Gharama za kuhamia Dodoma ni kubwa mno. Sasa hivi kuna wizara nyingi zina gharama mbali mbali katika miji miwili, Dar na Dodoma, na hivyo kuongeza gharama kubwa ya uendeshaji wa serikali. Pesa hiyo inaweza kutumika katika mambo mengine muhimu badala ya huu usanii wa kuhamia Dodoma ambao hautatekelezeka daima, maana sasa hivi ni zaidi ya miaka 30 bado 'tunahamia' Dodoma tu!!!
Kuhamia Dodoma kujadiliwa kitaifa
Shadrack Sagati, Dodoma
Daily News; Monday,June 23, 2008 @18:01
Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema serikali itaendesha mjadala wa kitaifa utakaowashirikisha wadau mbalimbali juu ya suala la kuhamishia Makao Makuu kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Katika hotuba yake ya makadirio ya matumizi yake aliyoisoma bungeni jana, Pinda alisema baada ya majadala huo serikali itaandaa mapendekezo ya kutunga sheria mpya ya kutambua rasmi Dodoma kuwa Makao Makuu ya Serikali.
Pinda pia alizungumzia maslahi ya Madiwani na kueleza kuwa katika mwaka ujao wa fedha Sh bilioni 4.8 zimetengwa kwa ajili ya posho za madiwani. Alisema Serikali itaandaa muswada wa marekebisho ya
Sheria ya Bima ya Afya utakaowezesha madiwani kupata matibabu kupitia mfuko huo na pia itaandaa marekebisho ya sheria ya fedha yatakayofanyika ili madiwani wafaidike na msamaha wa kodi kwa vyombo vya usafiri.
Waziri Mkuu pia alizungumzia muundo wa Jiji la Dar es Salaam ambalo lina manispaa tatu zinazojitegemea na kueleza kuwa uzoefu wa miaka minane wa utekelezaji wa mpango huo umeonyesha kuwa muundo huo una matatizo ya uendeshaji na hivyo kutokidhi matarajio yaliyokusudiwa ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Alisema Jiji la Dar es Salaam kwa sasa linakabiliwa na miundombinu ya barabara isiyokidhi mahitaji yanayopanuka kila siku na miundombinu ya maji safi na taka na ukuaji wa jiji usioenda sambamba na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hali hii inalifanya jiji lisionekane kama kioo cha nchi yetu, alisema Pinda na kuongeza Kuna haja ya kuliangalia kwa namna ya pekee. Alisema kwa kuzingatia hali hiyo serikali imeunda Kamati Maaluu ya kuangalia, kuchambua na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha muundo wa halmashauri za
Dar es Salaam na uendeshaji wake ili wananchi wafaidike na huduma bora zinazopaswa kutolewa na mamlaka hizo za Serikali za Mitaa. Kuhusu usafiri wa Jiji la Dar es Salaam, alisema fidia kwa wananchi ambao wameathirika na upanuzi wa miundombinu kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi itakamilika kulipwa mishoni mwa mwezi huu.
Alisema ujenzi wa miundombinu utaanza katika mwaka ujao wa fedha na utachukua miezi 24. Waziri Mkuu pia alizungumzia uchaguzi wa vitongoji ambao utafanyika Oktoba mwakani na kueleza kuwa Sh bilioni 4 kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi huo ikiwamo kuhakiki mipaka ya vitongoji, vijiji na mitaa, kufanya mapitio ya kanuni za uchaguzi na kufanya mikutano ya ushauriano na vyama vya siasa.
Kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, Pinda alisema katika mwaka ujao wa fedha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali utafanyika na mkazo zaidi utawekwa kwa tuhuma za mikataba mikubwa ambayo inaiingizia serikali hasara.
Akizungumzia sekta ya madini, Pinda alisema migodi mingi ya madini hasa ya wachimbaji wadogo haiko salama hivyo akatoa mwito suala hilo kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuhakikisha kwamba wamiliki wa migodi hiyo wanafuta kanuni zilizopo za usalama migodini kuepuka maafa kama yaliyotokea Mererani.
Kuhusu chakula, alisema katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha zimetengwa Sh bilioni 26.3 kwa ajili ya kununua tani 100,000 za mahindi na tani 5000 za mtama utakaofanywa na kitengo cha hifadhi ya chakula.
Pia amekiagiza kitengo hicho kununua nafaka kutoka kwa wakulima kwa wakati kuzuia uwezekano wa wakulima kuuza chakula kwa walanguzi na nje ya nchi na baadaye kukinunua kwa bei kubwa zaidi.
Waziri Mkuu pia alisema kituo cha uwekezaji katika mwaka unaomalizika Julai kimesajili miradi 902 yenye thamani ya Sh bilioni 8.1 ambayo imetoa ajira kwa Watanzania 127,588. Alisema kati ya miradi hiyo miradi 483 ni ya Watanzania na 196 ni ya wageni huku miradi 223 ni ya ubia.
Kwa upande wa ofisi za wabunge, Pinda alisema ofisi 40 zitakamilika kujengwa katika mwaka ujao wa fedha katika awamu ya kwanza na ofisi nyingine 10 zitaanza kujengwa. Sh bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kumalizia ofisi za awamu ya kwanza na kuanza ujenzi wa ofisi zilizoko katika awamu ya pili.