Sikukuu ya Nanenane; Wakulima na hatima tete ya kilimo chetu nchini

ACT Wazalendo

JF-Expert Member
May 5, 2014
610
1,540
1. Utangulizi
Leo ni siku ya wakulima nchini, ni sikukuu inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Agosti ndipo lilipokuja jina la Nanenane. Kabla ya kubadilishwa sikukuu ya wakulima ilikuwa inaadhimishwa tarehe saba Julai ya kila mwaka (Saba saba).

Sikukuu ya Nanenane inatumika katika kutafari na kutathmini mchango wa wakulima katika maendeleo ya watu na taifa kwa ujumla wake. Hivyo, kutoa nafasi ya kutazama changamoto zinazowakabili wakulima, maendeleo ya sekta ya kilimo na vikwazo vyake katika uchumi na maendeleo ya taifa.

Katika kuadhimisha siku hii ACT Wazalendo tunapenda kutazama namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakumba wakulima nchini. Kwa kuwa uelewa wa mabadiliko yanayopaswa kufanywa katika nchi yetu yanaanza na kuangalia uhusiano kati ya wakulima, kilimo na mfumo wa uzalishaji uliopo ili kuweza kuweka mkakati utakao lenga kubadili muundo (structure) na mfumo wa uzalishaji hivyo kuwezesha kukomesha, kuondoa vikwazo au mahusiano yasiyoleta tija ya kuendeleza kilimo na kuwanufaisha wakulima walio wengi. Sifa kuu za kilimo chetu kwa miaka mingi ambazo zinahitaji kufanyiwa mapinduzi ni kama zifuatazo;

Kilimo chetu kimetawaliwa na utumiaji wa nyenzo duni

a. Kuzalisha bidhaa za kilimo kwa ajili ya soko la nje.

b. Kiwango cha utegemezi kwenye soko la nje ni kikubwa zaidi.

c. Kukosekana kwa uhakika wa bei za mazao

d. Kutokuwepo kwa ruzuku za uzalishaji.

Ni ukweli kwamba bado Tanzania ni nchi ya wakulima, wafugaji na wazalishaji wengine wadogo waishio vijijini na mijini wanaotegemea mnyonyororo wa thamani wa kilimo.

Maendeleo ya nchi ni kuinua hali ya maisha ya asilimia 65% ya Watanzania wenzetu kwa kuboresha mfumo wa uzalishaji na kubadili uhusiano wa sasa.

2. Changamoto za wakulima
Nchi yetu inategemea mchango wa wakulima wadogo kwa asilimia 100 kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine ya viwandani, kuingiza fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa au mazao nje. Aidha, mchango wa kilimo kwenye ajira kwa sasa ni zaidi ya asilimia 61 wameajiriwa katika sekta ya kilimo.

Licha ya mchango mkubwa wa wakulima katika uchumi wa nchi yetu na taifa kwa ujumla bado kuna tishio kubwa kwa ustawi wa wakulima wetu. Changamoto kubwa ni wimbi kubwa la uporaji wa ardhi ya vijiji na za wakulima kwa kigezo cha uwekezaji katika Kilimo; Pia, tishio la kuporwa kwa uhuru wa wakulima katika uzalishaji, uhifadhi wa mbegu na mazao ya kilimo kupitia dhana ya kilimo biashara.

Tatu, kuwepo kwa tija ndogo katika uzalishaji kunakosababishwa na matumizi hafifu ya Teknolojia ya wakulima wenyewe.

Katika kutafakari Maendeleo ya Kilimo nchini kwa mwaka huu ACT Wazalendo tunaitaka Serikali isifanye mzaha kabisa kuhusu uwekezaji kwenye kilimo na wakulima nchini, haiwezekani nchi hii taswira ya umasikini iwe ni mkulima ni lazima hatua za makusudi zichukuliwe kwa ajili ya kufanya mapinduzi katika kilimo kwa kuifungamanisha sekta ya Kilimo na Viwanda, miongoni mwa hatua tunazozipendekeza ni kama ifuatavyo;

i. Serikali inapaswa kulinda uhuru wa wakulima juu ya uzalishaji na soko la mazo ya kilimo na kuweka mkazo kuwa chakula ni haki ya kila mwananchi ambayo haiwezi kuwekwa kwa vigezo vya kupata faida, pamoja na kuchukua hatua zifuatazo;

a) kuhakikisha uhifadhi, uzalishaji na usambazaji wa mbegu asili ima ziwe za jadi au zilizoboreshwa na kukomesha matumizi ya mbegu zilizofanyiwa uandisi jeni (genetically modified seeds).

b) Kudumisha na kuweka msisitizo wa matumizi ya mbinu za kilimo cha kiikolojia(kioganiki) zenye kutumia ujuzi asilia na kuachana na matumizi ya madawa ya viwandani ambayo huathiri mazingira.

c) Kuondoa unyonyaji wa watu wa kati (middlemen) kwenye soko la mazao kwa Kuimarisha mfumo wa taarifa ya masoko ya mazao na serikali kuhusika kikamilifu kwenye hifadhi ya mazao na kuanzisha mfumo wa soko kupitia soko la bidhaa (commodities exchange) ambao utashirikisha wakulima wenyewe.

ii. Serikali iimarishe uhakika wa upatikanaji, umiliki na matumizi ya ardhi ya kijiji kwa madhumuni ya kuzalisha au kukidhi haja ya kijamii (social function) na sio kulimbikiza faida, kuwekea rehani (dhamana) au kucheza bahati nasibu.

iii. Serikali isimamie kuanzishwa kwa viwanda vidogo maeneo ya vijijini vinavyoendeshwa, kumilikiwa na kusimamiwa na wakulima wenyewe kupitia vyama vyao vyao vya ushirika ambavyo vitaweza kuzalisha ajira na kuchakata mazao.

iv. Itunge Sheria ya kilimo ili kuwe na mifumo ya kikodi ya kisheria na si kila siku taasisi za serikali kujipangia kodi, ushuru na tozo na kumuumiza mkulima.

v. Kufungamanisha kilimo na viwanda illi viwanda vizalishe zana za kilimo na kupandisha thamani mazao na bidhaa za kilimo na kilimo kilishe viwanda nchini badala ya kuuza mazao ghafi kama ilivyo sasa.

vi. Kuchochea uzalishaji wa Mbolea nchini kwa kuharakisha ujenzi wa viwanda vya mbolea, Serikali iongeze mtaji shirika la Mbolea Tanzania (TFC) lifanye biashara na kufikisha mbolea mpaka vijijini, kubwa zaidi Serikali ifungamanisha utekelezaji wa mradi wa kuchakata Gesi asilia (LNG) na ujenzi wa kiwanda kikubwa cha Mbolea ya UREA ambayo inatokana na masalia ya Gesi ya LNG.

vii. kuimarisha Ushirika, vyama Msingi na Vyama msingi viendeshwe kidemokrasia kwa matakwa ya wakulima wenyewe.

ACT Wazalendo tunatuma salamu za mshikamano kwa wakulima wote nchini, tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kulisha, kuajiri na kukuza uchumi wa nchi hii ipo mabegani mwao, Tutaendelea kupigania haki na hali za wakulima nchini na kuhakikisha Kilimo kinalinyanyua Taifa.

Imetolewa na,
Ndugu. Mtutura Abdallah Mtutura
Msemaji wa Sekta ya Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika
ACT Wazalendo.
Dar es salaam- Tanzania
08/08/2023.
 
Back
Top Bottom