Kesho ya nishati yetu Tanzania ipo baharini (Sehemu ya Kwanza)

Feb 13, 2017
5
8
Kesho ya nishati yetu Tanzania ipo baharini

offshore wind farm.jpg



Miongoni mwa ajenda kuu kwenye Mkutano wa 28 wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP 28) pale Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu, ilikuwa nishati safi.

Mkutano wa mwaka huu ulioanza Novemba 30, ulihitimishwa siku ya Jumanne Desemba 12, mwaka huu baada ya mijadala ya maeneo kadhaa ikiwemo nishati safi.

Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine duniani ilihudhuria mkutano huo ikiwa tayari na miradi kadhaa ya nishati safi na rafiki wa mazingira inayoendelea kutekelezwa, hususani ile ya maji, lakini ikiwa imeipa mgongo fursa moja muhimu na iliyo peupe, katika mwelekeo wake kwenda kwenye matumizi kamili ya nishati safi.

Umeme unaozalishwa kwa upepo, ikiwemo ule wa mawimbi ya bahari ni fursa kwa Tanzania kuzalisha nishati safi na ya kutosha. Hata hivyo fursa hii haijatumika kulinufaisha taifa. Megawati nyingi za umeme zipo baharini lakini mipango kuhusu uchumi wa buluu au bahari, haitoi nafasi kwa fursa ya nishati kama ilivyo kwa sekta za uvuvi na kilimo cha majini.

Pamoja na sifa yake ya umeme ulio rafiki wa mazingira, umeme wa upepo na mawimbi bahari ni rahisi pia kuuzalisha.

Uchambuzi wa taasisi ya “Governance and Economic Policy Center,” yenye makao yake nchini, unaonyesha uwezo mkubwa uliopo Tanzania kwenye uzalishaji umeme kutokana na upepo na mawimbi baharini ambao ni kuzalisha zaidi ya GWh 17 (Gigawatt hours), zinazoweza kuzalishwa kutokana na upepo wa baharini pamoja na Kw/m 133 (kilowatt hour) kutokana na nguvu za mawimbi ya bahari.

Taarifa ya taasisi ya kimataifa inayohusika na mifumo ya taarifa za kijiologia, “Global Information Systems (GIS),” inaitaja Tanzania kuwa na upepo mkali wa baharini na pwani wenye uwezo wa kuzalisha Ghw 17 na nguvu ya mkondo wa mawimbi inayokadiriwa kuwa na Kw/m 133.

Hizi GWh 17, ni sawa na MW 17,000 za nishati safi, huu ni umeme mwingi sana, ni takribani mara nne ya lengo la uzalishaji nchini la MW 4,000, tena kwa vyanzo zaidi ya viwili, vikiwemo vinavyochafua mazingira.

Uchambuzi huo wa “Governance and Economic Policy Center, unaonyesha kutotumika kabisa kwa fursa hiyo nchini Tanzania ambapo takribani asilimia 60 au theluthi mbili ya watu wake hawana huduma ya umeme, hii ikiwa ni kwa takwimu za mwaka 2021.

Pamoja na kiwango kidogo cha wananchi waliounganishwa na huduma ya umeme nchini, katika miezi na miaka ya hivi karibuni hali ya upatikanaji wa nishati hiyo imekuwa sio nzuri, mgawo wa umeme ulifikia kiwango kibaya zaidi, ukidumu kwa hadi saa 12 kwa siku kutokana na gridi ya taifa kukabiliwa na uhaba wa umeme unaosababishwa na kuzidiwa na uchakavu wa miundombinu.

Hali hiyo ya mgawo imesababisha malalamiko huku wananchi wakilishutumu Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, TANESCO, kwa kuifikisha huduma hiyo katika kiwango ambacho sasa imekuwa kero sugu kwa watumiaji.

Lipo ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme hivi sasa nchini kutokana na kupanuka kwa shughuli za kiuchumi, hususani sekta ya viwanda na usambazaji nishati hiyo vijijini, mabadiliko hayo hayaendeni na uwekezaji hivyo umeme uliopo kutokidhi mahitaji ya sasa.

Taarifa zinaonyesha kuwa miundombinu iliyopo ni ya muda mrefu, tukirudi nyuma kwenye miaka ya sabini na kabla ya hapo, hivyo hivi sasa imechakaa, na wakati huo huo uzalishaji kutoendana na kasi ya ukuaji wa uchumi.

Hali ya upatikanaji umeme imekuwa mbaya zaidi katika mwaka huu wa 2023 ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita, na kuathiri kwa kiwango kikubwa shughuli za kiuchumi, kiuzalishaji na ukuaji.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, gharama ya ukatikaji wa umeme nchini huigharimu sekta ya biashara takribani asilimia 15 ya mauzo yote ya mwaka na mamilioni ya dola za Kimarekani kwa uchumi wa taifa.

