Maalim Seif Shariff na Vijana wa Tanzania Bara Uchaguzi Mkuu 1995 Sehemu ya Kwanza

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,261
MAALIM SEIF SHARIFF NA VIJANA WA TANZANIA BARA UCHAGUZI MKUU 1995 SEHEMU YA KWANZA

Miongo mitatu imepita, yaani miaka 30. Huwa napita Barabara ya Titi Mohamed nikitokea Mnazi Mmoja nakwenda nyumbani kwangu Magomeni Mapipa. Toka huko nilikotokea, jicho langu kila linapoangukia linatazama historia ya watu wa kawaida sana waliopigania uhuru wa Tanganyika.

Viwanja vya Mnazi Mmoja kila nikiviangalia vinanikumbusha mikutano ya kwanza ya TANU iliyokuwa ikihutubiwa na Rais wa TANU Mwalimu Julius Kambarage na Bibi Titi Mohamed. Ubongo wangu unatengeneza filamu. Naliona jukwaa la miti na viongozi wa TANU juu yake: Sheikh Suleiman Takadir, Rajab Diwani, Zuberi Mtemvu, Bibi Titi Mohamed, John Rupia, Julius Nyerere na Mama Maria. Filamu haijakamilika, nishafika Arnautoglo Hall. Hapa ndipo Julius Nyerere alipokabidhiwa uongozi wa TAA na kuwa Rais katika uchaguzi wa TAA wa mwaka 1953 alipomshinda Abdul Sykes. Naangalia kulia, Starlight Hotel. Ajabu ya Rahman. Filamu hii mbona imenigeukia mimi mwenyewe? Miaka 29 imepita, filamu inaendelea.

Nimeingia Barabara ya Morogoro na napita Mtaa wa Lumumba zamani New Street. Naiona Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM. Wazee wetu katika kiwanja hiki ambako leo limesimama jengo la fahari la CCM walijenga ofisi ya African Association kwa kujitolea, ujenzi ukifanyika kila Jumapili kati ya mwaka wa 1929 hadi 1933. Wakati ule New Street ilikuwa barabara ya vumbi. Katika waasisi hao wa African Association, Mzee Bin Sudi, Ramadhani Mashado Plantan, Schneider Abdillah Plantan, Thomas Saudtz Plantan, Ali Said Mpima kwa kuwataja wachache walishuhudia uhuru wa Tanganyika. Napita Viwanja vya Jangwani. Baada ya TANU kupata nguvu, Mnazi Mmoja ikawa hapatoshi, mikutano ya TANU ikahamia Jangwani. Katika uwanja huu wa Jangwani ndiko Bibi Titi alipompa Julius Nyerere lakabu ya "Mwalimu," jina lililomkaa hadi anaingia kaburini.

Naingia Mtaa wa Dosi naelekea nyumbani kwangu. Nauona Mtaa wa Jaribu ilipo nyumba ya Ali Msham. Hii ilikuwa ofisi ya TANU na Mama Maria Nyerere alikuwa na duka lake la mafuta ya taa pembeni, akishinda pale kutwa nzima huku anafuma sweta kuuza. Nyumba ya Ali Msham iko taaban. Imechoka na hakuna anaejua historia ya nyumba hii kuwa Mwalimu Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Zuberi Mtemvu na viongozi wengine wa TANU walikuwa hawapungui pale kuzungumza na wananchi.

Filamu ya historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika inavutia sana. Muongizaji filamu anarudisha kamera yake Starlight Hotel. Maalim Seif Mzanzibari kutoka Pemba anazungumza na watoto na wajukuu wa wazalendo waliopigania uhuru wa Tanganyika.


View: https://youtu.be/UYPiskVjJbg

Sehemu ya Pili soma Maalim Seif Shariff na Vijana wa Tanzania Bara Uchaguzi Mkuu 1995 Sehemu ya Pili
 
Back
Top Bottom