Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,783
- 14,975
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetoa tangazo kuhusu watu wanaohusishwa kwenye zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo limeanza kufanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam tokea Machi 17, 2025.
Taarifa kutoka kwenye tovuti rasmi ya Tume imeeleza "Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na Tume leo tarehe 19 Machi, 2025 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Ndg Kailima, R. K, uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania waliotimiza umri wa miaka 18 na zaidi na hawakuwahi kuandikishwa hapo awali."
Pia kwa mujibu wa taarifa hiyo tangazo hilo limetaja mambo mengine yanayohusika kwenye uboreshaji wa Daftari kuwa ni "kuandikisha wapiga kura ambao watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 siku ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025."
Imeongezwa kwamba Mambo mengine ni kuboresha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine la kiuchaguzi, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura ambao kadi zao zimepotea au kuharibika na kuboresha au kurekebisha taarifa za wapiga kura.
Aidha kwa mujibu wa tangazo hilo, mpiga kura anaweza pia kuwasiliana na Maafisa wa Tume waliopo katika Kituo cha Huduma kwa Mpiga Kura kwa kupiga simu bure kwenda namba 0800112100.
Pia soma ~ Zoezi la Uandikishaji na Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (Dar) halizingatii utambuzi wa wanaojiandikisha
==================================
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UANDIKISHAJI WA WAPIGA KURA MKOA WA DAR ES SALAAM
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkoa wa Dar es salaam, pamoja na zoezi hilo kuendelea vizuri kumejitokeza changamoto ya baadhi ya watu kujiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti. Kuhusu suala hili, napenda kutoa taarifa ifuatayo:
1. Baada ya zoezi la uandikishaji kukamilika katika vituo, Tume huchakata taarifa za watu wote walioandikishwa kupitia mfumo maalum (Automatic Fingerprint Identification System-AFIS), ambao una uwezo wa kuwabaini wapiga kura wote waliojiandikisha zaidi ya mara moja.
2. Aidha, Tume hufanya zoezi la kulinganisha sura za watu wote waliopo kwenda Daftari lengo ni kubaini iwapo kuna waliojiandikisha zaidi ya mara moja.
3. Iwapo itabainika mtu amejiandikisha zaidi ya mara moja. Yafuatayo yatafanyika:
Jina na taarifa za mtu huyo, hufutwa na mfumo katika vituo vingine na kubakizwa katika kituo cha mwisho alichojiandikisha katika Daftari. HIVYO, TAARIFA NYINGINE ZOTE ZA AWALI HUFUTWA.
(ii) Kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 114(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024 kujiandikisha zaida ya mara moja ni kosa la jinai na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani.
(iii) Baada ya uchakataji wa Daftari kwa mfumo wa AFIS watakaobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, orodha yao itakabidhiwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria; na
iv) Mpiga kura atakayejiandikisha zaidi ya mara moja, mbali ya kutenda kosa anaweza kushindwa kupiga kura kwa kuwa atafutwa katika vituo alivyojiandikisha na kuachwa kituo cha mwisho pengine siyo kituo chake sahihi anachopaswa kupiga kura.
Tunatoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam kuendelea kujitokeza katika siku nne zilizosalia kufikia tarehe 23 Machi, 2025 na tunaendelea kufuatilia zoezi hilo kwa karibu ili kila mwananchi aliyestahili kuandikishwa au kuboresha taarifa zake anapata haki hiyo.