambao sio askari Polisi watatoa ushahidi wakiwa wamelindwa.
Kanuni ya 6 ya Ulinzi wa Mashahidi inasema lengo ni kuwezesha kutoa ushahidi kwa kutumia kizimba maalumu.
Hivyo basi ni Mahakama ndio inayowezesha kizimba maalumu kwa shahidi aliyelindwa.
Shahidi huyu amelindwa ili yeye asimuone mshitakiwa na mtu mwingine. Mahakama ndio inazingatia mambo hayo na ndio imetengeneza kizimba hicho.
Mshitakiwa alisema Mahakama haimuoni. Sasa hilo ni suala la ushahidi kwamba mnamuona au hamumuoni. Hakusema anaomba apande kizimba cha ushahidi ili tumuulize maswali kuhusu majaji wanamuona au hawamuoni.
Sisi ni msimamo wetu kuwa Majaji mnamuona shahidi na hivyo tuendelee yeye amewazungumzia Majaji kuwa hamumuoni Shahidi sio jukumu lake.
Naomba niende hoja ya pili.
SEHEMU YA 154
Anaendelea Wakili wa Serikali Katuga.
Mahakama hii tukufu ijiulize je shahidi huyu P11 ni mashahidi ambao wamelindwa akirejea kanuni ya 3 ya Kanuni za ulinzi wa Mashahidi akiwaambia pia Shahidi anayelindwa ni shahidi ambae yupo kwenye amri ya Ulinzi.
Pia amewarejesha kanuni ya 5 inamuelezea shahidi gani ambae anapewa ulinzi au analindwa au amri ya ulinzi inatolewa kwake.
Naomba mrejee uamuzi wa Jaji Mtembwa wa Mahakama hii juu ya uamuzi wa kulinda mashahidi wa kesi hii.
Hoja hii ina majibu mawili kama ifuatavyo.
Jibu la kwanza ni kwamba kanuni ya 5 za ulinzi wa mashahidi kwa ujumla wake inahusu mambo ya kuzingatia kabla haijatoa ulinzi wa mashahidi.
Sasa hakuna mnachoweza kubadilisha katika amri iliyokwisha kutolewa na Jaji Mtembwa.
Hoja nyingine ya kwamba mashahidi hawajabainishwa kwa kutajwa kwa majina nayo pia haihusiani mahakama ilijiridhisha kuwa mashahidi ambao sio polisi ndio watafichwa.
Kifungu cha 194 Cha CPA yanafanywa kwa upande mmoja yaani exparte application lakini hakijaweka usiri wa matokeo hayo. Ndio maana amri ya Mahakama hii iko wazi na ipo kila mahali kuhusu ulinzi wa mashahidi.
Kama majina ya mashahidi kanuni inataka watajwe wakati wa maombi je italinda ulinzi wa mashahidi husika? Haitakuwa imelinda huo ulinzi wa mashahidi husika. Hayuko sahihi kusema wakati huu mambo haya wakati Criminal Revision No. 15655 Mahakama Kuu kupitia Jaji Mkwizu hoja hizi hizi zilisemwa.
Kumbuka hii kesi anayorefer hapa haihusiani na Uhaini. Anataja ile kesi nyingine ya kusambaza taarifa za uongo.
Lissu anamuomba hiyo nakala ya hiyo kesi. Katuga anasema ipo mtandaoni. Lissu anamuuliza uko serious kweli mimi niko jela unasema uamuzi wa Mahakama uko mtandaoni? Jamaa wameenda kutafuta huo uamuzi.
Katuga anaendelea.
Anasema anaomba aende kwenye hoja ya tatu.
Kaka yangu mshitakiwa anasema shahidi hawezi kutoa ushahidi akiwa kizimbani kwasababu haipo kwenye amri ya Tarehe 14/07/2025 ya Mahakama hii.
Hicho hakiwezi kuathiri chochote katika usikilizwaji wa kesi hii.
Kutumia kizimba ni procedure ya kumlinda shahidi aliyelindwa na kanuni zinasema mahakama itawezesha kupitia kizimba maalumu.
Hivyo ndio sheria inasema, haihusiani kitumike kutokana na mabadiliko ya shahidi.
Kwa mujibu wa kanuni ya 6(c) inatoa njia tofauti za ki procedure ya kuendelea kumlinda shahidi aliyepewa amri ya Ulinzi.
Mfano kama shahidi ni Kingwendu Ngwendurile atakuja kutoa ushahidi sauti yake ni maarufu mahakama itatafuta njia nyingine ya kulinda shahidi huyo.
Anaendelea hapa.
Mahakama ndio inaamua namna ya kumlinda Shahidi na si vinginevyo.
Hoja nyingine aliielekeza kwenye kanuni za Ulinzi wa mashahidi na hoja yake kuwa kanuni hizi zimeanza kufanya kazi wakati yeye alishaletwa mahakamani.
Je zinaweza kutumika retrospectively?
Sasa majibu yetu ni kwamba kanuni ni sheria za mwenendo kwahiyo zinaweza kutumika hata kama kesi ilishaanza kutumika.
Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha tafsiri ya Sheria kinasema ili sheria ianze kutumika pale inapokuwa gazetted au yenyewe imesema ianze lini kutumika kwake.
Katika uwasilishaji wake alisema kanuni za ulinzi wa mashahidi hazijachapishwa na hazipo kokote.
Wasilisho letu kuwa haya ni masuala la ushahidi tu.
SEHEMU YA 155
Naomba nimalizie kwa upande wetu wa Serikali na tumuachie mwenzetu aweze kujibu na kuwasilisha Rejoinder yake.
Jaji anawauliza mmemaliza Upande wa Mashitaka.
Wanajibu wamemaliza.
Mhe. Lissu anajiandaa kufanya rejoinder hapa.
Anasimama Mh. Lissu.
Nawashukuru Waheshimiwa Majaji.
Nimesikiliza hoja za Majibu ya Mawakili wa Serikali na nitajibu kama zilivyoletwa na Wakili wa Serikali.
Hoja ya kuhusu kizimba maalumu cha mashahidi. Swali nililouliza je hicho kizimba kinaendana na matakwa ya sheria?
Sheria inasema kizimba ni eneo ambalo sisi wengine haturuhusiwi kumuona shahidi ila nyie majaji pia mnayo macho ya kuona.
Upo msemo wa kilatin unasema Res Ipsa Loquitour, maana yake mambo yanajisemea yenyewe kama yalivyo.
Hivyo hicho sio kizimba cha mashahidi kwa mujibu wa kanuni.
Huyo shahidi haonekani na Mahakama.
Kwahiyo haihitaji maneno mengi na hizo sio kizimba lilichozungumzwa na sheria.
Jambo lingine ni kwamba je Mahakama iliyotoa ulinzi wa mashahidi ilijumuisha na kizimba hicho?
Jibu lake ni kwamba ruling ya Jaji Mtembwa walisema ilindwe kwa kutumia kizimba, Haikusema hayo yote.
Waheshimiwa Majaji Wakili wa serikali amerudia kifungu cha 6(c) za ulinzi wa mashahidi.
Kwamba mahakama inaweza kueleza utaratibu wa kutumika kwa kutumia kizimba cha mashahidi.
Sasa DPP lazima aombe namna gani anataka kulinda mashahidi.
DPP hakuomba namna ya kulinda mashahidi kwa kutumia kizimba cha mashahidi.
Walichoomba ni majina yasionekane na vingine na Jaji aliwapa walichokitaka.
Haya ya vizimba yametokea hapa, hawawezi kupewa ambacho hawakuomba.
Pia Kanuni ya 5(1) inasema amri ya ulinzi inatolewa kwa shahidi ambae amebainishwa sasa kama Shahidi hajabainishwa kwa lolote Mahakama inajuaje anayepaswa kulindwa ni nani?
Hawakubainisha Majina kwa Mahakama wakapata amri hiyo ya uongo na leo hawaonekani hapa Mahakamani, watatoaje ushahidi watu WASIOJULIKANA.
Hivyo mnachoombwa hapa ni kwamba kwenye kesi ya Uhaini ambayo adhabu yake ni kifo, hamumfahamu, humumuoni isipokuwa kwao na wao wanaita hiyo HAKI.
Nilisema kwenye hoja yangu ya msingi na haijajibiwa na utaratibu huo ni wa Star Chamber Court karne ya 16 ndio wanataka mahakama kuu ya Tanzania zitumie utaratibu wa giza au kwenye kesi yoyote ile nyingine.
Justice must seen to be done.
Mambo ya gizani hayo na haki gizani sio Haki.
Anaendelea Mh. Lissu.
Huyu Wakili wa Serikali anasema Mahakama ifanye rejea kwenye uamuzi wa Jaji Mtembwa. Nina majibu mawili hapo.
1. Hoja yangu inalenga kulinda integrity ya uamuzi wa Jaji Mtembwa. Wapewe majina ya bandia na maelezo yao yasitolewe kwenye nyaraka. Tukiruhusu mambo ya kizimba ambayo hayakusemwa na Jaji Mtembwa ndio tunataka kuyarekebisha.
2. Kwani ni kosa gani kubadilisha uamuzi wa Jaji mtembwa iwapo kuna sababu za msingi za kuubadilisha. Kanuni ya 8 inasema amri ya ulinzi inaweza kufutwa, kubadilishwa na Mahakama kwa utashi wake au kufuatia kuna mabadiliko ya hali fulani toka amri kutolewa.
Hakuna aliyekuwa anayajua mambo yote haya, tumekuja kuyajulia hapa na kwa vile tumeyajua leo kwa mujibu wa kanuni ya 8 inasema yanawezekana kutokea mambo yakabadilisha hali basi atoe ushahidi wake hapo kizimbani tumuone wote.
Narudia tena amri ya Jaji mtembwa haijataja kizimba lakini pia hakutajwa huyo.
Jambo lingine ni kwamba amri za ulinzi zipo 16 kwenye kanuni na wao waliomba amri nne tu.
Sasa Katuga amatuambia Mahakama inaweza tu kuongeza hizo amri za ulinzi wa mashahidi kwa kadri itakavyoona.
Hiyo haitakuwa Mahakama sasa kama ikifanya hivyo.
SEHEMU YA 156
Anaendelea Mhe. Lissu
Kifungu cha 282 cha CPA amekisoma Katuga hapa kwamba Mahakama inaweza ku regulate taratibu zake wakati wa kutekeleza wajibu wake wa jinai.
Msifungwe sana na hizi kanuni maana mnaweza kuregulate procedure zenu.
Sasa kifungu cha 282 sio kichaka cha kujificha ili kukiuka sheria na taratibu zilizowekwa wazi.
Utaratibu wa kulinda mashahidi umewekwa wazi kifungu cha 194 cha CPA na kanuni za ulinzi wa mashahidi.
Huu mualiko wa kwamba muache sheria inasemaje mtafute busara zenu nawashauri msikubali huu mwaliko wa Katuga wa kudharau sheria.
Anaendelea Mhe. Lissu.
Wakili wa Serikali anasema Haki itatendeka tu hata kama shahidi haonekani.
Sheria inasema amri yoyote ya kulinda mashahidi haipaswi kuathiri haki ya kusikilizwa kwa usawa.
Shahidi ambae wao wanamfahamu mimi simfahamu, wao wanamfahamu jina na taarifa zote mimi sifahamu kuna usawa hapo?
Mahakama itaeleza hatua za kulinda mashahidi kwa usawa wa pande zote.
Hiki wanachoomba kinakiuka kanuni ya 6(2) ya kanuni za kuficha mashahidi.
Waheshimiwa Majaji yote niliyosema nimeyazungumza kwa kulinganisha na Katiba ya Tanzania na sheria za Afrika na Dunia kote.
Nilieleza kwa kina namna sheria zote za kimataifa zimezungumzia suala hili ila wao hawajajibu hata moja.
Hawajajibu kwasababu hayajibiki Waheshimiwa majaji, na hayajibiki kwasababu ni ya kweli. Tuishie hapo.
Kuhusu kanuni kutumika retrospectively, imesemwa na Katuga kwamba kanuni zote za utaratibu zinatumika retrospectively.
Sasa waheshimiwa majaji kanuni za procedure ambazo haziathiri haki zina retrospective effect.
Kanuni za procedure zinapoathiri haki haziwezi kutumika retrospective.
Angalieni ukurasa wa 11 na 12 wa Hukumu aliyoleta Katuga inasema if the legislation affect substantive right it should not operate retrospective.
Sasa hapa tunajadili right to be heard na kanuni hizi mshitakiwa hawezi kumjua shahidi kuanzia majina na vingine.
Kanuni hizi zina affect substantive right.
Kanuni zinakiuka haki zangu za Kikatiba hatuwezi kuziacha hivi zilivyo zikatumika kama wao wanaona ni jambo dogo wamlete shahidi wao hadharani hapa tumenyane nae waone.
Anaendelea Mhe Lissu.
Hizi kanuni zenu mlitunga kwa ajili yangu na matakwa ya kisheria yanakataa.
Sio mnamkamata mtu, mnamfungulia kesi halafu baadae ndio mnaenda kutunga kanuni kwamba tumtungie sheria gani?
Wamepitisha hizo sheria zao ili waje kunishitaki nazo, hilo haliwezekani kabisa.
Huyu Katuga anapenda sana kusema mimi naitishia Mahakama labda hajui nashitakiwa kwa kosa gani?
Nisipojitetea kwa nguvu zangu zote itakuwaje?
If i dont defend myself to the best of my ability itakuwaje?
Nisipoibua yote haya consequences ni adhabu ya kifo.
Maisha ni matamu i am not ready yet to die kama kuna la kusema nitasema tu.
Nitatishaje majaji wa Mahakama Kuu niko Gerezani miezi 10 ila ninachotaka Majaji muyatizame mambo haya kwa kuangalia uzito wa kesi hii.
Naomba kumalizia kwa kusema yafuatayo:
Kwamba ile kesi ya Mahakama Kuu iliyokuwa mbele ya Jaji Mkwizu, Waheshimiwa Majaji mtajiridhisha wenyewe mtakaposoma hiyo kesi mtaona kwamba hiyo kesi haikuwa inahusu uhalali wa hizi kanuni, haikuwa inahusu uhalali wa mashahidi kutoa ushahidi kwa kificho. In fact iliishia kwenye PO (Pingamizi la awali) Jaji hakutaka kusikiliza.
Sasa imeletwa hapa ili iweje? Haina uhusiano wowote na constitutionality ya kanuni na suala la shahidi kutoa ushahidi.
Wameleta hapa ili muone kuwa walishinda hiyo kesi. Hawana kingine cha maana. In fact ilikuwa ni kesi ya cyber crime na sio kesi hii ya uhaini.
Naomba mtafakari hoja zangu na mkubali shahidi asiruhusiwe kutoa ushahidi kwenye hilo box kwasababu zote ambazo nimezieleza.
Nataka Majaji mumuone shahidi na mimi ambae wanasema ni muhaini nataka nimuone, nimuhoji na anijibu.
SEHEMU YA 157
Anamalizia Mhe. Lissu
Vinginevyo haitakuwa Mahakama ya Haki na kanuni zinataka usikilizwaji wa mashauri haya uwe wa haki kwa pande zote.
Ni hayo tu waheshimiwa majaji.
Anamaliza Mheshimiwa Lissu hapa.
Majaji wanateta huku wakiandika kidogo.
Mheshimiwa Lissu anakusanya makabrasha yake taratibu hapa. Bila shaka kesi itaahirishwa leo. Watahitaji kuandika uamuzi wa hoja zilizowasilishwa.
Anawasha kipaza sauti Jaji Ndunguru hapa akiwa serious sana na kama amechoka. Anaonesha hana nuru kabisa.
Naomba niseme yafuatayo kabla sijaahirisha shauri.
Mtakumbuka leo tumevumiliana sana kuhusu simu zinazopiga kelele kama tunashindwa kukaa na simu basi kwenye ukaguzi tutaomba mziache.
Naomba mtambue uvumilivu wa leo hautaendelea kuwepo kuhusu masuala ya simu.
Shauri linaahirishwa hadi Tarehe 11/02/2026 saa tatu asubuhi.
Mwenyekiti wa CHADEMA Tundu Lissu ameonekana kuwa mwenye uso wenye bashasha akisalimiana na wanachama wa chama hicho pamoja na watu wengine waliohudhuria kesi inayomkabili katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala ndogo ya Dar es Salaam leo.
Wakati akikusanya vitu vyake ili kushuka kizimbani ili kurudi rumande Lissu ameonekana kuwa na bashasha huku akionyesha alama ya CHADEMA ya vidole viwili.
Kesi imeahirishwa mpaka jumatano ambapo maamuzi ya mapingamizi aliyowasilisha Lissu yatatolewa.
"Mahakama imepanga kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo kwa mfululizo kuanzia tarehe 09 Februari 2026 hadi tarehe 06 Machi 2026. Kesi hi inasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, ambao ni: Mheshimiwa Jaji D. Ndunguru, Mheshimiwa Jaji J. Karayemaha, na Mheshimiwa Jaji Kiwonde."
"Kwa sasa, ipo katika hatua ya usikilizwaji wa mashahidi wa upande wa Jamhuri, ambapo ushahidi unaendelea kutolewa kwa kina na kwa mujibu wa taratibu za kisheria, Chama kinatoa wito kwa wanachama, wafuasi, wananchi wote, na Jumuiya ya Kimataifa kufuatilia mwenendo wa kesi hii. Kesi hii ni taswira muhimu ya demokrasia na haki nchini Tanzania."
Zaidi >
- Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kuendelea Februari 9 hadi Machi 6, 2026
- Shahidi wa Kesi ya Lissu (P7): Nauli ya kuja mahakamani leo nimepewa na mwanamke wangu. Ndiye ananiweka mjini
- Kesi ya Tundu Lissu kuendelea leo Februari 17, 2026, mashahidi wa Jamhuri wasiopungua watatu wangojewa
- Kesi ya uhaini dhidi ya Lissu: Shahidi wa saba kati ya 30 wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi
- Kesi ya Lissu | Shahidi wa Siri (P6): Lissu alisema tunakwenda kuvuruga uchaguzi na kukinukisha
- Kesi ya Lissu: Hiki ndicho Kizimba cha mashahidi wa kificho, kilichosababisha Kesi kuahirishwa
- Baada ya takribani miezi mitatu, kesi ya Tundu Lissu kuendelea leo Februari 9, 2026
- Kesi ya Lissu: Mahakama yaagiza Kizimba cha Mashahidi wa siri kirekebishwe Majaji wawaone. Kesi kuendelea Feb 12, 2026
- Kesi ya uhaini ya Lissu, mahakama kutoa uamuzi wa mapingamizi leo Feb 11, 2026
- Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kuendelea Februari 9 hadi Machi 6, 2026
- Shahidi wa kesi ya Lissu (P7) anasema alikamatwa mara tu baada ya kuangalia video ya Lissu iliyokuwa Jambo TV
- Kesi ya Lissu | Shahidi wa siri (P5): Niliona video ya Lissu akisema atakinukisha, uchaguzi mkuu hautafanyika
- Mama wa CHADEMA azimia mahakamani baada ya Lissu kudai kunyimwa chakula
- Mahakama kuu, Kanda ya Dar es salaam Tarehe 11 Februari, 2026 kutoa uamuzi mdogo katika kesi ya Uhaini inayomkabili Tundu Lissu