HakiElimu: Uzinduzi wa ripoti za makuzi, ulinzi na elimu bora ya awali inayowaandaa vyema watoto kujiunga na elimu ya msingi

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,982
Ripoti hizo mbili zinazozinduliwa ni:

Intergration of Child Protection into Early Childhood Development (Namna Bora ya Kujumuisha Dhana ya Ulinzi wa Mtoto Katika Elimu ya Awali)

Assessment of Learning and Teaching Environment for Pre-primary Education in Tanzania, 2019 (Mazingira ya Kujifunza na Kufundishia ya Elimu ya Awali)

Tafiti zote mbili zimefanywa na HakiElimu, huku wa Elimu ya Awali kwa watoto wenye mahitaji maalum umefanywa kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kwenye Mtandao wa mashirika yanayofadhiliwa na Comic Relief


Hali ya uandikishaji watoto katika madarasa ya awali siyo mbaya ukilinganisha na malengo. Katika wilaya ambako tafiti zilifanyika, wastani wa uandikishaji na matarajio ni zaidi ya asilimia 100, zaidi ya matarajio.

Mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa watoto wa madarasa ya awali bado ni changamoto. Takribani asilimia 100 ya wilaya zilizofanyiwa utafiti zinaonesha kuwa na changamoto ya uhaba wa miundombinu mbalimbali

Watoto wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu na jamii za wafugaji uandikishaji umebaki kuwa chini ya asilimia 70 ya malengo ya uandikishaji

Elimu ya awali ni taaluma Kama taaluma zingine. Isichukuliwe kiurahisi. Baadhi ya changamoto tulizoziona ni pamoja na weledi wa walimu katika kufundisha. Walimu wapewe mafunzio na kujengewa uwezo. Dr. Jackline Amani

"Kwa mujibu wa takwimu za elimu, mwalimu mmoja anahudumia wanafunzi 224 badala ya 25 inayotakiwa kwenye miongozo", John Kalage

"Watoto wanapaswa kufurahia shule, na waone mahala sahihi na salama kwao ili waweze kujifunza kwa ufanisi", Dr Maregesi Machumu

Kuna haja ya kutazama mazingira ya wafugaji na kutengeneza mfumo unaowafaa – Moses E Mzava

“Kuna utashi a wazazi ku-outsource malezi ya watoto wao kwa watu wengine…Kwa kawaida malezi ya mtoto wa miaka mitatu akae na wazazi wake. Mazingira bora ni vyema yakatengenezwa watatoto kukaa na kujifunza kutoka kwa wazazi” Generali Ulimwengu

Kuboresha elimu ni muhimu kuzingatia suala la vifaa vya kufundishia. Utamaduni wa kusoma unaanzia vitabu unapaswa kuanzia katika ngazi ya awali. Kwenye shule za umma kuna upungufu mkubwa wa vifaa vya kujifunzia ukilinganisha na shule za binafsi. - Dr. Shadidu

Tunachokifanya kama watu wazima ni matokeo ya mambo tuliyojifunza katika miaka minane ya mwanzo ya maisha yetu, kwenye elimu awali sio suala la KKK tu basi kufundishwa stadi za kuanza maisha, changamoto ni wanafundishwa nini huko madarasani - Maregesi Machumu

Susan Lyimo -- Ungefanyika tafiti kwenye vyuo vya elimu ya awali hapa nchini. Kuna umuhimu wa kuwa na vyuo vinavyotoa elimu ya awali pekee. Bajeti yao ni vyema ikazingatiwa kwani elimu ya awali ndiyo msingi wa elimu ulipo.

“Bado walimu wana changamoto ya kutambua wanafunzi wenye changamoto za ulemavu. Wazazi wengine wanapeleka watoto shule bila hata kuwajulisha walimu kuhusu matatizo ya watoto wao” Dr. Jackline Amani

“Ni vyema kuwa na utaratibu wa pamoja unaofanana kwa shule zote za umma na binafsi ili kufidia muda wa masomo uliopotea kufuatia janga la Covid-19” Dr. John Kalage

Hotuba ya Mkurugenzi wa HakiElimu Dkt. John Kalage, wakati wa Uzinduzi kwa Njia ya Mtandao wa Matokeo ya Tafiti zinazoangazia Makuzi ya Mtoto, Ulinzi na Maendeleo ya Elimu ya Awali nchini Tanzania

