Kada muhimu kuliko zote

Mlenge

R I P
Oct 31, 2006
2,125
2,291
Mfalme mmoja alitaka kujua ni kada gani muhimu kuliko zote?

1. Maaskari wakamwambia ni sisi: Tunaulinda ufalme wako; bila sisi maadui wangekuja kutuvuruga hapa.

2. Walimu wakamwambia ni sisi: Bila sisi hakuna kada yoyote nyingine.

3. Madaktari wakamwambia ni sisi: Bila sisi hakuna mtu mwenye afya kufanya kazi ya kada yoyote.

4. Kila kada ikasema ni sisi: Bila sisi hakuna...

Mfalme akakanganyikiwa. Nani sasa ndio kada muhimu kuliko wote? Ikiwa Maaskari ndio muhimu kuliko wote, ina maana walimu siyo. Ikiwa walimu ndio muhimu kuliko wote, ina maana madaktari sio. Ikiwa madaktari siyo muhimu kuliko wote, ina maana... Mfalme akakosa jibu. Akaamua kwenda kulisaka jibu lake kwa...


Hadithi imefasiriwa. Iliandikwa kwanza kwa kirusi ikiitwa три вопроса.

INAENDELEA POSTI TATU ZIFUATAZO.
 
SEHEMU YA 2

Siku moja Mfalme fulani alijiwa na wazo kwamba ikiwa angejua muda muafaka wa kutenda kila kitu; kama angejua nani ndio watu sahihi wa kuwasikiliza, na nani wa kuwakwepa; na, juu ya yote, kama nyakati zote angejua nini ndicho kitu muhimu kuliko vyote cha kutenda, hangeshindwa katika lolote ambalo angeamua kulifanya.

Na wazo hilo lilipomjia, alitangaza katika ufalme wote kwamba angetoa zawadi kubwa kwa mtu yeyote ambaye angemfundisha mfalme ni wakati upi ulio muafaka kwa kila tukio, na nani ndio walikuwa ndio watu muhimu kuliko wote, na ni vipi angefahamu kipi kilichokuwa ndicho kitu muhimu kuliko vyote kukitenda.

Ndipo wasomi wakaenda kwa mfalme, lakini kila mtu alijibu maswali ya mfalme kivyake.

Katika kujibu swali la kwanza, wengine walisema ili kujua muda muafaka kwa kila tukio, lazima mtu achore jedwali la ratiba ya siku, miezi, na miaka, na lazima aishi bila kukosea kuifuata ratiba hiyo. Ni hivyo tu, walisema, ingewezekana kufanya kila kitu kwa wakati wake muafaka. Wengine wakasema haiwezekani kujua kabla ya muda sahihi wa kila kitu, lakini kwamba, mtu akiacha kuzolewa na tabia za kizembe, mtu anatakiwa muda wote ashughulike na yatukiayo muda huo, na kutenda analoliona vema. Wengine, tena, wakasema kwamba hata Mfalme akifanyaje kujua yanayojiri, isingewezekana kwa mtu mmoja kuamua kwa usahihi muda muafaka wa kila tukio, lakini kwamba angekuwa na baraza la wazee wa busara ambao wangemsaidia kupanga muda muafaka wa kila kitu.

Lakini tena wengine nao wakasema palikuwa na mambo mengine ambayo hayangeweza kusubiri kikao cha baraza, lakini ambayo mtu alitakiwa mara moja kuamua kuyatenda au la. Lakini ili aweze kuamua hivyo, mtu lazima ajue mapema iwapo tukio hilo litakuja kutokea. Ni wapiga ramli tu wanaojua hayo; na, hivyo, ili kujua muda muafaka wa kila tukio, mtu shurti aende kwa wapiga ramli.

Kadhalika kulikuwa na majibu mengi kuhusu swali la pili. Wengine walisema watu ambao mfalme aliwahitaji sana walikuwa ni washauri wake; wengine, viongozi wa dini; wengine, madaktari; wengine wakasema maaskari ndio waliokuwa muhimu kuliko wote.

Kwenye swali la tatu, la ipi ndio ilikuwa kada muhimu kuliko zote, wengine walijibu kwamba kitu muhimu kuliko vyote duniani ni sayansi. Wengine wakasema ni mbinu za kivita; na wengine, tena, kwamba ilikuwa ni ibada ya kidini.

Kwa vile majibu yote yalikuwa yakipishana, mfalme hakukubaliana na jibu lolote, na hakumpa yoyote zawadi. Lakini kwa vile alitamani kupata majibu sahihi kwa maswali yake, aliamua kwenda kumuuliza mzee mmoja aishie maporini huko, akijulikana sana kwa busara zake.
ITAENDELEA SEHEMU YA 3
 
SEHEMU YA 3

Yule mzee aliishi maporini ambako hakuwahi kuhama, na hakupokea wageni mashuhuri ila wananchi wa kawaida. Kwa hiyo mfalme alivaa nguo za kawaida na, kabla hakufika kwenye nyumba ya yule mzee, alishuka kwenye farasi wake. Akawaachia walinzi wake, akaenda mwenyewe peke yake.

Mfalme alipokaribia, yule mzee alikuwa akilima ardhi iliyokuwa mbele ya nyumba yake. Alipomwona mfalme, alimsalimia na kuendelea kulima. Mzee alikuwa mkongwe na dhaifu, kila muda alipokita jembe ardhini na kugeuza udongo kidogo, alivuta pumzi ndefu.

Mfalme akamfuata na kusema: "Nimekuja kwako, mzee mwenye hikma, kukuuliza majibu ya maswali matatu: Nitawezaje kujua kitu sahihi cha kufanya kwa wakati sahihi? Nani ndio watu ambao ninawahitaji kuliko wote, na nani kwa hiyo inanibidi, nimsikilize kuliko wote wengine? Na, mambo gani ndio muhimu kuliko yote na yanahitaji niyaangalie kwanza?"

Mzee akamsikiliza mfalme, lakini hakumjibu kitu. Alijitemea mate tu mkononi mwake na kuendelea kulima.

"Umechoka," alisema mfalme, "nipe jembe nikusaidie kwa muda."

"Asante!" alisema yule mzee, na, akimpa jembe mfalme, aliketi chini ardhini.

Alipokuwa amelima matuta mawili, mfalme aliacha kulima na kurudia maswali yake. Yule mzee tena hakumpa majibu, bali aliinuka, akanyoosha mkono wake kupokea jembe, na kusema:

"Pumzika sasa kidogo -- na niache niendelee na kazi kidogo."


ITAENDELEA SEHEMU YA 4


 

Lakini mfalme hakumrudishia jembe, na akaendelea kulima. Saa nzima ikapita, na kisha nyingine. Jua likaanza kuzama nyuma ya miti, na mfalme mwishowe akakita jembe la mwisho ardhini, na kusema:

"Nimekuja kwako, mzee mwenye hikma, kwa ajili ya majibu kwa maswali yangu. Kama hunijibu kitu, niambie tu, na nitarejea nyumbani."

"Pana mtu hapa anakuja mbio," alisema yule mzee. "Ngoja tuone ni nani."

Mfalme akageuka na kumwona mwanaume mwenye madevu akija mbio kutokea machakani. Mtu huyo alikuwa ameweka mikono yake tumboni, na damu ilikuwa ikichuruzika chini yake. Alipomfikia mfalme, alidondoka, akigumia. Mfalme na mzee wakafungua vazi lake. Palikuwa na jeraha kubwa tumboni. Mfalme akaliosha vizuri kadiri alivyoweza, na kulifunga kwa leso yake na kwa taulo yule mzee aliyokuwa nayo. Lakini damu haikuacha kutoka, na mfalme tena na tena aliondoa bendeji iliyokuwa imelowa damu mbichi, na kuiosha na kumfunga tena jeraha lile. Pale ambapo hatimaye damu iliacha kutoka, yule mtu alizinduka na kuomba kitu cha kunywa. Mfalme akaleta maji safi na kumpatia. Wakati huohuo jua lilikuwa limeshazama, na ilianza kuwa baridi. Hivyo mfalme, akisaidiwa na yule mzee, wakambeba majeruhi mpaka kwenye nyumba na kumlaza kitandani. Alipolala kitandani, yule mtu alifunga macho yake na kuwa kimya; lakini mfalme alikuwa amechoka sana kutokana na kutembea na shauri ya kazi aliyokuwa ameifanya kiasi kwamba alijilaza chini, na kulala usingizi - usingizi mnono kiasi kwamba alilala usiku wote ule mfupi wa majira ya joto.


Asubuhi alipoamka, ilimchukua muda mpaka alipokumbuka yuko wapi, au ni nani mtu yule mwenye madevu aliyelala kitandani akimkodolea macho mfalme.

"Nisamehe!" alisema yule bwana madevu kwa sauti dhaifu, pale alipoona mfalme ameamka na anamtazama.

"Sikufahamu, na sina kitu chochote ulichonikosea mpaka nihitaji kukusamehe," alisema mfalme.

"Hunijui, lakini mimi nakujua. Mimi ndiye yule adui yako niliyeapa kujilipia kisasi kwako, kwa vile ulimhukumu kifo kaka yake na kuchukua mali zake. Nilijua umekuja peke yako kumuona huyu mzee, na niliazimia kukuua wakati ukirudi. Lakini siku ilipita nawe hukurudi. Hivyo nilitoka mafichoni kukutafuta, na nikakutana na mlinzi wako, naye alinitambua, na akanijeruhi. Nikawatoroka maaskari, lakini ningekufa kwa kutokwa damu usingenifunga majeraha yangu. Nilitaka kukuua, lakini umeokoa maisha yangu. Sasa, iwapo nitaishi, na kama ukiridhia, nitakutumikia kama mtumwa wako mwaminifu, na kuwataka wanangu wafanye vivyo hivyo. Nisamehe!"

Mfalme alifurahi sana kupatana na adui yake kirasihi vile, na kumpata kama rafiki mpya, na siyo tu aliamua kumsamehe, bali pia alisema angetuma watumishi wake na tabibu wake mwenyewe kwenda kumhudumia, na alimuahidi kumrejeshea mali yake.

Akiwa amemuacha yule majeruhi, mfalme alienda kibarazani na kumtafuta yule mzee. Kabla hakuondoka kwa mara nyingine alimuomba ampe majibu kwa maswali aliyomuuliza. Mzee alikuwa nje, amepiga magoti, akipanda mbegu kwenye matuta yaliyolimwa jana yake.

Mfalme akamsogelea na kumwambia, "Kwa mara ya mwisho, nakuomba unijibu maswali yangu, ee mzee mwenye hikma."

"Ushajibiwa tayari!" alisema yule mzee, huku akiendelea kuchutama miguu yake myembamba, na akimwangalia mfalme, ambaye alikuwa amesimama kando yake.

"Nimejibiwaje? Una maana gani?" aliuliza mfalme.

"Hauoni?" alijibu yule mzee. "Usingenionea huruma udhaifu wangu jana ile, na usingelima haya matuta kwa ajili yangu, lakini ukajiendea zako, yule mtu angeweza kukushambulia, na ungejuta kwa nini hukubakia kwangu. Kwa hiyo muda muhimu kuliko wote ulikuwa ni pale ulipokuwa ukilima matuta; na nilikuwa mtu muhimu kuliko wote; na kunitendea mema ilikuwa ndilo jukumu lako muhimu kuliko yote. Baada ya hapo, wakati yule mtu alipotukimbilia, muda muhimu kuliko wote ulikuwa ni ule ulipokuwa ukimhudumia, kwani kama usingemfunga majeraha yake angekufa bila kupatana nawe kwa amani. Kwa hiyo alikuwa ndiye mtu muhimu kuliko wote, na uliyomtendea ndio yalikuwa jukumu lako muhimu kuliko yote. Hivyo kumbuka: pana muda mmoja tu ambao ni muhimu – sasa! Ndio muda muhimu kuliko wote kwa vile ndio muda pekee ambamo unaweza kufanya chochote. Mtu muhimu kuliko wote ni yule ambaye uko naye, kwani hakuna mtu ajuaye iwapo atapata nafasi ya kushughulika na mtu mwingine yeyote zaidi; na jambo muhimu kuliko yote ni kumtendea mtu huyo yaliyo mema, kwani ni kwa dhumuni hilo pekee binadamu aliletwa kwenye maisha haya."

MWISHO
 
Akaenda kupata jibu kwa anayejichua

Mimi ndio muhimu mana hao wote kuwepo duniani inategemea na maamuzi yangu
 
Back
Top Bottom