Chilojnr
JF-Expert Member
- Jul 5, 2012
- 302
- 1,306
Mwandishi: Nyemo Chilongani.
0718069269.
Sehemu ya 01
“I need to see his picture,” (Ninahitaji kuiona picha yake) alisikika mwanaume mmoja kwa hasira, aliongea kwa sauti ya juu kiasi kwamba kila mmoja ofisini alishtuka, hakuamini kama ingetokea siku moja bosi wao angeongea kwa hasira kama alivyofanya siku hiyo.
Ilikuwa ni ndani ya makao makuu ya Shirika la Kijasusi la Kimarekani, CIA (Central Intelligence Agency) yaliyokuwa huko Langley, jijini Virginia nchini Marekani.
Mkononi mwake alikuwa na kifaa kidogo kiitwacho kindle ambacho hutumika kusomea vitabu mbalimbali, na wakati huo alikifungua kitabu kiitwacho There Is No God At All kilichomaanisha Hakuna Mungu Kabisa kilichoandikwa na mwandishi aliyejulikana kwa jina la Williams McCannon.
Mitaani kitabu hicho kilikuwa gumzo, kila mtu alikuwa akikizungumza, kwa watu ambao hawakuwa wamekisoma, haraka sana wakaingia kwenye tovuti ya Amazon na kuanza kukitafuta na kukinunua kwa dola 20 ambazo zilikuwa ni zaidi ya shilingi elfu arobaini na tano kwa pesa za Kitanzania.
Kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Twitter na sehemu nyingine ni jina lake tu ndilo lililokuwa likitawala. Kwenye televisheni, alikuwa akizungumziwa yeye na kitabu chake kilichokuwa na nguvu kubwa ya ushawishi.
Kila mtu aliyekisoma kitabu hicho cha simulizi alimwambia mwenzake. Kilikuwa kitabu kizuri, kilichokuwa na mvuto hata kwa kukiangalia kwa nje na ndani, kwa jinsi matukio yake yalivyokuwa yamepangwa, yalivyoelezewa kwa undani hapakuwa na mtu aliyeamini kama kungekuwa na mwandishi aliyekuwa na uwezo wa kuandika kitabu kizuri kama hicho kwani waliamini waliokuwa wakiandika vitabu vya namna hiyo walikufa miaka mingi iliyopita akiwemo William Shakespeares.
Kwa siku mbili tu, tayari kulikuwa na watu milioni moja ambao walikinunua kitabu hicho kwenye tovuti hiyo kitu kilichowashangaza hata wamiliki wa tovuti hiyo, walihisi kitabu hicho kilikuwa na kitu kikubwa sana hivyo hata nao kukichukua na kuanza kukisoma.
Mwandishi hakuwa akijulikana ila hakuwa mgeni katika tovuti hiyo. Watu walimtafuta humo, walihitaji kumjua, walitaka kujua huyo mwandishi aliyeandika vitu hivyo alifananaje, alikuwa na muonekano gani lakini kwa bahati mbaya, hakukuwa na picha yake yoyote ile kitu kilichomhuzunisha kila mmoja.
Kitabu hicho kilimzungumzia kijana mdogo, mwenye umri wa miaka ishirini na mbili ambaye alipotezana na mpenzi wake, alimpenda tangu walipokuwa wadogo kabisa, walipanga kuoana na kuwa pamoja lakini baada ya msichana huyo kusafiri na kwenda Marekani kusoma, kila kitu kikabadilika.
Msichana huyo wa kwenye simulizi aliyeitwa kwa jina la Esta hakuonekana tena, ilisemekana kwamba alifariki dunia katika shambulio la majengo pacha ya WTC (World Trade Center) ambayo yalishambuliwa mwezi Septemba mwaka 2001 huko New York nchini Marekani.
