wanabidii] RE: CLOUDS FM na Porojo Zake
Reply |Selemani ****** to wanabidii, ethinktanktz, mwananchi, wanazuoni
show details Apr 13 (6 days ago)
Wanabidii wote,
Samahani sana naomba kwa ruksa yenu nilete mada mpya kidogo ili tuijadili. Ninahuzunishwa sana na utendaji kazi wa watangazaji wa FM Clouds. Na hapa ni zuri nikawataja majina, hawa ni watangazaji wanaotangaza kipindi cha "Jahazi" nao ni ndugu Kibonde na Gardner Harbash. Hivi hawa ni watangazaji wa wapi!? Je wamesomea hii kazi ya utangazaji? Je wanafahamu maaadili ya utangazaji au wanazingatia maadili ya kazi yao? Naamini kabisa kazi hii ina maadili yake, hivi wanavyotangaza wanazingatia maadili hayo?
Siku mbili zilizopita CCM walizindua kampeni yao kukusanya bilioni 40. Kibonde alikuwa mshehereshaji katika shughuli hiyo. Sina tatizo na hilo kwani anatafuta ugali wa watoto. Nilihisi kuwa baada ya tukio hilo basi kipindi kinachofuata cha Jahazi kitatawaliwa na tukio hilo. Na ikawa hivyo. Ikawa kweli kabisa. Kibonde na Gardner wakatumia kipindi hicho kuwapigia kampeni CCM. Gardner akasema kuwa anaomba aelekezwe namna ya kuchangia kwani anapenda sana mambo yao (CCM), hivyo naye angependa kuchangia. Sina tatizo na yeye kuchangia, lakini ni muhimu ajue kuwa anazungumza na watanzania ambao wana itikadi tofauti. Yeye kama mtangazaji anao wajibu wa kuufanya uchaguzi uwe huru na wa haki. Na katika kufanya hivyo analazimika kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa. Kama anakipigia chama cha CCM basi ni lazima hakikishe kuwa anavipa nafasi na vyama vingine. Kutokana na na kuzungumza maneno yao yanayokera kwa kujitafutia maslahi yao binafsi, msikilizaji mmoja aliwatumia ujumbe na kuwaambia kuwa "kipindi chenu kimejaa UCCM, vipi mnatafuta ulaji wakati wa uchaguzi?" Walimjibu kwa kejeli lakini naamini ujumbe ulifika na walifahamu kuwa watu hawapendi hizo tabia zao za kuganga njaa na kutafuta ulaji. Labda wana ndoto kuwa watapata nafasi, sijui labda ya ukatibu wenezi msaidizi au uhamasishaji.
Mtangazaji au mwandishi wa habari una wajibu kwa jamii na si kwa watawala. Una wajibu wa kuwafunua macho wananchi ili wafanye maamuzi sahihi na wafanye informed choices. Na si kugeuka kuwa propagandist kwa ajili tu ya kuangalia maslahi yako, na mbinu za kutafuta cheo. Hawa ni lazima wakemewe na wasemwe. Katika kipindi hiki cha uchaguzi tutawaona wengi sana wa namna hii. Kwani kwa bahati mbaya wanajua mshindi ni nani, hivyo wanaanza kujipendekeza mapema ili awape nafasi waweze kujinufasiha wao na familia zao.
Wao kama ni watangazaji wa kweli kwa nini wasiseme wito aliotoa Mwenyekiti kuwa matajiri wawadhamini wagombea wa CCM. Je sheria aliyoipitisha kwa mbwembwe ndio inavyosema hivyo? Kwa nini hawaelimishi watu katika masuala kama haya ya msingi?
Hili ni moja tu, lakini nimewahi kuwasikia mara nyingi wakipotosha au wakisema maneno ambayo ni kinyume kabisa na maadili ya utangazaji. Ipo siku wamewahi kusema kuwa Kingunge ni Waziri anayeshughulikia siasa na jamii. Ilhali nafasi hiyo ilikwishaondolewa. Hata pale msikilizaji alipowakumbusha hawakuomba radhi, kwa sababu hawana maadili na wanadhani watu wanaosikiliza hawana upeo wa kuelewa mambo.
Wao wamekuwa ni wataalamu wa kila kitu, kila jambo wanalitolea ufafanuzi, liwe la kisheria, uchumi, siasa na hata la kidaktari wao ni wataalam!!
Juzi juzi wamemkaraibisha Mrema kwa sababu tu anapinga mgomo wa wafanyakazi. Leo hii amekuwa mtu wa maana na anapewa nafasi ya kuzungumzia suala hilo. Kinachosikitisha ni wao kulichukulia kirahisi sana na kuanza kuwalaumu viongozi wa muungano wa vyama vya wafanyakazi. Kwa nini hawajiulizi hivi kwa nini watu wanagoma? Chanzo cha migomo nchini nini? Kwa nini tumekuwa na wimbi kubwa la migoma nchini katika siku za hivi karibuni? Tumejenga utamaduni kuwa bila kugoma hupati haki yako. Hawa si kwanza; Wafanyakazi wa NMB waligoma wakapewa haki yao, mara ngapi wahadhiri chuo kikuu wanagoma? au kutishia kugoma? wafanyakazi wa reli mara ngapi wanagoma ndio wanapewa mishahra yao? Hapa ni nani wa kumlaumu? anayenyima haki au anayedai haki haki yake kwa kugoma?
Kwa kuwafahamisha, ukiona jamii yoyote inaingia katika utamaduni huu, ujuwe kuwa HAKUNA HAKI, hakuna sheria na kwa kweli kuna ombwe (vacuum) ya uongozi. Wananchi wanaona hawana njia yoyote isipokuwa kugoma. Kwani hawasikilizwi na hawathaminiwi. Wanapoamua kugoma ni lazima mjuwe kuwa wamejaribu njia zote za amani na imeshindikana. Kugoma ni hatua ya mwisho baada ya kuona kuwa madai yao yanapigwa danadana.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi; Kwa mfano kwa nini mpaka leo serikali haijaitoa hadharani ripoti ya Ntukamazina ambayo ilipewa kazi ya kuangalia mishahara ya wafanayakazi na kutoa mapendekezo? Kwa nini kuna usiri? Kwa nini hawazungumzii mabilioni ya pesa yanayotumika kuwalipa vigogo posho, allowances na per diem zisizokuwa na kichwa wala miguu? kwa nini hawazungumzii real issues badla yake wana trivialize issues?
Watangazaji kama hawa ni hatari sana. Hata katika dola ambazo zilikuwa na ukandamizaji mkubwa sana ambao ulileta maafa makubwa, watangazaji na redio kama hizi zilitumika ku perpetuate motives mbaya za watawala. Hata katika mauaji ya kimbali katika sehemu nyingi za dunia na hata kwa majirani zetu, redio zilitumika katika kufanikisha unyama huo. Hatutaki redio za namna hii, ziwe za umma au mtu binafsi hatuzitaki. Hatutarajii redio zitumike katika kuwafumba macho wananchi, tunataka redio zitakazowafanya watu kuhoji, kujiuliza maswali, kutafakari, redio zinazoongeza ufahamu wa watu. Na hilo litatuletea maendeleo ambayo kila mtu atanufaika nayo na si maendeleo tu yako wewe mmoja ya kutaka kupata ulaji ndani ya chama tawala.
Asante
Selemani