Kesho ya Nishati yetu Tanzania ipo baharini (Sehemu ya Pili)

Feb 13, 2017
5
8
Soma Sehemu ya Kwanza hapa: Kesho ya nishati yetu Tanzania ipo baharini (Sehemu ya Kwanza)

Nini kifanyike:

Umeme wa upepo ni moja kati ya vyanzo anuwai vya nishati mbadala vilivyopo, na ambavyo havijatumika kutatua tatizo la umeme nchini. Wakati mahitaji yakiogezeka maradufu, ni Dhahiri kwamba mtazamo bado ni ule ule unaotegemea zaidi vyanzo vya maji na gesi, pamoja na ukweli uliopo kwamba chanzo kimoja tu cha upepo kinaweza kuizalishia nchi zaidi ya MW 17,000.

Kuna mambo kaddhaa yanapendekezwa na “Governance and Economic Policy Center,” kwa Tanzania kunufaika na chanzo hicho ikiwemo kuchukuliwa kwa maamuzi ya makusudi ya kisiasa na kisera, ambayo ni pamoja na kuboresha Sera ya Taifa ya Nishati (National Energy Policy) na mapitio ya mkakati wa uendelezaji nishati safi izalishwayo kwa upepo na mawimbi ya bahari, lengo likiwa kuweka uzalishaji nishati hiyo kuwa sehemu ya mpango wa taifa wa mfumo wa uzalishaji nishati ya umeme (National Energy and Power Mix Master plan).

Inapendekezwa pia kufanyika mabadiliko katika muundo wa kitaasisi kwa kuzigawa na kusuka upya TANESCO na ZESCO ili kuruhusu uanzishwaji wa wakala maalumu utakaohusika na umeme utokanao na upepo na mawimbi ya bahari, kama ilivyo kwa nchi kama Marekani ambako jukumu hilo lipo chini ya shirika la usimamizi wa nishati ya bahari “Bureau of Ocean Energy Management-BOEM).

Wakala huyu apewe jukumu maalumu la kuendeleza sekta ya umeme unaozalishwa kwa kutumia upepo na mawimbi baharini, kwa kukusanya rasilimali ujuzi na fedha, kuvutia uwekezaji. Pia kuratibu na kuongoza sekta binafsi, kupunguza madhara kwa wawekezaji, waendelezaji miradi, na kuhamasisha ushirikiano na wadau katika sekta hii.

Governance and Economic Policy Center inapendekeza zaidi kwamba maelekezo mengine ya kisera yatahitaji serikali kununua angalau kiwango cha chini cha nishati ya upepo na mawimbi baharini kitakachozalishwa na wakala huyo apewe jukumu la kukipeleka kiwango hicho kwenye gridi ya taifa au ile ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa kituo hicho, hatua hiyo itatoa nafasi kwa makubaliano ya mpango wa muda mrefu wa ununuzi wa nishati (Power Purchasing Agreement-PPA) kati ya serikali na wawekezaji na kupunguza mashaka kwa wawekezaji kuingia hasara katika miradi hiyo.

Pendekezo jingine ni pamoja na serikali kufanya tafiti zaidi kusaidia miradi zaidi ya umeme wa upepo na mawimbi baharini ikiwemo ukusanyaji taarifa kuonyesha manufaa na uiano wa gharama ya uzalishaji wa umeme wa upepo wa bahari na mifumo mingine. Kwa sasa Tanzania inakosa tarifa za kitalam kama hizi.

Inahitajika pia utashi wa kisiasa na uthubutu wa kutafuta maeneo mapya ya nishati, na kujitoa kwa ajili ya siku zijazo za nishati safi.

Ili kupunguza misukosuko ya kisiasa kutokana na mfumo wa muungano wa pande mbili hizi za Jamuhuri ya Tanzania (Tanzania bara na Zanzibar) na kuweka mizania sawa katika miradi ya kimkakati kama hii, kituo hicho kinashauri mpango kama huu uwemo kwenye mipango ya uchumi wa buluu wa pande zote mbili.

Kwanini umeme wa upepo baharini una tija?

Yapo mashaka kuhusu muda na uwepo wa teknolojia itakayofanikisha uwekezaji kwenye umeme wa upepo na mawimbi ya baharini. Hofu hii inapatiwa majibu na wataalamu wakibainisha kuwa tafiti zao zinaonyesha kuwa miradi ya aina hii inawezekana hivyo kuhitaji uthubutu tu.