Kijana huyo ambaye aliachwa nchini Nigeria, akaamua kuondoka kwa njia za panya kuelekea nchini Marekani. Huko njiani alipitia vikwazo vingi mpaka kuingia, alipopata uhakika kwamba mpenzi wake aliuawa kwenye majengo hayo ndipo akaanza kufanya uchunguzi wa juu kuhusu shambulio hilo.
Kwa jinsi Williams alivyouelezea uchunguzi uliofanywa na mhusika huyo kwenye kitabu hicho ndicho ambacho maofisa wa CIA walipoamua kumtafuta mwandishi huyo.
Walijua kabisa kulikuwa na mengi aliyokuwa akiyafahamu, kusingekuwa na urahisi wa kuyazungumzia matukio hayo kwa kina zaidi na wakati alikuwa mwandishi tu na inawezekana hakuwahi kuishi nchini Marekani au hata kwenye nchi za Kiarabu.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Bwana Peter O’Brain alichanganyikiwa, aliwapanga vijana wake, aliwaambia wafanye kila liwezekanalo kuhakikisha mwandishi wa kitabu hicho anapatikana haraka sana kwa kuwa walihitaji kufahamu mambo mengi zaidi kuhusu yeye, kwa nini aliamua kuandika simulizi hiyo ambapo kulikuwa na vyanzo mbalimbali, vile ambavyo wao kama wapelelezi hawakuwa wakivifahamu kabisa.
Walipata mawasiliano yake, namba zake zilionyesha alikuwa akiishi nchini Nigeria. Walichokifanya ni kuwatuma wapelelezi huko kwa lengo la kumtafuta mwandishi huyo kimyakimya.
Walifika huko na kuanza msako wao kwa kutumia namba zilezile. Waliuliza sana, kila kona lakini hawakufanikiwa kumpata na kitu kilichowashangaza zaidi, hata Wanigeria wenyewe walisema hakukuwa na Mnigeria aliyekuwa na uwezo wa kuandika hadithi ya namna ile, inawezekana alikuwa ni Mmarekani ambaye hakutaka kugundulika.
“Mnigeria aandike hadithi ya namna ile, yenye vyanzo vya siri kiasi kile! Hakuna Mnigeria huyo,” alisema jamaa mmoja, alipinga kabisa, kwa jinsi kitabu kile kilivyokuwa kimeelezewa, ilikuwa ni vigumu kuamini kama kungekuwa na Mwafrika yeyote ambaye angekuwa na uwezo wa kuandika namna ile.
Namba zile hazikupatikana. Hilo halikuwa shida, maofisa hao wa CIA wakaondoka na kuelekea katika kampuni ya simu za mkononi ya MTN na kuulizia kuhusu namba hizo.
Haraka sana meneja wa kampuni hiyo akawachukua na kuwapeleka kwa vijana wa IT na kuwaambia kuhusu namba hizo, haraka sana vijana hao wakaanza kuangalia kwenye system zao kuangalia usajili wa namba hizo lakini kitu cha ajabu kabisa system ilionyesha namba hizo hazikuwa zimeanza kutumika.
“Unasemaje?”
“Hizo namba hazijaanza kutumika. Mna uhakika kwenye kitabu zimeandikwa namba hizo?” aliuliza kijana mmoja na hivyo ofisa mmoja kumuonyeshea kupitia simu yake.
“Hii ndiyo maana ya mwandishi. Huyu jamaa ni genius,” alisema jamaa mmoja miongoni mwa wale IT.
Maofisa wale wakaondoka, walichanganyikiwa, hawakuwa na mategemeo yoyote yale ya kumpata mwandishi huyo. Hawakujua alikuwa mahali gani lakini zaidi, kubwa kuliko yote ni kwamba hawakujua alifananaje kwa kuwa kwenye kitabu hicho cha mtandaoni hakukuwa na picha yake yoyote ile.
