Tovuti ya
A-Z Animals inaeleza kuwa Nyoka hawana sumu ya kuathiri wanapoliwa (poisonous), bali wana sumu wanayoingiza kwa kuuma (venomous). Pia ni miongoni mwa wanyama wanaoogopwa zaidi duniani, ingawa kutegemea na eneo unaloishi, huenda usiwahi kukutana na nyoka. Inakadiriwa kuwa takriban asilimia 85 ya spishi zote za nyoka duniani hazina sumu ya kuuma.
Kuhusu dhana ya kuwatofautisha nyoka wenye sumu na wasio na sumu kwa kuangalia umbo la kichwa ambapo wenye pembe tatu wanadaiwa kuwa na sumu huku wa duara wakidaiwa kutokuwa na sumu, tovuti ya
African snake bite institute inakanusha dhana hiyo kuwa haina uhalisia kwa nyoka wanaopatikana Afrika.
Inaelezwa tofauti na umbo la kichwa mchoro huo ulidai unaweza kutofautisha nyoka wenye sumu na wasio na sumu kwa kuangalia mboni za macho na mpangilio wa magamba chini ya mkia.
Madai hayo yanapotosha. Vigezo hivyo haviwezi kutumika kutambua nyoka wa Afrika. Kwa mfano, nyoka aina ya Boomslang na Black Mamba ni wenye sumu kali licha ya kuwa na sifa zinazopingana na maelezo yaliyopo kwenye mchoro. Aidha, nyoka wengi wenye sumu Kusini mwa Afrika wana magamba yaliyooanishwa chini ya mkia, tofauti na madai ya mchoro.
African Snakebite Institute inasisitiza kuwa hakuna njia rahisi au ya uhakika ya kutambua nyoka mwenye sumu kwa kuangalia mwonekano wake pekee. Ni hatari kutegemea michoro kama hiyo kwa kuwa inaweza kusababisha watu kufanya maamuzi yasiyo sahihi wanapokutana na nyoka.
Kwa mujibu wa tovuti ya
Huduma ya Hifadhi za Taifa ya nchini Marekani Nyoka wasio na sumu huwa si hatari kwa binadamu, lakini ni muhimu kuwaacha waishi kwa amani kwani wana mchango mkubwa katika mfumo wa ikolojia kwa kudhibiti wadudu na wanyama wadogo.
Nyoka wa kijani (Rough Green Snake) ni mwembamba, mrefu na mwenye rangi ya kijani angavu. Huishi zaidi kwenye miti na hula wadudu kama kriketi, buibui na nondo. Ni mtulivu na mara chache sana humng'ata binadamu. Hutaga mayai 4–6 mwishoni mwa kipindi cha masika au mwanzoni mwa kiangazi.
Milk Snake ana mistari myekundu, myeusi na meupe, huonekana zaidi usiku na hula wadudu, panya na wanyama wengine wadogo. Si mkali, lakini hufanana na Coral Snake mwenye sumu kali. Tofauti kuu ni mpangilio wa rangi kwenye mistari ya mwili. Kufanana huku ni mbinu ya kujilinda dhidi ya wawindaji (Batesian mimicry).
Common Garter Snake na Western Ribbon Snake wote ni nyoka wasio na hatari kubwa kwa binadamu na hula mijusi, vyura na wadudu. Hufanana sana kwa umbo, lakini Ribbon Snake hutambulika kwa mstari mweupe mbele ya jicho na taya ya chini yenye rangi nyeupe kabisa.
Ingawa nyoka wa jamii ya garter huzalisha sumu dhaifu, si hatari kwa binadamu. Pia wana uwezo wa kula vyura na newti wenye sumu bila kuathirika, na sumu hiyo inaweza kubaki mwilini mwao kwa muda.
Je, kwa muktadha wa Tanzania hali ikoje?
Tito Lanoy, ambaye ni mtaalamu na Mkufunzi kutoka Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka (Mweka Wildlife Management College) anasema hapa nchini Tanzania, tafiti zinaonesha kuwa karibu Asilimia 85 ya aina ya nyoka waliopo hawana sumu.
Kuhusu Nyoka Wenye Kichwa cha Pembetatu
Imani kuwa nyoka mwenye kichwa cha pembetatu ana sumu kali si kweli kwani wapo ambao kweli wana sumu na wapo ambao hawana. Baadhi ya nyoka wa aina hiyo wenye sumu kali ni Kifutu au vipili (Vipers na Adders).
Kuna nyoka hatari sana wenye sumu kali ambao hawana vichwa vya pembetatu. Mifano ya nyoka hao ni pamoja na Koboko mweusi (Black Mamba), Koboko wa kijani (Green Mamba), wengine ni Cobras kama vile Egyptian Cobra na Forest Cobra.
Jinsi ya Kumtambua Nyoka Mwenye Sumu Kitaalamu
Lanoy ameeleza kuwa njia sahihi na ya kitaalamu ya kutofautisha nyoka mwenye sumu na asiye na sumu ni kuangalia magamba yao (scales) na jinsi yalivyokaa, na si umbo la kichwa pekee.
Anaeleza kuwa maeneo makuu ya kuangalia ni pamoja na Magamba ya kichwani (Head scales), Magamba ya tumboni (Keeled scales / Belly scales), Magamba ya mgongoni (Dorsal scales) na Magamba ya kando ya macho na pua (Loreal scales / Labial scales).