HOTUBA ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani - Wizara ya Nishati na Madini 2012

Molemo

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
14,534
13,225
Tuchangie mjadala wa sekta hizi nyeti tukikumbuka manenoya hayati Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE cha mwaka 1962,nanukuu: "Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa nabinadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwakuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana"

John Mnyika anatikisa bunge sasa hivi.

Wabunge wa CCM wameshindwa kuvumilia wanamshangilia kwa nguvu sana.

Shangwe za bunge zima zimesababishwa na Mnyika kutoa shutuma nzito sana dhidi ya Mkurugenzi mtendaji wa Tanesco William Mhando aliyesimamishwa kazi. Mnyika amesema CDM inataka serikali imkamate na kumfungulia mashtaka mara moja.

Pia Mnyika ameshutumu vikali baadhi ya watu wakiwemo wabunge wanaohangaika huku na kule kutaka kusafisha mkurugenzi huyu kwa maslahi binafsi.

Tutaweka hotuba yote hapa muda mfupi ujao....

=============
Sehemu ya Hotuba:

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Julai 2011 niliwasilisha bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2010/2011 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Kufuatia maoni hayo, yapo masuala machache ambayo Serikali imeyazingatia kwenye utekelezaji na mengine mengi serikali haikuyazingatia pamoja na umuhimu wake kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi. Hivyo kupitia mapitio haya ya utekelezaji, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze hatua ilizochukua juu ya maoni hayo ambayo baadhi yalijitokeza pia kwenye maoni ya Kamati za Kudumu za Bunge na michango ya wabunge kwa nyakati mbalimbali. Hakuna sababu ya kutumia muda mrefu kutoa na kujadili maoni mapya ikiwa hakuna mfumo thabiti wa kuhakikisha maoni na maazimio yanatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipitia kitabu cha pili cha matumizi ya kawaida ya Wizara ya Nishati na Madini (Volume II Supply Votes) Fungu la 58 kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na kubaini kwamba ilikuwa ni bajeti ya mgawo mkubwa wa posho na ufujaji ya zaidi ya shilingi bilioni 7.9 ya posho na matumizi mengine yasiyo ya lazima. Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka serikali ifanye marekebisho kwenye bajeti ili fedha hizo zipunguzwe na kuelekezwa kwenye kuongeza ujenzi wa miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na kuongeza kiwango cha fedha katika mfuko wa wachimbaji wadogo wa madini. Aidha, yako matumizi mengine ya ujenzi wa maofisi na gharama kubwa za kisheria yaliyopaswa kuhamishiwa katika miradi muhimu ya maendeleo ikiwemo ya umeme vijijini. Kwa kuwa Wizara iliahidi kuufanyia kazi ushauri wa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza kiwango cha fedha kilichookolewa kutokana na kutekeleza ushauri huo na kutoa pia maelezo ni kwanini katika makadirio ya mwaka 2012/2013 pamejitokeza kwa mara nyingine tena matumizi yasiyokuwa ya lazima.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka kiwango cha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuongezwa ili vipaumbele vifuatavyo viweze kuzingatiwa kwa uzito unaostahili: Kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha. Hatua hizo ziambatane na kuwekeza katika Bomba la Gesi, pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika kwenye magari, viwandani na majumbani; kuhakikisha tunazalisha 360MW za umeme kila mwaka ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na kumaliza tatizo la mgawo wa umeme na mwisho kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya usafirishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi vijijini.

Kusuasua kwa utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme

Mheshimiwa Spika, ili kushinikiza nyongeza hiyo ya bajeti na utekelezaji wa vipaumbele hivyo, Kambi Rasmi Bungeni ilipendekeza bunge kupitisha azimio la kutangaza kwamba ukosefu wa nishati ni janga la taifa na kupitisha mpango wa dharura na maamuzi ya hatua za haraka ambazo serikali inapaswa kuzichukua kwa uwajibikaji wa pamoja. Tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini akaahidi kwenda kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha kwenye mradi wa dharura wa umeme.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo inaelekea ahadi hiyo ilikuwa hewa kwani tarehe 13 Agosti 2011 Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura tofauti ambao ulijikita katika serikali kuidhamini TANESCO kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya bilioni 400. Pamoja na kuikumbusha serikali bungeni kutekeleza ahadi hiyo ya Waziri Mkuu, serikali ilipuuzia ushauri uliotolewa. Matokeo yake mpaka sasa Shirika la Umeme (TANESCO) halikuwezeshwa kupata kiwango cha fedha kilichopangwa na utekelezaji wa mipango husika kusuasua.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Mpango wa Dharura ulipowasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 serikali ilieleza kuwa imepanga kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011. Kati ya hizo, MW 150 ilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano baina ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na TANESCO; ilitarajiwa kuzalishwe MW 50 Septemba, MW 50 Oktoba na MW 50 Novemba 2011. Kimsingi, kauli iliyotolewa bungeni kuwa mitambo ilikuwa imepatikana haikuwa ya kweli. Hivyo, ahadi ya kupata umeme huo ilikuwa hewa. Mpaka sasa hakuna hata MW moja ambayo imezalishwa kwa ushirikiano kati ya NSSF na TANESCO. Ujumbe ulipotumwa Marekani kwenda kuona mitambo iliyokuwa inaelezwa kwamba ipo haikukuta mitambo yoyote, walikuta kampuni ambayo haikuwa na uwezo kama ilivyokuwa kwa Richmond Development LLC; timu hiyo ya wataalamu ilibidi kwenda Ufaransa nako ikakosa mitambo ya dharura. Hivyo, fedha nyingi za umma zimetumika kufuatilia ahadi hewa na umeme mpaka sasa haujapatikana na taifa limerejea kwenye utegemezi wa mitambo ya kukodi ya gharama kubwa ya umeme kwa sababu ya udhaifu na uzembe wa kiutendaji. Hivyo, si kweli kwamba mpango wa dharura wa umeme umetekelezwa kwa mafanikio ya asilimia 64.5 kama inavyodaiwa na Serikali kwa kupunguza lengo lilopitishwa bungeni, bali mpaka sasa umetekelezwa kwa asilimia 47.6 tu; katika muktadha huo, serikali inabidi ieleze kwa ukweli ni kwa vipi mgawo wa umeme utaepukwa kwa kuzingatia pia barua ya Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO kwa Rais yenye kueleza uwepo wa tishio la mgawo wa umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine upungufu wa umeme unaojirudia rudia matokeo ya serikali kushindwa kutekeleza kwa wakati mpango wa kuweka mitambo ya MW 100 Ubungo (Dar es salaam) na MW 60 Nyakato (Mwanza) ambayo iliwekwa kwenye mpango wa umeme wa mwaka 2009 ambao ulicheleweshwa na hatimaye wakati wa Bajeti ya mwaka fedha 2010/2011 Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini wote waliahidi kukamilisha uwekaji wa mitambo hiyo mapema mwaka 2011. Hata hivyo pamoja na miradi hiyo kuingizwa kwenye mpango wa dharura tarehe 13 Agosti 2011 hakukuwa na usimamizi thabiti wa kufanya ikamilike kwa wakati. Kuzinduliwa kwa mtambo wa MW 100 Ubungo katika mwaka wa fedha 2012/2013 ni hatua ndogo kwa kuzingatia kwamba, ilipaswa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee taifa liongeze jumla ya MW 360 toka kwenye mitambo ya kununua na si ya kukodi ili kuendana na malengo ya mpango wa taifa wa miaka mitano. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa miradi hiyo na hatua za uwajibikaji zilizochukuliwa kutokana na udhaifu huo.