Haraka sana wakapiga simu nchini Marekani na kuwaambia kile kilichotokea, kwamba hawakufanikiwa kabisa kumpata mtu huyo na hata zile namba ambazo ziliwekwa kwenye kitabu kile hazikuwa zimeanza kutumika, ilimaanisha kuwa mwandishi huyo alijua dhahiri alikuwa akienda kutafutwa baada ya kukitoa kitabu kile na ndiyo maana aliamua kutokuandika namba zake halisi.
“Ila kuna barua pepe, kwa nini tusiidukue na kuangalia humo?” aliuliza ofisa mmoja.
Kwa jinsi walivyokuwa wamchanganyikiwa hakukuwa na mtu aliyelifikiria hilo. Haraka sana wakaingia kwenye barua pepe yake kwa njia ya udukuzi na kuanza kuangalia kile kilichokuwa kikiendelea.
Waliona jinsi jamaa huyo alivyokuwa amejisajili kwenye tovuti ya Amazon, alivyowasiliana nao na hatimaye kukiweka kitabu chake hicho.
Hakikuwa cha kwanza, waligundua kulikuwa na kitabu kingine ambacho alikiweka huko, hicho kiliitwa ‘The Blood City’ yaani kikiwa na maana ‘Jiji la Damu’.
Haraka sana wakakinunua na kuanza kuangalia tena namba zake. Zilikuwa humo, walijaribu kuzifananisha na zile ambazo ziliandikwa kwenye kile kitabu kipya.
Hazikuwa na utofauti, zilikuwa zilezile, kilichowaumiza kichwa ni kwa sababu gani mwandishi huyo aliamua kuandika vitabu hivyo na kuweka namba ambazo hazikuwa zikitumika?
“NI lazima tuwasiliane na Amazon kwanza! Kuna kitu nimewaza,” alisema jamaa mmoja, huyo aliitwa Sincliar, alikuwa na kipara, mmoja wa watu waliokuwa katika kitengo cha wale waliokuwa wakifikiria sana katika shirika hilo.
“Kitu gani?”
“Kitabu chake kinauzwa kwenye tovuti, si ndiyo?”
“Ndiyo!”
“Pesa si zitakuwa zinakwenda kwenye akaunti yake benki? Basi ni lazima tuijue hiyo akaunti kwanza,” alisema Sinclair.
Alichokisema kilikuwa sahihi kabisa, hakukuwa na muda wa kupoteza, haraka sana wakaondoka na kuelekea makao makuu ya Amazon yaliyokuwa huko Seattle, Washington.
Walipofika huko, wakaomba kuonana na meneja ambaye baada ya kusikia alikuwa akiitwa na maofisa wa CIA, haraka sana akawaita ofisini kwake na kuanza kuzungumza nao.
Alijua walichokuwa wakihitaji kuongea naye! Alisikia mambo mengi kuhusu kitabu kile, kilinunulika sana na katika siku ya nne tayari kulikuwa na watu milioni sita walipakua kitabu kile huku wengine wakiendelea kumiminika kila siku.
Walimwambia kuhusu jambo lao, walihitaji kumfahamu mwandishi ambaye aliandika kitabu kile kwani kwa jinsi ilivyoonekana, mtu huyo alikuwa akifahamu mambo mengi mno yaliyokuwa yametokea na hata yale ambayo yangeweza kutokea, ilikuwa ni lazima wayasimamishe hayo na njia nzuri ya kufanikiwa katika hilo ni kumtafuta mwandishi huyo.
“Hakutuma picha yake,” alisema meneja.
“Tunajua!”
“Ila si kuna namba zake za simu!”
“Hazipo duniani!”
“Unamaanisha nini?”
“Hazijawahi kutolewa!”
“Mh! Sasa mmekuja hapa kutafuta nini?”
“Kuangalia akaunti yake ya benki! Pesa zinaingizwa kwenye akaunti ipi,” alisema ofisa mmoja.
Kisheria hawakuruhusiwa kuziweka wazi namba za mteja wao ila kwa sababu watu waliofika mahali hapo walikuwa ni wa usalama wa taifa, hakuwa na jinsi, akatafuta na kuwapa watu hao.