Tarehe 28 Mei, 2020


Ndugu Washiriki, nadhani mtakubaliana nami kuwa ‘Elimu ya Awali’ ni sehemu muhimu sana ya dhana nzima ya Makuzi na Maendeleo ya Mtoto; kuanzia akiwa tumboni mwa mama yake hadi anafikisha umri wa kujiunga na Elimu Msingi. Umuhimu huu unajitokeza pia katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs); ambapo kupitia lengo namba 4.2 mataifa yote duniani yanasisitizwa kuhakikisha kuwa hadi ifikapo mwaka 2030 yanakuwa na uwezo wa kuwapatia watoto wote, wa kike na wa kiume makuzi bora, ulinzi na elimu bora ya awali ili kuwaandaa vema na hatua ya elimu ya msingi.

Kwa kutambua umuhimu huu, HakiElimu tumekuwa mstari wa mbele katika kutetea, kuelimisha na kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha mtoto wa Tanzania anapata makuzi, ulinzi na elimu bora ya awali itakayomuandaa vyema kujiunga na elimu ya msingi na baadae kuwa raia bora. Ushiriki wetu umekuwa zaidi katika maeneo ya ushawishi wa utungwaji na utekelezwaji wa sera bora za mtoto na elimu, uelimishaji na uhamasishaji juu ya umuhimu wa elimu na makuzi ya mtoto, ushiriki katika juhudi za jamii katika ujenzi wa madarasa na uboreshaji wa mazingira ya ujifunzaji shuleni; uhamasihsaji wa ulinzi wa mtoto shuleni ndani na nje ya shule n.k.

Ili kushiriki vema katika makuzi na malezi ya mtoto, mwaka 2019 HakiElimu tulifanya tafiti mbili kubwa ili kujifunza zaidi kuhusu eneo hili. Tafiti hizo ndizo tunazozizindua leo hapa. Utafiti wa kwanza unaangazia ‘Namna Bora ya Kujumuisha Dhana ya Ulinzi wa Mtoto Katika Elimu ya Awali (Integration of Child Protection into Early Childhood Education) na utafiti wa pili unaangazia Mazingira ya Kujifunza na Kufundishia ya Elimu ya Awali (Assessment of Learning and Teaching Environment in Pre-Primary Education) Tanzania. Kwa pamoja tafiti hizi zinaangazia mahitaji ya awali ya mtoto wa kitanzania nje na ndani ya mfumo rasmi wa elimu.

Ndugu Washiriki, malengo makubwa ya tafiti hizi yamegawanyika katika maeneo yafuatayo; katika utafiti wa kwanza ‘Integration of Child Protection into Early Child Hood Education; tulilenga kujifunza na kuonesha; -

  • Hali halisi ilivyo na namna ambavyo kama nchi tunazingatia ulinzi wa mtoto wakati wa makuzi na maendeleo ya mtoto.
  • Kutambua uelewa, mtazamo na namna ambavyo wazazi, jamii na walezi wa watoto wanazingatia ulinzi wa mtoto wakati wa makuzi na maendeleo ya mtoto.
  • Kutambua na kufafanua changamoto na fursa zilizopo katika kuleta mabadiliko na kuimarisha hali ya ulinzi wa mtoto wakati wa makuzi na maendeleo yake
  • Katika utafiti wa pili, ‘Assessment of Learning and Teaching Environment in Pre-Primary Education in Tanzania’, tulilenga kujifunza; -
  • Hali ya uandikishaji wa watoto katika elimu ya awali hapa nchini kwa kuzingatia hali ya ulemavu, jinsia, umri na jiografia ya maeneo wanayoishi watoto.
  • Mazingira ya kujifunzia na kufundishia ya elimu ya awali na namna yanavyochangia au kukwamisha upatikanaji wa elimu ya awali kwa watoto wa umri wa miaka 0-6.
  • Kuangalia hali ya ushirikiano kati ya walimu, wazazi na jamii katika kumhakikishia mtoto elimu bora ya awali
  • Kutambua uelewa na utayari wa walimu wa madarasa ya awali katika kuwapatia watoto maarifa na malezi yanayozingatia mahitaji na uwezo wa kila mtoto
Ndugu Washiriki, HakiElimu tumejifunza kuwa kama taifa kuna hatua nzuri ambazo tumezifikia katika eneo hili lakini pia ziko changamoto ambazo zinatupasa tuje pamoja kama taifa kuzishughulikia ili kumhakikishia mtoto wa kitanzania ulinzi, makuzi bora na elimu bora katika umri wake wa awali.

Mathalani, katika tafiti hizi tutaona kuwa Tanzania tumeweza kupitisha sheria na miongozo mbalimbali yenye lengo la kumlinda mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama yake hadi kufikia umri wa kujitegemea wa miaka 18 (kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977). Akiwa tumboni mwa mama mathalani, sheria zinazuia utoaji wa mimba (abortion) isipokuwa kama ni lazima kwa mujibu wa ushauri wa daktari na kwa sababu ya faida ya afya ya mama na mtoto. Baada ya kuzaliwa, Sheria ya Mtoto na miongozo mingine ya kiafya inatoa ulinzi kwa mtoto na kutamka haki zake ambazo ni wajibu wa wazazi, walezi na jamii nzima kuzilinda; haki hizi ni pamoja na haki ya kuwa hai, kutonyanyaswa na kupewa huduma muhimu za chakula, matibabu, malazi na elimu.

Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2008 na Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 zinatoa haki kwa kila mtoto kupata elimu ikiwemo elimu ya awali ambayo ni ya lazima. Sheria hizi zinaufanya kuwa ni wajibu kwa mzazi, mlezi na jamii kuhakikisha mtoto anapata elimu ya awali kabla ya kujiunga na elimu msingi.

Kwa miongozo hii takribani kila shule ya msingi Tanzania ina walau darasa la awali ambalo linafanya kazi ya kuwapatia elimu watoto wetu. Kwa mfano, kuna takribani shule au madarasa ya awali 17,493 sawa na asilimia 99.6% ya shule za msingi 17,562 za umma na zisizo za umma zilizopo kwa sasa (BEST, 2018). Hali ya uandikishaji watoto katika madarasa ya awali siyo mbaya ukilinganisha na malengo tuliyojiwekea.

Mathalani katika wilaya ambako tafiti zilifanyika, wastani wa uandikishaji ukilinganisha na matarajio ni zaidi ya asilimia 100. Changamoto ya uandikishaji inabaki kwa makundi ya watoto wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu na jamii za wafugaji ambako wastani wa uandikishaji umebaki kuwa chini ya asilimia 70 ya malengo ya uandikishaji.

Ndugu Washiriki, pamoja na mafanikio haya, kama nilivyogusia hapo awali, bado ziko changamoto mbalimbali katika makuzi ya watoto, ulinzi na elimu ya awali. Kwa mfano, pamoja na sheria nzuri zinazozuia utoaji mimba au ulinzi wa uhai wa mtoto akiwa tumboni, takwimu zinaonesha kuwa kuna
matukio ya utoaji mimba 36 kwa kila wanawake 1000 wanaopata ujauzito (NIMR & MUHAS, 2016). Aidha, matukio ya unyanyasaji wa watoto wadogo, na changamoto za malezi kwa watoto ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa ulinzi na huduma vinaongezeka. Idadi ya watoto wenye umri wa kuwa shuleni lakini hawako shuleni na waishio katika mazingira magumu inazidi kuongezeka.

Upande wa upatikanaji wa elimu ya awali tafiti zinaonesha changamoto nyingi licha ya mafanikio ambayo Tanzania imefikia. Hali ya mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa watoto wa madarasa ya awali bado ni changamoto sana. Takribani asilimia 100 ya wilaya zilizofanyiwa utafiti zinaonesha kuwa na changamoto ya uhaba wa miundombinu mbalimbali. Hizi ni pamoja na vyoo, madarasa, maji safi, lishe shuleni, madawati na mahali salama pa kuchezea watoto na vifaa vya michezo.

Aidha, tafiti zinaonesha kuwepo kwa changamoto kubwa ya uhaba wa walimu wenye sifa ya kufundisha madarasa ya awali pamoja na uelewa mdogo wa mbinu za kufundishia madarasa ya awali. Kwa mujibu wa tafiti hizi mathalani, katika shule zote zilizohusika kwenye utafiti hakukuwa na walimu wenye mafunzo maalumu kwaajili ya kufundisha madarasa ya awali. Hii inamaanisha kuwa katika shule hizo walimu waliokuwa wakifundisha madarasa ya awali hawakuwa na sifa stahili ya kufundisha madarasa hayo. Matokeo haya yanaakisi takwimu za kitaifa juu ya hali ya walimu wa elimu ya awali nchini; kwa mujibu wa takwimu za elimu (BEST 2018), mwalimu mmoja mwenye sifa anahudumuia wanafunzi 114 (1:114) wa darasa la awali badala ya wanafunzi 25 (1:25) kama inavyotakiwa katika miongozo ya elimu.

Takribani asilimia 52.6% ya walimu wa madarasa ya awali walioshiriki utafiti huu, hawana uelewa sahihi wa maana ya elimu ya awali na mahitaji yake. Hali hii imesababisha ufundishaji na malezi ya watoto wa awali shuleni kufanana kwa kushabihiana na na ile ya watoto wa shule ya msingi. Mathalani, takribani asilimia 50% ya walimu walioshiriki katika tafiti hizi, wanatoa adhabu kali kama za viboko na vitisho eti ili kuhakikisha watoto wanakuwa na nidhamu. Lakini mbinu hizi hazipendekezwi kutumika kwa watoto wa shule awali.

Tafiti pia zimebaini changamoto ya ushirikiano mdogo kati ya wazazi/walezi na walimu katika kuhakikisha mtoto anapata malezi na elimu stahili vinavyoendana na umri na mahitaji yake. Ushirikiano hafifu kati ya wazazi na walezi umesababisha watoto kukosa mahitaji ya msingi kama lishe shuleni na kukumbwa na matukio ya unyanyasaji kutokana na ulinzi hafifu.

Ndugu Washiriki, kutokana na tafiti hizi, HakiElimu tunapendekeza mambo makubwa yafuatayo ili kuendelea kupiga hatua katika utoaji wa elimu ya awali; -
  • Kuna haja ya kuzingatia suala la uandikishaji wa watoto wanaoishi na ulemavu pamoja na waishio katika mazingira magumu ambao hali ya uandikishaji wao iko chini.
  • Ni muhimu serikali iwekeze katika kujenga na kuboresha miundombinu ya shule yakiwemo madarasa ya awali ili iendane na hali na umri wa watoto husika.
  • Ni muhimu kuwahamasisha na kuongeza mafunzo na ajira kwa walimu wa elimu ya awali ili kuziba pengo kubwa la mahitaji ya walimu lililopo. Pamoja na hili, serikali inahitaji kuwajengea uwezo walimu waliopo ili wawe na uelewa wa kutosha juu ya dhana ya elimu ya awali na mahitaji yake.
  • Aidha, kuna haja pia ya kuhamasisha ushirikiano mkubwa zaidi baina ya wananchi na jamii pamoja na walimu. Makuzi na malezi ya watoto yatafanikiwa zaidi ikiwa kutakuwa na ushirikiano wa karibu zaidi kati ya wazazi, walezi na walimu wao.
  • Suala la ulinzi wa mtoto tangu akiwa tumboni mpaka anafikisha umri wa kwenda shule ya msingi ni la jamii nzima. Serikali iweke miongozo itakayoratibu ushirikiano huu juu ya malezi na makuzi ya mtoto.
Kama taasisi yenye lengo la kuona kila mtoto wa kitanzania anapata haki ya elimu bila kujali hali yake, tunashukuru na tumefurahia ushiriki wenu katika uzinduzi wa tafiti hizi mbili zinazoangazia masuala ya elimu ya awali kwa watoto wetu. Basi niwakaribishe kuzipokea ripoti hizi, kuzisoma na kuendeleza mjadala na mapendekezo ya njia za kutatua changamoto zilizoonekana.

Pamoja na kwamba mjadala mkubwa uliopo sasa nchini na duniani kote ni juu ya ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19), mjadala huu ni muhimu pia kwani maisha na mikakati yetu ya elimu ni lazima iendelee.Aidha, sekta hii ni mojawapo ya sekta zilizoathiriwa sana na janga hili la COVID 19.. Hivyo ni muhimu tuendeleze mjadala wa namna ya kujilinda, kutafuta tiba, na kinga lakini zaidi namna ambayo tutamlinda mtoto na kuendelea kumpatia haki yake ya kupata elimu na taarifa.

Dkt John Kalage
Mkrugenzi Mtendaji
HakiElimu
 
Back
Top Bottom