Kashfa ya Ununuzi wa mafuta ya kufua umeme
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tulitahadharisha kwamba mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta kwa ajili ya kufua umeme isitumike kama mwanya wa ufisadi na kuzalisha "Richmond nyigine". Inaelekea kansa hii ndani ya Serikali inayoongozwa na CCM ya kuachia dharura ziendelee kwa manufaa ya wachache imesambaa kwa kiwango cha kuwa vigumu kutibika isipokuwa kwa mabadiliko ya mfumo mzima wa utawala. Katika siku za karibuni kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wazabuni ambao wamekosa zabuni ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL kutokana na uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wa kuipatia zabuni kampuni ya PUMA Energy (Tz) Ltd. (zamani ikiitwa BP (Tz) Ltd.) ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 50. Licha ya malalamiko ya wazabuni hao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa imefanywa na inaendelea kufanywa ndani na nje ya Bunge hili tukufu ili uamuzi huu wa Katibu Mkuu Maswi ubatilishwe kwa maslahi ya makampuni hayo na wapambe wake wa ndani na nje ya Bunge lako tukufu. Aidha, wanaoendesha kampeni hiyo wanashinikiza Katibu Mkuu Maswi ajiuzulu kwa kile kinachoitwa kitendo chake cha kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa nyaraka ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, tarehe 10 Juni, 2011 aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO William Mhando alimwandikia Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo (RITA) – iliyokuwa inasimamia ufilisi wa IPTL – kumtaka aendeshe mitambo ya IPTL ili kufua MW 100 za umeme ili kuweza kuondoa mgawo wa umeme uliokuwa unaendelea sehemu mbalimbali nchini. Nyaraka hizo zinaonyesha kwamba mara baada ya kupata barua hiyo, tarehe 24 Juni 2011, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) akimwomba mwongozo na ushauri juu ya utaratibu wa manunuzi ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kwa dharura.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA alitoa mwongozo kwa RITA kwa barua yake ya tarehe 28 June, 2011 ambapo aliielekeza RITA itumie mamlaka yake chini ya kanuni ya 42 ya Kanuni za Manunuzi ya Umma zinazohusu Bidhaa, Kazi na Huduma zisizokuwa na Ushauri Elekezi na Mauzo ya Mali za Umma kwa Tenda, Gazeti la Serikali Na. 97 la mwaka 2005 (Public Procurement (Goods, Works, Non-Consultant Services and Disposal of Public Assets by Tender) Regulations, Government Notice No. 97 of 2005). Kanuni hiyo inamruhusu Afisa Masuhuli kuamua namna ya kufanya manunuzi kwa dharura bila kujali mipaka ya mamlaka yake endapo kwa kufanya hivyo kutahakikisha uchumi na ufanisi wa manunuzi hayo na endapo ataona ni kwa manufaa ya umma kwamba bidhaa au kazi zenye thamani inayozidi mamlaka yake zinunuliwe kama suala la dharura.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupata mwongozo huo wa PPRA, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia Katibu Mkuu Maswi barua ya tarehe 18 Julai, 2011 kumweleza kwamba katika makampuni matano yaliyoonyesha nia ya kuiuzia IPTL tani 500 za mafuta kwa siku zilizokuwa zinahitajika kuendeshea mitambo yake kwa mwezi Julai, 2011, kampuni za OilCom na Shell hazikuwa na akiba ya mafuta wakati ambapo kampuni ya Mogas ilikuwa na lita laki tatu tu. Kwa upande mwingine, kampuni ya Oryx ilikuwa na tani 6,000 lakini ilikuwa inauza mafuta hayo kwa dola za Marekani 1,069.30 au shilingi 1,668,456.02 kwa tani. Aidha, kampuni ya BP (sasa Puma Energy) ilikuwa na tani 9,000 na ilikuwa tayari kuuza mafuta hayo kwa dola za Marekani 901.02 au shilingi 1,405,864.77 kwa tani. Kwa kuzingatia maelezo hayo, Katibu Mkuu Maswi alitoa ridhaa kwa RITA kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa kampuni ya BP kwa bei iliyotajwa hapo juu.

Mheshimiwa Spika, licha ya ukweli kwamba mafuta ya BP yalikuwa na bei ndogo ikilinganishwa na bei ya Oryx, tarehe 27 Septemba, 2011 Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alisaini mkataba wa kununua mafuta kutoka Oryx kwa bei ya dola za Marekani 926.98 au shilingi 1,501,707.60 kwa tani. Aidha, wiki moja kabla ya hapo, yaani tarehe 21 Septemba, Mkurugenzi Mtendaji huyo alikwishasaini mkataba mwingine na kampuni ya Camel Oil kwa bei ya dola za Marekani 905.24 au shilingi 1,466,488.80 kwa tani. Kama inavyoonekana, mikataba yote miwili ilikuwa na gharama kubwa zaidi kwa tani kuliko bei ya BP. Hata hivyo, mkataba wa BP ulikatishwa na TANESCO ikaanza kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa makampuni ya Oryx na Camel Oil.