Wakaichukua na kuondoka nazo. Walipofika makao makuu wakaanza kutafuta ni akaunti ya benki gani iliyokuwa ikitumika. Kwenye kufuatilia, ilionekana ni Benki ya Barclays kwenye tawi lake moja nchini Nigeria ndipo ambapo mwanaume huyo alifungulia akaunti yake hiyo na wakati huo kulikuwa na kiasi cha pesa cha dola milioni nne, zaidi ya shilingi bilioni nane zilizokuwa zimeingizwa humo kutokana na mauzo ya kitabu.
“Wasilianeni na hawa Barclays wa Nigeria!” alisema O’Brain.
Haraka sana maofisa waliokuwa nchini Nigeria wakaondoka na kuelekea kwenye tawi la benki hiyo na walipofika, kitu cha kwanza kilikuwa ni kujitambulisha na kutaka kuonana na meneja wa benki hiyo.
Hakukuwa na tatizo lolote lile, wakaonana naye na kumwambia kile walichokuwa wakikihitaji. Hapakuwa na tatizo, mwanaume huyo akawachukua na kuwapeleka katika ofisi ya mhusika wa kile walichokuwa wakihitaji na kuwaonyeshea.
“Mtu mwenye akaunti ni huyu hapa,” alisema mfanyakazi huyo.
“Anaitwa nani?”
“Juma Hiza!”
“Juma Hiza? Mbona kwenye kitabu anajulikana kwa jina la Williams McCannon?” aliuliza ofisa mmoja huku akimwangalia meneja wa benki.
“Hata sisi hatujui! Nadhani ni kwa sababu ya kulenga soko la wasomaji!” alijibu.
“Mmh!”
Hawakutaka kupoteza muda, haraka sana wakaondoka mahali hapo na kurudi hotelini. Wakawasiliana na wenzao na kuwaambia kuhusu jambo hilo.
Walisema wazi kwamba walishangazwa, jina la mwandishi ambalo liliwekwa kwenye kitabu lilikuwa tofauti na lile lililokuwa likionekana kwenye akaunti yake ya benki.
“Mnamaanisha nini?”
“Anaitwa Juma Hiza!”
“Na picha yake?”
“Tunaituma!” alisema.
Haraka sana picha ya mwandishi huyo ikatumwa mpaka nchini Marekani ndani ya makao makuu ya CIA.
Picha ile ikapokewa na kuwekwa kwenye screen kubwa na kila mtu kuanza kuiangalia. Hakukuwa na mtu aliyeamini kama kijana yule mdogo, aliyeonekana kuwa na umri usiozidi miaka ishirini ndiye ambaye alikuwa ameandika kitabu kile.
Kwa kumwangalia tu, alionekana kutokuwa na uwezo mkubwa wa kuandika namna ile, ilikuwaje sasa atoe kitabu kilichouzwa kwa kasi na kumuingizia kiasi kikubwa cha pesa?
“Mna uhakika huyu ndiye aliyeandika kitabu hiki?” aliuliza O’Brain.
“Huo ni kwa mujibu wa picha kwenye akaunti yake ya benki!” alijibu jamaa mmoja.
“Ila mbona mdogo?”
“Kwa mtazamo, ila kiakili ni mkubwa mno!”
“Hii picha sambazeni kila kona, ninataka ndani ya saa kadhaa tujue yupo wapi, tunamtaka kijana huyu, hebu achaneni na kila kitu, tushughulikieni suala la huyu mtu kwanza,” alisema O’Brain huku akionekana kuchanganyikiwa, inawezekana kabisa kumpata Hiza ingekuwa moja ya mafanikio yake kujua ni kitu gani hasa alikijua kuhusu shambulio hilo ambalo liitemesha Marekani na nchi nyingine.
Je, nini kitaendelea?