Hatimaye nipo huru

JBourne59

JF-Expert Member
Joined
Jan 17, 2020
Posts
952
Reaction score
8,804
Hii ni simulizi ya yaliyomtokea mtoto wa marehemu rafiki yangu Mwinyi Mkila wa Bagamoyo.
***********

1. ALFA

Nilifahamiana na Mwinyi Mkila katika harakati za kutafuta shamba Bagamoyo na hatimaye kwa msaada wake nilipata shamba kubwa eneo la Sanzale miaka hiyo ya 1980's.

Mwinyi Mkila alikuwa na watoto kadhaa na mmoja wa watoto hao anaitwa Pazi. Kijana Pazi ndiye mzuwanda kwa Mwinyi Mkila kwa bi mdogo maana Mwinyi Mkila alikuwa na wake wawili.

Mwinyi Mkila mpaka mauti yanamkuta alikuwa akijishughulisha na shughuli za uvuvi na uchuuzi
wa mazao ya baharini. Alikuwa na Jahazi, Mashua, Dau, Ngalawa na Mitumbwi ambayo alikuwa akiwapa
wavuvi kwa mikataba maalumu ya kufanya nao kazi na kumuuzia kitakacho patikana.

Mazao hayo ya baharini hususani samaki yalikuwa yakipelekwa Dar es Salaam kwa ajili ya kuuzwa. Sasa huyu kijana Pazi ndiye aliyekuwa akisimamia zoezi zima la uuzwaji samaki hao na mazao mengine ya baharini katika soko la Feri (Dsm)

Miaka ya 1990's nilipokutana naye Feri wakati nimeenda kununua kitoweo, Pazi alikuwa hayupo kama kawaida, alikuwa amekonda na macho yamekuwa angavu zaidi na kama anatumia nguvu nyingi hivi
ili kuangalia.

Nilipo mjulia hali zaidi ndipo akaniambia kuwa amepata na maradhi yasiyo julikana na akasema kuwa hali yake kila siku inazidi kudhoofu.

Familia ya Mwinyi Mkila haikuwa na shida ndogo ndogo za kiuchumi kwani baba yao alikuwa mkwasi
na maarufu sana Bagamoyo na ukanda wa Pwani kwa ujumla na watoto wake karibuni wote wa kiume
walirithi kazi ya baba yao.

Bada ya mazungumzo ya muda mrefu na Pazi tukaagana na kila mmoja akaendelea na shughuli zake.
***********

Miaka kumi na moja hivi baadaye nilikutana tena na Pazi lakini katika hali tofauti sana na akiwa na afya njema na akaniomba nikapajuwe nyumbani kwake alipojenga sasa hivi.

Tulikutana na Pazi Long-room TRA mkabala na kituo cha mabasi Stesheni - Dar es Salaam siku ya Ijumaa. Akaomba niongozane naye hadi kwake 'Mbezi beach'. Kwa kuwa nilikuwa tayari nimeshamaliza shughuli zangu nilizojipangia kwa siku hiyo, nilikubali kuongozana naye na tukafika kwake eneo la Mbezi Juu kama unataka kwenda Salasala.

Baada ya mazungumzo ya awali ndipo akaanza kunihadithia.


"Baba, hujafa hujaumbika!" alisema Pazi.

"Enhe!?", niliitikia kwa shauku ya kutaka kujuwa zaidi na zaidi.

Pazi alianza kunisimulia:-
***********

Tangia nasoma shule ya Msingi Kizuiani Bagamoyo, nimekuwa nikimsaidia Baba kazi zake za uvuvi. Japo wakati huo nilikuwa siendi baharini kuvua, lakini vyombo (mashua nk) vinaporudi huwa nakuwa pwani ufukweni nikisimamia yale niliyopangiwa na wakubwa wangu.

Jahazi letu kazi yake kubwa ilikuwa ni kusafirisha mizigo kutoka huku Bagamoyo kwenda Unguja na mizigo ya Unguja kuileta Bagamoyo. Mashua ilikuwa kwa ajili ya kazi za uvuvi maalum ambapo chombo hukabidhiwa nahodha, yeye ndiye anakuwa na jukumu la kuwatafuta wavuvi atakao shirikiana nao katika zoezi zima la uvuvi. Dau mara zote tumekuwa tukiwakodisha 'Wakojani' kwa ajili ya shughuli zao za uvuvi wa 'juya' kisha wao huwa huru kuuza mavuno popote lakini hukilipia chombo kwa fedha taslimu kila siku warudipo kuvua kwa kadri tulivyo kubalina. Ngalawa na mitumbwi pia huwa wanalipa kwa fedha taslimu na wapo huru kuuza sehemu yoyote ingawaje mara nyingi huja kutuuzia sisi wenyewe.

Jahazi, Dau, Ngalawa wanatumia 'tanga', lakini mtumbwi wanatumia 'makasia' peke yake na kwenye Mashua wanatumia tanga pamoja na injini.

Baada ya kumaliza darasa la saba wavuvi wa mashua walipanga kwenda 'dago' maeneo ya Sadani na Mkwaja kwa ajili ya zoezi la kuvua 'kamba' na 'kaji' (prawns), na Kamba koche (robuster), niliamua kuongozana nao kwa kuwa sasa nilikuwa huru zaidi kuliko wakati nikisoma.

Tulijiandaa vyema kwa ajili ya safari hiyo ya kwenda kupiga kambi (dago) kwa kubeba unga wa ugali, mafuta kidogo ya kupikia na vifaa vya uvuvi kama vile nyavu maalumu kwa ajili ya kuvulia kamba na kaji, Petroli ya kutosha, tofali za barafu za kutosha na vifaa vingine.

Siku ya safari tulisubiri maji yajae kusogea ufukweni ili chombo kiweze kuelea kwa sababu 'yalikupwa'. Muda wa kuanza safari ulipowadia nahodha aliamrisha baharia mmoja ashike 'upondo' na kuanza kukitembeza chombo huku baharia mwingine akivuta kamba ya nanga kurahisisha uelekeo wa kuielekea nanga ili ipandishwe na safari ianze.

Nahodha aliwasha mashine Yamaha Enduro supa 40 (horse power 40), nanga ikang’olewa (ikaingizwa kwenye mashua) na safari ikaanza mdogo mdogo. 'Hatukutweka tanga' kwa kuwa hali ya bahari ilikuwa shwari hivyo hakukuwa na upepo wa kutosha kuiendesha mashua kwa kasi.

Ilikuwa mida ya alasiri ndipo tuling'oa nanga kuelekea dagoni, na tulifika Mkwaja usiku mwingi na nahodha aliamuru nanga ishushwe 'nje kidogo' kwenye maji mengi kabla ya kufika ufukweni ili tupate kulala kabla hapajakucha tukiwa ndani ya mashua.

Palivyokucha tulisogeza chombo ufukweni, tukashusha mizigo yetu na kuanza kuandaa kambi. Siku nzima siku hiyo ilikuwa ni kujenga vibanda. tulijenga vibanda vitatu ambapo banda kuu lilikuwa la nadhodha na wasaidizi wake wawili, na mizigo yote ilikuwa hapo, mabanda mawili yaliyobaki yalikuwa ya wavuvi ambapo wanne walikaa kwenye kila banda. Mabanda haya ni yale ya kusimikwa kwa miti na kuezekwa kwa makuti juu ambapo msuko wa aina ya 'kumba' na 'pande' ilitumika na pembeni kulizibwa vivyo hivyo kwa makuti ili kukabiliana na upepo kutoka baharini hususani nyakati za usiku.

Kwa kuwa nilikuwa kijana mdogo tena mfupi, sikuruhusiwa kuingia baharini kwa ajili ya kuvua, bali niliachwa kambini pamoja na msaidizi wa nahodha kama walinzi mashahidi wa kambi. siku ya kwanza hadi ya tatu zoezi liliendelea vizuri, na tulifanikiwa kupata kaji wengi sana pamoja na kamba wachache.
Wavuvi wenyewe hujuwa ni wakati gani na sehemu gani waende kuvua. kamba na kaji huvuliwa kwa nyavu moja kushikwa na wavuvi wawili mmoja huku na mwingine kule kisha wakianzia maji mengi na kutembea taratibu kuja maji machache na hatimaye kuwanasa kamba na kaji na mazao mengine ya baharini yaliyonasa kwenye nyavu kisha huja kando kando ya bahari na kuanza kuchambua, kamba na kaji huhifadhiwa kwenye tenga, samaki wengine waliwao huwekwa kwa ajili ya kitoweo na baadhi
ya viumbe wengine wa bahari hurudishwa baharini ama kuachwa tu wakizagaa.

Siku ya nne nilibaki peke yangu kambini na ndiyo nadhani ikawa ni sababu ya maradhi yangu yaliyonisumbua kwa muda mrefu sana.

Kambini kwetu asubuhi wavuvi hunywa supu ya samaki tu na kujiandaa na kazi kwa kuangalia mwenendo wa maji. baada la zoezi la uvuvi asubuhi, wakirudi hupikiwa ugali kwa samaki kisha kusubiri zoezi lingine kulingana na mwendendo wa maji, hivyo kwa siku
huwa kuna mazoezi mawili makuu ya kuvua kamba na kaji.

Sasa siku hiyo mida yao kurudi ili wapate chakula cha mchana ilikuwa majira ya saa sita hivi, hivyo nami katika harakati za kumsaidia mpishi wa zamu (msaidizi wa nahodha) kuwasha moto, nikapatwa na gumbizi (kuzunguzungu) na kuanguka chini. Sikuelewa kilichondelea hadi baadaye nilipopata fahamu nikawaona wavuvi wote wamenizunguka huku nahodha akiniuliza ninajisiaje sasa.

"Najisikia vizuri ila nahisi uchovu tu, kwani kimetokea nini?" nilijibu na kuuliza.

Nahodha akaniambia kuwa nilianguka na kusogezwa kibandani na msaidizi wake na nikawa kama nimezimia na kupoteza fahamu, wao waliitwa kuja kunisaidia haraka kwa kunipepea na kunimwagia maji ndipo nikazinduka.

Nikapewa supu ya Samaki aina ya 'Songolo' nikanywa nikapata nguvu kidogo na ugali ukasongwa
wengine wote walikula lakini mimi nilitosheka na supu ya samaki sikujisikia kula tena. Zoezi la jioni walibaki watu watatu pale kambini pamoja nami, yaani nahodha na wasaidizi wake wawili, wavuvi wengine waliendelea kuvua.

Kwakuwa ilikuwa msimu wa 'bamvua' lenye samaki wengi, haikutuchukua zaidi ya siku kumi kujaza
vyombo vyetu vyote samaki aina ya kamba na kaji. Lilifanyika zoezi la ziada kwa ajili ya uvuvi wa maji mengi ili kupata samaki wakubwa kwa njia ya 'mishipi', basi wiki hiyo iliyofuata tulitumia usiku wa kiza kwenda kuvua Jodari, Sehewa, Papa, Chewa na Nguru. Kambini tulikuwa tunawaacha wavuvi wanne wakilinda samaki na kambi kwa ujumla, mimi hawakutaka kuniacha kwa kuhofia nisije nikaanguka tena wao wakiwa mbali.

Zoezi hili la usiku nilikuwa nikilifurahia kwa kuwa hatuingii ndani ya maji, bali tunawasha tu 'karabai' na kuweka chambo kwenye ndoano na kuanza kuvua huku 'mishoto' ikiwa jirani kwa ajili ya 'kuwatuliza' samaki wasumbufu kabla ya kumtoa kwenye ndoano.

Tulipata Jodari wachache, sehewa wengi, nguru wachache, papa mmoja na chewa mkubwa mmoja kwa zoezi zima la wiki hiyo. Chakula Unga kutoka mjini Bagamoyo tulichukuwa wa kutosha wiki nne, lakini Nahodha aliamuru turudi mjini baada ya wiki tatu na nusu kwa kuwa tulishapata mavuno ya kutosha.
***********

Safari ya kurudi ilianza, lakini kwa upande wangu niliona vituko njiani kadha wa kadha, tulianza safari
jioni sana ili tutembee usiku kucha na asubuhi tuwe tumefika. Ilikuwa ni kawaida ya vyombo vyetu kuja 'kutua' maeneo ya pwani ya msikiti wa Ijumaa Bagamoyo "nchi pana", (siku hizi wanapaita kwa Zakaria / Alfazul).

Kituko cha kwanza ni kuona moto mwekundu ukiwaka baharini pasipo na chombo chochote,
awali nilidhani ni wavuvi wenzetu wakivua lakini nilipo muuliza nahoda alinijibu kuwa hapana,
siyo wavuvi, wale ni "vibwengo"

'Wakati nasoma kizuiani, nimesikia simulizi nyingi za vibwengo, leo hatimaye naaza kushuhudia
mubashara', nilijisemea.

Vimbwengo kwa simulizi ni aina fulani ya viumbe ambavyo aghalabu hupatikana maeneo yenye maji mengi mfano wa mabwawa makubwa, mito, maziwa, bahari. Viumbe hivi husemekana vina uwezo wa kujibadilisha muonekano wao, na wakiwa katika umbo la mfano wa mwanadamu basi huwa wafupi. wana uwezo wa kuonekana na kupotea kwa ghafla. hupenda kuwatisha binadamu lakini inasemekana hawana madhara makubwa kwa binadamu.

Inasemekana pia ni aina fulani ya kabila moja ya jamii (specie) ya majini. Sasa ile mioto ilikuwa inaonekana na tunapoikaribia inapotea na kuonekana umbali mwingine.
************

Inaendelea...
 
2. MALARIA NA TIBA

Tulivyo anza kuona nchi kavu kwa mbali, nahodha aliamuru kibendera kipandishwe ili iwe kama ishara ya maandalizi makubwa yanahitajika, wakati huo hatukuwa na simu, 'rediokol' wala vifaa vya kutuongoza zaidi ya ujuzi wa nahodha na mabaharia wengine kwa kutumia elimu ya nyota angani na uzoefu maeneo na miamba bahari.

Tulifika majira ya saa moja hivi asubuhi, maana muda mwingi tulitumia upepo kama nishati ya kutusafirisha kwa sehemu kubwa ya bahari tukiweka akiba petroli kwa dharura.

Mwinyi Mkila akiwa na wafanyakazi wake wengine walikuja kutupokea, wakiwemo 'bwana samaki' (afisa wa Serikali anayehusika na mali bahari), watu wengine wengi wakiwemo watoto wa rika tofauti maana ilikuwa ni siku ya Jumamosi.

Kwa mazingira ya pwani, ni kawaida ya watu kujaa wakati chombo kikiingia kutoka uvuvini, wengine kutafuta kitoweo, wengine kuchuuza na wengine kuburudisha macho tu.

Kwakuwa uvuvi ule ulikuwa ni maalumu, watu wa nje wigo wa Mwinyi Mkila walibaki kushuhudia tu kilichoendelea.

Kamba na kaji walipimwa kwenye mizani ili kupata idadi ya kilo zilizopatikana. Kaji huhifadhiwa peke yake na kamba peke yake kwenye matenga makubwa ambapo nyumbani tena hufungwa upya na kuwekewa barafu mpya tayari kwa safari ya kwenda Dar es Salaam alfajiri kwa kutumia mabasi ya SIKINDE na CHAMPSI MULJI.

Wale samaki wengine pia Mwinyi Mkila alipatana na wavuvi na kujuwa bei.

Baadhi ya wachuuzi waliomba wauziwe wale Jodari na Sehewa kwa ajili ya vitoweo, na ilifanyika hivyo.

Injini ilibebwa kwa toroli kurudishwa nyumbani, matenga ya samaki nayo vivyo hivyo. Mashua alikabidhiwa kijana mwingine ambaye hakwenda dagoni kwa ajili ya ukaguzi na kuiweka sehemu salama.

Wavuvi wote pamoja nami tulifika nyumbani salama na zoezi la kupewa ujira likaendelea.

Baada ya hilo zoezi wavuvi wote wakiwa na tabasamu walielekea kupumzika majumbani kwao, mimi nikabaki na baba huku akinidadisi uzoefu nilioupata huko dagoni.
****

Siku ilienda vyema na muda mwingi niliutumia kupumzika, lakini jua lilivyoanza kuzama tu nikaanza kusikia (kuhisi) baridi isiyo ya kawaida. Nilihisi homa maana tulivyokuwa dagoni tuliumwa na mbu pamoja na usubi ingawaje nyavu (mosquito net) za kuzuia mbu tulikuwa nazo.

Nilipewa panadol ili kujaribu kutuliza homa lakini kadri muda ukivyokuwa unakwenda ndivyo homa ikawa inazidi.

Baba aliamuru kaka yangu mkubwa anipeleke hospitali, hapakuwa mbali sana maana ni mwendo wa kutembea kiasi cha robo saa tu.

Nilifika hospitali giza likiwa limeshaingia nikiwa natetemeka sana, nikapelekwa kuonana na daktari wa zamu, akaniandikia kwenda kupima damu kwa ajili ya malaria na homa ya matumbo.
*****

Nilipata matibabu sawia na vipimo vilivyoonesha, sikuwa na malaira kali, ilionekana kwa mbaali tu (scanty) na sikuwa na homa ya matumbo wala maradhi mengine kwa mujibu wa vipimo.

Nilipewa dawa za kushusha homa pamoja na kuanzishiwa dozi ya klorokwini (chloroquine) kwa ajili ya kutibu malaria iliyoonekana kidogo.

Baada ya siku 3 nilipata nafuu kiasi, bahati nzuri sikuwa mvivu wa kumeza dawa, hata hizo klorokwini nilizimeza kwa kuweka kidonge kwenye ndizi mbivu ndogo na kupita kooni bila tabu hadi nilipo maliza dozi ya 4-4-2. Wakati mwingine pia nilitumia tonge la ugali kuweka dawa na kumeza.

Siku ya nne nikazidiwa tena, safari hii sikuwa na homa bali nilikuwa napata gumbizi mara kwa mara. Nikapelekwa tena hospitali na kupimwa wingi wa damu lakini nilikuwa na damu ya kutosha (13 na) hivyo daktari alishauri nipelekwe Muhimbili kwa ajili ya vipimo vya magonjwa ya moyo.
*****

Muhimbili walianza upya kunipima vipimo vyote muhimu lakini hawakuona ugonjwa wowote wa kuweza kunipa kuzunguzungu ninachojisikia.

Ikashauriwa nipimwe kipimo cha mionzi kwenye kichwa ili kuangalia kama kuna tofauti yoyote humo.

Vipimo vyote vilionesha nipo kawaida, lakini wakaamua kunitoa damu na kuipeleka maabara kwa ajili ya uchunguzi zaidi nikaambiwa majibu yatapatikana baada ya siku thelathini.
***

Ndani ya siku 30 za kusubiri majibu kutoka maabara nilikuwa napitia nyakati ngumu na za ajabu ajabu mara kizunguzungu, mara homa lakini havidumu sana kwa maana inakuwa kama homa ya vipindi.

Majibu yalikuja kuwa sina tatizo lolote, na ndipo daktari mmoja wakati wa 'clinic' akatushauri tujaribu dawa za mitishamba.

"Jaribuni kienyeji inawezekana huu siyo ugonjwa wa hospitalini" alisikika yule daktari mtu mzima hivi.

Pilika zikaanza sasa, baada ya kikao vya kifamilia Bagamoyo.

Katika kile kikao ndio nikaelezea kuwa wakati nipo dagoni nilipatwa na gumbizi na kuanguka na kupoteza fahamu.

Ikaamuliwa tuende kwa Zahiri aliyekuwa akiishi Mangesani.

Baada ya kuelezewa hali ilivyonitokea, atatuambia tuende siku ya alhamisi ambapo pia kuna wagonjwa wengine wengi watakuja siku hiyo ili kufanya tiba ya pamoja.

Zahiri (R.I.P) ni tabibu aliyekuwa akitibu maradhi yahusianayo na 'mashetani' ya kijini.

(Alikuwa maarufu sana Bagamoyo na alikuwa shabiki (mwanachama) wa Simba sports club. Mara nyingi Simba wakienda Bagamoyo lazima wafike kwake).

Siku ya alhamisi ilipowadia nilienda kwa Zahiri nikisindikizwa na kaka yangu mkubwa, wagonjwa tukatengwa peke yetu eneo la uani (kwenye uzio wa nyumba) uliozungushiwa kwa makuti, na wasindikizaji waliamriwa wakae pembeni lakini ndani ya uzio huo huo.

Maandalizi ya utabibu yakawa tayari nikaona vigoma (vyapuo) vikipigwa kwa mdundo wa aina yake mara wagonjwa ambao wengi wao walikuwa akina mama walianza kutikisa vichwa, mie nilikuwa dhahiri bila kupata athari za midundo hiyo.

Hali ya ngoma na kucheza iliendelea hadi wengine walianza kugalagala na wengine kuanza kuzungumza maneno yasiyoeleweka, kiarabu si kiarabu, kihindi si kihindi ilimradi vurugu ya mchanganyiko wa lugha, mie nikishuhudia yoye kwa macho.

Nashangaa siku hiyo sikupatwa na homa wa gumbizi badala yake nilikuwa nipo kawaida tu nikishuhudia yote yaliyokuwa yakiendelea.

Baada ya muda fulani kupita, Zahiri alimfuata mgojwa mmoja mmoja na kumshika sikio na kuzungumza sikioni mwa mgonjwa huyo kwa kiswahili na kiarabu.

Wagonjwa wengine walijibu, wengine walipiga kelele tu, wengine walikaa kimya, na alipofika kwangu akanishika sikio nikasisimka lakini nikarudi kawaida.

Alizungumza maneno mengi ya kiarabu na kiswahili lakini mie nilikuwa namuangalia tu.

Mwishowe akamuambia kaka kuwa turudi jumamosi kwa ajili ya tiba zaidi.

Hatukupewa dawa yoyote wala kuombwa pesa.
****

Jumamosi tulifika pale wagonjwa wachache maana wengi siku ya alhamisi walipatiwa dawa za kutumia.

Tukakuta kumeandaliwa sinia zenye vyakula vitamu vitamu vya aina mbalimbali ikiwemo tende, halua, peremende, ndizi mbivu (kisukari), sharubati nk.

"Leo ni siku ya 'chanu' maalum" alisema tabibu Zahiri.

Akashika kitabu na kusoma meneno ambayo sikuyaelewa na vigoma vidogo viaanza kupigwa huku yeye akiendelea kusoma maeno katika lugha isiyokuwa kiswahili wa kiarabu.

Wale wagonjwa wengine mara nikaona wanajongea kwa mitindo tofauti kwenye sinia za vyakula na kuanza kula, lakini mimi nilikuwa nimekaa tu kwenye jamvi pale chini huku nikiziangalia zile ndizi maana napendaGa sana ndizi.

Hali ile iliendelea na mara wale wagonjwa wakawa kawaida, wakapewa dawa zao za kutumia majumbani mwao ikiwemo dawa kama karatasi nyeupe iliyoandikwa maneno na namba za ajabu ajabu kwa wino kama wa rangi ya machungwa hivi (zafarani?) Kwa ajili ya kuloweka kwenye maji kwa ajili ya kunywa na mengine kuogea.

Wakaondoka wagonjwa wote nikabakia mimi na kaka.

Tabibu Zahiri akanisogelea, akaniangalia usoni kwa kunikazia macho na kuzungumza lugha mbalimbali lakini nilikuwa nimetulia tu.

Akachukuwa karatasi nyeupe na peni nyekundu akaanza kuandika andika kwenye karatasi mfano wa kuchora chora kisha akawa kama anakatakata aliyoyaandika na hatimaye akaja na kauli kwamba nipelekwe kwenye kitabu.

"Huyu si wa hapa, mpelekeni kwa Sheikh Mohamed"

Sheikh Mohamed (Allah amwie radhi) wakati huo alikuwa ni kiongozi mkubwa wa dini hapo Bagamoyo na alikuwa ana wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya kuwafundisha elimu ya dini ya kiislamu.

Ilikuwa ni kawaida ya Sheikh Mohamed kukaa nje ya baraza yake kila siku asubuhi baada ya kuswali na kuendea kufanya ibada mbalimbali ikiwemo kupokea salamu za wapita njia.

Hivyo haikuwa vigumu kumpata Sheikh Mohamed kama alivyokusudia tabibu Zahiri.

Jumapili asubuhi mimi na kaka yangu tulifika nyumbani kwa Sheikh Mohamed si mbali sana kutoka kwa tabibu Zahiri ambapo ni umbali wa kuvuka barabara moja ya lami tu.

"Assalaam aleikum" tulimsalimia kwa pamoja

"Wa aleikum salaam, karibuni" alijibu kwa sauti yake nzito huku akituonyeaha sehemu ya kukaa kwenye kibaraza kando ya 'kiambaza' cha nyumba yake, maana dalili zote tulikuwa tunaonesha sisi siyo wa kusalimia na kupita.

"Sheikh tumekuja tuna shida, ndugu yangu huyu anasumbuliwa na maradhi tusiyoyajuwa..." Kaka alieleza historia nzima.

"Haya karibuni ndani" Sheikh alijibu huku akiinuka na kuelekea sebuleni ambapo kulikuwa na busati.

Wakati huo wote mimi nipo kawaida kabisa, sina dalili zozote za maradhi.

Baada ya utangulizi wa kaka, Sheikh akasema "al faat'ha"

Tukaanza kusoma sura ya ufunguzi kutoka kitabu cha Qur’an.

Hii sura waumini wote wa kiislam wanaijuwa maana ndiyo hutumika katika ibada ya swala mara kwa mara.

Baada ya kumaliza kusoma sura ya ufunguzi, akaanza kusoma yeye sura mbalimbali kwa ufupi ufupi na kwa haraka haraka sana, kisha akaagiza yaletwe maji kwenye bilauli akayasomea kisha akaniamuru niyanywe palepale.

Baada ya kunywa akasema turudi Jumatatu baada ya swala ya alasiri kwa ajili ya kisomo maalum.

Siku hazikuganda, Jumatatu ikafika na muda ukawadia tukaenda kwa Sheikh.

Tulivyofika alitukaribisha na kutuambia kuwa amefanya dua kisha akasema:-

“Maradhi haya ni ya bara huko, inabidi tiba aanzie huko”

Neno Bara kwa wakazi wa Pwani hulitumia kama vile kusema ‘mikoani’

Tukaangaliana na kaka pale kisha tukaaga na kuondoka.
***********

Inaendelea
 
3. MIZUNGU

Kauli ile ya Sheikh kuwa kwa maradhi niliyonayo ni ya bara ilitukatisha tamaa kiasi cha kufanya tusijuwe la kufanya, tukarudi nyumbani kwa ajili ya kupeleka mrejesho na kufikiria kutafuta waganga wa kienyeji.

“Msiende kwa waganga wa kienyeji, nendeni kwanza kwa Shariff mtoto…” hii ilikuwa kauli ya baba baada ya kuona tutapotea njia maana yeye hakuwa mtu wa kufuatilia tabibu za kienyeji ingawaje pia hakuwa mtu wa kusali sana msikitini.

Shariff mtoto wakati huo alikuwa kiitwa Hanssen. Shariff huyu asili yao ni maeneo ya Mkwaja pia ambapo ndipo matatizo yangu yalipoanzia. Hakuwa mtoto kihivyo lakini watu walizoea kumwita hivyo maana alianza huduma za maombezi akiwa kijana mdogo kabisa.

Mashariff kwa mukhtadha wa hapa ni wale watu wanaume ambao wamekirimiwa zawadi na Mwenyezi Mungu ya kuweza kukusudia jambo na likawa. Watu walikuwa wanasema wana ‘makarama’. Wapo mashariff wa aina kuu nne kama sijakosea, wapo wale wa nasaba (kutokea kwenye kizazi cha wajukuu wa Mtume Mohammad, rehema na amani zimfikie), wapo wale wa ucha Mungu (kila mwenye kuitakasa nafsi basi aweza kuwa shariff) na wapo wale wa kukirimiwa tu na Mwenyezi Mungu kupitia mawalii wake. Inasemekana kuna hata kizazi cha paka (nyau / pussy, cats) ambao ni mashariff. Ndiyo maana haishauriwi kuwapiga paka hovyo bila sababu ya msingi maana kuna wengine ni uzao huo, wakikusudia baya basi litakupata, na hii imeenda mbali kwa viumbe wengine wengi wataambao, warukao na watembeao. Pia kuna Mashariff ‘jina’. Hawa wamepewa tu jina hilo na wazazi wao ama kujiita wao wenyewe pasi na karama zozote ama kwa kujifanya wana karama za kutibu nk.

(Habari za Mashariff ni pana na linafaa kuwa na uzi wake.)

*************

Siku iliyofuata tulienda kumtafuta Shariff mtoto, lakini hatukumkuta, tulirudi jioni nyumbani kwake ndipo tukamkuta lakini cha ajabu tulimkuta akiwa amelewa pombe aina ya mnazi.

Mnazi ni aina ya pombe igemwayo kutoka kwenye mti wa mnazi kama vile pombe aina ya ulanzi inavyogemwa.

“Njooni kesho asubuhi, muda huu siwezi kufanya kitu…” ilikuwa kauli ya Shariff Hanssen.

Tuliondoka kwa unyonge sana huku tukiwaza kama huduma ya maombezi itafanikiwa kwa hali ya ulevi ule wa pombe.

“Makarama yatamwisha huyu kwa sababu ya ulevi” kaka alisema kwa kulalamika wakati tunarejea nyumbani.

Asubuhi yake tulifika kwa Hanssen mapema ili kuona kitakachoendelea, alitukaribisha kwenye mkeka na baada ya maelezo marefu ya kaka akachukuwa kitabu kidogo akaanza kusoma kiarabu kwa haraka haraka sana kiasi kwamba hata sikuweza kujuwa anasoma kitu gani. Aliendelea kusoma hivyo kwa muda mrefu, kisha akaingia ndani akaleta ‘chetezo’ na ubani aina tatu tofauti na kendelea kusoma huku akiweka ubani kwenye chetezo chenye moto.

Baadaye akatuamuru tuwe tunaitikia dua kwa kusema ‘amin’, tulitikia dua kwa muda mrefu hatimaye akamaliza.
**********


Hali yangu kiafya ilitulia kiasi cha kama miezi miwili hivi lakini baadaye maruweruwe yakanirudia tena. Nakawa nikilala usiku naona ndoto za kama napaa hivi juu ya ardhi na kuiangalia dunia kama mwewe vile aangaliavyo chini akiwa hewani, siku nyingine naota nipo msituni peke yangu kama nimepotea hivi natafuta njia ya kutokea barabarani, siku nyingine naota nipo mwenye mji wa ajabu wenye miamba ya mawe mengi watu wakiwa wanataabika na hali za huko mie nakuwa nawasaidia nk.

Siku nikiota ndoto za namna hiyo tu, asubuhi yake napata homa kali kiasi cha kushindwa kula vizuri hali iliyopeleka afya yangu kuzidi kudhoofu, lakini pia nikawa kama vile naona yatakayotokea muda ujao japo siyo kwa asilimia mia lakini inakuwa vivyohiyo. Kwa mfano, naweza kulala hata mchana nikaona / kuota kama kutakuwa na msiba jirani, basi kweli haipiti muda tunapata taarifa za msiba na mambo ya ajabu ajabu kama hayo.

Hali yangu iliendelea kuwa mbaya mpaka familia ikaamua nianze kujaribu tiba za kienyeji. Ndipo nilipo pelekwa Mlingotini – Bagamoyo. Tulipitia njia ya kaole kisha kuingia ndani upande wa kulia ndani ndani kabisa kwa kuulizia kwa Mzee wa tiba, mganga maarufu Mlingotini. Nilikuwa kijana barobaro tu wa miaka kumi na mitano hivi kuelekea kumi sita na wala sikuwa nawajuwa wanawake.

Elimu ya sekondari sikuchaguliwa kuendelea na wala wazazi hawakujishughulisha kuhusu mimi kwenda Sekondari, haikuwa kipaumbele sana kwa watu wa ukanda wetu, tulikuwa tunarithi kazi za baba zetu tu.

Baada ya mapokezi ya pale kwa mganga tulisubirishwa na kundi wa wateja wengine wapatao wane hivi pale. Kila mmoja alikuwa anaitwa ndani kwenye kilinge cha Mzee wa tiba.

Ilipowadia zamu yangu niliitwa na kuelekezwa kukaa kwa kunyoosha miguu uelekea upande jua linapo chomozea (mashariki). Mpaka hapo hatukuwa tumesema chochote kwa mganga. Akauliza jina langu na la mama yangu kisha akaanza kusema maneno yasiyoeleweka pale na vimbwanga kibao hatimaye akatikisa kichwa na kutulia.

“Kijana!” aliniita yule mganga, nikatoa tu macho kwa kumuangalia. Yeye akaendelea kusema kwa sauti nzito…

“Kijana, umerogwa!”
“Umehangaika sana bila suluhu lakini hapa sasa umefika!”

Kwa mganga huyu tulienda watu watatu, yani mimi, Kaka mkubwa pamoja na mama yangu mzazi. Ilikuwa ni mwendo mrefu wa kutembea, maana tulivizia basi la MFDC (Mbegani Fisheries Development Centre) lililokuwa likiwapeleka wafanyakazi na familia za wafanyakazi kwenye Chuo cha maendeleo ya uvuvi Mbegani Bagamoyo. Tulishukia mbele kidogo ya kaole na safari ya kutembea kwa miguu ikaanza kuelekea huko kwa Mzee wa Tiba Milingotini ndani ndani.

“Eeee wanatakiwa kuku wawili, jogoo mwekundu na tetea mweusi…” alisema yule mzee wa tiba kwa sauti nzito.

“Eeee kuku wawe wamekomaa kiasi cha kuwa na ukucha mrefu juu ya miguu…” aliendelea.

Mimi na kaka tukawa tunatazamana, lakini mama akawa anasikiliza kwa makini.

“Baba, tumetoka mbali, hao kuku tutawapata wapi na ni hatua kurudi kuwatafuta…” Mama alimsemeza yule mganga.

“Hahahahhaa…. Hahahahaha…” Mganga alicheka kwa sauti nzito kisha akasema kuwa kuku watapatikana.

“kuku watapatikana, kuku watapatikana, kuku watapatikana…” sauti ya mganga ikawa inafifia kisha akainamisha kichwa.


Pale kilingeni kulikuwa pia kuna wasaidizi wawili wa mganga, mmoja ni kijana wa kiume na mwingine ni mdada wa makamo ambao wote walikuwa wamevaa kawaida tu isipokuwa mganga mwenyewe alikuwa amevaa kaniki, kilemba cheupe huku ameshika usinga wenye shanga kadhaa .

Pembeni ya chumba kulikuwa na makopo mengi yaliyo na mizizi iliyosagwa (dawa) na upande mwingine kulikuwa na vibuyu vidogo vidogo kadhaa ambavyo sikujuwa mara moja ndani yake kuna nini. Sehemu nyingine kulikuwa na kitambaa chekundu kilichofunika vitu ambavyo pia sikujuwa ni nini.

Mara yule mzee wa tiba akainua kichwa na kuwauliza wale wasaidizi wake…

“Wamesemaje…?” aliuliza mganga kwa sauti ya kawaida huku akiwaangalia wale wazaidizi wake.

Wakaumueleza kuwa kunatakiwa jogoo na tetea. Basi mganga akawambia yule kijana akachukuwe hao kuku bandani.

Kulikuwa na banda maalumu la kuku wenye rangi moja moja tofauti. Yani kuku weupe tu, kuku weusi tuu na kuku wekundu tu lakini wote waliweka pamoja.

“Tiba yako kijana itaanza kwa kafara ya kuku hao wawili… hebu nifuateni” alisema yule mganga huku akitoka nje ya kilinge na kwenda eneo la uwazi ambalo kwa dalili zote palikuwa panaonyesha kuwa ni machinjio ya kuku maana kulitapakaa damu za kuku zilizoganda.

Kuku wale walichinjwa kila mmoja kwa wakati wake, baada ya kuku kupapatika na kufa mzee wa tiba alikuwa ‘anatolea macho’ miguu, mabawa, shingo na ueleko wa kuku maana walikuwa wakichinjwa wanaachwa wapapatike hadi wafe.

“Njia imefunga” alisikika mganga akisema baada ya kumchinja yule tetea mweusi.
“Magharibi” aliropoka yule mzee wa tiba, hiyo ni baada ya kumchinja kuku wa pili ambaye ni jogoo.

Basi tukaambiwa tukae nje tusubiri na wale kuku walichukuliwa na yule mdada msaidizi na kutoweka nao upande mwingine wa nyumba.

Mganga aliingia tena kilingeni na kuita wateja wengine waliokuja baada ya sisi.

Tulisubiri pale nje hadi njaa ikaanza kuniuma maana ilikuwa inakaribia saa nane mchana. Mara akaja yule kijana msaidizi wa mganga na kutuita ulekeo wa jamvi safi kwa ajili ya chakula. Kilikuwa chakula maalumu kilichoandaliwa kwa ajili yetu sisi, kulikuwa na ugali, samaki pamoja na vibakuli vitatu vya finyango za kuku.

“Wewe bakuli lako hili” alisema yule kijana huku akinionesha upande wa kukaa.

Wakati nakula ndiyo nikagundua niliwekewa maini, firigizi na miguu ya kuku wakati mama na kaka wao niliona baadaye wakila vipapatio.

Kulikuwa na makundi mengi yanayokula muda huo na mtindo ulikuwa ni huo huo wa vibakuli vibakuli.

Baada ya maakuli, kila mteja alikuwa akiitwa kilingeni na kupewa dawa na maelekezo ya kutumia. Zamu yetu ilipofika mganga akasema, kazi yangu kubwa maana imeegemea magharibi na njia imefunga. Hivyo tujiandae kwa kafara kubwa ya kondoo. Tutafute wenyewe. Ujira wa kazi alisema tuweka kwenye mtungi kiasi chochote ambapo mama alienda kuweka, sikujuwa hata ameweka kiasi gani lakini nilisikia sauti za sarafu zikilia, pia tulilipishwa kuku wawili kwa bei ya sokoni tu.

Hata hivyo nilipewa dawa za kutumia na maelekezo yake. Baadhi ya dawa zilikuwa majani fulani sijapata kuyaona tangia nizaliwe, yanalowekwa kwenye maji ya kuogea kisha kila nikitaka kuoga niliambiwa niwe nachanganyia maji hayo ya majani ya ajabu ajabu, dawa nyingine ilikuwa ya kupaka kama mafuta lakini yalikuwa meusi ti! Yalikuwa kimiminika, unajipaka mwili mzima, kali kupita yote nilipewa mafuta fulani ya kupata nyayoni, viganyani na usoni usiku tu wakati nataka kulala lakini ilikuwa inanuka balaa! Ilikuwa inanuka kuliko mafuta yatumikayo ‘kukarafati’(siyo kukarabati) vyombo vya baharini kwa sufi na mafuta ‘makasamala’.
**********

Inaendelea
 
4. KAFARA

Nilitumia dawa zile kwa wiki moja na hali yangu ilionekana kama kutulia, kaka mkubwa naye aliagizwa aende mazizini (Bagamoyo jirani na kwa Kafumbo ambaye alikuwa anamiliki mgodi wa kutengeneza chumvi), kule kulikuwa na mazizi mengi ya mifugo ambayo yalikuwa yanamilikiwa na wafugaji mbali mbali.

Siku hizi eneo hilo kumejaa mahoteli ya kitalii sijui kama bado kuna mazizi ya mifugo.

Baada ya siku kumi hivi tangia nitumie zile dawa kutoka Mlingotini, safari ya kwenda huko tena ikawadia ambapo safari hii Baba, Mama, kaka mkubwa, dada yangu tulienda wote. Baba alienda kwa mzee Kafumbo kuomba usafiri wa kutupeleka Mlingotini.

Mzee Kafumbo alikuwa na gari zuri Landrover 109 pickup TZ-61.

Tukapakia Kondoo wetu mwenye rangi mchanganyiko wa nyeupe na nyeusi kwa maelekezo ya mzee wa tiba, alikuwa na pembe zilizopinda na sikujuwa hata alinunuliwa kwa kiasi gani, baba na mama wakapanda mbele, mimi , kaka na dada tukapanda nyuma, dereva alikuwa mtoto wa mzee Kafumbo.

Haikuchukuwa muda mrefu tukafika, tukapokelewa kisha kijana wa Kafumbo akaondoka na land rover kurudi mjini kuendelea na majukumu mengine.

Ilikuwa majira ya saa tatu hivi asubuhi tulipo wasili eneo hilo kwa mzee wa tiba, tulikaribishwa vizuri kisha yule kondoo akachukuliwa na kijana wa mzee wa tiba na kufunga kwenye kigogo pembeni kidogo ya eneo la machinjio ya kuku.

“Tiba ya leo ni kiboko!” alisikika yule mzee akisema kwa sauti ya kawaida.
“Tiba hii kwa hapa Tanzania nimeifanya kwa watu wawili tu kwa umri wangu huu” aliendelea yule mzee wa tiba kuongea huku akiendelea kufanya kazi zake ndogondogo.

“Mtu wa kwanza kumfanyia tiba hii ni kiongozi mkubwa wa kisiasa na wa pili ni mama mmoja hivi miaka ya nyuma…” aliendelea huku akifungua kasha maalumu liliokuwa na vitu mfano wa visu.

“Kafara nyingi za wanyama wenye miguu mine huwa nafanya kwa kuchinja, lakini kwa aina ya maradhi ya huyu kijana imenibidi nifanye kafara hii ambayo najuwa haiwezi kudunda…” alisema kwa kujigamba.

Mara akamwita yule kijana msaidizi wake na kumkabidhi visu vikali vitatu na kumwambia akamchune / kukwangua yule kondoo manyoya yake abakie na ngozi tu tena akiwa hai.

Nilishtuka sana kuona kondoo anaenda kuchunwa ngozi akiwa hai, nikamuangalia kaka mkubwa naye akanitazama lakini hatukusema neno. Mganga akatuamuru sisi tubaki nje na yeye akaingia ndani na wazazi watu. Huko sikujuwa kilichoendelea.

Huku nje, yule kijana akawa anamnyoa manyoya yule kondoo, kidogo moyo wangu ukatulia maana nilidhani anachunwa ngozi akiwa hai. Kwa ustadi mkubwa aliendelea kumnyoa zoezi lililochukuwa saa kadhaa kabla ya kumaliza na wakati huo tayari juwa lilikuwa juu ya utosi, ambapo ndio muda aliosema mzee wa tiba kuwa unafaa kwa kuanza kufanya kafara.

Kondoo akiwa hai, tayari akiwa amekwanguliwa manyoya yake karibu yote, akachukuliwa na mzee wa tiba na kuanza kumchorachora mavitu ambayo sikuyaelewa kwenye mwili wake kwa kutumia kijiti maalum na wino mwekundu (zafarani?)

Wakati yeye akiendelea kumchora yule kondoo, alimuambia yule kijana aandae ‘ziara’. Sikuelewa mara moja ziara ipi tena lakini nikaona yule kijana ameenda kuchukuwa jembe na sepetu / beleshi (spade) na kwenda pambeni kidogo ya msitu wa miembe iliyopo hapo jirani na kuanza kuchimba. Baadaye nilikuja kujuwa kumbe alikuwa anachimba kaburi. Moja kwa moja nikajuwa hapa ndipo atakapozikiwa huyu kondoo.

Muda wa kula ukafika, safari hii tulikuwa kwa jumuiya lakini wanaume peke yetu na wanawake peke yao na wala hapakuwa na vibakuli vya kupimiwa finyango za nyama ya kuku. Tulikuwa vyema tukashiba kisha mzee wa tiba akaendelea na zoezi lake la kuandika kwenye mwili wa kondoo na yule kijana akimalizia kuchima kaburi maana ardhi ya eneo lile haikuwa ngumu.

Mzee wa tiba akamaliza zoezi la kuandika kwenye mwili wote wa kondoo kisha akachukuwa shuka nyepesi nyeupe nayo akaanza kuichorachora mistari mistari na mikato mikato isiyoeleweka na maandishi kama ya kiarabu lakini yenye usanifu tofauti kabisa sijapata kuona, shuka lile lote likaenea wino wa michoro na maandishi. Alikuwa ananakili kutoka katika kitabu fulani hivi kuukuu. Sanjali na kondoo pia kulikuwa na ‘nazi kavu’ saba (inasemekana zilizo anguka zenyewe kutoka juu ya minazi), mayai viza saba, chungu cha kupikia na vifaa ambavyo sikuona vyote mara moja kwenye ambayo vilikuwa kwenye ungo, lakini niliona chumvi, mtama, kitu kama buni (kahawa) na vingine vingi sivikumbuki.

Tukaiwa wote kwenye kilinge cha nje ya nyumba, tukakaa kama nusu duara hivi, kukaletwa jiko la mkaa na chungu kikabandikwa, kondoo akasogezwa jirani, mayai na nazi nazo ziliwekwa chini kwenye jamvi. Mzee wa tiba akaanza kwa kusoma pale haraka haraka sana kisha akawa anaweka mavitu yale yaliyokuwemo kwenye ungo ndani ya chungu huku yule msaidizi wa kike akikoroga…
Zoezi iliendelea kwa muda, yule kijana akaamriwa amfungue kondoo Kamba zote, muda wote kondoo alikuwa akilia kwa namna ya kuomba msaada
(wafugaji watanielewa)

Baada ya kufunguliwa Kamba, kondoo badala ya kukimbia, aliendelea kutulia huku makamasi yake yakimchuruzika. Mzee alizidi kusoma mavitu yake, chungu kilizidi kukarangizwa mavitu yasiyoeleweka na kutatarika na kondoo alizidi kutulia, akaacha kulia na hatimaye akalala kwa namna ya kupumzika huku akihema kwa kasi.

Chungu kilikamilika kukarangizwa kikaipuliwa na kubandikwa chungu kingine chenye majani ya aina tofauti tofauti na kufunikwa. Kondoo aliendelea kulala chini na safari hii alilaza kichwa chake chini kama vile amezirai au amekufa. Yule mgaga akachukuwa lile shuka lenye maandishi mengi mekundu na kumfunika na akaendelea kusoma.

Baada ya muda mzee wa tiba alimuamuru yule kijana msaidizi wake ambebe yule kondoo akiwa na shuka lake waelekee kwenye kaburi. Pia sisi alitupa ishara ya kwamba tumfuate, tulienda sote isipokuwa yule dada msaidizi na mama. Kufika kule yule kijana akaambiwa amuweke kondoo kwenye kaburi, ambapo alivyomshusha tu, kondoo hakulala tena bali alisimama lakini bila kupiga kelele, alikuwa kama amezubaa hivi, huku akiwa na shuka lake mgongoni.

Mzee wa tiba aliendelea kusoma mavitu yake hadi kondoo akalala tena chini, kijana akaambiwa amfunike vizuri shuka kisha akaendelea kusoma huku anaweka udongo kwenye kaburi. Zoezi liliendelea hadi kondoo alipozikwa (akiwa hai?)

Juu ya kaburi halikuinuliwa kama makaburi mengine bali paliwekwa ‘levo’ ya usawa wa ardhi, kisha akatuambia turudi kule kilingeni zoezi bado linaendelea.

Kufika kule kilingeni nikapewa kidoga na kuamriwa nikae hapo, kisha kile chungu ambapo kilikuwa tayari kimechemka haswa kikaletwa mbele yangu na kisha nikaona nafunikwa shuka kubwa na kuambiwa niachame mdomo halafu chungu kikafunuliwa.
Lo salale! Hewa ikaanza kuwa nzinto ndani ya shuka nikawa kama nakosa hewa (nakosa pumzi), mwili wote ukajaa jasho kiasi cha nguo nilizovaa kulowa chapachapa. Baadaye nikazoea hali hile ya hewa chache na baada ya dakika chache tu nikafunuliwa wakaniangalia kisha wakanifunika tena. Zilikuwa ni zoezi la kama dakika kumi hivi lakini niliona kama ni saa nzima.

Baada ya zoezi hilo niliambiwa nikae kwenye mkeka nivue shati ambalo kwa wakati huo lilikuwa halitamaniki kwa jasho. Nikamuona yule dada msaidizi wa mganga ameshika kiwembe kipya aina ya topaz…
“Tulia nikuchanje eee mdogo wangu, utapona tu” alisema yule dada.

Kusema ukweli baada ya kutoka ndani ya lile shuka nilijisikia vizuri sana, nilipumua vizuri na kujihisi nina afya ‘tele’. Katika maisha yangu hadi wakati huo nilikuwa sijawahi kuchanjwa hata mara moja, hivyo lile zoezi lilikuwa la kuogofya sana kwangu. Nahisi yule dada aliniona na kuelewa hisia zangu ndiyo maana akanituliza kwa maneno yake na sauti nyororo ya kuliwaza.

Nilichanjwa kichwani chale mbili mbili utosini, kwenye paji la uso mwanzo wa nywele na kisogoni. Pia aliendelea kunichanja kifuani, mikononi na miguuni halafu akazunguka mgongoni ambapo alinichanja nyuma ya shingo na kiunoni. Mwote humo alikuwa akichanja chale mbilimbili ndogo ndogo kwa haraka sana na kila sehemu alipochanja damu ilikuwa inatoka.

Yule dada akaletewa kibuyu ambacho ndani kulikuwa na dawa ya kimiminika kama mafuta hivi meusi na kuanza kupipaka kwa mtiririko kama alivyo nichanja. Alipomaliza akapewa kikopo kingine cha dawa ya unga unga mweusi na kupaka sehemu zote zilizochanjwa bila kufuata mpangilio. Alipomaliza alinielekeza nitulie pembeni kwenye mkeka. Hapo nilikuwa nasikilizia maumivu ya chale pamoja na hii dawa ya pili ya unga unga maana ilikuwa inauma sana.
**********

Zoezi liliisha kwa wazazi wangu kupewa maelekezo mengine kisha wakapewa zile nazi zote na mayai yote tukaanza safari ya kurudi barabarani ili kufika njia kuu ya Kaolee. Wakati tupo njiani kabla ya kufika barabara kuu ya Kaole kuna njia panda fulani hivi za watembea kwa miguu, nikaona baba anavuja zile nazi moja baada ya nyingine huku mdomo kama anasema vitu ambavyo sikuvisikia. Nazi zote saba zikaisha, tukawa tunaendelea na safari ya kwenda barabara kuu.

Kabla hatujatokeza barabara kuu, nikapewa yale mayai moja baada ya jingine na kuamriwa kurusha kinyume nyume bila kuangalia nyuma hadi yakaisha yote. Muda huo wote tupo kimya na tukawa tumekaribia kabisa barabara kuu ambayo ilikuwa ni ya vumbi.

Ilikuwa inaelekea majira ya saa kumi na moja hivi jioni, hivyo tulichelewa lile basi la Mbegani, ikabidi tuketi chini kusubiria usafiri mwingine lakini ni wa kubahatisha maana mabasi ya kutokea Dar es Salaam yalikuwa yakipita njia ya Zinga-Kiromo-Ukuni hadi mjini Bagamoyo wakati sisi njia tuliyopo ni ya Zinga -Pande -Kaole -Mjini Bagamoyo.

Kwa bahati nzuri baada kama ya dakika arobaini hivi za kusubiri likaja basi moja kutoka Dar es Salaam linalomikikiwa na Shariff wa Bondeni, basi hilo kwa jina maarufu likikuwa linaitwa UWEMBE na kwa siku hiyo alikuwa analiendesha dereva mmoja aitwaye Mantibo.

Basi lilikuwa limejaza sana maana lilikuwa ‘linaokota’ abiria wote kwa kuwa njia hiyo haikuwa na mabasi mengi hivyo ilikuwa ni namna pia ya kusaidia abiria licha ya jambo la biashara.

Tulifika nyumbani jua likiwa limeshazama, Mama aliniambia nisioge siku hiyo hadi kesho, nikapewa dawa na mama za kunywa usiku huo na asubuhi pia na kuendelea kufanya hivyo kwa siku saba.
**********

Inaendelea
 
Iko poaa
 
5. MAPENZI, WIVU, FITNA NA KUSAKA SULUHU

Kusema ukweli baada ya yale matibabu ya siku saba kutoka Mlingotini nilianza kujisikia vizuri, maruweruwe yaliisha, sikuwa na gumbizi wala kuhisi kuchanganyikiwa au kuota ndoto za ajabu ajabu.

Hali yangu iliendelea kuimarika na kuendelea na majukumu ya kusaidia baba hadi siku ile ulivyonikuta feri.
“Yaani pale nilikuwa tayari nimeimarika…” alisema

Tukacheka sana maana nilivyomuona siku hiyo Feri alikuwa dhoofu sana sasa sijui kabla ya hapo alikuwa dhoofu kiasi gani. Nilimuonea huruma sana hadi hapo lakini aliendelea kunisimulia.

Familia ya Mwinyi Mkila ilikuwa na familia rafiki na familia yangu, hivyo nilizoeana sana na watoto wake hususani wa kiume maana walikuwa wanapenda sana kuja kwangu Sanzale kuchukuwa maembe dodo, maembe sindano na mbichitamu. Ni familia iliyochangia kwa kiasi kikubwa kuwasilimisha mdogo wangu na mke wake ambao ndio walikuwa makazi yao hapo kwangu Sanzale kwa ajili ya kuendeleza ufugaji wa kisasa na kilimo mihogo, mbaazi, kunde, kutunza miembe, minazi na kuna kasehemu kidogo kuna bonde ambalo tulitumia kulimia mpunga.

Basi baba, niliendelea na majukumu yangu hadi nikaamua nibakie huku huku Dar es Salaam kwenye nyumba yetu tuliyopangisha maeneo ya Kariakoo mtaa wa Livingstone na Mkunguni. Nikapewa chumba kimoja na kuanza maisha hapo. Niseme tu ukweli hadi muda huo nilikuwa sijawajuwa wanawake, sijui kwa sababu ya maradhi kunipelekesha au namna gani. Lakini nilivyohamia tu hapo kwenye nyumba yetu ya Dar mambo yalianza kubadilika.

Nilihamia nikiwa na godoro tu na stuli moja na feni ya umeme ambayo niliinunua wakati nahamia rasmi hapo. Nyumba ilikuwa ya vyumba sita yaani ukiingia vyumba vitatu upande wa kulia na vyumba vitatu vingine upande wa kushoto. Mimi nikapewa chumba cha katikati upande wa kulia ambapo mpangaji aliyekuwa humo alihama baada ya kupata kazi nje ya Dar es Salaam hivyo nikachukuwa nafasi hiyo kuwasilisha ombi langu kwa baba na akanikubalia.

Nadhani alinikubalia kwa sababu ya kwanza nianze kujitegemea na kujifunza maisha, pili inakuwa rahisi mimi kufanya kazi ya kupokea matenga ya samaki na kuyauza kwa kuwa sasa utaratibu wa usafirishaji ulizidi kuwa bora baada ya kuamua kutumia Datsun pickup za baadhi ya wamiliki hapo Bagamoyo. Hivyo badala ya kuamka saa kumi alfajiri kama Bagamoyo nilikuwa naweza kulala hadi saa moja kasoro na kuwahi Feri kabla gari haijafika na kupokea mzigo na kuuweka sokoni kwa mauzo.

Nilianza kupewa ujira rasmi badala ya posho ya kujikimu pekee na nikaanza kununua vitu vya ndani kama vile kitanda, nikachongesha kochi la mtu mmoja, nikanunua friji dogo na redio kwa ajili ya kusikilizia taarifa za habari, vipindi vya michezo saa mbili karorobo usiku na kusikiliza matangazo ya moja kwa moja ya mipira. Hakika chumba changu kilipendeza kwani niliweka na kapeti la plastiki lenye nakshi za drafti draft.

Kazi za Feri zilikuwa zinaisha mapema sana kabla ya saa sita mchana, hivyo nilikuwa napata muda mwingi wa kupumzika na kuzurura jijini. Kuzurura huku kulinikutanisha na Sinasudi binti ambaye alitokea kunipenda sana. Tukaanzisha uhusiano wa kimapenzi na akawa anakuja nyumani kunifulia nguo na kunipikia siku moja moja.

Kumbe nisijuwe mle mle ndani ya nyumba, kuna mtoto (mwari) wa mpangaji wetu alikuwa akinipigia mahesabu. Mara aje kuomba maji ya baridi, mara aje kunipigisha stori lakini mimi wala sikuwa na hili wala lile, nilimchukulia kama mdogo wangu tu. Nilijuwa haya siku ambayo Sinasudi alikuja mapema na kunipikia chakula cha mchana akanifulia nguo zangu kisha akaondoka. Nilivyorudi nilimkuta binti huyo mwari akiwa amevimba kwa kununa, nikamsalimia lakini alijibu kwa sauti ya chini. Nilivyomsogelea na kumuuliza kulikoni akanijibu…

“We si unatuona wengine hatufai..!” alisema binti mwari.

“Hee, kwani vipi?” niliuliza kwa udadisi

“Watu tupo humu humu unajifanya hautuoni na kwenda kuokota mishangingi huko barabarani” alisema binti mwari kwa kulalamika.

Hapo sasa ndio nikaunganisha na matukio ya nyuma na kuelewa.

Kwa kuwa tayari Sinasudi alishanifundisha nanma ya kuwajuwa wanawake, nikamwambia yule mwari kuwa kesho nitampeleka kwa Bahresa (Kariakoo) kwenda kula ashkrim (ice cream). Alifurahi sana na sura yake ikakunjuka. Kweli kesho yake baada ya kutoka Feri nilienda nyumbani na kumkuta tayari akiwa amejiandaa.

“Mama natoka na Pazi twaenda kwa Bahresa hapo jirani” alisema kwa kupasa sauti akimuaga mama yake.

Wazazi wa maeneo ya Pwani malezi yao wanayajuwa wenyewe. Maana unaweza ukasikia ama kuona mama akimwita mwanawe wa kumzaa kama hivi…

Ashakum si matusi

“We mwana K-mamayo! Njoo hapa!”

Yani hapo ndio amemuita mwanawe wa kumzaa labda mara ya kwanza hakusikia ndio akapasa sauti, da!

Ama unaweza kusikia baba akimtukana mwanawe

“K-mamayo!” mbele ya mama yake mzazi lakini cha ajabu mama mzazi atajibu “ya shangazi yake!” na kila mmoja akaendelea na shughuli zake kana kwamba hakuna jambo liliotokea.

Tulifurahia ‘mtoko’ ule na kurudi jioni sana, maana baada ya kula ice cream tulienda ‘fete’ viwanja vya mnazi mmoja ambapo kulikuwa na mabembea yaliwekwa kwa ajili ya kufurahisha watu hususani watoto ingawaje huwa yanaondolewa na kupelekwa sehemu nyingine kwa madhumuni hayohayo ya kibiashara na ustawi wa jamii.

Nilimnunulia zawadi ndogo ndogo mbalimbali ikiwemo leso, mkufu na hela kiasi. Alifurahi sana. Tukiwa huko matembezini nilimueleza kuwa Sinasudi ni mchumba wangu, hivyo asinivurugie maana yeye nilimuona mdogo hivyo wala sikumuweka akilini, alikuwa ana miaka 16 hivi.

Mwari alitulia kidogo na kutuachia nafasi lakini alihakikisha nimemtoa ‘utepe’ wake wiki chache zilizofuta na fujo za hapa na pale siku moja moja.

'Udongo' wa kizazi cha maeneo ya pwani huwafanya mabinti wadogo katika umri wa miaka 15 tu kuwa na maumbile makubwa hususani matiti, na imekuwa kawaida kwao (siyo wote lakini) kuanza ngono mapema sana.

Uhusuiano wangu na Sinasudi ulizidi kuimarika hadi ikabidi ahamie kwangu kienyeji. Tukawa tunapika na kupakua.
***********

Maisha yalienda vizuri kwa miaka miwili hapo Dar es Salaam, nikiendelea kuwa na uhusiano na wanawake wawili kwa wakati mmoja huku mmoja akiwa hamjui mwenzake.

Kwa kuwa nilidhamiria kumuoa Sinasudi basi bidii za kumpatia ujauzito zilikuwa kubwa lakini bila mafanikio, hadi nikaona bora nijaribu kwa binti mwari kama atashika maana nilianza kupata wasiwasi na afya yangu ya uzazi.

Basi ile kujaribu tu kufanya naye katika siku zake za uchevusho, haikupita wiki mbili akaniambia hajisikii vizuri, anahisi kichefuchefu sana asubuhi akipigwa mswaki na akila baadhi ya vyakula.

Miezi miwili ilipopita alimshirikisha mama yake, mama yake wala hakushtuka sana bali alikuwa kama amefurahi hivi.

Siku moja katika maongezi yangu na Sinasudi nikagusia kuhusu mimi kumpa ujauzito binti mwari. Alishtuka sana na kuanzisha varangati ndani. Nilijitetea kuwa sikuwa na uhusiano naye bali nilimshawishi tu ili mimi nijaribu kuona kama mbegu zangu zipo vizuri...

Haikusaidia kitu, vurugu ilikuwa kubwa hadi nami ikabidi nianze kupandisha sauti.

"Kwa kawaida mimi ni mpole kama unavyo nifahami mzee... "Alisema

" Lakini ikabidi nianze kupaza sauti kwa kumlaumu yeye kuwa mwanamke gani asiyeshika mimba licha ya kuwa naye kwenye mahusiano kwa miaka miwili." Alisema Pazi.

Sinasudi ni mwanamke rika langu lakini yeye alitangulia kuyajua mapenzi kabla yangu, hivyo alishakuwa na uhusiano na wanaume wawili kabla yangu.

Hakika ndiye aliyenifundisha kuwajuwa wanawake hadi nami nikawa mwalimu kwa binti mwari.

Varangati lilipokuwa kubwa mle chumbani kwangu upepo ulimgeukia nilimuona akijirudi na kianza kuwa mpole kisha kuniomba msamaha na kunieleza ukweli.

"Samahani Pazi, kutokushika mimba si kwa makusudi, mimi wala siyo tasa, nilishawahi kushika ujauzito..." Aliongea Sinasudi kwa sauti ya kutia huruma.

"Baada ya kuachana na bwana niliyekuwa naye kabla yako, niliumia sana na wakati huo nilikuwa nina ujauzito wake wa miezi mitatu. Tuligombana, alinipiga sana na kuniumiza, makovu haya unayoaona siyo ya kuanguka na baiskeli kama nilivyokuambia awali, nilikudanganya, hiki ni kipigo kutoka kwa yule baba wa kikurya ambaye alikuwa mwanajeshi" Sinasudi aliendelea.

"Mimi nilikuwa ni mwanake wake wa pembeni na yeye alikuwa ameoa na alikuwa akiishi na mke wake kijiji cha Mwenge kwenye Maghorofa ya Jeshi... "Aliendelea

"Nilipatwa na hasira sana kiasi kwamba nikaamua kuachana naye na wala sikutaka kubaki na kumbukumbu yake hivyo nilienda Mwananyamala kuitoa Mimba" Alitulia kisha akaendelea...

"Nakumbuka kwa hasira nikamwambia yule daktari anichome sindano ya kuzia nisipate ukauzito, nadhani alinichoma ya muda mrefu ndio maana sijapata ujauzito kwako na hata siku zangu huwa sizioni" Aliongea akiwa amejiimamia na kulia kwa kwikwi.

Basi ikawa ndio mwisho wa varangati tukasameheana na kuamua kuendelea na maisha.
***********

Wiki mbili baadaye mama wa binti mwari akaniita na kuniambia kuwa ana mazungumzo na mimi.

Nilivyorudi kazini baada ya kuoga na kubadili nguo nilienda kumgongea chumbani kwake, alifungua mlango na kuniambia nimsindikize Al Uruba Hotel.

Al Uruba hotel haikuwa mbali na nyumbani ni kiasi cha dakika tano tu kufika.

Ni hoteli ambayo wakati huo wasomali wengi walikuwa wakifikia hapo na kuna mghahawa (restaurant) ipikwayo vyakula vizuri sana.

Tulienda na kufika hapo mara moja na kukaa kwenye viti vya pembezoni. Mhudumu alifika na kuagiza maziwa ya ngamia na mama aliagiza mishikaki ya samaki.

Mama akanifungukia kuwa eti anajuwa kuwa mimi nampenda mwanaye, hivyo nimtunze vizuri nisimchezee...

Mama akazunguka zunguka weee mwisho ndio akalipasua jipu kuwa...

"Mwenzako Salma ujauzito umeporomoka!" Alisema

"Tangia jana usiku aliona damu zikimtoka na asubuhi ulipokwenda kazini kwako sisi tulienda hospitali na kuambiwa kuwa mimba imetoka. (Miscarriage)

Nilipatwa na ganzi fulani hivi na kuzubaa hadi aliponistua kwa kuniita jina...

"Pazi, we Pazi!..." Aliita

"Naam mama" nilitikia kwa unyonge.

"Mbona nakusemesha hujibu kitu... Nakuuliza swali hujibu, umezubaa tu vipi kwani?!" Aling'aka

"Hapana mama, nipo sawa, kwani umeniulizje?! " Nilihoji.

Akaniambia kuwa aliniuliza, je Sinasudi hahusiki katika kuporomoka kwa mimba ya mwanaye?!

Akaniambia "mimi nitafuatilia na nitajuwa tu"

"Ole wake" alionya.

Basi tukamalizia tulichokuwa tunakula na kila mmoja alirudi nyumbani kivyake.

Siku hiyo nililala nikiwa na mawazo sana kiasi ya kuhisi kuchanganyikiwa.

Asubuhi nikamwamuru Sinasudi arudi kwao kwanza, alikuwa akiishi Sharifu Shamba.

Asubuhi nilijivuta kazini lakini nikatoa taarifa kwa Mzee Muhisani ambaye ndiye aliyekuwa dereva na mmiliki wa Datsun pickup iliyokuwa inatuletea samaki Feri kuwa hali yangu kiafya haipo vizuri hivyo kesho aje na mtu wa kunisaidia.
*********

Wiki ile yote haikuwa njema kwangu maana nilianza kuona maruwerue kama ya miaka ya nyuma baada ya kutoka Mkwaja .

Hali ilipoendelea kuzidi niliamua kurudi Bagamoyo nyumbani.

Tulienda tena Mlingotini, mzee wa tiba akafanya dawa zake wee lakini sikuwa napata nafuu...

Wazazi wakaamua tujaribu kwa watu wengine.

Tukaenda kwa Mwalimu Mwaloki, amabaye inasadikiwa ni mmoja wa walii wa Mwenyezi Mungu, yeye akatusomea dua kutoka vitabu vitakatifu na kutuambia yataisha Mwenyezi Mungu akitaka.

Mwalimu huyu alikuwa ni Mwalimu wa Madrasa (chuo) maarufa sana maeneo ya Dunda hapo Bagamoyo. Alikuwa ana kila sifa ya kuitwa mcha Mungu.

Akatupatia na maji kwenye chupa ya 'orange squash' ambayo alisema ameyasomea (ameyaombea) ili niwe nakunywa kidogo kila nikihisi hali ya mvurugano inataka kunijia.

Hali ilitulia kwa wiki kama tano hivi mambo yakarudi tena...

Shangazi yangu akaaye Morogoro akapewa habari zangu na akafunga safari kuja kunijulia hali.

Shangazi " Huyu niachieni, nitazunguka naye atarudi mzimaa!" Alisema kwa sauti yake nyembamba na kali.
*********

Safari ikaandaliwa ya mimi na Shangazi kwenda Morogoro.

Tulianza Turiani, haikufaa, tukaenda Mbingu haikufaa, tukaenda Ifakara haikufaa, kote tulikuwa tunapata nafuu tu lakini baada ya siku 2 au tatu mwendo ni ule ule.

Shangazi akawasiliana na shoga yake aishie Kinondoni Dar, hivyo safari nyingine ya kwenda Dar ikaandaliwa.

Kufika Dar baada ya maongezi yao ya kina, ikaamuliwa tuende Mbwewe.

Ya Mbwewe ikawa kama Morogoro.

Tukaenda Handeni, ikawa kama Mbwewe tu.


Tukaenda Tanga mjini.

Kwa kweli tulizunguka sana, japo sikupata nafuu lakini nilijifunza mengi ya dunia.

"Baba, nimeona mengi sana, hakika hujafa hujaumbika, na wengine husema hujafa hujaumbuka." Alisema Pazi

Tanga tulielekea njia ya kwenda Mombasa sehemu wanaita Kikiboni, kweli tulimkuta mganga lakini alasema yeye hatibu maradhi hayo bali anatibu mifupa pekee lakini akatuelekeza turudi kama tunaenda Tanga mjini kisha tuingie ndani kulia kwenye machimbo ya chokaa jirani na Amboni twende ndani ndani huko hadi tukute mashamba ya mkonge kisha tuulizie.

Kwakuwa tulikuwa hatuna usafiri ilibidi twende hadi Tanga mjini kisha tukodi gari ya kutupeleka.

"Mnataka kwenda kwa Mukulu... Mie napajuwa, nimeshawahi kumpeleka mama moja kule, ila mbali, nijazieni mafuta tu full tank tukifika mtanipatia chochote baada ya kuona safari yenyewe.

Hakika watu wa Tanga wakarimu sana, hawana makuu labda uwakirofishe.

Yule dereva alitupeleka hadi kwa huyo Mganga, ni kweli palikuwa mbali maana tulifika hapo kwenye kambi ya mkonge na kuvuka daraja refu jembamba na kuelekea huko kwa Mukulu.

Baada ya kupokelewa tukakaribisha kwenye sehemu ya kusubiri, ni kwa nje palitandikwa mkeka.
Mganga Mukulu alikuwa na mteja mmoja ndani na mweingine tulikmkuta pale nje mwanamke.

Zamu yetu ilipofika, Mukulu akapiga ramri zake weee na kurudia rudia mara nyingi sana kisha akasema kuwa kuna mwanamke amenichezea... Akasema inahusiana na mambo ya mapenzi.

Shangazi akaniuliza kuhusu mahusiano (uhusiano) wangu na wanawake nikamueleza historia nzima nikaona ananiangalia kwa huruma tu

"Hao hao wanawake zako ndio wamekuchezea" alisema shangazi.

Lakini moyoni haikuniingia akilini kabisa maana maradhi yangu yalinjjia hata kabla sijawajuwa wanawake.

Lakini pia nikakumbuka kauli ya mama Salma na jinsi nilivyo muondoa Sinasudi nikahisi labda nao wanachangia kuumwa kwangu.

Tukapewa dawa za kutumia na vitu vya kufanya ikiwemo kuwasha kibatari (koroboi) bila kukizima na kuchoma makaratasi aliyotupatia yenye maandiko yasiyojulikana na kutamka manuizo wakati wa kuchoma karatasi hizo, dawa za kuoga na kupaka.

Huku hapakuwa na chale, nilishangaa sana maana kote tulipopita ilikuwa ni mwendo wa kuchanjwa tu, bahati nzuri zilikuwa chale ndogo ndogo ambazo hupotea baada ya siku kadhaa.

Siku ya tatu tulirudi wa usafiri wa kuunga unga hadi tukafika Tanga mjini maeneo ya Chumbageni jirani na mwembe mawazo sijui mwembe tayari sikumbuki vizuri.

Hapo palikuwa ni nyumbani kwa rafiki yake shoga yake Shangazi.

Ilibidi kupiga kambi hapo ya wiki moja kwa ajili ya kufanya yale mambo ya kibatari.

Siku ya kwanza kulikucha salama, lakini siku ya pili usiku ilikuwa ni vurugu mechi.

Inasemekana maeneo hayo ni makutano ya wanga usiku hivyo huenda kulikuwa na miingiliano ya masafa ya kibatari na mambo yao.

Vishindo usiku vilikuwa vingi hadi jirani nyumba hiyo hiyo tulimofikia akapandisha mashetani.

Kupandisha mashetani ni kupagawa ama kupatwa na mapepo na kuanza kuongea ongea yenye mantiki na yasiyo na mantiki.

Yule rafiki yake shangazi nikamsikia akimsemesha yule aliyepandisha usiku uleule...

"Taratibu taratibuu, njooni taratibu..." Shoga wa shangazi alisema

"Akina nani nyie na mwatoka wapi" aliuliza kama vile anaona hao anawao waongelesha ilhali hapo alikuwa huyo mama jirani aliyepandisha mashetani.

Sauti ya kiume kutoka kinywa cha yule mama ilisikika akisema wao wametoka mbali, wamekuja kuokoa jahazi, vinginevyo tutampoteza kijana wetu.

Eti tiba yangu si ya kuwasha moto bali ni ya majani tu tena inapatika bara na wala siyo pwani.

"Mpelekeni Pangani atapata njia ya kufika bara" sauti iliishia hivyo

Sasa nikawa najiuliza, Pangani na bara wapi na wapi! Maana Pangani kutokea tulipo ni mwendo wa masaa mawili au matatu tu kwa kuwa ni chini ya kilomita 80.

Shangazi na shogaye na wenyeji wetu, maana sasa watu walijaa kushuhudia wakashauriana ikaonekana nipelekwe Pangani kule kwa wajuzi wa tiba asili na Mashariff.

Jambo la koroboi likaishia palepale na asubuhi yake sote, mimi, shangazi, shogaye na rafiki yake shogaye tukaelekea Pangani.

Tukavuka mto Pangani na kufika eneo liitwalo Kikokwe.
***********

Itaendekea kesho panapo majaaliwa
 
tofauti ya mashua ,jahazi,dau,ngalawa na mtumbwi ni nini ....
Jahazi ni sawa na kusema Merikebu, ni chombo kikubwa kilichotengenezwa kwa mbao mfano wa meli

Mara nyingi hakitumiki kwa uvuvi bali hutumika kwa usafiri na usafirishaji.

Nishati kuu itumikayo ni upepo, kwa kupuliza tanga lililotwekwa na siku hizi baadhi wanatumia mashine za dizeli.

Mashua ni ndogo kulinganisha na jahazi, mbele imechongoka lakini nyuma ipo bapa, nishati kuu ya mwendo ni upepo na sikuhizi pia mashine.

Mashua hutumika kwa uvuvi na usafirishaji pia japo kwa kiwango kidogo.

Dau ni kama jahazi tu lakini lenyewe limechongoka mbele na kwa nyuma.

Nishati kuu - upepo na siku hizi mashine pia

Ngalawa nishati kuu yake pia ni upepo, lakin kuna mabaharia watundu hutumia injini ndogo pia mfano za pikipiki...

Ngalwa ina "mabawa koshoto na kulia kwa ajili ya kubalansi chombo kisiegemee upende mmoja hadi kufikia kuzama.

Mtumbwi ni mfano wa gogo lililochongwa vyema na kuwekwa uwazi katikati na kufanya lielee majini, halina mabawa ya balansi, na kwa asili nishati yake ni makasia (vitu kwa mwiko) na upondo (kitu kama mti ambao unachomekwa chini ya maji na kusukuma, ingawaje vyombo vyote pia vina upondo na makasia.

Pichani hapo imekosekana dau tu ambapo inafanana na mashua laki yenyewe imechongoka mbele na nyuma
View attachment 2397836View attachment 2397837View attachment 2397838View attachment 2397839
 
Kaka Jamaal karibu tena jukwaani kwa simulizi zako za kutukuka

Ikikupendeza naomba kujua kuhusu ile safari ya utalii was ndani iliishia au imefikia wapi
Safari niliacha kuratibu baada ya kupokea taarifa kuwa ingekuwa siyo salama kwangu

Lakini watu waliandaa safari na kila wiki watu hufanya safari japo za siku chache lakini watu wana enjoy

Nami nilijumuika kwenye ruti moja ingawaje sikuingia kwa majina yangu ya humu
 
Ohooh sante kwa ufafanuzi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…