Mheshimiwa Spika, kitu cha ajabu ni kwamba licha ya mikataba ya makampuni ya Oryx na Camel Oil kuonyesha bei za shilingi 1,501.70. na shilingi 1,466.49 kwa lita, TANESCO ilianza kununua mafuta ya makampuni hayo kwa shilingi 1,850 kwa lita! Kwa maana hiyo, kwa mikataba ya kununua jumla ya lita 16,110,000 kwa mwezi kutoka kwenye makampuni hayo, TANESCO ilikuwa inayalipa makampuni hayo jumla ya shilingi 29,803,500,000 kwa mwezi. Kwa ulinganisho, mafuta yaliyouzwa na BP kwa mkataba na RITA yaliigharimu Serikali shilingi bilioni 13,140,000,000 kwa bei ya shilingi 1,460 kwa lita. Hii ndio kusema kwamba kama TANESCO ingeendeleza mkataba na BP badala ya kuuvunja, gharama ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL ingekuwa shilingi 23,520,600,000 na hivyo TANESCO ingeliokolea taifa shilingi 6,282,900,000 kila mwezi!

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine kumekuwa na taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari kwamba Mkurugenzi Mtendaji Mhando hakutendewa haki aliposimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi juu ya utendaji kazi wake. Nyingi ya taarifa hizo zimetolewa bila kuwa na faida ya kuangalia nyaraka zinazohoji uadilifu na uaminifu wa Mkurugenzi Mtendaji Mhando.

Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi Mkuu Mhando ni mkurugenzi na mwanahisa wa kampuni binafsi inayoitwa Santa Clara Supplies Co. Ltd. ya Dar es Salaam. Wakurugenzi wengine ni mke wake Eva Martin William, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji, na watoto wao. Kwa mujibu wa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, mnamo tarehe 20 Desemba, 2011, Santa Clara Supplies iliingia mkataba na TANESCO ambapo Santa Clara Supplies ilikubaliwa kuwa mgavi wa vifaa vya ofisini vya TANESCO kwa gharama ya shilingi 884,550,000. Mkataba huu ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando kwa niaba ya TANESCO na mkewe Eva Martin William kwa niaba ya Santa Clara Supplies. Aidha, barua ya TANESCO iliyoitaarifu Santa Clara Supplies kwamba imepatiwa zabuni hiyo iliyoandikwa tarehe 24 Novemba, 2011 ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaelekeza kwamba "… kiongozi wa umma hatajiweka katika hali ambayo maslahi yake binafsi yatagongana na wajibu wake kama kiongozi wa umma." Aidha, "… kuhusiana na uwazi kwa wananchi, viongozi wa umma watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi na umma na haitatosheleza kwao kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu." Vile vile, "… kuhusiana na utoaji wa maamuzi, viongozi wa umma watatekeleza wajibu wao kufuatana na sheria na kwa maslahi ya umma." Zaidi ya hayo, "… kuhusiana na maslahi binafsi, viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya." Mwisho, "… kuhusiana na maslahi ya umma, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, viongozi wa umma watapanga masuala yao kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma."

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ushahidi huu wa maandishi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mbunge yeyote wa chama chochote cha siasa chenye uwakilishi ndani ya Bunge lako tukufu, anayefuata imani yoyote ya dini aseme kama, kwa mujibu wa vifungu hivi vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mkurugenzi Mtendaji Mhando ana sifa za kuitwa kiongozi mwadilifu wa umma. Hivyo, pamoja na uchunguzi wa kawaida unaoendelea, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mkurugenzi wa Mashtaka aamuru hatua za uchunguzi wa kijinai zichukuliwe dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji Mhando kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Mheshimiwa Spika; hata hivyo hatua hizo dhidi ya Mkurugenzi wa TANESCO na watendaji waliohusika zisigeuzwe kuwa kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa Serikali kwa ujumla wake kwa kuwa taarifa za utendaji wa TANESCO kuhusu mpango wa dharura wa umeme pamoja na ununuzi wa mafuta uliokuwa ukifanyika zilikuwa zikiwasilishwa kwenye vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na hata vikao vya baraza la mawaziri. Hivyo, ili ukweli wa kina uweze kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme. Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (Sasa PUMA Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme. Izingatiwe kwamba masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila mtu "… kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu….".

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani tuliitaka Serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 itoe taarifa kuhusu utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) sanjari na kutoa ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mpango maalum wa kurekebisha hali ya kifedha ya shirika (2006-2010). Hata hivyo, katika mwaka husika wa fedha utendaji wa TANESCO na hali yake ya kifedha imeendelea kususua huku ukigubikwa na tuhuma za ubadhirifu na udhaifu wa kiutendaji hali ambayo imepelekea pia mkurugenzi mtendaji na maafisa wengine waandamizi kusimamishwa na kuchunguzwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba hali hii ni matokeo ya udhaifu katika uteuzi na usimamizi wa serikali kwa mashirika ya umma na inataka uwajibikaji kutokana na hali hiyo kudumu kwa muda mrefu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iwaeleze watanzania ni mikataba mingapi mibovu yenye kuipa mzigo mkubwa wa kifedha TANESCO na kuongeza gharama kwa wananchi imefanyiwa mapitio katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Takribani nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi sasa unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari wa biashara na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei. Hivyo, Watanzania hivi sasa wanabeba mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha kwa ujumla kutokana na ufisadi kwenye mikataba, ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na upungufu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya nishati.

Mheshimiwa Spika, mzigo huu usingekuwa mkubwa iwapo Serikali ingetekeleza katika mwaka wa fedha 2011/2012 maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya kuhakikisha nyongeza ya fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa upande wa sekta ndogo ya Gesi kwa ajili ya mitambo ya umeme na kuharakisha kuwekeza katika Bomba la Gesi pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant).

Kutokana na hatimaye Serikali kuzindua ujenzi wa Bomba la gesi katika mwaka wa fedha 2012/2013 na ahadi ya Wizara ya Nishati na Madini kuwa ujenzi huo utakamilika katika kipindi cha miezi kumi na nane ijayo, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali kutoa kauli ya uhakika kwa taifa; je, katika kipindi hiki cha mpito imeweka mikakati gani ya kuhakikisha mitambo ya kufua umeme iliyopo inayotumia gesi itapata gesi inayohitajika kuliondoa taifa katika upungufu wa umeme.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 tuliitaka Serikali iache kutoa kisingizio cha ‘ufinyu wa bajeti' katika kutekeleza maoni na mapendekezo ya kuongeza fedha za Miradi ya maendeleo ya sekta za nishati na madini na tulipendekeza vyanzo vya nyongeza vya mapato kwa ajili ya sekta tajwa ikiwemo: kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa Kampuni za Madini peke hatua ambayo ingeongeza mapato ya mapato ya shilingi bilioni 59; Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta ya madini kwa kurekebisha kodi sekta ya madini peke yake tungeweza kukusanya shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Kambi rasmi ya Upinzani inataka maelezo toka kwa Serikali ni kwa kiwango gani ushauri huo umezingatiwa.

Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 ulionyesha uwezo mdogo na kasi ndogo ya kufikisha umeme vijijini kwa upande wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Kasi ndogo ya kusambaza umeme ilielezwa pia mijini kutokana na idadi kubwa ya maombi ya wananchi wanaotaka kufungiwa umeme huku Shirika la Umeme (TANESCO) likiwajibu kuwa halina uwezo kwa sasa mpaka lipate miradi. Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka ufanyike ukaguzi wa kiufanisi kuhusu utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme; hivyo, serikali inapaswa kueleza iwapo ukaguzi husika ulifanyika na hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze katika mwaka wa fedha 2011/2012 imetekeleza kwa kiwango gani mkakati wa kupunguza gharama za manunuzi na pia kupunguza kiwango cha uagizaji wa nguzo na vifaa vingine kutoka nje ili kutumia rasilimali za ndani ili kuchangia katika kukuza uzalishaji na uchumi wetu. Izingatiwe kwamba malalamiko yameendelea kuhusu mazingira ya kupitishwa kwa zabuni za ununuzi wa nguzo, transforma na nyaya za umeme kwa kiwango kikubwa toka nje ya nchi huku viwanda vya ndani mathalani TANALEC ABB, East African Cables (hususani kampuni tanzu ya Tanzania Cables) na vingine vikididimia. Hali hii imesababisha pia kukwama kwa utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kusambaza umeme kutokana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni vifaa kutokupatikana kwa wakati toka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa na kasi ndogo ya serikali wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/212 kuhusu kupunguza gharama wanazotozwa wananchi za kuunganishiwa huduma ya umeme suala ambalo linapunguza kasi ya uunganishwaji wa umeme. Bado tumeendelea kupokea malalamiko toka kwa wananchi wanaotakiwa na TANESCO kulipia nguzo na gharama nyingine za kuunganishwa umeme kwa viwango ambavyo ni vigumu kwa wananchi wa kawaida kumudu. Hivyo, tunaitaka Serikali ieleze hatua za ziada inazokusudia kuchukua pamoja na kutekeleza maoni yetu ya kutaka TANESCO ibadili mfumo wa ankara ili kuruhusu kuingiza kwa mteja gharama hizo kidogo kidogo katika kipindi hiki cha mpito. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inawahimiza wananchi kutumia Kanuni za Sheria ya Umeme zilizotolewa kwenye gazeti la Serikali tarehe 4 Februari 2011 (GN 63) ambazo kifungu cha nne kinaeleza namna mteja atakavyofidiwa na kampuni ya usambazaji pale ambapo mteja anajigharamia mwenyewe kuvutiwa umeme ili fursa hiyo iweze kutumika ipasavyo; hata hivyo kanuni hizo zinahitaji pia kufanyiwa marekebisho kwa kuwa zimeweka mkazo katika fidia kutolewa kutokana na malipo ya wateja wengine badala ya mapato ya Shirika kwa ujumla wake.
 

