Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amesema kauli ya hivi karibuni ya kiongozi wa chama tawala, Paul Chacha, kwamba vyombo vya ulinzi na usalama ni mali ya CCM, imethibitisha kuwa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, ni ya uongo iliyotengenezwa na vyombo vya dola ili kulinda utawala wa CCM dhidi ya ushindani wa kweli wa kisiasa.
Akiandika kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii leo, Jumapili, Septemba 27, 2026, Heche ameeleza kuwa madai hayo ya Chacha yamewathibitishia Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa ukweli ambao CHADEMA imekuwa ikipigania kwa miaka yote kuhusu ukosefu wa haki na matumizi mabaya ya vyombo vya dola katika Mfumo wa Vyama Vingi nchini.
Heche amehoji halali ya kisheria na kimaadili kwa mamilioni ya Watanzania kulipa kodi zinazotumika kuhudumia Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakati viongozi wa CCM wanavitangaza hadharani vyombo hivyo kuwa ni mali halali ya chama chao.
"Hii ni kauli muhimu sana, imethibitisha yale ambayo tumeyasema kwa miaka yote. Leo kiongozi wa juu wa CCM amethibitishia Watanzania na Dunia kuwa Polisi, Usalama wa Taifa na JWTZ ni mali ya CCM na viongozi wake ni makada wa CCM. Je, vyombo hivi vinaweza kutendea haki wapinzani? Katika mazingira haya aliyoyasema Chacha, kesi ya Mwenyekiti wetu ni ya uongo aliyobambikiziwa na vyombo vya CCM kwa sababu ya kulinda chama chao dhidi ya ushindani wa kweli kutoka kwake," amesisitiza John Heche.
Kiongozi huyo wa CHADEMA ameongeza kuwa matukio ya utekaji, kupotezwa na kuuawa kwa raia yanayofanywa na vyombo vya dola yanaakisi mpango wa kuisaidia CCM kujitangaza washindi kwa njia zisizo halali, akibainisha kuwa mfumo huo unathibitisha umuhimu wa msimamo wa "No Reforms, No Election" na hitaji la haraka la Katiba Mpya kabla ya uchaguzi wowote.
#SasaLive #JohnHeche #CHADEMA #TunduLissu #PaulChacha CCM VyomboVyaDola KatibaMpya Tanzania