Heche: CCM kinaiua CHADEMA!

Heche: CCM kinaiua CHADEMA!

Salary Slip

Platinum Member
Joined
Apr 3, 2012
Posts
52,962
Reaction score
166,343
HALI ya kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inaonekana kuingia doa, baada ya kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare, anayetuhumiwa kupanga njama za utekeaji na kudhuru watu na uvunjifu wa amani.

MTANZANIA Jumatano limefanya mahojiano na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa chama hicho (BAVICHA), John Heche, ambaye pamoja na mambo mengine, anaeleza kuwa misukosuko inayokiandama sasa CHADEMA inapangwa na kutekelezwa na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotaka kife.

MTANZANIA JUMATANO: Kukamatwa kwa Lwakatare kunaonekana kuvuruga mambo ndani ya chama chenu, BAVICHA haina shaka mlikuwa mkifanya kazi kwa karibu zaidi na Lwakatare kwa sababu jukumu la ulinzi na usalama linawahusu, sakata hili mnalizungumziaje?

HECHE: CHADEMA ni chama kikuu cha upinzani na kinapendwa na Watanzania wengi kwa sasa, hivyo ni tishio kwa CCM. Kwa sababu hiyo, kila mara kimekuwa kikitishiwa na Serikali ya CCM, hilo liko wazi.

Kwa sababu hiyo, sisi CHADEMA tunaamini kabisa kuwa haya yaliyomkuta Lwakatare yametengenezwa, ni vitu vya uongo kuhusu Lwakatare. Mimi ninasema ukweli utajulikana taratibu, kiujumla hizi ni propaganda za kuchafua Chadema, ili kichukiwe na Watanzania, lakini nasisitiza mipango hiyo itashindwa.

Hivi, katika hali ya kawaida, unawezaje kumkamata mtu aliyerekodiwa bila kumtafuta aliyeweka ile video kwenye mitandao ya kijamii.

Sasa tutasemaje kuhusu gazeti la Mwanahalisi lililofungiwa baada ya kuwataja waliohusika kumteka na kumtesa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka. Wale waliotajwa na Gazeti la Mwanahalisi hawakuhojiwa na badala yake, gazeti lilifungiwa. Hii inaleta picha gani?

Majuzi, gazeti lenu lilimtaja Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, likimnukuu kuwa aliwahi kueleza kwenye televisheni kwamba anao maadui 11, wawili waandishi na akasema atakuja kuwashughulikia na hata kuwahamisha nchi, lakini hawajawahi kukamatwa na polisi wala kuhojiwa.

Lakini kwa Lwakatare, mara moja amekamatwa, tutasemaje katika hili. Hawa jamaa wanatumia kila aina ya mbinu kukichafua CHADEMA ili kichukiwe na Watanzania, lakini ipo siku najua ukweli utakuja kujulikana.

Ninawaomba Watanzania wasiamini mambo ya uongo kama hayo, waamini kuwa CHADEMA ni chama safi na hakiwezi kufa, japo maadui zetu wanatumia kila aina ya mbinu wanazozijua kutumaliza lakini mwisho watashindwa.

CHADEMA kinakichukulia CCM kuwa ni genge la watu wapiga kelele ambao wamejaa rushwa kwa kununua madaraka na propaganda chafu kama wanazofanya sasa.

MTANZANIA JUMATANO: Kuna tetesi kuwa utagombea ubunge wa Jimbo la Tarime katika uchaguzi mkuu ujao, tetesi hizi zina ukweli?

HECHE: Hizo siyo tetesi, bali ni ukweli. Nimekwishasema mara kadhaa kuwa nitagombea Tarime, hilo lieleweke hivyo.

Nimewahi kugombea mwaka 2008 katika uchaguzi mdogo ulioitishwa baada ya aliyekuwa Mbunge, Chacha Wangwe kufariki dunia. Na niligombea tena mwaka 2010, bahati mbaya nilishindwa nikashika nafasi ya tatu.

Sijakata tamaa, bado nia yangu iko pale pale ya kuwatumikia wananchi wa Tarime na nikipewa nafasi, nitaipeperusha vema bendera ya chama chetu.

MTANZANIA JUMATANO:
Ukifanikiwa kuwa Mbunge, nini matarajio yako.

