Kama huu ndio udikteta na Kushindwa kwa rais Magufuli basi tunamhitaji kwa zaidi ya miaka 100!

Chabruma

JF-Expert Member
Sep 19, 2013
5,660
1,777
Na Joseph Martin, Nottingham, UK.

NIKIWA katikati mwa viunga vya jiji la London mwishoni mwa wiki, nilipata fursa ya kupumzika katika eneo maarufu la kitalii “the London Eye.” Nikiwa pale, pembezoni mwa Mto Thames, nikipitia habari za nyumbani katika mitandao nikamsikia kiongozi mkuu wa Chama cha ACT, Zitto Kabwe.

Katika hoja kadhaa wa kadhaa kuhusu Bajeti ya Serikali, Bw. Zitto alisikika akisema kitu ambacho nilipata kuwasikia pia wabunge kadhaa wa kambi ya upinzani wakikisema huko nyuma; kwamba Rais John Pombe Magufuli (JPM) anaiendesha nchi kidikteta!

Wakati Zitto akitoa tuhuma hizo nzito alikuwa katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika hadharani, kama sikosei, kwenye ofisi za chama hicho jijini Dar es Salaam. Naamini hata baada ya mkutano huo alirudi salama kabisa nyumbani kwake na kuendelea na shughuli zake salama akiwa katika ardhi ya “Rais Dikteta.”

Kabla ya kauli ya Zitto, kama nilivyosema awali, wabunge kadhaa wa kambi ya upinzani akiwemo Tundu Lissu, Freeman Mbowe, Joseph Mbilinyi, Peter Msigwa na wengineo, tumepata kuwasikia wakitoa tuhuma kama hizo. Ni kama vile ni tuhuma ya kimkakati.

Wote hao naamini siku walizotoa kauli hiyo nzito na hata sasa wanapoendelea kutoa kauli hiyo tena na tena, bado wanaendelea kufurahia maisha ya amani, yasiyo ya bughudha wala mikwaruzo katika nchi ya “Rais Dikteta.”

Unapoyasikia haya hasa kwa sisi tulioko nje ya Tanzania na tuoliona Bara la Afrika lilivyo na tunaofuatilia kwa karibu kinachoendelea na kinachotokea huko nyumbani unapata mashaka maradufu; kuna nini kinaendelea Tanzania? Siasa zetu zimekumbwa na mdudu gani hasa?

Hivi Tanzania hii inayotajwa kila mahali tunapojitambulisha kuhusika nayo kama nchi yetu ya asili na ya mfano leo imepatwa na nini kuona watu waliohuru, wanaofikiria huru, wanatembea huru inapotokea wakazuiwa kutenda jambo tena kwa sheria walizoshiriki kutunga wenyewe wageuke kuipaka nchi matope kiasi hiki?

Miaka michache nyuma sote tulipaza sauti kulalamikia ufisadi, uzembe Serikalini, Serikali kutokusanya mapato, wafanyakazi hewa na hata kulalama kuwa kuna taasisi nyingi mzigo na zinazoongeza tatizo jingine; matumizi mabaya na ya hovyo ya fedha za umma

Pamoja na hatua kuchukuliwa na viongozi waliopita, ilifika hatua kambi hii ya kina Zitto, Mnyika, Lissu, Msigwa na wengineo ilitamka moja ya kauli za kuudhi kupata kutokea kwa kadiri ya umri wangu pale walipoitangaza Serikali ya Awamu ya Nne kuwa ni dhaifu.

Nini kimetokea kutoka “Serikali dhaifu” hadi “Serikali ya Kidikteta.” Nikiwa mtafiti niliamua kuzama kidogo katika kuangalia suala hili kwa kina na kujiuliza maswali kadhaa.

Kosa ni mageuzi?

Inaonekana dhahiri kuwa kosa moja kubwa la Rais Magufuli ni kutaka kuleta mageuzi na utendaji wa mambo tofauti na watu walivyozoea. Kama tumepata mtu anayetaka kuleta mageuzi haya nadhani tulipaswa hata kama si kumuunga mkono basi kumpa muda.

Nimuonavyo, Rais ameanza vyema kusafisha nyumba yake kwa kupambana na uzembe Serikalini, ufisadi kwa ujumla wake, ameanza kuzipa mamlaka taasisi za Serikali na mihimili ya dola uhuru wa kutenda mambo kwa ufanisi yeye akitaka matokeo zaidi, ameanza kuwapa wananchi sauti na nguvu ya kudai na kupata huduma nzuri. Kama huu ndio udikteta wa Magufuli basi tunauhitaji miaka 100!

Kosa ni kuongeza mapato?

Katika taswira yake ya kimageuzi, Rais Magufuli ameanza na eneo hili kwa nguvu zake zote. Nilikuwa napitia hesabu za Serikali. Mpaka mwaka jana tulikuwa na ukusanyaji wa mapato chini ya shilingi trilioni moja kwa mwezi.

Alipoingia na kashikashi zake, bila hata kubadili sheria, sera wala taasisi, ufuatiliaji tu wa kile ambacho Serikali inapaswa kukipata kuna miezi nimeona mapato kwa mwezi yalifika mpaka trilioni 1.4 na sasa yamesimama katika wastani wa juu ya trilioni moja. Kama huu ndio udikteta wa Magufuli basi tunauhitaji miaka 100!

Kosa ni nidhamu Serikalini?

“Kule Bagamoyo ulikokuwa mara nyingi ukinipigania nakuwa nimekwenda hadi ukashangaa kuna nini sasa hivi ni zaidi ya miezi minne sijafika. Huyu Mwamba katutumbua,” ni kauli ya mjomba wangu mmoja aliyeko katika utumishi wa umma akiongeza:

“Kuna kazi kwa utendaji ule wa kimazoea wa zamani mngeweza kuzifanya ofisini kwa siku hata tatu lakini mnalipana kwenda hoteli za Bagamoyo au Morogoro au Dodoma kukaa hata wiki mbili.”

Ingawa sijawahi kufanya kazi katika ofisi za umma, kwa mfano huu tu wa jamaa yangu huyo ni dhahiri kuwa eneo hili lilikuwa likipoteza mapato mengi ya Serikali. Amekuja “mwamba” kama anavyosema mjomba wangu na kubadili namna watendaji wanavyopaswa kuenenda katika utumishi wao wa umma na bahati mbaya “mwamba” amegusa hadi wanasiasa wenzake tena wakiwemo wale waliokuwa wakitaka mabadiliko, imekuwa balaa!

Tulitaka watumishi wa umma waendelee “kugongana” angani kama alivyopata kusema Waziri mmoja wa zamani? Tulitaka magari ya umma yaendelee “kugongana” katika miji ya Bagamoyo, Morogoro, Dodoma na kwingineko watu wakihama ofisi zao kwenda kutumbua fedha za umma bila sababu? Kama kufanyiakazi haya ndio udikteta wa Magufuli basi tunauhitaji miaka 100!

Kosa ni kuchukua hatua?

Niliwahi kurejea nyumbani kipindi flani kwa kazi za utafiti nikafanikiwa kuingia Bungeni mjini Dodoma. Sikumbuki siku hiyo kulikuwa na mjadala wa nini lakini namkumbuka mbunge Peter Msigwa alivyokuwa akipigiwa makofi wakati akijenga hoja kuwa Serikali ya CCM ilikuwa imechoka kwa viongozi wa Serikali yake kushindwa kuwachukulia hatua mafisadi.

Leo ameingia “mwamba” na akaanzia na Bandari-chanzo muhimu cha mapato kwa nchi kilichokuwa “shamba la bibi.” Hadhi ya Bandari imerejea. Akaingia katika mashirika ya umma na kuchukua hatua muafaka: Takukuru, Shirika la Reli, Mamlaka ya Vitambulisho na kwingineno.

Kuna watendaji wa umma waliokuwa wakiaminika kuwa “untouchables” kwa kiasi cha hata kambi ya Zitto na wenzake kuwalalamikia sana huko nyuma, alipoingia “Mwamba” leo wako wanakokujua wenyewe huenda “wakilimia meno.”

Kijana wangu mmoja barobaro na mbunifu mkubwa katika eneo la teknolojia baada ya kuhaha sana juzi ananiambia kwa sasa ukienda kuongea na kiongozi wa ofisi ya umma kuhusu ubunifu wako walau unapata nafasi ya kusikilizwa. Waliokuwa hawana muda hata wa kuwasikiliza wananchi sasa wanajua wasipofanya hivyo yatawafika.

Nikiwa Dodoma katika safari hiyo ya kitafiti nilipata fursa ya kuelewa maisha ya kisiasa ya wabunge. Rafiki yetu mmoja mbunge kijana hivi siku moja alilazimika kupita katika duka moja kununua kamusi.

Tulipomuuliza kamusi ile ilikuwa ya nini, akajibu kuna hoja angewasilisha kesho yake, kuchangia katika mjadala wa moja ya taasisi za umma. Akasema kuna kipengele ametakiwa kukichangia kwa nguvu zake zote kwa faida ya taasisi hiyo na akadai, bila kupepesa macho, amepewa “deal” zuri tu.

Mchango wa mbunge huyo unaonekana ungeisaidia taasisi hiyo kufikia malengo yake hivyo baadhi ya misamiati ya mbwembwe kutoka kwenye kamusi hiyo ingempa msamiati ambao wakati anachangia angehalalisha “deal” hilo. Leo wabunge kadhaa zama za “mwamba” wako mahakamani kujibu tuhuma za “deal.” Kama huu ndio udikteta wa Magufuli basi tunauhitaji miaka 100!

Haki za Kisiasa na Kiraia

Nimemsikia Zitto akilalama kuwa haki hizi zinabinywa. Kadiri alivyoongea nilipata picha kuwa mikutano ya kisiasa na kiraia nchi nzima imezuiwa. Nilipata hasira kidogo na Serikali katika hili. Lakini nilipofuatilia nikabaini kuwa taasisi mbalimbali za kisiasa na kiraia zinaendelea na mikutano yao kama kawaida isipokuwa tu pale Jeshi la Polisi linapotoa maagizo vinginevyo.

Nikatathmini hali hii na kuona kwanza kuna upotofu mkubwa wa aina mbili. Mosi, haki za kisiasa na kiraia kama zilivyoainishwa katika Mkataba wa Kimataifa wa Geneva (Covenant on Civil and Political Rights, 1966) hazikutolewa kijumla jumla tu, zinavizuizi na ndio maana unaona hata leo wale waandamanaji huku Ulaya hasa kule Ufaransa wanakumbana na vichapo vikali kutoka kwa polisi.

Mkataba huo na mingine ya kimataifa imeainisha sababu bayana kama nne hivi za kuzuiwa utekelezaji wa haki hizo. Kuna sababu kama usalama wa nchi, amani na mengineo na mikataba hii inasema nchi wanachama wataweka utaratibu wa namna ya kutekelezwa haki hizi.

Sasa haiwezekani kila mtu au kikundi kikaamka asubuhi na kusema tunaandamana huku au kule au tunamjadala huu au ule, lazima pawepo na mpangilio. Hoja hii inatuleta katika upotofu wa pili. Hapo Tanzania nafahamu kwamba Jeshi la Polisi ndilo lenye mamlaka ya kuona katika kusanyiko fulani suala la amani na usalama wa raia litakuwaje?

Nimeshangazwa kusikia yanapotokea masuala mengi yanayoratibiwa na mihimili au taasisi nyingine kwa mujibu wa sheria analaumiwa Rais na hata kutakiwa avunje sheria kuingilia mihimili hiyo.

Hivi Rais wa nchi gani anayeshughulika na kila kitu. Kukitokea tatizo Bungeni, Rais anasema nini?Kukitokea tatizo Mahakamani Rais yuko wapi? Na hata hili, badala ya kuhoji polisi walitumia hoja gani kuzuia mikutano ya wapinzani na hata kama wameenda nje ya uwanda wao wa kisheria tuwashtaki, tunakimbilia kumkejeli Rais eti amekuwa dikteta?

Hivi Sheria ya Haki na Madaraka ya Bunge kwa mfano inayolipa Bunge mamlaka ya kuamua na kuendesha shughuli zake ni wapi inamruhusu Rais kulipangia Bunge muda gani liwe live na muda gani lisiwe live?

Ni wapi katika Sheria ya Jeshi la Polisi kuna kifungu kinachomtaka Rais, hata kama polisi wameona kusanyiko Fulani lisiwepo, yeye asewe liwepo? Kama Rais kuacha mihimili/taasisi ziendeshe shughuli zake kisheria kama zilivyopitishwa na Bunge ndio udikteta wa Magufuli basi tunauhitaji miaka 100!

Ningeweza kuandika na kuandika lakini yatosha tu kuhitimisha kwamba kwa kadiri ya nilivyomsikia Zitto Kabwe na viongozi wengine wa upinzani, wana baadhi ya hoja nzuri tu za kusikilizwa kuhusu bajeti au masuala mengine ya umma. Na naamini zile hoja za0 zenye mantiki zinaonekana dhahiri na wahusika watazifanyiakazi.

Lakini si hili la kubeza jitihada za Rais na Serikali yake eti kuwa ni “dikteta” kwa sababu tu anafanya yale ambayo yako tofauti na mitazamo yao, mazoea yao au matakwa yao au kwa sababu yamegusa maslahi yao. Rais Magufuli, ninavyoamini, anapigania maslahi mapana zaidi ya Taifa na ni dhihaka kwa Taifa hili, vizazi vyake vya sasa na vijavyo, kumkatisha tama mwanamageuzi huyu.

Ndio maana kwa haya ambayo kwa sasa anayafanya nimeshawishika kuamini kuwa kama huu ndio udikteta anaolaumiwa nao Rais Magufuli basi ni aina ya staili ya utendaji ambayo tungehitaji iendelee hata kwa miaka 100 ijayo!

========

Maoni Mengine kuhusu Mafanikio ya Rais John Pombe Magufuli;
Wapo watu kadhaa ambao wamekuwa wakidai eti Rais wetu ameshindwa katika utawala wake. Nakubaliana nao kwa asilimia 100 kwani hakuna mtu aliye mkamilifu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Katika uzi huu, nimeorodhesha mambo kadhaa ambayo Rais wetu ameshindwa na akiendelea kwa mwendo huu hakika mpaka 2020 wananchi watakuwa wamepoteza matumaini naye na Edward Lowasa atatinga kwa kishindo magogoni. Mambo haya niliyoorodhesha ni yale tu ambayo Rais wetu ameshindwa kwa kipindi cha miezi saba aliyokaa madarakani.

1. Kama kutumbua majipu kwa waliofilisi nchi hii ni kushindwa, acha ashindwe tu

2. Kama kutenga fedha trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge nimkushindwa, acha ashindwe.

3. Kama kuwabaini zaidi ya watumishi hewa 12,000 ni kushindwa, naomba aendelee kushindwa.

4. Kama kuboresha huduma za matibabu pale Muhimbili ni kushindwa, aendelee kushindwa

5. Kama kuwapatia madawati watoto wetu ni kushindwa, na aendelee kushindwa

6. Kama kuwapatia elimu bure watoto wetu kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne nimkushindwa, namtakia kila la kheri katika kushindwa kwake.

7. Kama kufunga Flow Meters mpya pale Bandarini ili kudhibiti wizi wa mafuta ni kushindwa, natamani aendelee kushindwa milele

8. Kama kubaini makontena yaliyoibwa pale Bandarini na kuwashinikiza wahusika walipe na wamefanya hivyo ni kushindwa, aendelee kushindwa

9. Kama kutenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa flat 20 za ghorofa 3 ambazo zitaaccomodate wanafunzi 4,000 pale UDSM ni kushindwa, na ashindwe

10. Kama kupanua barabara ya Morocco hadi Mwenge kwa fedha zilizopangwa kwenye sherehe ya Uhuru ni kushindwa, aaaaah. Naomba aendelee kushindwa

11. Kama kununua ndege tatu kwa shirika letu la ATC ili kuhuisha safari zake ni kushindwa, naungana na wanaosema kashindwa.

12. Kama kurejesha shirika letu la TTCL na sasa linamilikiwa kwa asilimia 100 na umma ni kushindwa, hakika namtakia kila la kheri katika kushindwa.

13. Kama kuanzisha mahakama maalum ya Majizi na Mafisadi ni kushindwa, hakika anastahili kuitwa Rais aliyeshindwa.

14. Kama kushinda kwa kishindo uchaguzi Mkuu na kukipatia chama cha Mapinduzi majority bungeni ni kushindwa, sina shaka na kushindwa huko

15. Kama kurejesha mahusiano na nchi ya Rwanda ambayo yalidhorota awamu ya mwisho ya utawala wa Kikwete ni kushindwa, basi na ashindwe

16. Kama kushinda zabuni ya ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga ni kushindwa, kwa kiroho safi namtakia aendelee kushindwa.

17. Kama kuwapatia tume ya taifa ya uchaguzi shilingi bilioni 12 ili wajenge Ofisi yake na Hostel Dodoma ili kuokoa zaidi ya bilioni 1 wanazolipa kama pango kwenye majengo waliyopanga Dar es Salaam ni kushindwa, natamani aendelee kushindwa daima.

18. Kama kuwapatia mikopo ya kutosha wanafunzi wa elimu ya juu ni kushindwa, hakika nampongeza kwa kuendelea kushindwa

19. Kama kupunguza kodi kwa wafanyakazi kutoka asilimia 11 hadi asilimia 9 ni kushindwa, nakubaliana na wale wote wanaosema Rais kashindwa.

20. Kama kuiwezesha TRA kukusanya mapato ya kodi hadi kufikia trilioni 1.4 kwa mwezi ni kushindwa, safi sana.

Kwa hakika orodha ni ndefu na nina hakika na wewe msomaji utaendelea kuweka orodha ya mambo ambayo Rais Magufuli kashindwa. Tukumbuke kuwa Rais ameshindwa kwenye mambo haya yote kwa muda mfupi tu aliokaa madarakani ambao hauzidi miezi 7. Ninaamini akiendelea kukaa kwa muda wa miaka tano ya utawala wake madarakani, atakuwa ameshindwa vibaya mno na 2020 hatapata kitu.

Nawasilisha
 
mtoa mada naomba uniambie kwanza wewe unaelewa nini maana ya udikteta? tuanze hapo kwanza...
 
Endelea kubeba mabox.Halafu kesho uje na mada ya Diaspora.
 
Waraka mzuri sana na wa kizalendo haswa, bahati mbaya ni kwamba watakaokuelewa ni wale wenye kutanguliza uzalendo wa nchi mbele na sio vyama vyao.

Inasikitisha kuona kwamba kundi kubwa la watu mitandaoni especially vijana wenzangu wanatanguliza uchama mbele kuliko utaifa kwanza, yaaani imekua vita ya ccm vs wapinzani na sio vita ya wananchi vs umaskini.

Natamani sana kuona nchi yangu ikikua kiuchumi na maendeleo yakionekana kwa macho na sio kwenye takwimu za kwenye makaratasi ya waheshimiwa lakini hatutaweza kamwe kufanya mageuzi ya kiuchumi kama tutaendelea kama nchi kushupalia mambo ambayo hayatusaidii sisi kwa namna yoyote ile, ni lazima wananchi tukubali kuachana na mijadala inayojikita katika kujadili watu na kuanza kuipa kipaumbele mijadala ambayo itajadili issues zinazogusa moja kwa moja uchumi na maendeleo ya nchi yet, na ni muhimu sana wananchi tukaacha kuruhusu kupelekeshwa na wanasiasa hata kama tunashabikia itikadi zao.
 
waraka mzuri sana na wa kizalendo haswa, bahati mbaya ni kwamba watakaokuelewa ni wale wenye kutanguliza uzalendo wa nchi mbele na sio vyama vyao.
inasikitisha kuona kwamba kundi kubwa la watu mitandaoni especially vijana wenzangu wanatanguliza uchama mbele kuliko utaifa kwanza, yaaani imekua vita ya ccm vs wapinzani na sio vita ya wananchi vs umaskini,
natamani sana kuona nchi yangu ikikua kiuchumi na maendeleo yakionekana kwa macho na sio kwenye takwimu za kwenye makaratasi ya waheshimiwa lakini hatutaweza kamwe kufanya mageuzi ya kiuchumi kama tutaendelea kama nchi kushupalia mambo ambayo hayatusaidii sisi kwa namna yoyote ile, ni lazima wananchi tukubali kuachana na mijadala inayojikita katika kujadili watu na kuanza kuipa kipaumbele mijadala ambayo itajadili issues zinazogusa moja kwa moja uchumi na maendeleo ya nchi yet, na ni muhimu sana wananchi tukaacha kuruhusu kupelekeshwa na wanasiasa hata kama tunashabikia itikadi zao.
Mkuu, kwani aliyeandika makala hii kajitambulisha ni mfuasi wa chama gani?
 
Back
Top Bottom