Sosoma Jr
JF-Expert Member
- Aug 7, 2020
- 312
- 281
HATUA ZA KUACHA KUVUTA SIGARA
Madhara ya kiafya yatokanayo na uvutaji sigara ni makubwa na yanahatarisha si tu uhai wa mvutaji bali hata na watu wengine wanaovuta moshi kutoka kwa mvutaji. Kwa upande mwingine, hakuna faida yoyote anayopata mvutaji, hivyo wavutaji wa sigara wanashauriwa waache uvutaji.
Zifuatazo ni hatua saba zilizothibitishwa zinazoweza kukusaidia kuacha uvutaji wa sigara.
1. ELEWA KWAMBA KUVUTA SIGARA NI DHAMBI DHIDI YA MWILI WAKO NA MUNGU WAKO
Zaidi ya kuharibu afya ya kimwili, sigara pia huharibu afya ya kiroho ya mvutaji. Biblia inautaja mwili wa mwanadamu kuwa ni hekalu la kiroho ambamo Mungu Roho Mtakatifu anaishi, soma katika 1 Wakorintho 6:19-20 na Warumi 12:1. Uvutaji wa sigara huharibu hekalu hilo. Roho Mtakatifu hawezi kuishi katika hekalu lililoharibika. Kwa sababu hiyo, Mungu anatuonya dhidi ya kuharibu hekalu lake. Ukijua kuwa kuvuta sigara ni dhambi, utaamua kuacha.
2. KIRI KWAMBA WEWE NI MDHAIFU NA HUWEZI KUACHA MWENYEWE
Inawezekana umehangaika sana ukijaribu kuacha kuvuta sigara. Inawezekana umetafuta msaada kwa miaka mingi kama yule mgonjwa aliyekuwa ameugua kwa muda wa miaka 38 (soma Yohana 5:5-8). Ili uweze kushinda tabia hii, kubali kwamba wewe ni dhaifu. Kiri kwamba huwezi kufanikiwa wewe mwenyewe. "Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote." (Yohana 15:5). Kwa kukiri hivi utajikabidhi mikononi mwa Mungu Akusaidie.
3. AMINI KWAMBA JAPOKUWA WEWE NI MDHAIFU, MUNGU ANA NGUVU JAPOKUWA HUWEZI, YEYE ANA UWEZA WOTE
Tunapoamua kuweka makusudi yetu dhaifu yenye kusitasita chini ya makusudi ya Mungu, uweza wote uliomo ulimwenguni utakuwa wetu. Tukimwomba Mungu atatuwezesha kushinda tusiyoyaweza. "Nayaweza yote katika Yeye anitiaye nguvu" (Wafilipi 4:13).
4. JITOE KWA MUNGU
Ili Mungu aweze kukupa ushindi dhidi ya tabia hii ya uvutaji ni lazima ujitoe kikamilifu kwake. Mungu hawezi kukupa ushindi bila wewe kukubali kushirikiana naye. Soma 2 Wakorintho 6:2. "Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure."
5. AMINI KWAMBA SASA USHINDI NI WAKO KISHA MSHUKURU MUNGU
Baada ya kukubali na kujisalimisha kwa Mungu sasa umeshinda na umshukuru Mungu kwa kukupatia ushindi dhidi ya kuvuta sigara. "Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo." (1 Wakorintho 15:57).
6. HARIBU SIGARA ZOTE
Ili usipate tena ushawishi wa kuvuta sigara inabidi ukae mbali na sigara. Kama ulikuwa na sigara nyumbani kwako amua kuzitupa au kuziharibu zote na usibakize hata moja mahali ulipo. Jitoe kwa Mungu na umpinge shetani. "Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili." (Yakobo 4:7-8).
7. FUATA KANUNI ZIFUATAZO ZITAKUSAIDIA
Hata baada ya kuacha kuvuta sigara, bado kuna wakati utakuwa unajisikia hamu ya kuvuta. Zaidi ya kufuata hatua zilizotajwa hapo juu, unaweza kuchukua hatua zingine kwa ajili ya kukusaidia kuepukana na majaribu ya kuvuta sigara. Ili kuondoa hamu ya kuvuta sigara, fanya yafuatayo:
- Unapokuwa na hamu ya kuvuta sigara, vuta pumzi taratibu kwa kina hadi hamu itakapokwisha.
- Kunywa bilauri (glasi) 10 hadi 12 za maji kila siku kwa siku tano mfululizo.
- Pumzika kwenye maji ya uvuguvugu katika bafu kabla ya kulala.
- Panga kulala saa zisizopungua nane kila siku.
- Epuka kutumia kinywaji cha kahawa au pombe.
- Fanya mazoezi ya kutembea kwa dakika zisizopungua 30 mara mbili kwa siku.
- Endelea kumsifu Mungu kwamba uweza wake ni mkubwa.
Ewe ndugu yangu mpendwa tafuta kanisa la Waadventista wa Sabato linaloabudu siku ya jumamosi na ibada inaanza saa tatu asubuhi mpaka saa sita mchana hudhulia hapo hutajuta kamwe kwa mafunzo utakayoyapata ya kiroho na kimwili. Barikiweni nyote.