Hadithi Fupi: Ni kiwango gani cha Ardhi anachohitaji mwanadamu

Wildlifer

JF-Expert Member
May 12, 2021
1,883
5,190
Wapenzi wa simulizi, hii ni Simulizi iliyotoka mwaka 1886 huko Urusi iliyotungwa na Nguli wa Fasihi, Leo Tolstoy. Mwanafasihi huyu ameandika Riwaya na Hadithi fupi fupi nyingi sana. Riwaya zake Maarufu ni Anna Karenina na War and Peace.

images (18).jpeg

Hadithi hii fupi iliitwa : WHAT AMOUNT OF LAND DOES A MAN NEED. Ni simulizi kumuhusu Mkulima aliyeitwa Pahom aliyekuwa ni mwenye tamaa ya Kumiliki ardhi kwa ajili ya shughuli zake za kilimo na ufugaji.

images (20).jpeg

Licha ya kuwa ni Simulizi yenye umri wa takribani miaka 150, ujumbe wake bado unaishi.

Enjoy!

Dada Mkubwa alikuja kumtembelea mdogo wake aliyekuwa akiishi kijijini. Yeye alikuwa anaishi mjini na ameolewa na mfanyabiashara, huku mdogo wake alikuwa ameolewa na mkulima. Jioni wakiwa wamekaa na kupata chai, dada mtu akaanza kujisifu kuhusu uzuri wa maisha ya mjini; akijinasibu namna wanaishi kwa starehe, nguo nzuri ambazo watoto wao walivaa, vyakula na vinywaji vizuri walivyokuwa wakila na kunywa na namna alivyokwenda kwenye makumbi ya sinema, starehe na burudani.

Mdogowe, kwa ghadhabu, alimjibu kwa kuyapondea maisha ya shemeji yake mfanyabiashara na kuyasifu yale ya mmewe mkulima.

'kamwe siwezi badilisha maisha yangu na yako', alimueleza. 'Tunaweza kuwa tunaishi duni, lakini hatuna wasiwasi. Mnaweza kuwa mnaishi kisasa, lakini siku zote mnapata zaidi ya mnachohitaji, mko kwenye uwezekano mkubwa wa kufirisika kuliko sisi, unafahamu ule msemo kuwa 'kupata na kupoteza ni mapacha'. Mara nyingi hutokea, matajiri leo, kesho wanaomba chakula. Maisha yetu ni salama. Ingawa maisha ya mkulima sio ya kifahari, lakini ni marefu. Kamwe hatuwezi tajirika, lakini siku zote tunapata chakula cha kututosheleza'

Dada mtu, kwa hamaki kubwa alimjibu;

'Umemaliza? Ndio, kama unamaanisha kula pamoja na nguruwe na ndama! Mnajua nini kuhusu usafi au kanuni za kula? Hata mmeo afanye kazi za kitumwa namna gani, mtakufa kama mnaoishi kwenye lundo la samadi, wewe na wanao pia'.

'Ni kweli, lakini kwa kipi?' aliuliza mdogowe, 'Ni kweli kazi zetu ni ngumu na chafu, lakini hatusujudii watu. Nyie wa mjini mmezungukwa na vishawishi wakati wote. Leo kila kitu kinaweza kuwa sawa ila kesho yake Shetani akmashawishi mmeo kwa pombe, au kamali au wanawake na vyote vikapotea? Je, hayatokei hayo?'

Pahom, mwenye nyumba aliyekuwa chumba jirani, alikuwa akiyasikiliza na kuyafuatilia mazungumzo ya wanawake hao.

'Kuna ukweli', alijiwazia. 'sisi wakulima toka tukiwa watoto tumekuwa bize na kulima, haturuhusu upuuzi utawale akili zetu. Tatizo letu ni moja, hatuna ardhi ya kutosha. Ningekuwa na ardhi ya kutosha, hata shetani mwenyewe nisingemuogopa'.

Wale wanawake walimaliza chai zao, wakazungumza kidogo kuhusu mavazi, wakatoa vyombo vya chai, kisha wakalala.

Lakini shetani alikuwa nyumba ya nyumba, na alikuwa ameyasikia mazungumzo yote. Alifurahi kuona namna mke wa mkulima alivyomsifia mmewe, kiasi cha kujinasibu kuwa akiwa na ardhi ya kutosha, hatomuogopa shetani.

'Haina shida', aliwaza shetani. 'Tutaingia kwenye ushindani'. Nitakupa ardhi ya kutosha, na kupitia ardhi hiyo hiyo, nitahakikisha umeingia kwenye himaya yangu'.
 