Uhaba wa nishati ya umeme unaozalishwa na kusambazwa na shirika pekee lenye jukumu hilo, TANESCO, unaviathiri pia visiwa vya Zanzibar vinavyohudumiwa na shirika hilo kwa kutumia mkonga wa chini ya bahari.

Visiwa hivyo vinaitegemea TANESCO kwa asilimia 100 kupata huduma hiyo kupitia mikonga iliyopitishwa chini ya bahari yenye uwezo wa MW 100 na MW 25.

Umeme unaozalishwa kutokana na upepo na mawimbi baharini, utaviwezesha visiwa hivyo kuondokana na utegemezi kwa TANESCO ikizingatiwa kuwa linakabiliwa na uhaba wa nishati hiyo.

Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (EWURA) kuhusu utendaji sekta ya umeme inaeleza kuwa hadi Juni 2021 uwezo wa kuzalisha umeme wa shirika hilo ilikuwa MW 1,609, wakati mahitaji ya juu yakiwa 1,201.02.

Lakini katika chapisho lake la hivi karibuni kuhusu mabadiliko ya tabianchi, mwelekeo wa nishati na COP28, Governance and Economic Policy Center, inakielezea kiwango cha jumla cha usambazaji umeme nchini hadi mwaka huo wa 2021 kufikia MW 1,605.86.

Kituo hicho kinabainisha kuwa mahitaji ya nishati hiyo nchini yataongezeka maradufu hadi kufikia MW 4,000 ifikapo mwaka 2025, na kwamba katika kukabiliana na ongezeko hilo Tanzania imelenga kuongeza uwezo wa uzalishaji kufikia GW 10 ifikapo mwaka huo wa 2025.

Mpango Mkuu wa Mfumo wa Umeme wa mwaka 2020 unaonyesha sura pana zaidi ya mahitaji ya nishati hiyo ifikapo mwaka 2044 ambapo yanakadiriwa kufikia MW 17,611 kutoka MW 1,120 yaliyokuwepo mwaka 2019. Mpago huo unaonyesha zaidi kwamba mwaka 2015 mahitaji yatakuwa MW 2,677 na kwa mwaka 2030 yatafikia MW 4,878.

Hivyo umeme unaozalishwa kwa upepo na mawimbi ya baharini, pamoja na ule wa nchikavu ni fursa muhimu katika kuifikia azma hiyo ya serikali,tena mapema zaidi yam waka huo wa 2044.

Sekta ya nishati ya umeme nchini inakabiliwa na changamoto za uchakavu wa miundombinu yake na uhaba wa maji katika mabwawa ya uzalishaji umeme wa maji, uhaba unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, hivyo kusababisha upungufu wa MW 400, kitendo kilichochochea mgawo wa umeme kwa nchi nzima.

Kwa Watanzania walio wengi, suala la giza hivi sasa ni jambo la kawaida, kunakucha bila umeme na kuchwa bila umeme, na kwa mujibu wa takwimu za serikali, takribani theluthi mbili ya Watanzania hawana umeme.

Moses Kulaba kutoka “Governance and Economic Policy Center,” anauelezea uendelezaji wa umeme unaozalishwa kwa upepo na mawimbi ya bahari kuwa fursa muhimu kwa Tanzania, bara na visiwani, ukitumika kuongeza nguvu kwenye vipindi ambavyo nishati hiyo inatumika zaidi na kupunguza mzigo wa mahitaji unaobebeshwa gridi ya taifa, na kuwapatia nishati hiyo wateja wengi zaidi wenye kuihitaji.

Iwapo miradi hiyo itaendelezwa, ni wazi itachochea mabadiliko katika sekta ya nishati itaiharakisha zaidi nchi kufikia lengo lake la upatikanaji wa nishati hiyo ikilinganishwa na jirani zake, na kufikia lengo lake la mpango wa punguza mabadiliko ya tabia nchi na joto duniani yaani, “Nationally Determined Contribution (NDC),” katika muelekeo wa nishati safi.


Itaendelea……….. Hapa > Kesho ya Nishati yetu Tanzania ipo baharini (Sehemu ya Pili)
 
Moja ya ugonjwa wa nchi hii ni kutochangamkia fursa zilizopo kwa wakati muafaka, ajabu hatua huchukuliwa wakati tumepitwa na mabadiliko ya teknolojia.

Tulizembea kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia mkaa wa mawe, ikaja oil and gas, na sasa upepo, hapa ni nchi kavu na baharini kote fursa zipo.

Nalo hili la upepo litapita😳
 
Back
Top Bottom