Jamhuri waomba kuwaficha mashahidi wao kesi ya kina Boni Yai na Malisa

Jamhuri waomba kuwaficha mashahidi wao kesi ya kina Boni Yai na Malisa

CHRC

Senior Member
Joined
Aug 2, 2011
Posts
166
Reaction score
226
Kesi ya Jinai nambari 11805/2024 Jamhuri dhidi ya Boniface Jacob na Godlisten Malisa imeendelea leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Ifuatayo ni sehemu ya kilichotokea mahakamani leo.
____
JAMHURI: Mheshimiwa, ikupendeze, naitwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Clemence Kato, nikishirikiana na Wakili Cathbert Mbiling'i kuwakilisha upande wa Jamhuri. Tunaomba wenzetu nao wajitambulishe.

KIBATALA: Mheshimiwa, ikupendeze, naitwa Wakili Peter Kibatala, nikisaidiana na Wakili Dickson Matata na Wakili Michael Lugina tunawakilisha upande wa utetezi.

JAMHURI: Mheshimiwa, kesi hii imeitwa leo kwa ajili ya kusikilizwa. Upande wa mashtaka tulipewa amri na mahakama hii tuje na mashahidi watatu leo. Hata hivyo, kama ambavyo mahakama yako inafahamu, tuliwasilisha maombi ili mashahidi wetu watoe ushahidi kwa siri, lakini mahakama yako ilitupilia mbali maombi hayo. Hivyo basi tumekata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo.

HAKIMU: Namba ya rufaa?

JAMHURI: Mheshimiwa, namba ya rufaa ni 439/2025.

(Hakimu anaangalia kwenye mfumo kuthibitisha kama kweli wamekata rufaa).

HAKIMU: Endelea.

JAMHURI: Kwa kuwa sheria inataka kukiwa na kesi ndogo mahakama ya juu basi kesi ya msingi inasimama, nasi tunaomba kesi hii isimame kwanza hadi Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi kuhusu rufaa yetu.

KIBATALA: Mheshimiwa, hii ni suprise kwetu. Leo ndio tunajua kwamba Jamhuri ilileta maombi ya kutaka mashahidi watoe ushahidi kwa siri bila kutujulisha? Hata hivyo, tunafahamu kuwa taratibu zinawaruhusu kuleta maombi na yasikilizwe upande mmoja (ex parte), lakini kwa uungwana wangetujulisha tu.

KIBATALA: Lakini hii ni habari njema kwa wateja wangu na sisi mawakili pia. Kwamba Jamhuri imeleta maombi kimyakimya mahakamani bila kutujulisha. Yakasikilizwa bila sisi kujua, na bado Jamhuri ikashindwa. Ni jambo la kutia faraja kuona Jamhuri inaweza kushindwa kesi hata pale inapokuwa yenyewe mahakamani.

KIBATALA: Hata hivyo napenda kuwahakikishia kwamba kama walishindwa hapa wakiwa peke yao, basi huko Mahakama Kuu tutawashinda pia, kwa kuwa tutakuwa na nafasi ya kucounter hoja zao. Kwahiyo wajiandae kisaikolojia kwa kushindwa tena.

KIBATALA: Mheshimiwa, hoja walizowasilisha wenzetu hazina authority. Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, toleo la 2022, ilifanyiwa marekebisho ili kupunguza ucheleweshaji wa kesi usio wa lazima. Wenzetu walidai wana mashahidi wengi lakini wameshindwa kuwaleta. Badala yake wanaomba watoe ushahidi kwa siri. Mahakama imekataa. Sasa wamekata rufaa. Hii ni abuse of court procedures. Ni mbinu ya kuchelewesha kesi. Kama hawana mashahidi waseme tu.

HAKIMU: Maombi yako ni nini?

KIBATALA: Mheshimiwa, naomba mahakama ikatae ombi la kuahirisha kesi. Mashahidi waletwe ili kesi iendelee. Vinginevyo, washtakiwa waachiwe huru kwa mujibu wa Kifungu 226(1) cha CPA.

JAMHURI: Mheshimiwa, ni kweli hatukutoa "authority" kwa sababu hoja yetu haijajikita katika kutafsiri kama suala hili statutory au non statutory. Tumeiachia Mahakama Kuu iamue. Tunachosema ni kuwa, rufaa imeshakatwa, hivyo shauri hili lisimame hadi uamuzi wa rufaa utolewe.

KIBATALA: Mheshimiwa, bila kuwakosea adabu mawakili wenzetu wa Jamhuri, tunawaomba watupatie authority ya kisheria inayozuia kesi kuendelea.

HAKIMU: Upande wa Jamhuri, mna authority yoyote?

JAMHURI: Ndiyo, Mheshimiwa. Civil Appeal Na. 227/2018 ya Sauda Juma Urassa dhidi ya Coca-Cola Kwanza, Mahakama Kuu iliamua kuwa mara kesi inapokatwa rufaa, shauri la chini husimama hadi rufaa itakaposikilizwa.

KIBATALA: Mheshimiwa, tunaomba rejoinder.

JAMHURI: Mheshimiwa, nadhani wao ndio wana rejoinder.

KIBATALA: Mheshimiwa, wenzetu hawajielewi. Walitoa hoja, sasa wanataka wao tena watoe rejoinder? Huwezi kula keki na bado ukaendelea kuwa nayo. Ni ama ule au ubaki nayo. Wachague moja.

HAKIMU: Upande wa Jamhuri, mmeelewa?

JAMHURI: Ndiyo Mheshimiwa.

(Upande wa Jamhuri unawasilisha nakala ya kesi waliyoitumia kama marejeo kwenye rufaa. Upande wa utetezi wakiongozwa na Wakili Kibatala wanaipitia nakala hiyo).

KIBATALA: Mheshimiwa, kesi ya Sauda Juma Urassa dhidi ya Coca-Cola Kwanza ambayo wenzetu wameitumia kama rejea sio ni distunguishable and non applicable kwenye shauri hili. Kesi ile ilishafikia hitimisho na Mahakama Kuu ikatoa uamuzi. Upande mmoja ukaomba kurudi Mahakama ya chini kwa ajili ya marekebisho, mahakama kuu ikakataa.

Sasa ni tofauti na shauri letu kwa kuwa bado mashahidi wanaendelea kutoa ushahidi wao na mahakama haijatoa uamuzi. Tunaomba mahakama ipuuze hoja zao na iamuru mashahidi waletwe. Tunaelewa kwa leo muda hautatosha, lakini waamriwe kuwaleta kesho, ili kesi iendelee.

HAKIMU: Jamhuri mna la kuongeza?

JAMHURI: Hapana Mheshimiwa.

(Hakimu anajipa muda wa kupitia vifungu vya sheria kabla ya kutoa uamuzi.)

HAKIMU: Nimesikiliza hoja za pande zote mbili. Jamhuri waliwasilisha maombi ya kutaka mashahidi wao kutoa ushahidi kwa siri. Nilisikiliza maombi hayo na kuyatupilia mbali kwa sababu mbalimbali (ikiwa ni pamoja na kwamba kesi hii ina maslahi ya umma).

Baada ya kutupilia mbali maombi yao, walikata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo. Kama nitaamuru kuleta mashahidi it means watatoa ushahidi wao kwa uwazi. Sasa ikitokea Mahakama Kuu ikakubaliana watoe ushahidi kwa siri, ina maana uamuzi huo wa Mahakama Kuu hautakuwa na maana.

Kwa hiyo, kwa kuheshimu taratibu za kimahakama, ninaliahirisha shauri hili hadi Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi kuhusu rufaa iliyokatwa.
_____
Baada ya Mahakama Wakili Dickson Matata anazungumza na vyombo vya habari:

MATATA: Jamhuri iliwasilisha maombi ya kutaka mashahidi wao kutoa ushahidi kwa siri, yani wawe ndani ya box, wasionekane bali isikike sauti tu. Maombi hayo yaliwasilishwa bila kutujulisha, lakini hata hivyo walishindwa. Sasa wamekata rufaa Mahakama Kuu. Kwa sasa tunasubiri Mahakama Kuu ituite, tuende tukapambane nao huko.

Mahakama itasikiliza hoja zote na kutoa uamuzi. Ikikubalina na upande wa Jamhuri it means tutarudi hapa Kisutu na mashahidi watakuwa ndani ya box. Lakini tunaamini Mahakama Kuu itatenda haki kwa kuzingatia kuwa kesi hii ina maslahi ya umma hivyo si sahihi kuwaficha mashahidi kwenye box. Umma unataka kuona mahakama ikifanya kazi kwa uhuru na ushahidi ukitolewa kwa uwazi.!

Credit: Malisa Page Fb
 
Watu wasio julikana wanataka wasijulikane hadi mahakamani??
“Lakini hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa, wala lililofichwa ambalo halitajulikana. ”
Luka 12:2
 
Mnawaficha kwanini wakati wao walishuhudia, wanafiki wawekwe peupe
 
Back
Top Bottom