KWELI Uvutaji wa Sigara huchangia ugumba kwa wanaume

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
Source #1
View Source #1
istockphoto-1218068130-612x612.jpg
Matumizi ya tumbaku ni moja ya maafa ya afya ya umma yanayojulikana sana. Licha ya ripoti nyingi kuhusu afya ya umma, matumizi ya tumbaku yanazidi kuongezeka katika nchi zinazoendelea na zilizoendelea.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takriban watu Bilioni 1.3 duniani wanavuta sigara ambapo 80% kati yake wanatoka kwenye nchi zenye uchumi mdogo na uchumi wa kati. Aidha, takriban watu Milioni 7 hupoteza maisha kutokana na athari za moshi wa sigara unaotokana na kuvuta sigara moja kwa moja au pia kuvuta moshi uliotolewa na mvutaji wa Sigara.

Tumbaku huathiri karibu kila kiungo na mfumo katika mwili, ikisababisha matatizo mbalimbali kama vile saratani, Magonjwa ya mfumo wa upumuaji, Ugonjwa wa Mishipa ya Moyo, Kiharusi, kuharibika kwa Meno pamoja na kudhoofika kwa afya ya mifupa.

Swali la Mdau wa JamiiCheck
Moja ya eneo linalozidi kuwa na wasiwasi ni athari ya matumizi ya tumbaku kwenye afya ya uzazi, hali iliyomfanya mdau wa JamiiCheck Stormryder , Machi 11, 2024, ahoji kama uvutaji wa bidhaa hii unaweza kusababisha ugumba kwa wanaume.

JamiiCheck imepata ufafanuzi wa swali hili kutoka kwa Afisa Usajili wa Dawa, Denis Mwangomo wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) aliyebainisha mambo haya;

Uvuta sigara umehusishwa na athari mbaya kwa ubora wa manii na vigezo vya manii. Utafiti umeonesha kuwa wanaovuta sigara wana viwango vya chini vya manii, majibu madogo ya manii, na viwango vya juu vya uharibifu wa DNA ya manii ikilinganishwa na wasiovuta.

Pia, Moshi wa tumbaku huwa na kemikali zinazovuruga utendaji wa homoni, husababisha mvurugiko wa homoni zinazohusika na uzazi wa mwanaume. Kuvuta sigara kumehusishwa na kupungua kwa viwango vya testosterone, viwango vya juu vya estradioli, na mabadiliko katika homoni zingine za uzazi, ambazo zinaweza kuharibu utengenezaji wa manii na uzazi kwa ujumla.

Aidha, Matumizi ya tumbaku ni sababu kubwa inayopelekea kutokea kwa tatizo la Upungufu wa nguvu za kiume (ED) kutokana na athari yake mbaya kwa afya ya mishipa ya damu. Kuvuta sigara kwa muda mrefu huchangia kuziba kwa mishipa ya damu hivyo kupelekea kupungua kwa mtiririko wa damu kwenye uume hivyo kupunguza (kudhoofisha) ufanisi wa kushiriki tendo la ndoa.

Mwangomo ameelezea pia uhusiano wa uvutaji wa Sigara na Kusababisha Ugumba wa wanaume. Amesema tafiti kadhaa zimeonesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya matumizi ya tumbaku na ugumba kwa wanaume. Wanaume wanaovutaji sigara wana uwezekano mkubwa wa kupata shida katika kutungisha mimba, na viwango vya chini vya uzazi huonekana zaidi miongoni mwa wanaume wanaovuta mara kwa mara.

Mbali na ufafanuzi wa Mwangomo, utafiti huu, huu, huu na huu unaweka bayana pia athari za Uvutaji wa Sigara kwenye afya ya uzazi wa mwanaume.

Hivyo, JamiiCheck inahitimisha swali la Mdau kwa kuweka mkazo kuwa Uvuaji wa Sigara unaweza kusababisha Ugumba.

CC: stormryder
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom