Jaji aonya wazazi kuwatumia watoto kutoa ushahidi wa uongo

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Jaji Paul Ngwembe amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi wanaowatumia watoto kutoa ushahidi wa uongo mahakamani.

Jaji Ngwembe amesema hayo wakati akitoa elimu ya msingi ya sheria kwa wananchi mkoani Morogoro wanaofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kwa ajili ya masuala mbalimbali, ikiwemo kupata elimu hiyo.

Amesema katika jumuiko la utoaji wa elimu, kitendo cha kupeleka ushahidi wa uongo kimekuwa kikipelekea watuhumiwa kutumikia adhabu ya muda mrefu, ikiwemo kifungo cha maisha gerezani, bila kuwa na hatia.

“Nyie ndiyo mnakuja kushtakiana, tunawaomba wananchi kujiepusha na vitendo hivi kwani ikibainika umefanya uongo sheria zipo wazi kwa mtu anayetoa ushahidi wa uongo mahakamani na hatua zitachukuliwa dhidi yake,” amesema Jaji Mfawidhi huyo.

Ameeleza kuwa baadhi ya kesi zilizokatiwa rufaa baada ya washtakiwa kupewa adhabu ya kutumikia miaka 30 gerezani baada ya watoto kutumika kutoa ushahidi.

“Lakini uchunguzi unapofanyika upya ikagundulika kuwa mshtakiwa hakutenda kosa hilo, isipokuwa walitiwa hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani baada ya mtoto kufundishwa kusema uongo aliyefanya kosa hilo lazima achukuliwe hatua,”amesema.

Sambamba na hilo Jaji Ngwembe amezungumzia mmomonyoko wa maadili katika jamii na kuwaasa wananchi kukemea kwa nguvu zote.

Ameongeza kumekuwa na kesi nyingi za ulawiti kwa watoto wadogo, hivyo ni jukumu la kila mmoja anaposhuhudia vitendo hivyo kutoa taarifa kwenye vyombo husika ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.

“Sisi wasomi tusiipotoshe jamii kuwa hili linaruhusiwa kisheria, kanuni ya adhabu kifungu cha 154 kinatamka wazi kuwa kosa hili la mapenzi ya jinsia moja adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30 gerezani,”amesisitiza.

Katika jumuiko hilo, Jaji Mfawidhi huyo pia alifundisha masuala mbalimbali ya ulinzi wa mtoto, maadili katika jamii na malezi ya mtoto, ulinzi wa mtoto kuanzia akiwa tumboni mwa mama yake.

Mmoja wa wananchi, Jane Smart aliyefika kituoni hapo kwa ajili ya usikilizaji wa kesi amesema kuanzishwa kwa darasa la elimu ya msingi ya sheria kwakuwa wanapata mambo mengi ya msingi, aliahidi kuwa balozi wa kukemea ukatili kwa watoto ambao kwa sasa umekidhili.

Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro tangu kuanza utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 200,000.

Mpango huu wa kutoa elimu ya sheria awamu ya pili unatarajiwa kufanyika ndani ya kipindi cha mwaka mzima wa 2023, ambapo mada mbalimbali zitafundishwa na wataalamu wa sheria kwa kusaidiana na wadau wa Mahakama na Haki Jinai.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom