Katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu shahidi wa tano wa upande wa utetezi na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche ameieleza Mahakama kuwa madhila mbalimbali ambayo CHADEMA ilipitia katika chaguzi zilizopita ndiyo yaliyochochea kamati kuu kupitisha msimamo wa “No Reforms, No Election”… yaani, bila mabadiliko hakuna uchaguzi.
Heche ameyasema hayo mbele ya Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo inayosikilizwa na jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dustan Ndunguru.