Kampuni ya Mohamed Enterprises (METL) yatakiwa kujieleza kuhusu kutoendeleza mashamba ya chai na viwanda vilivyokabidhiwa kwao

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,501
9,280
SERIKALI imeitaka Kampuni ya Mohamed Enterprises (METL) kujieleza kuhusu mashamba ya chai na viwanda vilivyokabidhiwa kwao tangu mwaka 2007.

Agizo hilo limetokana na mashamba hayo yaliyopo Tukuyu kuonekana kutoendelezwa huku viwanda vya kuchakata chai vikiwa havifanyi kazi na hivyo kuwakosesha wakulima wa chai soko la majani mabichi.

Akizungumza na uongozi wa kampuni METL juzi wakati alipotembelea kiwanda cha chai Chivanjee kilichopo Tukuyu, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alisema hajaridhishwa na sababu za kufungwa kwa viwanda vya chai na kutoendelezwa kwa mashamba hayo.

Katibu Mkuu huyo alifanya ziara katika shamba la chai Tukuyu na kujionea kiwanda kikiwa kimesitisha ununuzi wa majani mabichi ya chai na uchakataji tangu Aprili mwaka huu, hali inayoathiri wakulima wa Rungwe.

“Binafsi kama Katibu Mkuu sijashawishika kama kampuni ya METL ina jitihada za makusudi za kufungua viwanda hivi vya Chivanjee na Musekera ili wakulima wa chai wapate soko na nchi ipate mapato yake,” alisema Kusaya.

Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu huyo alitoa maagizo mawili kwa wamiliki wa viwanda hivyo kuwa kabla ya Julai 30 mwaka huu wawasilishe ofisini kwake Dodoma taarifa ya kina inayoonesha ukubwa wa eneo, kiasi kilichopandwa chai na ipi mikakati ya kampuni kuendeleza ardhi waliyopewa na serikali.

“Katika taarifa hiyo nataka METL muwe wakweli kabla ya kuileta kwangu ili tujiridhishe na ukubwa wa shamba hili na matumizi yake,” alisisitiza.

Kusaya alitaja agizo la pili kuwa METL iwasilishe taarifa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara kabla ya Julai 30 mwaka huu, kuelezea mikakati na mpango kazi wa kufufua viwanda vyote viwili.

“Kama mtaleta taarifa isiyo na ushawishi kwa serikali, nitazungumza na wenzangu wa Viwanda na Ardhi kwenda kumuomba Rais Dk John Magufuli ili ayatwae mashamba na viwanda vilivyopewa METL kwa mujibu wa sheria ili apatiwe mtu mwingine mwenye uwezo wa kuendeleza,” alisema Kusaya.

Kwa upande wake Mwakilishi wa kampuni ya METL, George Mwamakula alisema sababu kubwa ya kiwanda cha Chivanjee kusitisha ununuzi wa chai zilitokana na watu waovu kuiba mashine pamoja na miundombinu ya umeme, mota, vyuma na mfumo wa maji.

Kuhusu kiwanda cha Musekera kufungwa kampuni ya METL ilisema imepanga kianze kazi mwaka 2022 baada ya ufungaji mitambo mipya na kukarabati miundombinu.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Kusaya amekitaka Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (ROTCO) cha Tukuyu kuacha kugomea kuuza chai yao kwenye kampuni tanzu ya Wakulima Tea(WATCO) .

Mgogoro wa ushirika na wakulima wa chai Rungwe umefanya wanachama wa ROTCO kutotaka kwenda kuuza majani mabichi kwenye kiwanda cha WATCU wakidai kuwa hawatambui umoja huo na kutaka serikali iwazuie kufanya kazi hadi utatuzi wa mgogoro utakapoisha.

Katibu wa ushirika wa ROTCO, Amos Mwakasengo aliomba serikali iagize kampuni ya Mohamed Enterprises kutekeleza mkataba wa mauzo ya chai na ushirika huo kutokana na kusitisha ununuzi wa majani ya chai bila taarifa kunakoathiri wakulima.

Kusaya alitoa mwito kwa wanachama wa ROTCO wakati majadiliano ya kutafuta suluhu yakiendelea wapeleke majani mabichi ya chai kiwanda cha WATCU kuuza na kujipatia kipato, badala ya kuacha ikiharibika shambani.

Aidha Kusaya alitembelea Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Chai Rungwe na Busokelo ( RUBUTCO-JE) ambapo amewataka wakutane na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kuona namna watakavyoweza kupata mtaji wa kuanzisha kiwanda cha chai cha ushirika huo ili kuwa na uhakika wa soko la chai.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo alitembelea pia kiwanda cha parachichi Rungwe (RAC) na kukitaka kisitishe uamuzi wake wa kutonunua parachichi za wakulima kwa kigezo cha kukosa ubora.
 
Safi sana, huyo Muhindi halafu eti anajifanya anapenda Bongo Flava yetu, ni way man, aridishe mashamba yetu, ...
 
Hawa METL wachague wanachokimudu, siyo lazima kuhodhi kila Mradi; Mkonge, Chai, Ngano
 
Hii cartel ya wafanyabiashara ya chai hapa bongo inabidi ifumuliwe/isambaratishwe haswa katika wakati huu ambao serikali inataka kuanzisha soko la chai kuu la chai hapa nchini. Wata collude na majirani hapo ili ku destabilize hizo juhudi maana kuna nchi na kampuni zitakosa mapato.
 
Jamii forum tuna hitaji thread Kama hizi sio zile "sijui ananipenda !? Au anapenda hela zangu ushauri wenu"

Big up miss zimboka umeandika kitu chenye maelezo ya kina hapo hakuna swali
Pia hongera kwa aliyekuoa.😁😁
Anafaidi umbea, maarifa na akili yako.
 
Back
Top Bottom