Interest
JF-Expert Member
- Apr 11, 2015
- 3,434
- 7,069
Zao la Soya lina protini nyingi yenye ubora wa hali ya juu kuliko iliyoko katika aina nyingine ya mazao ya mimea. Kiasi cha protini katika soya inazidi hata kiasi cha protini katika nyama, mayai na maziwa.
Sifa nyingine za zao la soya ni pamoja na kuwa na mafuta yasiyo kuwa na lehemu (cholesterol), uwezo wa mmea wa soya kuongeza mbolea aina ya nitrojeni kwenye udongo, gharama ndogo za uzalishaji ukilinganisha na mazao mengine, uwingi wa protini unaoweza kuondoa utapiamlo hususani kwa watoto na kinga kwa magonjwa ya kansa, shinikizo la damu na kuwaongezea nguvu wagonjwa wa UKIMWI na magonjwa mengine.
Aidha, uwezo wa soya kustawi katika maeneo yanayostawisha mahindi na maharage unamaanisha kwamba zao hilo linaweza kulimwa sehemu nyingi nchini Tanzania. Sifa hizo zimefanya zao la soya kuwa muhimu katika chakula cha binadamu na mifugo na katika kutengeneza bidhaa mbalimbali za vyakula na madawa. Pamoja na manufaa hayo ya zao la soya, zao hilo halifahamiki kama ilivyo mazao mengine mfano maharage na mahindi. Wakulima wengi hawazijui kanuni za kilimo bora cha soya.
Hii inatokana na kutojua umuhimu wa zao hilo na hivyo kutotilia maanani katika kulilima na kulitumia kuboresha afya na kipato hasa katika ngazi ya kaya. Lengo kuu la kijitabu hiki ni kuwafahamisha wakulima, maafisa ugani na wadau wengine faida zinazotokana na uzalishaji na matumizi ya soya.
Pia kijitabu hiki kina lengo la kuhamasisha wakulima na kuendeleza uzalishaji na matumizi ya zao hilo lililoingizwa nchini kwa mara ya kwanza mwaka wa 1907.
Ni matarajio ya Wizara ya kuwa wakulima na wadau wengine watafaidika kwa kutumia kijitabu hiki kwa ajili ya kuendeleza na kuongeza uzalishaji, tija na matumizi ya soya hapa nchini..