HECHE: Tarime kuna matatizo mengi, kuna mauaji yanafanyika katika mgodi wa Nyamongo, wananchi wengi wamepoteza maisha huko, lakini sauti zao hazisikiki, Mbunge wao hajawahi kusema chochote bungeni kuhusiana na unyama huo.

Wananchi wa Tarime hawana msemaji bungeni, maendeleo yao yamedumaa, hawana mtu wa kumpelekea kilio chao ili sauti zao zisikike.

Sasa nikiwa Mbunge, ninatarajia kuwa mwakilishi wa kweli wa wana Tarime, nitalisimamia hili kadiri ya uwezo wangu na nitahakikisha haki ya wanyonge inapatikana pamoja na kuwaletea wananchi wangu maendeleo.

MTANZANIA JUMATANO:
Je, utagombea tena uenyekiti wa BAVICHA?

HECHE:
Hapana, sigombei tena, nina utaratibu wangu niliojiwekea ambao ni lazima niufuate. Kipindi changu kikiisha nitawaachia vijana wengine na wao wajaribu kuongoza baraza letu.

MTANZANIA JUMATANO: Nini matarajio ya CHADEMA katika uchaguzi mkuu ujao wa 2015.

HECHE: Matarajio yetu ni kushinda tu, hilo wala halina mjadala na ndiyo maana hivi sasa tumegawa kanda 10 kuanzia kusini, kaskazini, magharibi na mashariki.

Tumeamua kujigawa katika kanda hizi tukiwa na lengo la kuwahamisha wananchi na kuwaeleza sera zetu. Operesheni hizi zinaanzia katika ngazi za Kata, Wilaya hadi mikoa yote na zitaendelea hadi uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

MTANZANIA JUMATANO: Yapo madai yaliyokwishatolewa kuwa John Heche siyo jina lako, bali wewe unaitwa Wegesa Suguta, ukweli ni upi hapa?

HECHE: Mimi ni Mkurya. Wakurwa kawaida yetu tuna majina ya asili, jina la Wegesa ni la kwangu wala sijawahi kukataa, ni jina la ukoo na John ni jina langu la ubatizo, Suguta ni jina la babu yangu kwa hiyo hakuna kitu cha siri hapo.

Sioni kama kuna tatizo hapa kwa sababu sisi Waafrika, hatuna jina moja, hao wanaodhani kuwa Wegesa si jina langu wanaibua propaganda za kitoto. Ni watu waliochoka, waliokosa la kusema, nasisitiza hayo majina yote ni ya kwangu.

MTANZANIA JUMATANO:
Ipo minong'ono pia kuwa CHADEMA sasa kinaanza kupoteza mvuto wake wa kisiasa na mfano unaotolewa ni hivi karibuni ambapo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alipata watu wachache waliohudhuria kwenye mkutano wake uliofanyika Dar es Salaam. Jambo hili unalizungumziaje.

HECHE:
Unajua siasa zina ‘dynamic,' ina maana kwamba kushindana kwa sababu kuna hujuma nyingi zimekuwa zikifanyika, hasa wakati wa uchaguzi ukizingatia mfumo wa siasa za hapa nchini umewekwa na CCM.

MTANZANIA JUMATANO: Uliwahi kuwa diwani wa Tarime mjini baada ya kifo cha Chacha Wangwe, kwa nini hukugombea tena nafasi hiyo mwaka 2010?

HECHE: Niligombea lakini nikashindwa kwenye kura za maoni.

MTANZANIA JUMATANO:
Inadaiwa huna maelewano mazuri na Naibu Katibu Mkuu wa chama chenu, Zitto Kabwe, hili nalo likoje?

HECHE: Hizo porojo tu, wala hazina ukweli wowote. Sijawahi kukosana na Zitto na wala sitarajii kufanya hivyo, sisi sote ni chama kimoja, hivyo hakuna sababu ya kukosana kwa kuwa lengo letu ni kuwatumikia wananchi.

MTANZANIA JUMATANO:
CHADEMA kinaandamwa na mdudu wa kufukuzana, unadhani huo ni utaratibu mzuri wa demokrasia.

HECHE: Chama kina kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa na wanachama wote, hata enzi za Mwalimu Julius Nyerere, wakati CCM iko chini yake alikuwa na utaratibu kama huu.

Sisi siyo kama CCM ya hivi sasa, ambayo ni genge la wapiga kelele, tunaendesha chama kwa mujibu wa taratibu tulizojiwekea, sasa akitokea mtu anakiuka tu anaondolewa.

Sisi Chadema tunapoona mtu anavunja kanuni na taratibu zetu tunamuonya na kumchukulia hatua na pale tunapoona anaendelea kufanya hivyo tunamfukuza ndani ya chama kama tulivyokwishafanya kwa wengine.

MTANZANIA JUMATANO: Mahasimu wako kisiasa wanasema wewe unajipendekeza kwa viongozi wa juu wa chama na kwamba ni mmoja wa watu wanaokiharibu chama kwa ajili ya matakwa ya viongozi wa juu, unasema?

HECHE: Mimi ni kiongozi wa vijana wa chama na pia ni mjumbe wa kamati kuu na vikao vyote tunafanya kwa pamoja ndani ya kamati, sijawahi kufanya maamuzi yangu mwenyewe na siwezi kufanya hivyo hata siku moja.

Chama chetu ni taasisi kubwa na hakuna anayefanya jambo kwa mawazo yake mwenyewe, lazima tufuate taratibu zetu na kanuni, pia tumejiwekea misingi ya kujiongoza.

Hao wanaozusha hayo maneno lengo lao ni kunichafua ili nionekane sifai mbele ya jamii, ukweli ndiyo huo, sijawahi kufanya kitu kwa maamuzi yangu, lazima tukae kwenye kamati tujadiliane.

CHANZO
: MTANZANIA JUMATANO LA TAREHE 20/03/2013.
 
Mbona kichwa cha habari na habari yenyewe ni Mashariki na Magharibi?
 
Wanaodhani CHADEMA itakufa sijui nani kawaroga...wanazidi kuipa umaarufu CHADEMA na kwa nguvu wanachadema tuko nayo tutapigania chama chetu hadi wanafki na maadui zetu waaibike.
 
CHADEMA haitakiwi kufa. Inachotakiwa ni kutambua kuwa haiko tayari kuongoza nchi na kwamba jukumu lake pekee ni kuikumbusha CCM isijisahau...
 
Mbona kichwa cha habari na habari yenyewe ni Mashariki na Magharibi?

Mkuu ni kweli lakini mimi nilichofanya ni ku-copy na ku-paste heading kama ilivyo katika gazeti lenyewe.

Nimalizie kwa kusema "mjumbe hauwawi"
 
Chadema haitakiwi kufa.
Inachotakiwa ni kutambua kuwa haiko tayari kuongoza nchi na kwamba
jukumu lake pekee ni kuikumbusha CCM isijisahau...

hapa hujafikiria mkuu, na kwa mawazo yako, m4c inabidi ikeshe usiku kucha kuelimisha watz wanaofikiri kama wewe
 
Hapa kila chama kinajaribu kukiua chama kingine kisiasa.Kinachoniudhi ni njia wanazotumia kupambana ambazo pia zinagharimu maisha ya watu. Mwananchi mwenye akili anauelewa vizuri mchezo huu
Mie nadhani CHADEMA ndio inaiua CCM!
 
Hapa kila chama kinajaribu kukiua chama kingine kisiasa.Kinachoniudhi ni njia wanazotumia kupambana ambazo pia zinagharimu maisha ya watu. Mwananchi mwenye akili anauelewa vizuri mchezo huu

CCM kilikuwa hai kinachopendwa mno na watu!! Lkn sasa kinachukiwa mno na wengi tu...
CHADEMA haikuwepo kabisa wakati CCM iko hai na inapendwa, imekua inazidi kupendwa na kuaminiwa na watanzania wengi tu....mbinu inayotumiwa na CCM ya Kui 'Jasusi' haikubaliki na watashindwa tu.....na walaaniwe!
 
Hivi tafsiri ya SIASA tanzania ni migogoro tuu ?? sio kuzungumzia ustawi wa jamii, sera na maendeleo?
 
Daaah jama anajua kujibu maswali vyema! Safi sana heche!
 
Back
Top Bottom