Attachments

  • HOTUBA YA MSEMAJI NISHATI NA MADINI 2012 full final version.doc
    172 KB · Views: 368
Moderator nadhani ungekuwa unaleta zote na za wizara na za kamati za bunge kipindi hiki na uzi stick juu ili tuendelee na majadiliano yakinifu ya hotuba zote.
 
Hali ya hewa imebadilika bungeni Myika anamwaga data za ufisadi wa Mhando bungeni baada ya kuipa kampuni ya familia yake ya St. Clause tender ya ku-supply vifaa TANESCO. Hii ni aibu kwa wote wanaomtetea Mhando kuwa ni Mwadilifu na Myika ameshauri sheria ichukuwe mkondo wako. Makofi yatawala bungeni hivi sasa. Mkataba ulisainiwa kati ya Mhando na Mke wake.

Je wanao mtetea Mhando kuwa ni mtu safi wanalijua hili?
 
John Mnyika anatikisa bunge sasa hivi.Wabunge wa CCM wameshindwa kuvumilia wanamshangilia kwa nguvu sana.
Kaa huku ndo kuripoti, Naomba Mod wakushushe hadhi toka "JF Senior Expert Member" kwenda "Junior Member"
 
Unajua hao Magamba inafika wakati wakisikia ukweli unazungumzwa wao wenyewe wanaguswa lakini kutokana na shida ya kuchumia matumbo ndio hivyo wanafunika kombe mwanaharamu apite.....watu wa ajabu kabisa mambo yanaharibika lakini wako tayari kukaa kimya hata kama kufanya hivyo kutagharimu roho za watu...
 
Hakuombewa mwongozo na Wapuuzi?. Maana nukuu hii inaelekeaelekea kwenye kumdhalilisha DHAIFU, na WAPUUZI wake.
 
Kaa huku ndo kuripoti, Naomba Mod wakushushe hadhi toka "JF Senior Expert Member" kwenda "Junior Member"

Punguza munkari mkuu.Hotuba yote itawekwa muda mfupi ujao...
 
Wakuu, hii ni sehemu ya nukuu ya hotuba ya JJ Mnyika leo bungeni; Nitawawekea hapa chini mjionee namna ambavyo CCM inalea kansa inayozidi kulitafuna taifa. The state capture...institutionalized fraud. Ni uozo uozo mtupu.

"
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani tulitahadharisha kwamba mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta kwa ajili ya kufua umeme isitumike kama mwanya wa ufisadi na kuzalisha “Richmond nyigine”. Inaelekea kansa hii ndani ya Serikali inayoongozwa na CCM ya kuachia dharura ziendelee kwa manufaa ya wachache imesambaa kwa kiwango cha kuwa vigumu kutibika isipokuwa kwa mabadiliko ya mfumo mzima wa utawala," JJ Mnyika

Ukifuatilia kwa makini yanayoendelea katika ubadhirifu wa rasilimali zetu katika baadhi ya sekta, hasa nishati, madini, maliasili na utalii, utakubaliana na nukuu hii "Mabadiliko ya kweli katika taifa hayawezi kuletwa na watu wale wale, wa chama kile kile, wenye sera zile zile, wakiendeleza yale yale, ETI kwa ari zaidi, nguvu zaidi, na kasi zaidi! Kwa falsafa ya Chuku Chako Mapema, yaani CCM, Tanzania yenye neema haiwezekani (kwa kuwategemea hawa-mine)".


 
WanaJF
Mnyika anawasilisha maoni ya kambi rasm ya upinzan Nishati na Madini, kila Nutka yake anaendelea kuonyesha udhaifu wa Serikali na Bunge kudharauliwa na serikali,
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom