Lycaon pictus
JF-Expert Member
- Jan 31, 2021
- 10,884
- 18,824
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA UNGUJA
MWALIMU JULIUS K. NYERERE
KWENYE MKUTANO WA VIONGOZI WA NCHI ZA AFRIKA, MJINI CAIRO
Tarehe 20 Julai, 1964
NINATAKA kuwaunga mkono katika kutoa shukurani zangu kwa Rais Nasser, serikali yake na kwa watu wa Jamhuri ya Nchi za Kiarabu, kwa ukarimu na kutupokea kwa kidugu. Katika kutoa shukurani hizi ni rahisi kueleweka kwamba ni jambo la wajibu wa kawaida tu, kumbe ni shukurani za moyoni hasa.MWALIMU JULIUS K. NYERERE
KWENYE MKUTANO WA VIONGOZI WA NCHI ZA AFRIKA, MJINI CAIRO
Tarehe 20 Julai, 1964
Kwa hiyo, kwa jambo hili la shukurani za kawaida ningependa kudokeza tu kwa kuwakumbusha wenyeji wetu mambo ambayo hayana haja hata kidogo kukumbusha. Kwamba bila ya juhudi ya waganga wa mvua wetu huko Afrika Mashariki, watu wa Misri wangepatwa na taabu ya kutukarimu kama vile sasa! Tukiachia mbali waganga wa mvua wenyewe, ni jambo la kututia moyo mkuu sisi sote kuona mambo makuu yaliyofanywa na Jamhuri ya Mwungano wa Nchi za Kiarabu kwa uongozi wa busara kubwa.
Kabla ya kuja hapa, nilitumaini kwamba hatutaanza tena kawaida ya kutoa hotuba. Nilifikiri kwamba mwenyeji wetu atatoa hotuba ya kufungua mkutano; na mmoja wetu atajibu na kisha tutaanza mara moja mambo yaliyopangwa tuyafanyie mashauri. Walakini naona kwamba sote imetubidi tutoe hotuba. Naambiwa kuwa huu ndio utaratibu wa kawaida wa Baraza la Umoja wa Mataifa. Lakini nadhani ziko sababu mbili za maana ya kutosha zinazoweza kutufanya tusifuate mwendo wa Baraza la Umoja wa Mataifa.
Kwanza, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hukutana kwa muda mrefu sana. Mkutano wetu hapa ni wa siku chache. Pili, Umoja wa Mataifa haukukusudiwa kamwe na hao waliouanzisha kuleta umoja wa nchi zote ulimwenguni. Nia maalum ya Jumuia yetu ni kuleta Umoja wa Afrika. Nionavyo ni kwamba ingetupasa tuwe na nafasi zaidi ya kujadiliana na kupunguza utoaji wa hotuba za kawaida na zenye kueleza mambo hayo ambayo kila mmoja wetu anayazingatia.
Kwa hiyo, hata sasa ambapo mkutano umekwisha anza, naomba Jumuia yetu ifikirie kubadili utaratibu wa shughuli zetu ili tuwe na nafasi zaidi ya kupeana vyema mawazo kati yetu badala ya kutoa hotuba za kueleza tu maoni ya kila mtu.
Hili ni ombi langu na pia maelezo ya mambo nitakayosema hapa; maana hotuba yangu ni fafanuzi zaidi juu ya mambo yaliyokwisha semwa hapa.
Tangu tulipoanzisha Jumuia yetu hii kubwa sasa imepita miezi 14. Kwenye mkutano wetu wa kwanza nilisema kwamba niliona matatizo yetu ni ya namna mbili Ila kwanza ni hilo la kuondoa kabisa masalia ya ukoloni katika Kontinenti letu, na la pili, tatizo la Umoja wetu.
Tangu hapo nchi kadhaa za Kiafrika zimepata uhuru wake; yaani Kenya, Unguja na Malawi. Na tena toka hapo Tanganyika imeacha kuwa peke yake katika macho ya ulimwengu ila pamoja na Unguja sasa ni Jamhuri ya Mwungano wa Tanganyika na Unguja. Twajua kuwa Zambia nayo itakuwa huru kabla ya mkutano wetu mwingine.
Lakini ijapo wengine wamekwisha kutoa pongezi zao, nami pia nataka kuwaunga mkono wenzangu kwa kuzikaribisha nchi za Malawi na Kenya kwenye Jumuia hii. Hasa nataka kuwakaribisha katika Jumuia hii yetu Dr. Kamuzu Banda na Mzee Jomo Kenyatta. Ni ajali mojawapo ya historia kwamba wakati baadhi yetu sisi vijana tumepata bahati ya heshima kubwa ya kushiriki katika kuunda Umoja wa Kiafrika, Jomo, jogoo mkubwa wa Uhuru wa Afrika na mzee wetu, hakuweza kushiriki kwa sababu Kenya haikuwa huru bado.
Lakini, tunaposhangilia mafanikio ya mwaka huu uliopita, tatizo letu lingali liko pale pale hasa. Uingereza na Ureno zingali zinatawala sehemu kubwa za Afrika. Matatizo yanayoletwa na nchi hizi mbili ni mbalimbali.
Uingereza inakubali kwamba ina makoloni katika Afrika. Ureno haikubali. Kwa hiyo, kazi yetu kwenye mkutano wa wakuu wa Jumuia za Madola huko London, ilikuwa kuitaka Serikali ya Uingereza kuchukua hatua za lazima ili hasa Rhodesia ya Kusini ipate uhuru wake kwa kutawaliwa na watu walio wengi zaidi katika nchi hiyo. Tumeondoka katika mkutano huo tukiwa na hakika kwamba hatua hizo zitachukiliwa.
Lakini Ureno haikubali kwamba ina makoloni katika Afrika. Ureno yadai kwamba imeenea mpaka katika Afrika. Kwa hiyo kazi yetu hapa siyo kuiomba Ureno itoe uhuru kwa makoloni yake; kazi yetu ni kuiomba Afrika; ni kujishawishi sisi wenyewe tuchukue hatua za lazima ili nchi za Angola, Msumbiji na Guinea ya Kireno ziwe huru kabisa. Kwa koloni tatu hizi maneno ya kubembeleza hayatafaa kitu. Kusema kweli naamini kwamba kadri tunavyobembeleza bembeleza zaidi ndivyo tunavyoleta madhara kwa heshima ya Afrika kama maneno hayo hayatafuatwa kwa vitendo. Maneno ya kubembeleza tu hayatawapa ndugu zetu wanaoteseka matumaini na yatapuuzwa kabisa na wakorofi wa Ureno.
Kwa hiyo, ombi langu ninalolitoa hapa ni matendo: matendo ya kuzipatia uhuru koloni za Kireno. Afrika ina nguvu za kutosha kumfukuza Mreno katika Kontinenti letu. Ebu tunuie katika mkutano huu kuchukua hatua ya lazima.
Lawama za uongo zimetolewa kuhusu Halmashauri ya nchi Tisa iliyowekwa na Umoja huu kushughulikia vyama vya wananchi ambao bado katika utawala wa kikoloni. Kwa kuwa mashtaka haya yamefanywa na nchi—nchi moja tu—ambayo haijalipa hata senti moja kwenye Halmashauri hiyo toka kuanzishwa kwake, sina haja ya kushughulika sana na mashtaka hayo. Lakini nataka kuutoa shaka mkutano huu juu jambo moja au mawili.
Kutokulipa katika mfuko wa fedha za kuwasaidia kuwakomboa ndugu zetu katika ukoloni hakuhusikani na ulegevu unaosemwa wa kazi ya Halmashauri hiyo. Nia ya kutolipa ilifanywa kabla ya Halmashauri hii kuanza kazi yake, na sababu yake ilikuwa ya kipuzi kabisa. Nia hiyo ya kutolipa fedha ilifanywa kwenye mkutano wa Addis Ababa mara tu mkutano huo ulipotenda dhambi ya ajabu ya kutoitia Ghana katika Halmashauri hiyo na ya kuichagua Dar es Salaam kuwa makao makuu ya Halmashauri hiyo. Ni wivu huu wa kitoto ndio ulioifanya nchi ya Kiafrika ati iache kutoa fedha kwa ajili ya kuwakomboa ndugu zetu wanaoteseka katika nchi za Msumbiji, Angola na Guinea ya Kireno.
Bwana Mwenye Kiti, lazima tutende vitendo. Tunao uwezo wa kuzikomboa Msumbiji, Angola na Guinea ya Kireno. Basi na tuutumie. Wale wasiokuwa tayari bado kushiriki kweli katika juhudi hii, waache kabisa kuvunja juhudi na kazi bora za Halmashauri ya Ukombozi pamoja na hiyo Komiti ya nchi tisa za Kiafrika.
Katika kuishambulia Halmashauri ya Ukombozi, Rais wa Ghana alifanya mashtaka ambayo maana yake nashindwa kuifahamu. Nayataja maneno yake: "Kuchagua Congo (Leopoldville) kuwa ndipo mahali pa kufunzia wapiganiaji uhuru lilikuwa jambo sawa na kulikuwa kila sababu njema kukubali Serikali ya Congo itoe maofisi na makazi kwa wajumbe wa Halmashauri ya Ukombozi. Kwa hiyo isingalifaa kwa wapiganiaji uhuru wa Afrika kuwekwa mahali palipo wazi kufikiwa na ujasusi bila wasiwasi na kukatishwa tamaa mambo ambayo wameyapata katika muda wa miezi minane iliyopita. Je, matokeo gani yanaweza kupatikana kwa kuwaaminisha wapiganiaji uhuru wafundishwe katika mikono ya kibaraka wa Wakoloni wapendao kuwatawala wenzao".
Kwa kuwa Komiti ya Ukombozi inafanya kazi yake mjini Dar es Salaam, na siyo Leopoldville, naweza kuelewa maana moja tu kwa maneno haya ya kushangaza. Ni lazima yawe na maana kwamba maofisi na makazi ya Komiti ya Ukombozi yangalikuwa Congo (Leopoldville). Lakini badala ya kuchagua mahali hapo, Umoja wa Nchi za Afrika ukachagua mahali pengine, mahali ambapo nikirudia tena maneno ya huyo msemaji, “pako wazi kufikiwa na majasusi wenye hila na kuzuiwa kazi zao na hata kukatishwa tamaa”, katika miezi minane iliyopita.
Halafu Mkombozi huyo Mkubwa (Great Osagyefo) anaendelea kuuliza swali: "Je, matokeo gani yanaweza kupatikana kwa kumwamini kibaraka wa ukoloni awafundishe wale wanaopigana na ukoloni?"
Kwanza, Bwana Mwenye Kiti, kama nilivyoeleza ni sawa, na kwamba maana yake hasa ni kwamba Rais wa Ghana anaamini kuwa Komiti ya Ukombozi ingalifaa iwekwe Leopoldville, basi yote niwezayo kufanya ni kuwauliza ninyi wenyewe mfikirie matokeo yake yangelikuwa nini.
Pili, kama mashtaka haya ya "kibaraka wa Wakoloni" yanahusu nchi yangu, au kiongozi wake ye yote, basi wale wanaojua nchi yangu, viongozi wake na watu wake, na wale wote wapendao ukweli, watafahamu kabisa kwamba mashtaka haya ni uwongo mtupu.
Tatizo letu jingine ni hilo la Umoja. Hapa tena wakati wa maneno matamu umekwisha. Sisi katika Afrika, tumekwisha sema yote yapasayo kusema juu ya haja ya umoja. Hakuna Kontinenti jingine lililofanikiwa katika jambo hili hata nusu ya vile ulivyofanikiwa sisi katika Afrika. Jumuia hii na mkutano huu peke yake ni ushahidi uonekanao wazi kuthibitisha mafanikio haya.
Kwa kweli tumefanikiwa mno hata hakuna kiongozi ye yote wa Kiafrika ambaye hata kama haamini katika umoja huu aweza kusubutu kusema kinyume. Kwa hiyo jambo linalotakiwa sasa siyo kuhubiri zaidi habari za umoja, ila kutimizatimiza zaidi umoja huo.
Pingamizi zilizopo nazijua. Wala sijadharau pingamizi hizi juu ya umoja. Kwa kweli ni kwa kuzifahamu sana pingamizi hizi katika kujenga umoja ndiyo maana nikatoa shauri kwa wenzangu katika Afrika Mashariki kwamba tujiunge hata kabla ya kupata uhuru wetu. Lakini hata shida hizi ziweje kwa ukubwa, zaweza kuondolewa. Shida zenyewe ni kama miguu ya jongoo tu. Mtoto wa jongoo alimwuliza mama yake: "Mama, mbona nina miguu mingi, je nianze kwenda kwa mguu au miguu ipi?" Nasi hapa tulitoe jibu hilo hilo la mama jongoo kwa mwanawe : "Nenda mwanangu, nenda tu”.
Jambo tunalohitaji ni kuwa na mazoea ya umoja na ushirika. Tusijiulize kama tungoje mpaka sote tutakapokuwa tayari kwenda. Lazima tuchukue kila hatua ya kweli inayotupa moyo wa kuungana. Lazima tuwaulize ndugu zetu wa Afrika Kaskazini, “Mbona hamjaungana zaidi?" "Kwa nini msifanye vitendo vya kuleta tamaa ya kuwa na umoja mkubwa zaidi kati yenu ?”
Lazima tuhimize nchi za Afrika Magharibi ziungane, na lazima tuhimize nchi za Afrika Mashariki pia ziungane. Hatuwezi kusaidia njia za kuleta umoja wa Afrika kwa kuvunja matendo yake. Maana ni kutenda ndiyo kutaleta umoja kwa Kontinenti lote, siyo mawazo ya kufikiria umoja peke yake.
Hapo kwanza, nilifikiri kwamba sote tulikuwa na nia ya kweli ya kutaka iwepo Serikali moja Kuu ya Kontinenti la Afrika; na ya kuwa tofauti kubwa kati yetu ilikuwa tu njia ya kuiunda. Nasikitika kwamba sasa naanza kuingiliwa na mashaka juu ya jambo hili. Ninazidi kuamini kwamba tumegawanyika katika jambo hili baina ya wale wenye nia ya kweli ya kutaka Serikali kuu ya Kontinenti zima na kufanya jitihada kubwa ya kuleta mafanikio kwa kuondoa vipingamizi kimoja kimoja na wale ambao kazi yao ni kutumia tu neno "Serikali Moja" kwa madhumuni ya kudanganya watu.
Hakuna hila mbaya zaidi ya kuharibu azimio hili la kuleta Serikali moja ya Afrika yote kama vile utumiaji huu wa daima wa maneno ya kudanganya.
Nchi za Uhabeshi na Usomali zina ugomvi juu ya mpaka wa nchi ambao ni wa hatari. Lazima tuwe na matumaini kwamba nchi hizi mbili ndugu zitamaliza tatizo hili gumu. Lakini baadhi ya watu wengine jambo hili wanalichukulia kuwa nafasi ya kuwadanganyia wengine ati laweza kumalizwa tu kwa kuwa na Serikali moja Afrika nzima na kama waongo hawana nia hiyo.
Kwa bahati mbaya, nchi ya Kenya na Usomali pia zina tatizo namna hiyo hiyo. Jibu lake nini? Ati rahisi tu— "Serikali Moja ya Afrika nzima".
Ugomvi mwingine kuhusu mpaka wazuka kati ya nchi ndugu mbili za Algeria na Morocco. Kadhalika, lazima tuwe na matumaini na kuomba kufanya yote tuwezayo kuwasaidia ndugu zetu wagundue njia ya suluhu. Lakini kwa wale wapiga domo la uwongo wanalitumia jambo hili kudanganyia ati ni kisingizio cha kuwa na Serikali moja ya Afrika nzima.
Na jambo la mzaha na kichekesho kabisa katika yote: Nchi ya Upper Volta inalalamika kwamba Ghana imechukua kipande cha nchi yake; inaitaka kirudishwa. Jibu lake nini? Tunaweza kubahatisha. "Serikali Moja ya Afrika”.
Jambo hili la "Serikali Moja katika Afrika" limekuwa kisingizio kwa kufanyiana baadhi ya mambo yasiyokuwa ya kidugu kabisa katika Afrika hasa katika sehemu yetu ya Afrika.
Tulipatwa na maasi ya Jeshi katika Afrika ya Mashariki, na ilitupasa bila kutaka kwa hiari zetu kuomba masaada kwa serikali ya kikoloni ya zamani katika nchi zetu. Lakini katika nchi yangu Balozi mmoja wa nchi ndugu ya Kiafrika, alishangilia, nami yanibidi kuomba mtu huyo aondolewe. Ni kisa gani kilichomfanya afurahi hivi wakati nchi ya ndugu yake ya Kiafrika ilipopata maafa? Jawabu "Serikali Moja Afrika nzima". Mambo hayo ya maasi ati yakawa kisingizio cha kutaka Serikali moja Afrika nzima.
Nchi za Kenya, Uganda na Tanganyika zinatamka kwamba zinataka ziungane ziwe nchi moja. Zinatamka hivi kuamini kabisa kwamba jambo hilo litakuwa la manufaa makubwa kwa nchi zake na chanzo cha kuunda umoja wa Afrika. Lakini tamko hili limeleta mashambulio makali sana na kunafanywa jitihadi kubwa iwezekanavyo kuzuia kuleta umoja huu. Kwa nini? Ati mpaka tuwe na "Serikali Moja Afrika nzima" kwa kuwa ati inafikiriwa kwamba Mwungano wa nchi za Afrika Mashariki ni kinyume cha azimio la Mkataba wa Addis Ababa. Hoja ajabu inaletwa kimbelembele eti kadri tunavyokaa tumetengana ndiyo rahisi kupatikana "Serikali Moja ya Afrika nzima". Na sasa hapa hapa, hoja hii tena ya ajabu inayodai shabaha hiyo hiyo imezidi kuletwa tena kimbelembele.
Tunaambiwa kwamba tusimweke Katibu Mkuu wala tusichague mahali pa Makao Mkuu pa Jumuia hii ya Umoja wa Afrika. Sababu yake nini? Tumeambiwa kwa maneno mengi mengi eti "Serikali Moja ya Afrika nzima!"
Na kwa kumaliza mfululizo huu wote wa upuuzi; baada ya kuleta hoja hizi za ajabu kupinga umoja katika Afrika Mashariki sasa twaambiwa kwenye kinara hiki hiki tena kwamba wale walio tayari waungane. Ajabu, ati sasa twapewa ruhusa tuungane. Kwamba Umoja wa Nchi za Amerika ulianza na nchi kumi na tatu; Urusi ilianza na nchi tano. Kama ningalikuwa mtu wa kujali ningesema kuwa sisi wa Jamhuri ya Mwungano wa Tanganyika na Unguja tuko tayari; na tungaliiomba Ghana ijiunge na Jamhuri yetu ya Mwungano. Lakini mimi si mtu wa kujali. Najua ni vigumu ya kutosha kuleta mwungano katika Afrika Mashariki bali ya maneno maneno ya watu wa nchi za nje kuyaleta ili wazuie mwungano huo.
Bwana Mwenye Kiti, lazima tuseme kweli.
Baadhi ya watu wako tayari kutumia akili zao nyingi kwa kuangamiza nafasi ye yote ya kuleta umoja katika Kontinenti letu mradi ati mwandishi mjinga wa historia ataweza kuandika kuwasifu kwamba ni wao peke yao walitaka sana umoja wa Afrika.
Bwana Mwenye Kiti, unaweza kuwafanya baadhi ya watu kuwa wajinga wakati fulani fulani, lakini ilivyo kweli kabisa, jitihadi hiyo ya kuwafanya watu wote wajinga kwa wakati wo wote haionyeshi heshima wala upendo mkubwa kwa Afrika.
Pia nataka kutoa oni kwamba kuna tofauti kubwa baina ya maana ya Serikali ya Kontinenti zima la Afrika ambayo sisi sote twaitaka kwa moyo wote, na Serikali Moja Kuu ya kupiga domo tu. Kuwa na Serikali moja ya Afrika ndiyo kuifanya Afrika nchi moja hata kama — ikiwa ni lazima, Mwungano wa nchi. Sifa muhimu ya taifa lenye kuheshimika ni ile ya kuwa na mamlaka. Maana yake ni kwamba zile ambazo zamani zilikuwa nchi mbali mbali lazima zitoe mamlaka yake kwani ni taifa hilo tu linalokuwa lenye mamlaka.
Lakini tunaambiwa kwamba hiyo Serikali Moja Kuu haihitaji nchi zake ndogo kuvua mamlaka yake. Kiongozi huyo atakuwa wa ajabu sana, ambaye nchi zetu mojamoja hazitaki kuyavua mamlaka yake kumpa, na bado anakuwa mwenye nguvu sana, na ambaye tunamtaka kutimiza madhumuni ya taifa la kisasa.
Bwana Mwenye Kiti, wazo hili la kuwa na Serikali ya Kontinenti la Afrika, ni kubwa na la maana sana. Tuwezalo kufanya juu ya jambo hili ni moja tu, yaani kufikiria sana namna ya kulitimiza.
Bwana Mwenye Kiti, ningependa kueleza mawazo ya nchi yangu mbele yenu juu ya jambo hili la umoja wa Afrika. Tumeamua kupata umoja wa Afrika kwa kuwa na Serikali moja ya Kontinenti zima. Tumekwisha kubali kuvua mamlaka yetu kwa kupata Mwungano. Tutakuwa tayari kuvua tena mamlaka yetu kupata umoja mkubwa kabisa.
Hatuamini kwamba tunachagua baina ya kupata umoja wa Afrika hatua kwa hatua, na kuupata umoja wa bara lote mara moja. Jambo hili la kupata umoja mara moja haliwezekani kwetu isipokuwa labda kwa wale wenye fikara za ajabu.
Sisi binadamu hatukupewa uwezo wa kutaka vitu, vikawa hapo hapo. Baina ya kutaka kitu na kupatikana kwa kitu hicho pana muda. Muda huu wakati mwingine ni mrefu, na wakati mwingine ni mfupi, na kwa kweli, kadri kitu chenyewe kilivyo kikubwa zaidi, ndivyo muda wake unavyokuwa mrefu zaidi. Lakini muda uwe mfupi au mrefu, ni muda tu. Kukataa maendeleo ya hatua kwa hatua katika mwendo huu wa kuunda umoja, ni sawa na kuukataa umoja wenyewe.
Kukataa maendeleo ya hatua kwa hatua katika kuunda umoja wa Africa, ni sawa na kutumaini kwamba siku moja Mwenyezi Mungu atasema: "Na pawe umoja katika Afrika", na hapo pawe na umoja! Au kuomba tupate jambazi moja mshindi litakaloishinda Afrika nzima kwa mabavu. Lakini hata huyo mshindi itambidi kwenda hatua kwa hatua. Kusema kwamba njia ya hatua kwa hatua iliundwa na wakoloni ni upuuzi mtupu. Nimesikia wakoloni wakilaumiwa kwa mambo mengi, lakini sio kwa shida za binadamu. Wao sio Mungu!
Njia moja tu iliyo wazi kwetu, ni ya kuunda umoja hatua kwa hatua baina ya nchi kwa nchi na kwa matendo kadhalika. Kwa mfano, kama nchi za Afrika Kaskazini zingekuwa tayari kuungana kufanya ushirika wa nchi moja kubwa, mimi binafsi ningeshangilia hatua hiyo kuwa ni hatua ya kufikia umoja wa Afrika.
Kila moja katika nchi hizo ingeweza kuamua kama wakati umewadia wa kuunda umoja huo utakiwao. Walakini, kama kwa upande mwingine watu wa nchi hizo wakiona kwamba mambo yao ya kuunganisha nchi bado hayajawa tayari, bali wao wenyewe wako tayari kushirikiana katika mambo mengine, hapo pia, mimi binafsi ningeshangilia ushirika huo kuwa ni hatua ya kufikia umoja wa Afrika.
Jambo la lazima ni kwamba hatua hizi zote lazima zifuate shabaha ya Umoja wa Nchi za Kiafrika. Ndiyo maana nchi yangu inayo hamu sana kutaka kuona moyo huu na matakwa haya ya umoja vimetiwa nguvu kwa kila hali, pamoja na kuchaguliwa kwa Katibu Mkuu wa kuwekwa kwa Makao Makuu ya Umoja huu.
Bwana Mwenye Kiti, kama nilivyokwisha eleza mwanzo wa hotuba yangu, sikuwa na haja ya kutoa hotuba ndefu. Nimekwisha tumia muda mrefu mno wenu juu ya mambo ambayo hakika hayapendezi. Sasa nataka kumaliza hotuba yangu fupi juu ya jambo jingine kabisa.
Tatizo kubwa linalotukabili juu ya Kontinenti letu, tukiungana au tukiwa tumetengana, ni lile la maendeleo. Tunalo tatizo la kuinua hali ya maisha ya watu wetu kufikia upeo unaofikiriwa wafaa kulingana na hali za maendeleo ya kisasa. Jambo hili nimelisema kwanza na sasa nalisema tena hapa, kwamba mwaka huu 1964 ni mwaka wa 1964 kwa watu wote. Mmasai anayeishi Afrika Mashariki, mkulima wa Misri na mwenyi mali nyingi anayeishi New York huko Amerika au mjini London Uingereza.
Maji safi au afya njema vinahitajiwa sawa kwa Waafrika, Wazungu na Waamerika ya Kaskazini. Mama ye yote anayeishi katika sehemu isiyokuwa na maendeleo kabisa katika nchi yangu, huwa hana raha sawa na mama aliye tajiri kabisa anayeishi Paris kama watoto wao hawana afya na ni wanyonge.
Lakini maendeleo ya kisasa hutegemea sana biashara ya ulimwengu. Lakini biashara ya ulimwengu ni kama bomba lenye midomo miwili; linayonya zaidi kutoka nchi zinazoendelea na kutia katika nchi zilizokwisha endelea kuliko linavyotia katika nchi zetu kutoka katika nchi zilizokwisha endelea. Matokeo yake ni kwamba pengo baina ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea katika ulimwengu linazidi kupanuka, halipungui!
Tunatumaini kwamba mkutano wa biashara uliofanywa hivi karibuni huko Geneva, labda waweza kuleta mabadiliko katika mambo haya.
Lakini jambo moja lililokwisha tajwa hapa, na ambalo lazima tulipe moyo, ni biashara baina yetu sisi wenyewe. Ndiyo kusema lazima tuuziane vitu.
Huko katika Afrika Mashariki tunao Umoja wa Kazi za Kushirikiana. Ujuzi tuliokwisha pata juu yake umeonyesha kuwa ushirika wa biashara hauna maana ye yote usipotoa faida sawa sawa kwa wote waliouunda. Kutokana na maarifa hayo, imetubidi tukae kitako tupatane juu ya kugawana viwanda katika nchi zetu. Kila nchi yetu moja imepewa baadhi ya viwanda vinavyohitajiwa kwa biashara ya Afrika Mashariki nzima.
Bwana Mwenye Kiti, nataka kuongeza neno langu moja kuunga mkono wale waliokwisha toa ombi hili, nami nafurahi kuona kwamba ombi hili lilitolewa na Rais wa Ghana, kwamba tufikirie kwa makini kabisa uwezekano wa kugawanya baadhi ya viwanda kwa kufuata hali ya Kontinenti letu, au, japokuwa kwa kufuata majimbo. Jambo hili litatuwezesha kujifaidia kwa biashara inayofanywa na watu millioni 250 wa Afrika, biashara ambayo sasa inawafaidia watu wengine; na hasa watu walio matajiri zaidi katika ulimwengu.
Na mwisho, Bwana Mwenye Kiti, hebu niombe dua. Dua kwa sisi tuliokusanyika hapa; dua kwa watu wengi sana Waafrika wanao hangaika sana, wote tutumie nafasi tulizopata kwa uhuru wetu na ufundi wa kisasa, tujikomboe katika makombo ya ukoloni, na tuwainue watu wetu kwa kuwafungulia pingu za umasikini, ujinga na maradhi.