SoC02 Jiwe La Msingi 5 (ukombozi wa fikra, elimu na uchumi)

Stories of Change - 2022 Competition

onea 22

Member
Jul 31, 2020
34
20
CHANGAMOTO KWENYE MFUMO WA ELIMU NCHINI TANZANIA.

Utangulizi
Siku za nyuma nikiwa kidato cha kwanza, katika Shule ya Sekondari Uluguru, tuliwahi kuwekewa mada ya kujadili kwa hoja. Mada hiyo ni maarufu kidogo miongoni mwa wanafunzi waliowahi kupitia elimu ya sekondari, ”Education is better than money” ikiwa na maana kwamba elimu ni bora kuliko pesa, jadili.

Kwa kipindi kile sikuwa na upeo wa kuchanganua mambo kupata jibu sahihi zaidi. Miaka mingi kidogo imepita na leo nimepata jibu langu kwa swali hili. Ni njia rahisi tu inayoweza kukupa jibu la swali hili.

Elimu ni bora kuliko pesa? Sisi tunajibu kwa kusema hivi ukitaka kujua umuhimu wa kitu kwanza kitoe kabisa hicho kitu kwenye mazingira yako, kisha jaribu kuangalia maisha yatakavyokuwa bila ya hicho kitu.

Vuta picha dunia nzima bila ya kuwa na pesa (huko nyuma dunia ilishapata kuwapo bila ya pesa na mambo yakaenda). Lakini pia umewahi kuwaza ni vipi dunia ingekuwa bila ya kuwepo kwa elimu? Baada ya kupata majibu hayo kila mtu achague dunia atakayotaka aishi ndani yake, dunia yenye pesa bila ya elimu au dunia yenye elimu bila pesa?

Tukiachana na mada hiyo, je ni vipi elimu inaweza kuwa na manufaa kwenye jamii kwa jumla? Ni vipi elimu inaweza kuboresha maisha ya watu wote kwenye jamii ambayo watu wake wanategemea kwayo ili kumaliza changamoto zao?

Ubora wa elimu Tanzania unaonekana kuwa chini, si kwa shule binafsi wala shule za serikali wote ni walewale tu. Nimefikia kusema kwamba wanafunzi wa shule zote nchini ni sawa kwa sababu wote hao wapo kwenye jamii ya Tanzania na changamoto za Watanzania nyingi zimebaki kuwa palepale ukilinganisha na idadi kubwa ya wasomi waliopo.

Hawaonekani watatuzi wa changamoto zilizopo nchini. Kama hilo ni gumu basi wapatikane hata wa kuzimulika ili wale ambao hawana elimu kubwa pia wazione, nalo limekuwa gumu.

Je, ni sababu zipi zinaipelekea elimu wanayopewa vijana wetu isiwe na manufaa mapana kwa taifa?

Malengo chanya kwenye matumizi ya elimu
Sababu kubwa inayotugharimu Watanzania ni kwamba wengi wanaotafuta elimu kuwa na malengo ambayo hayana tija kwa jamii kwa ujumla.

Lengo lao kuu ni kuja kuwa na maisha mazuri, kumiliki majumba makubwa magari ya kifahari na anasa nyingine. Na wengi wanaona kwamba njia ya kufikia ndoto zao hizo ni kusoma.

Matokeo yake wanapokuja kuajiriwa wanakuta mishahara yao haitoshelezi matakwa yao na kuamua kuiba ili tu waishi ndoto zao. Elimu wanaipata lakini hiyo elimu inatumika kuiangamiza jamii yaTanzania, badala ya kuikomboa.

Dhana ya ubinafsi iliyojengeka vichwani mwa Watanzania walio wengi ndio kitu kinachoitafuna jamii yetu. Usahihi wa mambo ni kwamba ili jamii ya Watanzania iwe salama, lengo la elimu linatakiwa kuwa ni moja tu kwa wanafunzi wetu wote.

Lengo ambalo si lingine bali kuweza kumaliza au kupunguza matatizo ya jamii kwa ujumla. Kama kila Mtanzania atajitoa kutumia elimu yake au ujuzi wake kuisaidia Tanzania basi jamii nzima itakuwa salama, kwa kuwa lengo letu litakuwa moja.

Ni hapo tu ndipo jamii ya Tanzania itakapofaidi matunda ya elimu wanayopata vijana wetu. Kinyume na hapo ikiwa kila mtu anasoma kwa ajili yake binafsi, kila mmoja atakuwa anafikiria tumbo lake.

Na katika mafanikio binafsi mtu huwa haridhiki kwa chochote ambacho atakipata. Hata apewe mlima uliojaa almasi amiliki peke yake bado atataka aendelee kupata mali zaidi. Tena kibaya zaidi mali hiyo atainyang’anya kutoka kwa watu wasiojiweza na rungu lake analolitumia kujinufaisha ni elimu. Mfano hai ni kwamba kuna baadhi ya Watanzania, kwao Tsh. Bilioni 1 ni vijisenti tu.

Ila ukiangalia kwa makini chanzo cha yote haya ni kwamba wanafunzi wetu ambao baadaye wanakuja kupewa jukumu la kuendesha jamii kuwa na mawazo ya ubinafsi.

Katika vitabu vya dini na historia anatajwa mtumishi wa Mungu Yusufu kama mtu ambaye alipewa elimu na Mungu. Yusufu aliitumia elimu yake kuikinga jamii yake na janga la njaa lililokuwa linakuja mbeleni.

Sisi kizazi hiki tuna wasomi wangapi mpaka sasa? Je, wasomi hao wanatusaidia nini kwenye kutokomeza matatizo yetu yanayotukabili? Tofauti ya elimu ya Yusufu na ya wasomi wetu wengi wa sasa ni nia/malengo ya elimu wanayoipata.

Kuwajengea vijana ujuzi kabla ya kumaliza shule
Suala jingine ambalo ni changamoto kwenye elimu yetu ni kwamba, shule za msingi kuanzia darasa la tatu mpaka saba kuna somo zuri sana la stadi za kazi. Ni somo zuri sana hasa katika kipindi hiki ambacho watu wanahimizwa kufanya shughuli za ujasiliamali.

Katika somo hili kuna mafundisho mengi ambayo yanahitajika kwenye jamii yetu. Masomo kama ya ufugaji wa kuku, useremala, kutengeneza vigoda, usukaji wa vikapu, uvuvi, kutengeneza batiki n.k.

Tatizo nilionalo ni dogo sana hapa. Elimu kubwa na ya muhimu imepelekwa kwa vijana ambao kiumri ni wadogo mno kutambua umuhimu wa masomo hayo adhimu. Vijana hao wa shule za msingi bado wana mawazo ya kuwa wahandisi, marubani, madaktari na wengine hata hawafahamu wanafanya nini shuleni kwa wakati huo.

Ni sahihi kwa vijana wetu kuwaza hivyo wanavyowaza lakini ni muhimu sisi kama wakubwa wao kuwaonesha uhalisia wa maisha. Waelezwe changamoto za jamii yetu na mahitaji ya jamii yetu ili waje kutoa huduma hizo kwa Watanzania.

Lakini pia hayo yote hayawezi kufikiwa ila tu hadi pale umuhimu wa somo la stadi za kazi utakapopenya kwenye mioyo ya wanafunzi.

Kwa kuwa wanafunzi wanasomeshwa stadi za kazi wakiwa wadogo hivyo hawaoni umuhimu wake na kulipeleka somo hilo Sekondari ni kuwaongezea mzigo wanafunzi ambao tayari pia wana mambo mengi ya kusoma.

Jambo la msingi ni kuwaacha wanafunzi wasome hilo somo la stadi za kazi wakiwa shule za msingi ili wawe na msingi wa hilo somo. Lakini msisitizo lazima uwekwe ili wawe wanazingatia mambo wanayojifunza.

Tunataka tuone matokeo ya wanachojifunza shuleni huku mitaani. Tuone wanafunzi wanatengeneza majiko, wanashona nguo, wanalima bustani kwa kutumia taaluma wanayopata shuleni.

Hivyo basi kutokana na umuhimu wa somo hili wanafunzi wakimaliza kidato cha nne wakati wakiwa wanasubiri matokeo yao basi waendelee kwenda shuleni kujifunza somo hili la stadi za kazi kwani katika umri huu walau mwanafunzi wanakuwa wameanza kuona changamoto za maisha hivyo watajifunza kwa bidii shughuli mbalimbali watazokuwa wanajifunza.

Katika kipindi hiki wanafunzi wanakuwa hawana uhakika kama wataendelea na shule ama la. Na kwa miaka minne ambayo anaitumia sekondari nina uhakika hakuna ujuzi wowote ambao mwanafunzi atakuwa ameubeba.

Hivyo basi kipindi hiki na mpango huu ni muhimu sana kwenye kujenga jamii yenye watu wenye ujuzi na fani mbalimbali.
 
Back
Top Bottom