II

Jirani na Kijiji hicho, aliishi mwanamke mmoja aliyekuwa ni bwenyenye, akimiliki takribani ekari mia tatu za ardhi. Aliishi kwa amani na wapangaji wake, hadi pale alipomuajiri mwanajeshi mmoja mstaafu kama msimamizi na mkusanya faini wake. Pahom alijitahidi sana kuwa makini, lakini ilitokea mara kwa mara mifugo yake ikiingia shambani kwa mama huyo, na kulazimika kulipa faini.

Pahom alilipa faini hizo, lakini ilimtia ghadhabu na hasira, kias cha kuwa mkorofi hadi nyumbani. Kipindi cha kiangazi alikuwa na misuguano ya mara kwa mara na msimamizi huyo wa shamba, hadi masika ilipoingia, ambapo malisho yalikuwa sio shida tena. Kipindi hiki zilivuma habari kuwa yule mama anauza shamba lake. Lakini kuna tajiri mmoja anataka linunua.

Wakulima waliwaza, 'kama huyu bwana akinunua hilo shamba, basi atatupiga faini kubwa kuliko yule mwanajeshi, nao ndio wanalitegemea hilo shamba'.

Wakaamua kwenda kwake yule mama, kwa niaba ya kijiji wakimsihi awauzie wao, watatoa ofa nzuri zaidi. Yule mama akawakubalia. Wakakubaliana wakulima walinunue na itakuwa mali ya kijiji. Walikutana mara mbili kujadili, lakini hawakufikia muafaka. Shetani alitengeza mgogoro kati yao. Wakaamua kila mtu anunue kivyake kwa njia zake. Yule mama akaridhia pia mpango huo.

Pahom akapata habari kuwa jirani yake ananunua ekari 50, ambapo nusu ya malipo analipa kisa nusu iliyobaki anakamilisha baada ya mwaka. Pahom akaona wivu.

'Hebu tazama' alimueleza mkewe. 'Ardhu inauzwa yote, na watu wanainunua, sintopata kitu'. 'Itabidi nami ninunue. Tununue walau ekari 20. Maisha yatakuwa magumu sana. Yule mwanajeshi anatuumiza na faini zake.'

Walianza umiza vichwa namna ya kupata fedha. Walikuwa na Rubles 100 tu. Waliuza mizinga ya asali na nyuki wake, wakamkodisha kijana wao kama kibarua na kuchukua malipo ya awali na kukopa kwa shemeji yake, wakawa wamekamilisha fedha ya nusu malipo.

Wakaenda kuchagua eneo la ekari 40. Likiwa na miti ndani yake, kisha kumfuata mama muuzaji. Wakavutana kisha kuafikiana na kuandikishana na wakalipia nusu kwa ahadi ya kulipa nusu ya pili baada ya miaka miwili.

Sasa Pahom akawa ana miliki ardhi yake mwenyewe. Akaazima mbegu na kuzipanda. Mavuno yakawa mazuri, na ndani ya mwaka mmoja akawa amefanikiwa kulipa deni la yule mama bwenyenye na la shemeji yake. Alilima shamba lake mwenyewe, miti alikata shambani kwake, mifugo alilishia shambani kwake. Kila alipolitazama shamba hilo, moyo wake ulijawa na furaha sana.

Kila kitu kilikuwa sawa, lakini jambo moja lilimsumbua shambani kwake, wavamizi. Hawa mara kwa mara waliharibu mazao yake. Alijaribu kuwasihi kwa ustaarabu lakini hali hiyo iliendelea. Wafugaji walichungia shambani kwake mara kwa mara. Kila mara alikuta farasi wamepitishwa shambani kwake. Asubuhi akienda shamba anakuta mazao yamevurugwa. Alivumilia, hakushitaki, mwishowe akachoka. Akaenda fungua mashitaka mahakama ya wilaya.

Alijua fika, kwa wavamizi hao hawakuwa na nia ovu, bali ni shida ya ardhi ndio imewafanya wayafanye hayo. Lakini aliwaza; 'siwezi kukaa tu na kwaangalia, wataharibu mazao yangu yote. Ni lazima wafunzwe somo'.

Hivyo wakaadhibiwa. Wa kwanza, mwingine, kisha wengine wawili watatu walilipishwa faini. Majirani wakaanza tengeneza chuki na Pahom. Wakaanza achia mifugo yao iingie shambani kwake kwa makusudi kabisa. Mkulima mmoja aliingia shambani usiku, akakata milimo ili tu achune magome yake. Asubuhi akakuta hali hiyo. Kwa hasira akajisema, 'angekataa miti michache hapa na pale isingekuwa mbaya sana, ila huyu mshenzi amekata kitalu chote cha milimao. Ningemjua, ningemlipisha'.

Pahom akawaza na kuwazua, kumjua ni nani anayeweza kuwa amefanya hivyo? Akahitimisha, ni Simon tu, hakuna mwingine, hivyo akaondoka kwenda kwake, lakini hakumkuta, hasira zikamjaa zaidi. Akaamini kitendo cha kutomkuta akaamini zaidi kuwa anahusika. Pahom akafungua Mashitaka. Kesi ya kwanza, Simon akashida, rufaa akashinda sababu hakukua na ushahidi.

Pahom akashikwa na hasira na kuwabwatukia mahakimu na wazee wa mahakama; 'mmeruhusu wezi walainishe mikono yenu, mngekuwa waadilifu, msingeruhusu wezi wawe huru'. Sasa Pahom akakorofishana na mahakama na majirani. Akaanza kutishiwa kuchomewa nyumba yake. Hivyo, licha ya kuwa sasa ana ardhi kubwa, lakini sasa mahusiano yake na jamii yalikuwa mabovu, kuliko kabla hajawa na ardhi.

Wakati huu zikaanza tetesi kuwa watu wengi walikuwa wakihamia maeneo mengine. 'Mimi sina haja ya kuhama', aliwaza. 'wakiondoka wengine, tutabaki na ardhi wazi hivyo nitanunua na kuishi kwa amani. Kwa sasa ardhi niliyonayo hainitoshi kukaa kwa amani'.

Siku moja akiwa amekaa kwake, alipita mgeni. Akamkaribisha na kumruhusu kulala hapo. Usiku baada ya chakula wakiwa wanazungumza, Pahom alimuuliza anakotoka. Mkulima huyo alimjibu kuwa anatoka Volga, alipokuwa akifanya kazi huko. Mazungumzo yaliendelea hadi yalipowafikisha sehemu ya mgeni huyo kumuambia Pahom watu wengi wanahamia eneo hilo. Kijiji kinawapa hadi ekari 25 kwa kila mtu. Akimueleza eneo hilo ngano inakuwa urefu wa farasi. Na ukikata mundu tano tu, zinajaza lundo moja. Kuna mtu amehamia kule akiwa hana chochote sasa hivi ana ng'ombe sita, wake mwenyewe.

Moyo wa Pahom ulijawa furaha na shauku na kuwaza 'kwanini niendelee kuhangaika hapa kwenye hiki kijishimo wakati ninaweza kuishi kwa amani sehemu nyingine? Nitauza kila kitu changu hapa nikaanze maisha huko, vitarudi tena. Ila itabidi niende mwenyewe huko nikajionee kwanza'.

Kiangazi kilipofika alifunga safari ya kwenda huko. Alipanda Treni ya volga hadi samara, kisha akatembea kwa miguu takribani Kilomita 480. Kila kitu kilikuwa kama alivyosema yule mgeni. Kila mtu alipewa ekari 25 za kijiji, na kama una hela unaweza nunua zaidi kwa shilingi 2 kwa kila ekari, kwa kiwango chochote utakacho. Alipojiridhisha alirudu nyumbani Kipindi autum imeanza. Alipofika nyumbani aliuza ardhi yake,kwa faida, nyumba yake, mifugo na akachukua akiba yake kwenye mfuko wa kijiji, spring alipoanza akaanza safari ya kwenda alikokulenga.

Alipofika makazi mapya, alisajiri uanachama wa kijiji baada ya kuwasilisha nyaraka takiwa, akapewa vipande vitano vya ardhi (ekari 125) kwa ajili yake na wanae nje ya eneo la kijiji la malisho ya mifugo, akanunua mifugo kutoka kijijini, akajenga nyumba na kuanza makazi. Sasa alimiliki eneo kubwa, mara tatu ya alikotoka, ardhi nzuri kwa kulima nafaka, eneo kubwa kwa kufugia.


 
III

Awali, Pahom wakati anajenga na kuhamia, aliridhishwa na kila kitu, lakini alipoanza kupazoea, aliona hata hapo ardhi aliyonayo bado haitoshelezi. Mwaka wa kwanza alilima ngano kwenye shamba alililopewa na kijiji na alipata mavuno ya kutosha. Mwaka uliofatia alipotaka tena kulima, ardhi haikutosha, hata ile ya awali haikuwepo tena kwani eneo hilo, ngano hulimwa kwenye ardhi ambayo haijalimwa kabisa au iliyopumzishwa kwa kipindi fulani. Wengi walikuwa ni wenye uhitaji kama wake, hivyo ardhi ikawa ni ya kugombania. Wenye kipato kikubwa waliitaka kwa ajili ya kulima ngano, wenye kipato kidogo waliitaka kwa ajili ya kukodisha na kupata fedha ya kulipa kodi.

Pahom aliamua kukodi ardhi. Ardhi aliikodi kwa mkodishaji na kulima kwa mwaka mmoja. Mavuno yalikuwa mazuri, lakini changamoto shamba lilikuwa mbali mno. Ilimlazimu kuyasafirisha umbali wa kilomita 16. Baada ya muda, Pahom aligundua kuwa, wakulima ambao walikuwa ni wapangishaji, walikuwa wakiishi sehemu tofauti na mashamba yao na walikuwa wakitajirika sana. Hivyo akawaza; 'Kama naweza nunua pori, na nikajenga nyumba ndani yake, itakuwa vyema.

Wazo hili lilikuwa likijirudia mara mara kichwani mwake, na alikaa nalo kwa miaka mitatu. Aliendelea na mfumo wake wa kukodi mashamba na kulima ngano. Mavuno yalikuwa mazuri, na hivyo alikuwa akitunza fedha.

Changamoto iliendela kupata ardhi ya kukodi. Ilikuwa ya kugombania, na wakati mwingine hakuna hakika ya kupata. Mwaka mmoja, alikodisha eneo na kulima ukatokea mgogoro na kupelekana mahakamani, na akashindwa hivyo akawa amekula hasara ya kulima. Akawaza sana; 'kama ardhi ingekuwa yangu binafsi, nisingekuwa na kero hizi'.

Alipatana na mkulima mmoja aliyepata matatizo na kutaka kumuuzia ekari 1,300 kwa Ruble 1,500 ambapo atalima kwa awamu mbili. Kabla hajamaliza mauziano haya, Pahom alipata mgeni, mpita njia, ambaye alimkirimu na kumueleza atokako.

Mgeni huyo mfanyabiashara alimueleza kuwa ametoka kununua ardhi huko kwa watu wa Bakshir kiasi cha ekari 13,000 kwa Ruble 1,000 tu. Pahom akamdadisi zaidi, mgeni akamueleza; 'Unachotakiwa ni kuwa na urafiki tu na chifu, basi ardhi umepata. Mimi nilimpa zawadi ya gauni la Ruble 100, jagi la chai, mvinyo kwa wanaokunywa na nilipata ardhi kwa thamani ya chini ya pensi 2 (senti 2) kwa kila ekari'. Akamuonyesha Pahom hatimiliki, na kumuambia; 'ardhi yote iko kando ya mto, haijawahi limwa'. Akaendelea mueleza; 'wana ardhi kubwa hata ukiambiwa utembee mwaka mzima huwezi imaliza, na yote ni mali ya wana Bashkir, ni watu rahisi kama kondoo, na ardhi unaipata karibu na bure'.

'Sasa je!' alijisemea Pahom, 'kama kwa Ruble 1,000 napata ardhi mara kumi zaidi ya hapa, tena ikiwa na deni, kwanini nijiangaishe kununua hapa?. Alimdadisi na ya namna ya kufika huko.

Punde mfanyabiashara huyo alipoondoka, alianza maandalizi ya kwenda huko. Alimuachia mkewe nyumba na kumchukua kijana wake, na safari ikaanza.

Walitembea, kutembea, na kutembea umbali mrefu. Njiani walinunua mvinyo, jagi la chai na vyote walivyoshauriwa na yule mgeni wao. Kwa takribani siku 70 wakiwa wamesafiri kilomita takribani 500, walifika eneo wabakshiri walipokuwa wameweka mahema yao.

Kama alivyosema yule mgeni, ndio ilivyokuwa, watu hawa waliishi kwenye mahema, kando kando ya mito. Hawa kulima wala kula mkate. Ng'ombe wao na farasi walijilisha kwenye maeneo ya wazi. Walipelekewa farasi mara mbili kwa siku ambazo walizikamua na kutengenezea pombe (Koumis). Ni wanawake ndio waliotengeneza pombe na maziwa samli pia. Wanaume maisha yao ilikuwa wanachojali ni kunywa chai na pombe, Kula nyama ya kondoo na kupuliza filimbi. Kiangazi chote hawakufanya kazi, na walikuwa ni mbumbumbu na hawakujua kuongea Kirusi lakini walikuwa ni watu waadilifu.

images (15).jpeg
 
III

Wabashkiri walipowaona walitoka na kuwapokea, mkalimani akapatikana na kisha kujieleza kuwa wamekuja kununua ardhi. Wenyeji waliwafurahia na kisha kuwakaribisha. Walipewa hema lao, kutandikiwa godoro na kuchinjiwa kondoo na kumlaa. Nao walitoa zawadi zao na kuwapatia. Waliwafurahia sana.

Kisha mazungumzo kupitia mkalimani yalianza; 'tunawashukuru kwa zawadi zenu nzuri,na ni hulka yetu kuwakirimu wageni, sasa tuambie kipi mlichokipenda toka kwetu tuwape'. Pahom akawajibu; 'kituvutiacho sisi ni ardhi, kwetu sisi ardhi imejaa na imechoka sana, ninyi hapa mna ardhi kubwa na yenye rutuba sijapata iona'.

Wenyeji walizungumza, wakionyesha kubishana kwa hamasa huku wakicheka na kuwatazama. Pahom hakuelewa kilichokuwa kikizungumzwa.

'Wamefurahishwa sana nanyi, na wako tayari kuwapa ardhi yoyote uitakayo, ni kiasi cha wewe kuionyesha tu ipi', mkalimani alisema.

Baadae wakawa na mabishano, Pahom akamuuliza mkalimani kutaka kujua wanabishania nini na kumuambia kuwa wengine wanasema wasifanye maamuzi bila chifu kuwepo, wengine wakisema hakuna haja ya kumsubiri hadi arudi.

Wakiwa wanaendelea na mabishano, mtu mmoja aliyefaa kofia moja kubwa ya manyoya ya mbweha alifika, wote walikaa kimya na kusimama. 'huyo ndio chifu wetu', mkalimani alisema.

Pahom alisimama na kuchukua gauni na majani ya chai aliyoleta kama zawadi. Chifu akazipokea na kukaa, kisha watu wake wakaanza kumuelezea vitu fulani, kisha akawaamuru kuwa kimya na kuanza kuzungumza na Pahom, kwa kirusi; 'Utapata, chagua tu ardhi uitakayo na itakuwa yako, tunayo ya kutosha'. Pahom akawaza, 'nawezaji tu kuchukua kiasi nitakacho? 'maana wanaweza nipa leo, halafu baadae wakaja nigeuka na kuninyanganya'.

'Nashukuru kwa maneno yako ya hekima', alisema kwa sauti, 'Mna ardhi kubwa nami ninataka kidogo tu, haiwezekani nikaambiwa yangu ni ipi na ikapimwa na kukabidhiwa? Maisha na kifo vipo mikononi mwa Mungu. Nyie watu waungwana mnanipa, ila inaweza tokea watoto wenu wakaja ninyanganyana'. Chifu akamjibu, 'uko sawa, tutakubidhisha'.
Nilisikia kuna mfanyabiashara alikuwa hapa, na mkapa ardhi kidogo na hatimiliki, ningependa pia nipewe namna hiyo'. Chifu alimuelewa.

'Tunao mkataba, tutaenda mjini na utasainiwa'.

'Ardhi itakuwa bei gani?' Pahom aliuliza.

'Bei yetu ni moja tu, Ruble 1,000 kwa siku' Chifu alimjibu.

'Kwa siku? Hicho ni kipimo cha namna gani? Hiyo ndio itakuwa sawa na eka ngapi kwa siku?'

'Hatujui tukuelezaje, sisi tunauza kwa siku. Kiasi cha ardhi utachoweza kukitembea na kukizunguka kwa siku kitakuwa chako, na tunauza Ruble 1,000 kwa siku.

Pahom alishangazwa. 'Kwa siku unaweza kutembea kiasi kikubwa cha ardhi'.

Chifu alicheka; 'Yote itakuwa yako', alimueleza. 'Ila kuna sharti moja, ukishindwa kurejea ndani ya siku hiyo sehemu uliyoanzia, basi fedha yako itakuwa imepotea'.

'Sasa nitaweza vipi alama sehemu nilizopita?' Pahom aliuliza.
'Tutasimama wote sehemu utayoanzia. Na utaenda na koleo, kila sehemu utakayoenda unaona muhimu chimba weka alama, baadae tutapita wote, zunguka utavyoweza, ukirejea ulipoanzia kabla jua halijazama, ardhi yote itakuwa yako.'

Walikubaliana kukutana kesho yake asubuhi mapema. Pahom alipewa godoro la manyoya kulala, na wabakshiri baada ya kupata nyama ya kondoo, kunywa kumiss na chai walienda kulala.

Pahoma hakupata usingizi, alikuwa na mawazo juu ya kesho.

'Nitapata ardhi kubwa sana' aliwaza.
'Naweza tembea takribani kilomita 60 kwa kutwa, mchana ni mirefu siku hizi. Kwa mzunguko wa Kilomita 60 nitakuwa na ardhi kubwa kiasi gani. Ardhi mbaya nitaiuza, au nitawauzia walima, mimi nitalima kwenye ardhi bora zaidi. Nitanunua ng'ombe bora wakulimia, na kuajiri wafanyakazi wawili zaidi, takribani ekari 150 nitalima nyingine itakuwa ya kulishia mifugo.'

Pahom hakupata usingizi kabisa, hadi karibu kupambazuka ndipo alilala. Usingizi wenyewe ulikuwa wa mang'amung'amu. Alikuwa kama anaota. Anaota yuko ndani ya hema, halafu kama kuna mtu yuko nje anacheka. Akawaza ni nani huyo, kutoka nje akamkuta ni yule Chifu ndio amesimama ana cheka. Pahom akamsogelea na kumuuliza, 'Unacheka nini?'. Lakini alipomsogelea karibu akagundua sio yeye Chifu, ni yule mgeni aliyekuja nyumbani na kumuelezea kuhusu ardhi huko Bashkir. Lakini alipokuwa akimfata na kutaka kumuuliza kuwa 'umekuwepo hapa muda mrefu', akaona sio tena yule mfanyabiashara, bali ni yule mkulima kutoka volga aliyemtembelea kwake zamani sana kule kwenye mji wake wa kwanza, baadae akaona sio huyo mkulima bali ni shetani mwenyewe. Mwenye kwato zake na Mapembe yake. Akicheka, huku chini yake mtu akiwa amelala, pekua, huku akitweta. Pahom alijaribu kwa makini, kuangalia yule mtu aliyelala chini ni nani. Akagundua mtu huyo amekufa. Na mtu huyo ni yeye mwenyewe. Alistuka toka usingizini, akiwa amejaa hofu.

Akatazama nje na kuona kumekucha. Akawaza; 'Ni muda wa kuwaamsha, inabidi tuanze'. Akanyanyuka na kumfuata kijana wake kumuasha, aliyekuwa amelala kwenye gari lao la farasi.

images (17).jpeg


Wenyeji waliamka, wakanywa pombe na kumpa chai Pahom, lakini alikuwa ni mwenye haraka ya kuanza. 'Kama tunaenda, twendeni, huu ndio muda muafaka'. Walianza safari ya kwenda, kwa usafiri wa farasi, wengine gari la ng'ombe na kufika kwenye mwamba wa kilima, wao wanaita Shikhan.

Chifu aliweka kiti, akavua kofia yake ya Manyoya, akaichomeka kwenye mti; 'Hii ndio itakuwa alama yako, anzia hapa na utarudi hapa, nenda uwezevyo, ardhi yote itakuwa yako'.

Pahom alitoa fedha na kuziweka kwenye kofia, akavua koti na kubaki na nguo ya ndani isiyo na mikono, akachukua mkate wake na maji na koleo, akaamua kuanza tembea upande ambao analitazama jua.

'Sipaswi poteza muda, ni rahisi kutembea jua kabla halijawa kali'.

Alianza kutembea taratibu, baada ya elfu kadhaa za futi, akajichimba, na kuweka alama inayoonekana. Akaendelea na safari tena, hadi alipogeua na kile kilima alichoanzia kiko usawa wa jua, na kukadilia kuwa ametembea takribani Kilomita 5, akaweka alama tena. Akawazia chai; 'awamu ya kwanza imekamilika, bado nne, na bado mapema sana kurudi, ila itabidi nivue buti'. Alipomaliza, akavua viatu, na kujiona anatembea kwa wepesi. 'Nitaenda kilomita 5 kisha nikate kushoto.

Alianza kwenda, njiaa nyoofu kwa muda mrefu na kisha kugeuka nyuma. Aliwaona wenyeji wake pale kwenye kilima wa wadogo kama siafu, akaona sasa imetosha. 'inabidi kukata kona sasa. Hata hivyo nimetoka jasho sana na nina kiu'. Alikunywa maji, akachimba kuweka alama. Haraka akaanza kutembea. Alitembea, kutembea, akaanza choka. Jua kali. Ila kuwa majira ya saa 6.

'Inabidi nipumzike' aliwaza. Alikaa chini, akala mkate, akanywa maji. Akasita kuegama, kwa kuhofia kusinzia. Muda kidogo akaanza tembea. Chakula kilimpa nguvu, lakini jua lilikuwa ni kali sana, na alihisi usingizi. Alitamani kupumzika lakini aliwaza; 'saa moja la mateso, linakupa starehe ya kudumu maishani'.

Alitembea kwa umbali mrefu na kutaka kukata kona, lakini aliliona bonde kubwa, akaona ni ujinga kuliacha eneo hilo kuwa katani ingestawi vyema hapo'. Akaendelea hadi kuliacha ndani, ndipo akachimba na kuanza kukata kota.

Jua lilikuwa ni kali sana, kiasi chakufanya hata kule walipo wenyeji wake asiwaone sawa sawa. Pahom alianza kuwaza, 'upande huu nimeufanya mrefu sana, na nimetembea kilomita 3 tu bado maili takribani 10 kukamilisha'.

Pahom alitembea umbali mnyoofu, akachimba shimo, na kukata kona kuanza kukifuata kilima alichoanzia.

Pahom alianza kukifuata kilima, lakini alitembea kwa shida sana, joto lilikuwa limemchosha, miguuni alikuwa pekua, miguu imemchika na kuchubuka. Alitamani kupumzika, lakini angechelewa maana jua lilikuwa linaelekea kuzama. Jua halimsubiri mtu.

'Oh, Mungu wangu' alijiwazia. 'Kama isingekuwa kutaka ardhi kubwa. Vipi kama nimechelewa?'

Alikitazama kilima. Alikuwa bado yuko mbali na jua linaelekea kuzama.

Pahom aliendelea, ingawa ni kwa shida ila alijitahidi kutembea haraka haraka. Alizidi kwenda, bado alikuwa yuko mbali, alitupa koti lake, mabuti, chupa la chai, akabaki na koleo tu kama egemeo lake.

'nitafanya nini?' alianza kuwaza kwa kujilaumu. 'Nimepata ardhi kubwa sana, lakini nimeharibu kila kitu. Siwezi liwahi jua'.

Woga aliokuwa nao ulimfanya achoke zaidi, aliendelea kukimbia. Shati na suruali vikimbana, pumzi ikimuisha, moyo ukidunda kama nyundo, miguu alihisi kuwa sio yake.

Licha ya kuhofia kifo, hakukubalia kuacha. 'nitaonekana mpumbavu umbali wote nilioenda niishie hapa'. Aliendelea kukimbia kwa kujilazimisha. Wenyeji wake wakimpungia mikono kumuhamasisha awahi. Alikusanya nguvu na kuendelea kukimbia.

Aliendelea kujikaza, sasa jua lilikuwa likizama kabisa, wenyeji wake akiwaona, kofia ya chifu akiiona, hela pia akiziona. Wakimsihi ajikaze kufika kwenye alama aliyokuwa akiiona. Akakumbuka ndoto yake.

'Kuna ardhi kubwa mno'. Aliwaza. 'lakini je, Mungu ataniruhusu niishi ndani yake?. Nimepoteza maisha yangu. Nimepoteza maisha yangu'

Alijikaza kukimbia, miguu akiibuluta. Sasa jua lilikuwa limezama nusu. Akiwa amefika eneo la kilima. Giza lilianza, akaanza kulia. 'Jitihada zangu zote zimekuwa ni bure kabisa'. Kelele za wenyeji wake zikimuhimiza kukimbia, zilimstua. Akawaza, alikuwa chini ya kilima hivyo jua lilionekana kuzama, lakini ilikuwa bado. Akaanza tena kukimbilia kilima.

Alijikaza, akafika kileleni, miguu imechoka akakumbuka ndoto yake, akaanza kulia. Akifikia kofia. Chifu akampokea kwa furaha.

'mwamba kabisa huyu' alimfurahia chifu 'amepata ardhi kubwa sana'

Mfanyakazi wa Pahom akaja kumsaidia na kumnyanyua. Damu zikimtoka mdomoni.

Wabakshiri walisikitika sana.

Yule mfanyakazi wa Pahom, akachukua koleo. Akachimba kaburi refu kumtosha Pahom na kumzika.

Futi sita za ardhi kutoka kichwani kwake hadi miguuni, ndizo alizokuwa akihitaji.
images (21).jpeg
 
Nimeisoma yote,
Ila mbna kama mwishon inaishia kijanja janja
Imeisha kwamba Pahom amefariki.

Huyu Pahom alikuwa na tamaa sana ya kupata ardhi. Na kuwa na tamaa sana katika jambo lolote inaweza kukufanya ukapoteza vyote ulivyo navyo.

Pahom tayari alikuwa na ardhi ya kutosha lakini akawa na tamaa ya kumiliki ardhi zaidi bila kujua kwamba hiyo ni tamaa tu ila all he needed was six feet under (kaburi). Hiyo ndio kiasi cha ardhi ambacho binadamu anastahili.

Huyu Pahom baada ya kufariki sehemu ya kuzikwa mwili ilikuwa na ukubwa wa futi sita tu. Na ndicho alistahili na sio zile tamaa za kutaka kumiliki ardhi yote.

Thank you OP.
 
Nimejifunza yatupasa kuwa na kiasi kwa kila jambo. Pale unapohisi unafanya sahihi ya kukutosha kumbe ndio twajimaliza wenyewe.

Too much of anything is harmful
 
Imeisha kwamba Pahom amefariki.

Huyu Pahom alikuwa na tamaa sana ya kupata ardhi. Na kuwa na tamaa sana katika jambo lolote inaweza kukufanya ukapoteza vyote ulivyo navyo.

Pahom tayari alikuwa na ardhi ya kutosha lakini akawa na tamaa ya kumiliki ardhi zaidi bila kujua kwamba hiyo ni tamaa tu ila all he needed was six feet under (kaburi). Hiyo ndio kiasi cha ardhi ambacho binadamu anastahili.

Huyu Pahom baada ya kufariki sehemu ya kuzikwa mwili ilikuwa na ukubwa wa futi sita tu. Na ndicho alistahili na sio zile tamaa za kutaka kumiliki ardhi yote.

Thank you OP.
Pengine kilichomsababishia masahibu huyu bwana ni uduni wa teknolojia?

Mfano, eneo la kwanza TRESPASSERS walimsumbua kungekuwa na fensi ya ukuta, asingepata shida nao, na asingepata tabu ya kuhama hapa.

Na hata alipoenda nunua ardhi sehemu aliyofia, kungekuwa na vipimo vya kisasa vya ardhi, asingepata masahibu hayo.
 
Pengine kilichomsababishia masahibu huyu bwana ni uduni wa teknolojia?

Mfano, eneo la kwanza TRESPASSERS walimsumbua kungekuwa na fensi ya ukuta, asingepata shida nao, na asingepata tabu ya kuhama hapa.

Na hata alipoenda nunua ardhi sehemu aliyofia, kungekuwa na vipimo vya kisasa vya ardhi, asingepata masahibu hayo.
Inawezekana. IMO naona hii hadithi ni zaidi ya “mkulima”. Mkulima ametumika tu kama mfano lakini ujumbe mkubwa ilikuwa ni tamaa na arrogance.

Huyu mkulima amevalishwa sura ya tamaa na asiyeridhika. Kipimo cha mtu wa tamaa ndicho kilichosababisha kifo chake. Ardhi anapewa sawa na “bure”. Aliweza kuchukua kiasi cha kawaida tu lakini yeye alitamani kama ilikuwa ndani ya uwezo wake angechukua hata eneo lote. Hiyo ni tamaa.

Ni sawa na upewe chakula kingi sana vya kila aina. Uambiwe kwa kuwa upo na njaa kula hadi ushibe kinabaki acha. Kwakuwa haujaambiwa ule kiasi gani na wewe una tamaa unakula hadi kusimama utembee ni shida. Ila uliweza kula kiasi ukashiba ukaacha.
 
Inawezekana. IMO naona hii hadithi ni zaidi ya “mkulima”. Mkulima ametumika tu kama mfano lakini ujumbe mkubwa ilikuwa ni tamaa na arrogance.

Huyu mkulima amevalishwa sura ya tamaa na asiyeridhika. Kipimo cha mtu wa tamaa ndicho kilichosababisha kifo chake. Ardhi anapewa sawa na “bure”. Aliweza kuchukua kiasi cha kawaida tu lakini yeye alitamani kama ilikuwa ndani ya uwezo wake angechukua hata eneo lote. Hiyo ni tamaa.

Ni sawa na upewe chakula kingi sana vya kila aina. Uambiwe kwa kuwa upo na njaa kula hadi ushibe kinabaki acha. Kwakuwa haujaambiwa ule kiasi gani na wewe una tamaa unakula hadi kusimama utembee ni shida. Ila uliweza kula kiasi ukashiba ukaacha.
Alichopitia Pahom, 99% ya wakulima duniani, tungefall kwenye same fate. Shetani hupitia kwenye madhaifu yetu na kutuumizia hapo.
 
Inawezekana. IMO naona hii hadithi ni zaidi ya “mkulima”. Mkulima ametumika tu kama mfano lakini ujumbe mkubwa ilikuwa ni tamaa na arrogance.

Huyu mkulima amevalishwa sura ya tamaa na asiyeridhika. Kipimo cha mtu wa tamaa ndicho kilichosababisha kifo chake. Ardhi anapewa sawa na “bure”. Aliweza kuchukua kiasi cha kawaida tu lakini yeye alitamani kama ilikuwa ndani ya uwezo wake angechukua hata eneo lote. Hiyo ni tamaa.

Ni sawa na upewe chakula kingi sana vya kila aina. Uambiwe kwa kuwa upo na njaa kula hadi ushibe kinabaki acha. Kwakuwa haujaambiwa ule kiasi gani na wewe una tamaa unakula hadi kusimama utembee ni shida. Ila uliweza kula kiasi ukashiba ukaacha.
Mabishano ya wale kina dada, mwanzoni mwa simulizi. Your views please!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom