Hadithi zilizofundisha na kujenga "Utu wa mtu"

Samahani

JF-Expert Member
Oct 29, 2018
222
335
Kuna mengi naweza kuyasahau kati ya yale niliyopata kuyasikia na kuyafanya katika utoto wangu, hasa katika kipindi nilipokuwa shule za awali, msingi na sekondari. Hata baadhi ya majina na sura za wale ambao nilitumia muda mwingi nikiwa nao katika kipindi hiki nimevisahau kabisa, na mara kadhaa nimekuwa nikipishana nao barabarani pasi na kukumbukana. Tunapokumbukana na wachache, wote tunakuwa na jukumu walau la kujitambulisha upya ili kuweza kuboresha kumbukumbu zetu, na hapo ndipo tuanze kukumbushana yale ambayo tunayakumbuka yahusuyo kipindi kile.

Lakini kati ya mengi ninayoyasahau kila siku, imekuwa vigumu sana kusahau baadhi ya simulizi (hadithi) na tungo mbalimbali nilizozisoma wakati ule. Hizi zimekuwa zikiyaandama maisha yangu kwa muda mrefu, na zipo ambazo kila ninapopata nafasi ya kuzisoma upya (ingawa kwa nadra kutokana na kupotea kwa vitabu), najikuta Napata msisimko na hisia za kipindi kile zinamea kwa kasi sana! Nyingi ya tungo hizi zililenga kujenga “UTU” wa kweli miongoni mwa wanaozisoma au kuzisimulia. Nitatoa mifano michache.

Tungo kama Tola anakula gizani ingawa iliishia kutuchekesha sana kwa kumsoma bwana yule aliyekuwa na “mkono wa birika” mpaka kwa familia yake, leo zinaainisha namna ambavyo familia nyingi zinaathirika kutokana na uchoyo na ubinafsi wa viongozi wa familia (wazazi/ walezi). Hii huwa inanyima raha ninapoagiza kinywaji cha gharama wakati nyumbani hawana “mboga ya maana”. Hakika mpaka leo, simulizi hii ni kama vile inanifuata kila nilipo!

Wale vijana Sadiki na Chitemo mpaka leo wananifikirisha juu ya madhara ya uvivu katika majukumu ya kila siku. Wakati fulani tunaporekebishwa kutokana na uvivu, tunakuwa na hasira ya kufanya maamuzi fulani. Lakini kila nikifikiria kilichomkuta Chitemo kwa kuamua kujiondokea na “Kwenda kuteseka mbali na nyumbani peke yake”, najikuta nakubali kupokea ushauri wa kubadilika mara moja ninapoonywa juu ya tabia zangu na maamuzi yangu ya ovyo.

Yule mfalme mkorofi aliyesababisha ikaandikwa simuliza ya Laa Laa Laaaa mara nyingi huwa ananikumbusha madhara ya ubaya unaoweza kuwa unawatendea wengine walio chini yako. Kumbe, wakati ninapokuwa kwenye nafasi, ni vema kuwa na nidhamu binafsi nikielewa kuwa, pamoja werevu nilionao, wapo werevu wanaoweza kuniliza na kuniwajibisha siku yangu inapofika.

Kuna kinyozi mmoja alikosa siri kabisa, akashindwa kujizuia kuutangazia umma kuwa Mfalme ana masikio kama ya Punda. Kumbe dunia haina siri!! Naweza kuwa mwerevu na kuamua kuificha siri yangu pahala ambapo nina hakika hakuna kiumbe anaweza kuigundua, lakini ghafla, kumbe siri ile ni kama tu nimeiweka hadharani. Pia, kumbe ni vigumu kwa binadamu kuishi na siri peke yake!!

Kuna jababi mmoja hakupenda kabisa masihara, huyo wa kuitwa Kibanga. Kibanga bwana akaamua alichoamua baada ya kuyachoka madhila na manyanyaso ya mkoloni. Kibanga akampiga Mkoloni. Katika zama hizi ambapo tunahaha na ukoloni mambo leo pamoja na mifumo mingine ya kinyonyaji katika jamii zetu, kumbe bado wanaweza kuwepo majasiri ambao hawataishia kulalamika tu, watachukua maamuzi kama Kibanga! Kuna wakati natamani sasa mimi ndio niwe Kibanga!!

Wachache watakuwa wanaukumbuka ule Muwa uliozamisha meli. Sijui mkulima wa miwa yule alikuwa ni wa wilaya gani hapa nchini ili eneo hilo kijengwe kiwanda cha sukari upesi. Nahodha na wasaidizi wake waliacha kabisa kujishughulisha na meli wakaanza kujishughulisha na miwa. Waliitafuna na kuifakamia mpaka chombo kikaenda kombo. Leo hii nikihusianisha hadithi ile na maisha ya sasa, naona namna ambavyo wenye mamlaka katika ngazi zote kuanzia familia mpaka taifa wanavyoweza kuzamisha jamii yao kutokana na kukumbatia “utamu na starehe” za muda mfupi. Kuna wakati najiuliza, kwanini wasingesubiri mpaka wafike ng’ambo kisha ndio wale kwa starehe shehena ile ya miwa? Ah, lakini ndio hivyo tena, hata mimi kuna nyakati nimeshazamisha kabisa maisha yangu kwenye matatizo makubwa kwa starehe za muda mfupi kama pombe na wanawake. Lakini katika hali hii, simulizi hii daima haiwezi kufutika kichwani.

Yule Jogoo wa ajabu mnamkumbuka? Alikapelekesha kadogo Pazi mpaka kakaomba radhi! Siku zote Pazi alipenda kuwaonea “wanyonge”, lakini siku alipokutana na Jogoo yule wa ajabu, hapo aling’amua kuwa hakuna alichokuwa anajua! Aligeuzwa kichwa chini miguu juu na kutembezwa mpaka karibu na gulioni. Leo hii kuna maeneo tunaendekeza ubabe na manyanyaso yasiyo na maana. Sasa kila ninapokuwa katika “anga zangu”, huwa nakumbuka kuwa kama Pazi alivyonyanyasika na jogoo ambaye hakumdhania, hata mimi yanaweza kunikuta. Mara moja huwa najirudi na kukaa kwenye mstari!

Kuna “mpare mwenzangu” alibahatika kuwa tarishi. Kujifungia kwake “upareni” bila kupanua wigo na kujifunza lugha za wengine kukamnyima haki yake ya kuelewa mambo. Yeye akaishia kumtambua bwana Sikuelewi kuwa ndiye mmiliki wa mali nyingi popote alipoenda. Alipouliza umiliki wa Ng’ombe, wanawake, nyumba nzuri na vingine vingi alivyoviona katika kazi yake ya utarishi, kwakuwa alikuwa akizungumza kipare tu, alipewa jibu rahisi; Sikuelewi! Yeye akaishia kujiaminisha kuwa, mmiliki hasa ndiye alikuwa akitambulika kwa jina hilo. Hii inanipa tamaa ya kujua lugha na tamaduni za wengine kwenye ulimwengu wa sasa. Hakika tarishi yule amenisaidia kuona umuhimu wa kujifunza.

Pasi na shaka mtamkumbuka huyo wa kuitwa Chopeko. Yule bwa’mdogo mwenye tamaa ya nyama ambazo mwisho wa siku zingeiva nayeye angekula zikiwa mezani kwa starehe kubwa, lakini akaamua kuanza “kuzichopoa” zingali jikoni, tena moto kweli kweli (nna hakika zilikuwa hazijaiva). Chopeko na mnofu vinanikumbusha kuacha udokozi! Niwapo kazini, nyumbani, kwenye taasisi mbalimbali za kijamii, niache mara moja tamaa ya kudokoa dokoa ili nisije nikapelekwa kwa tabibu mwenye spoku ya moto, akaunguza shavu moja, kisha la pili halafu nikatema donge la nyama nililolificha awali. Si mnaona wahujumu wanavyozirudisha au kuishia kwenye vifungo vya aibu?

Ah… Siwezi kuzimaliza kwakweli! Lakini zote zimenifanya, na zinaendelea kunifanya nione umuhimu wa kuwa MTU! Zote zililenga kujenga heshima, maadili mema, kujiamini, kuwathamini wengine, kuwa na ujasiri, kukwepa matatizo ya kujitakia, kuepuka dharau kwa wengine, kujali maslahi ya pamoja, uzalendo na mafunzo mengine mengi mno ya muhimu.

Fikiri habari za Pamela na kipini chake inavyoweza mara zote kukuzuia kuyatamani yaliyo juu ya uwezo wako ili usije kubaki na kovu maishani. Kumbe pamoja na jitihada zetu, kuna wakati tunapaswa kuwa na utu wa kusema Sizitaki mbichi hizi!! Ah!! Hebu kumbuka jinsi kilimo kilivyowasaidia vijana wale wawili wa yule baba Aliyerudi kutoka safari ya mbali! Kumbe ni kweli jembe halimtupi mkulima “aliyeko serious”.

Simulizi hizi hakika zilikuwa ni chemchem ya fikra zisizokauka kichwani. Huenda kuna wenzangu wengi ambao kama nilivyo mimi, wanaishi maisha yao leo kwa kurejea sehemu ya simulizi hizi!

Hata nyimbo na tungo nyingine tulizoimba shuleni zilikuwa na lengo hilihili, kujenga utu! Wakati ule, tulikimbia mchakamchaka tukihamasisha mambo fulani katika jamii kama vile usafi, kujitambua na kuwaenzi wakombozi wan chi. Hivi mpaka leo vimeacha doa fulani lisilofutika abadani katika mioyo na Mawazo yetu! Wengi tunajikuta tunatamani kuviishi vile tulivyovisoma au kusimuliwa, hata kama hatufanyi hivyo! Ndio, kujua ukweli ni jambo moja, na kuufuata ni jambo linguine tofauti kabisa! Ndio maana kuna mtu aliwahi kuambiwa Mwanangu Pepe huna masikio.

Sina hakika sana na mtaala wa sasa ikiwa bado hadithi zile au walau zinazofanana na zile vinafundishwa na kusomwa. Nitajitahidi kufuatilia hili. Najua kuna wataalamu humu, mtanisaidia kunijuza ikiwa bado yale ambayo tuliyasoma wakati ule kwasasa yapo, na ikiwa hayapo, nini kinasomwa kama m’badala wake.

Wasalaaaaaaam!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom