Kesi ya diamond karanga, Wasafi na Kusaga ilivyofika mwisho mahakamani

lord atkin

Senior Member
Sep 30, 2018
197
683
DIAMOND PLATNUMZ NA DIAMOND KARANGA ILIVYOGEUKA TALAKA YA CHOZI

Na Luqman MALOTO

INGEWEZEKANA, yaliyowezekana kwenye movie ya Superman mwaka 1978, yangewezeshwa katika ulimwengu halisi. Superman alipaa nje ya dunia, akailazimisha sayari kurudi kinyumenyume.

Kwa sayari kurudi reverse, muda nao ulirudi nyuma, matukio ya nyuma nayo yalirejea, Superman akapata nafasi ya pili ya kuiokoa siku. Kila mtu anayo siku ambayo anatamani muda urudi nyuma aiokoe!

Juni 29, 2017. Ni miaka sita na miezi miwili iliyotimia. Viwanja vya Mchikichini, Kariakoo, vilikuwa shereheni. Offspring wa Tandale, Diamond Platnumz, alikuwa kwenye moja ya mapigo makubwa ya kimaendeleo.

Ilikuwa harusi ya kibiashara baada ya kutangulia ndoa. Diamond Platnumz na Diamond Karanga ni kupika na kupakua hadi kifo kiwatenganishe. Diamond ali-appeal kwa Watanzania: “Nunueni karanga zangu mniunge mkono.”

Mzunguko halisi wa dunia si maigizo ya dhahania outer space. Diamond si Superman, hawezi kupaa arudishe tarehe nyuma. Inabaki historia kuwa once upon a time at Mchikichini, ilifanyika harusi ya kukata na shoka. Watu walitafuna karanga na walicheza muziki.

Hata mama mzaa chema. Mama mzazi wa Diamond, Sanura binti Kassim, alikula karanga, akafurahia mkwe kwa muziki. “Young love in the sun", hadithi ya Spice Girls kwenye Viva Forever. Kumbe yote ni ndoto. Baada ya kuamka, mke hayupo, ndoa hakuna, bali talaka!

Waliimba Msondo “Kwenye Penzi Hapakosi Tenzi". Maofisa wa nongwa walisengenya kuwa Diamond ni mchepuko wa Diamond Karanga. Mwenye mali yupo. Walifika mbali na kusema ndoa ya Diamond Platnumz na Diamond Karanga ni mazingaombwe kama Irene Uwoya na Dogo Janja.

Kanuni ni ilele ya Msondo, ndoa ikishakuwa ndoano mambo yote yanakuwa hadharani. Kumbe Diamond Karanga ilikuwa ndoa ya mtaala. Tena ya mabwana watatu (trilateral); Diamond (Wasafi Limited), Joseph Kusaga na Smart Industry Limited.

TALAKA MAHAKAMANI

Somewhere in 2020, Diamond kupitia kampuni yake, Wasafi Limited, aliwafungulia mashitaka Smart Industry kwa kukiuka makubaliano. Shauri lilisajiliwa kama Kesi ya Madai Namba 160, 2020. Mahakama Kuu, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Jaji Sedekiah Kisanya, Agosti 18, 2023, Wasafi waliwalalamikia Smart Industry kwa kuvunja mkataba wa makubaliano ya watatu (tripartite agreement), uliowahusisha Wasafi, Smart na Joe Kusaga.

Mkataba huo uliingiwa Juni 8, 2017, ukihusisha utengenezaji wa bidhaa za Diamond Karanga, kuzibrand na kuziuza. Wasafi waliomba Mahakama iwaamrishe Smart kuwalipa fidia, jumla Sh2.75 bilioni.

Mchanganuo wa maombi hayo ya Wasafi kwa Mahakama ni kuwa Sh2.25 bilioni ni fidia ya madhara mahsusi (specific damages) na Sh500 milioni ni kwa ajili ya kufidia madhara ya jumla (general damages).

Smart baada ya kupokea hati ya mashitaka kutoka Wasafi, waliandika maelezo ya utetezi, vilevile wakajibu mapigo kwa kupandishia madai (counterclaim) dhidi ya Wasafi na Joe.

Counterclaim ya Smart ilikuwa na maombi kwa Mahakama, iwaamrishe Wasafi na Joe, kuwalipa dola za Marekani 37,207 (Sh93.2 milioni) na Sh1.442 bilioni. Hapo jumla ni Sh1.535 bilioni. Hiyo ni fidia ya madhara mahsusi.

Smart pia waliomba fidia ya Sh3 bilioni kwa ajili ya madhara ya jumla. Hivyo, jumla ya fedha ambazo Smart waliiomba Mahakama dhidi ya Wasafi na Joe ni Sh4.535 bilioni.

Zaidi, Smart waliomba Mahakama iwatoze Wasafi na Joe riba (kwa viwango vya mahakama), kuanzia siku ambayo hukumu ingetoka hadi pale wahusika wangekamilisha malipo ambayo yangekuwepo kwenye amri ya Mahakama. Kingine, Smart waliomba kulipwa gharama za kesi.

Wasafi walijibu counterclaim ya Smart. Joe sio tu hakufika mahakamani wala kutuma wakili, bali pia hakufaili majibu kwa maandishi kama ilivyopaswa.

Kwa mujibu wa Jaji Kisanya, kabla ya kesi kuanza kusikilizwa, Wasafi na Smart, waliomba wazungumze na wakubaliane nje ya Mahakama. Ombi hilo lilikubaliwa na Mahakama.

Novemba 8, 2022, mawakili wa Wasafi na Smart, waliwasilisha hati ya makubaliano, iliyosainiwa Oktoba 31, 2022. Wasafi na Smart walikubaliana mambo manne;

Mosi; Pande zote zilifikia mwafaka bila kubebeshana dhima (mzigo), katika madai ya kila upande.

Pili; Wasafi walikubali kuondoa kesi yao mahakamani dhidi ya Smart. Kadhalika Smart nao walifuta counterclaim yao dhidi ya Wasafi.

Tatu; Makubaliano waliyosaini ni kamili na ya mwisho dhidi ya madai ya pande zote mbili.

Nne; Pande zote zilikubaliana kuwa hati ya makubaliano waliyosaini, inahusu pia madai yote mengine ambayo yalikuwa pending.

SMART VS JOE

Baada ya Wasafi na Smart kumalizana mahakamani, kilichobaki kikawa ni counterclaim dhidi ya Joe, ambaye hakutokea mahakamani na hakufaili maelezo ya utetezi kwa maandishi.

Smart waliomba kesi iendelee kwa kusikiliza upande mmoja (ex-parte), kwa kuwa Joe hakutoa ushirikiano kwa Mahakama. Pamoja na kuwa shauri ni la upande mmoja, Jaji Kisanya, aliitisha ushahidi aweze kuilewa kesi vema.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulionesha kuwa Smart ndio wamiliki na wazalishaji wa Diamond Karanga. Juni 8, 2017, waliingia makubaliano na Wasafi pamoja na Joe kwa ajili ya masoko. Umri wa mkataba ni miaka 20.

Makubaliano waliyoandikiana ni kuwa kwa kila mfuko mmoja wa Diamond Karanga, Smart wangewalipa kamisheni Wasafi Sh1,650 na Joe Sh1,350.

Smart waliwasilisha ushahidi mahakamani ulioonesha kuwa kati ya Julai 2017 na Februari 2019, waliwalipa Wasafi Sh269 milioni na Joe Sh221 milioni, kama kamisheni.

Kwa mujibu wa Smart, wakati wao wakilipa kamisheni kama ilivyopaswa, Wasafi na Joe walipuuza wajibu wao wa masoko, kwa kutofanya promotion, hivyo kuwapa hasara kubwa.

Smart walidai mahakamani kuwa Wasafi na Joe, walitimiza wajibu wao wa promotion Julai, Agosti na Septemba 2017, vilevile Februari 2018, baada ya hapo walikaa kimya, hivyo kuwasababishia hasara ambayo waliomba Mahakama iamuru wafidiwe.

HUKUMU

Akitoa hukumu, Jaji Kisanya, alisema asili ya makubaliano ya Smart dhidi ya Wasafi na Joe, yapo wazi kuwa fidia inapaswa kulipwa kwa pamoja (Wasafi na Joe) na wakati huohuo, Smart walishaondoa kesi yao dhidi ya Wasafi.

Ufafanuzi wa Jaji Kisanya ni kuwa endapo angeamuru Smart walipwe fidia kulingana na kesi iliyokuwepo mahakamani, maana yake Wasafi na Joe, wangepaswa kushirikiana kulipa, wakati Smart na Wasafi walishamalizana.

Jaji Kisanya, aliiondoa kesi (counterclaim) hiyo mahakamani, kwa maelezo kuwa Smart wanaweza kumfungulia kesi tofauti Joe. Jaji amekwepa kumhukumu Joe peke yake katika kesi aliyoshitakiwa pamoja na Wasafi. Rufaa imeachwa wazi kwa asiyeridhika na uamuzi.

Hivyo ndivyo ndoa ya Diamond Karanga ilivyogeuka Talaka ya Chozi, kama riwaya ya legend Hemed Kimwanga. Ilianza kwa mapenzi shatashata. Matangazo na minada ya ubora, uzuri na utamu. Mara, ikawa kimya, ikasikika kuwa mwali (Diamond Karanga), alirudi kwao.

Kishindo mahakamani kimeibua yaliyokuwa sirini yaje hadharani. Kumbe Diamond Karanga ni mwali wa Smart, akamposa kwa partners in crime, Diamond na Big Joe. Hatuwezi kurudisha siku nyuma. That’s business nature, anyway!

Ndimi Luqman MALOTO
 
Bwana maloto kaandika vingi lakini lengo lake hasa ni lipi, kumcheka diamond ama.. mbwembwe za superman sijaelewa maana yake, diamond arudishe siku nyuma kwa kipi yaani amengia hasara kiasi anatamani angebadilisha hiyo siku, ama vipi?
 
Kuna moja toka huko huko,sijui iliishaje

Wakati yeye alivyokuwa bado hana power ,alikuwa analalamika wanalipwa kidogo hivyo akawa anapamba ili wasanii walipwe kikubwa ,cha kushangaza na yeye ana so called chombo cha habari lakini anawalipa kiduchu wasanii kwenye matamasha ya hicho chombo ,Juma nature Kiroboto kaamua kumtolea uvivu.
 
Wakati yeye alivyokuwa bado hana power ,alikuwa analalamika wanalipwa kidogo hivyo akawa anapamba ili wasanii walipwe kikubwa ,cha kushangaza na yeye ana so called chombo cha habari lakini anawalipa kiduchu wasanii kwenye matamasha ya hicho chombo ,Juma nature Kiroboto kaamua kumtolea uvivu.
Hahahahahaaha
 
Back
Top Bottom