Gharama ni nafuu, technologia ipo na jiografia ya bahari ya Tanzania inaruhusu uwekezaji na uzalishaji.

Kwa upande wa gharama, inaelezwa kuwa miradi ya umeme wa upepo na mawimbi ya bahari inawezekana kutokana na uwepo wa upepo zaidi kwenye pwani kuliko nchi kavu, ukiwa na kasi ya wastani wa zaidi ya 50m. Mabadiliko ya teknolojia ya mitambo, uzoefu katika ufungaji umewezesha uchumi mdogo na gharama ya uzalishaji umeme wa upepo wa bahari kushuka kwa kiwango kikubwa.

Gharama hiyo ya uzalishaji umeme wa upepo wa bahari inatarajiwa kushuka kwa asilimia 40 katika muongo ujao, wakati kiwango cha uuzaji umeme katika soko kimeshuka mitambo ya upepo imepanda.

Governance and Economic Policy Center kinabainisha zaidi kuwa gharama ya kuuza umeme imeshuka kwa takribani dola za Kimarekani 50/Mwh, hivyo kusababisha umeme wa upepo kuwa miongoni mwa nishati rahisi zaidi ikilinganishwa na unaozalishwa kwa gesi, makaa ya mawe na jua (solar PVs).

Kituo hicho kinaielezea Tanzania kuwa na faida za kipekee ikilinganishwa na majirani zake katika kunufaika na miradi ya umeme wa upepo na mawimbi baharini, ikiwemo ukubwa wa nchi ikilinganishwa na jirani zake kama vile Kenya, kilometa za mraba 64,000 za bahari na kilometa za mraba 223,000 za ukanda maalumu wa kiuchumi (EEZ).

Faida nyingine kwa Tanzania, ni ukanda wake mrefu wa pwani katika Bahari ya Hindi wenye km 1,424 na nguvu ya mawimbi ya wastani wa KW/m 7.5 na makisio ya juu ya TWh/y 94.

Idadi ya watu katika ukanda huo tu wa pwani ni asilimia 30, jambo linalotoa uhakika wa soko kwa umeme utakaozalishwa.

Sifa zingine ni kwa Tanzania kuwa na kina kifupi cha maji kwenye ukanda wake wa pwani na miamba baharini ambayo itaruhusu ujenzi na uendelezaji wa miradi ya upepo kwa kutumia teknolojia iliyopo.

Pia ukanda mpana wa kipekee wa uchumi (Exclusive Economic Zone-EEZ) unaovuka mwambao wa Zanzibar ufaao kwa vyombo vinavyoelea kwenye kina kirefu cha maji kutia nanga hivyo kuwezesha kupata upepo kwenye kina kirefu Zaidi cha maji kwenye eneo lote la EEZ.

Nishati kutokana na mawimbi ya bahari nayo ni ya uhakika kwani mfumo wa mienendo ya upepo na mawimbi baharini yanatabirika kwa miaka ya mbele, na kwa sababu hiyo inawezekana kukadiria muda na ukubwa wa mawimbi utakavyokuwa na kiwango cha nishati kitakachoweza kuzalishwa.

Mwenendo wa kidunia kuhusu sekta ya nishati inaonyesha kuwepo ongezeko la uzalishaji umeme wa upepo katika jitihada za kuelekea kwenye matumizi ya nishati iliyo safi ifikapo mwaka 2050.

Ni mwenendo ambao, teknolojia ya upepo wa baharini itakuwa teknolojia ya nishati mbadala iliyo nafuu na uchaguzi mzuri ambao nchi zinazoendelea zinaweza kuifikiria zinapoendeleza njia kuelekea kusitisha uzalishaji hewa ukaa katika mifumo yao ya usambazaji umeme.

Uzoefu kutoka nchi nyingine kama Marekani, Uingereza na Canada unathibitisha kwamba mfumo wa mfungamano wa nishati wa aina hii waweza kuwa wa mabadiliko makubwa katika kukabiliana na uhaba wa nishati, na kuielekeza nchi kwenye uzalishaji nishati safi.
 
Back
Top Bottom