Inawezekana hoja ya Profesa Assad ilikuwa na mashiko

GoldDhahabu

JF-Expert Member
Apr 29, 2023
4,694
6,396
Mwezi April 2021, tarehe 10, CAG Mstaafu, Profesa Assad, aliitoa kauli ambayo ilizua gumzo kwa watu wengi. Wapo walioiunga mkono, huku wengine wakiipinga vikali.

Nafikiri wafuatiliaji wa Habari wangali wakikumbuka. Profesa alisema kuwa asilimia sitini ya viongozi wa Serikali hawana uwezo mzuri wa kiutendaji.

Kauli ya Profesa ina mashiko?

Kuna mambo ambayo ukiyatafakari, huenda ukajikuta unauunga mkono msimamo wa huyo msomi.

Fikiri! Kipindi cha utawala wa JPM, kuliibuka wimbi la wanasiasa wa upinzani kutimkia chama tawala kwa kisingizio cha kuunga mkono jitihada za Rais wa kipindi hicho. Cha kujiuliza, walishindwa kumuunga mkono wakiwa kwenye Vyama vyao? Labda walizuiliwa na Viongozi wao, pengine. Lakini kwa nini sababu za karibia wote, kama si wote za waliovikimbia Vyama vyao zifanane?

Ingelikuwa ni mtihani, kwa mfanano huo wa majibu, kungeweza kupelekea kufutiwa matokeo. Mfanano wa aina hiyo huweza kuleta hisia za kuwepo kwa uongo uliokosa ubunifu. Kwamba, wahusika ni waongo wajinga. Hawana uwezo wa kuyapamba majibu kwa namna ambayo yanaweza yakamshawishi msahihishaji aamini kuwa wameyatoa vichwani mwao.

Fikiri, kumekuwepo na kelele nyingi dhidi ya Wabunge 19 wanaosadikika kuwepo bungeni kinyume cha Sheria. Lawama zimeelekezwa kwa uongozi wa bunge na Serikali. Si Serikali wala bunge walioweza kutoa sababu zenye mashiko juu ya huo utata. Kwa hapo utasema Serikali inao watu wenye uwezo mzuri wa kufikiria?

Fikiri, kumekuwepo kelele za muda mrefu juu ya unyonyaji wa Muungano. Mara kadhaa, watu wenye "akili" wametoa ushauri wa jinsi ya kuyamaliza hayo manung'uniko, lakini mara zote maoni yao yameishia kutupwa kapuni.

Hiyo haiwezi kuleta hisia kuwa ushauri wanaopewa ni mzito sana kuzidi uwezo wa viongozi wengi kuuelewa?

Fikiri, baada ya Lissu kupigwa risasi, watu kadhaa wameinyooshea Serikali kidole kwa kuituhumu kuwa ilihusika. Mpaka sasa, Serikali haijaweka wazi kama inastahili lawama au la.

Kama haikuhusika, imeshindwa kuwahakikishia watu wake kuwa haina hatia katika hilo? Hilo nalo linamuhitaji mtu mwenye akili sana kufahamu linalostahili kufanyika?

Fikiri! Suala la bandari za Tanganyika limeibua mzozo wa aina yake. Watu wa kada tofauti wamepiga kelele kuonesha kutoridhishwa na mkataba huo.

Lakini Jana, Chama tawala kimetoa tamko la kujiunga Serikali mkono kuendelea na mchakato wa huo mkataba.
Cha kushangaza ni kuwa Mwenyekiti wa hicho kikao ndiye pia aliyekuwa mwenyekiti wa kikao cha baraza la Mawaziri, ambalo kimsingi, lilisharidhia huo mkataba kabla ya wengine kufahamu. Ikiwa mwenyekiti ni yule yule, na pengine wajumbe ni wale wale, kulitarajiwa tamko liwe la tofauti na la awali ikiwa mwenye Serikali hajaamua vinginevyo?

Fikiri, mwaka 2018, Paschal Mayalla aliandika makala gazetini yenye kichwa: BUNGE LINAJIPENDEKEZA KWA SERIKALI?

Lilikuwa ni Gazeti la Raia Mwema la tarehe 09/04/2018. Badala ya bunge kujibu hoja zake, liliishia kumweka kitimoto kupitia kamati yake ya kudumu ya HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE.

Lakini miaka michache baadaye, ilithibitika kuwa aliyoyaandika yalikuwa na ukweli ndani yake. Kiongozi wa bunge alipojaribu kutoa maoni yake kama kiongozi wa mhimili unaojitegemea, kiongozi wa mhimili uliojichimbia chini zaidi alimshukia mithili ya mwewe mwenye njaa, na kilichofuatia kila mmoja anafahamu. Kwa lililompata mkuu wa mhimili, ni wazi kuwa haliko huru, ingawa katiba inalitaka liwe huru. Na kutekwa kwa uhuru wake kumechangiwa na uwezo finyu wa kufikiri wa viongozi waliopewa dhamana ya uongozi.

Kwa mifano hiyo michache, ni wazi kuwa huenda hoja ya msomi, Pro. Mussa Assad ilikuwa, na ingali na mashiko.

Ni busara Serikali ingewasikiliza akina "Assad" kwa maslahi mapana ya Taifa badala ya kuendelea kukumbatia ushauri wa watumishi wake ambao wengi wao wanasadikika kuwa ni vilaza!
 
Back
Top Bottom